Sura 7 · dakika 6 za kusoma · dakika 8 za kusikiliza
Jinsi ya Kuwashughulikia Wale Wasio na Uhakika na Waliorudi Nyuma
I. Wale Wasio na Uhakika.
Wale wasio na uhakika wanaweza kugawanywa katika makundi mawili.
1. Wale wasio na uhakika kwa sababu ya kutojua. 1 Yohana 5:13, litawaonyesha wote walio hivyo kwamba tunaweza kujua kwamba tuna uzima wa milele. Mara nyingi unapowauliza watu kama wanajua kwamba wameokoka, au kama wanajua kwamba dhambi zao zimesamehewa, au kama wanajua kwamba wana uzima wa milele, watajibu, “Aa, hakuna mtu ajuaye jambo hilo.” Waweza kuwaambia, “Ndiyo, Biblia inasema kwamba wote waaminio wanaweza kulijua,” kisha uwaonyeshe 1 Yohana 5:13. Yohana 1:12 linaonyesha kwamba Kristo huwapa wote wampokeao uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu. Njia nzuri ya kuutumia mstari huu ni kumwuliza mtafutaji maswali juu yake. “Kila mtu ampokeaye hupewa uwezo wa kufanyika nini?” Mtafutaji, kama anautazama mstari huo kwa makini, atajibu, “Mtoto wa Mungu.” Kisha uliza swali linalofuata, “Je, wewe umempokea?” Akijibu “Ndiyo,” basi mwulize, “Basi wewe ni nini?” Huenda itakuwa lazima kulirudia mara kadhaa, lakini mwishowe mtafutaji ataliona na kusema “Mimi ni mtoto wa Mungu.” Yohana 3:36 laweza kutumiwa kwa njia kama hiyo. Mwulize mtafutaji “mistari hii inasema ni nani aliye na uzima wa milele?” “Amwaminiye Mwana.” “Je, wewe unamwamini Mwana?” “Basi una nini?” Baada ya muda mfupi ataliona na kusema “Uzima wa milele.” Kisha mwache aseme tena na tena “Nina uzima wa milele,” na umwache apige magoti amshukuru Mungu kwa kumpa uzima wa milele. Usiku mmoja, mwishoni mwa ibada, nilimkuta kijana mmoja amepiga magoti akiwa katika dhiki kuu. Nilimwonyesha kutoka katika Biblia jinsi Yesu Kristo alivyozichukua dhambi zake, nikamwuliza kama angempokea Kristo kuwa Mwokozi wake; akasema angempokea; lakini ilionekana hakupata nuru yo yote, akatoka mkutanoni akiwa katika dhiki nzito. Usiku uliofuata alikuwapo tena, akikiri kwamba amempokea Kristo, lakini bila uhakika wo wote kwamba dhambi zake zimesamehewa. Nilijaribu kumwonyesha kutoka katika neno la Mungu yale ambayo Mungu alisema juu ya wale waliompokea Mwokozi, lakini nuru haikuja. Mwishowe aliinuka ili atoke mkutanoni. Nilikuwa nimetoka tu kumwonyesha kutoka Yohana 3:36 kwamba Mungu alisema kwamba “Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele.” Alipogeuka kuniacha, akasema, “Je, utaniombea?” Nikasema “Ndiyo.” Akatembea hatua chache kufuata njia iliyo katikati ya viti, nami nikamwita, nikasema, “Je, unaamini kwamba nitakuombea?” Akageuka akiwa na sura ya mshangao, akajibu, “Ndiyo, bila shaka.” “Kwa nini unadhani nitakuombea?” nikamwuliza basi. “Kwa sababu umesema hivyo,” akajibu. Nikasema “Je, neno la Mungu si la kuaminika kama langu?” Akaliona mara moja, kwamba ingawa alikuwa tayari kuliamini neno langu, hakuwa tayari kuliamini neno la Mungu; akapata uhakika papo hapo, akajua kwamba ana uzima wa milele. Yohana 5:24 na 1 Yohana 5:12 yanaweza kutumiwa kwa njia kama hiyo.
Matendo 13:39 lafaa sana katika kuwashughulikia watu wa kundi hili. Mwulize mtafutaji: “Mstari huu unasema wote waaminio ni nini?” “Wamehesabiwa haki.” Kisha mwulize, “Je, wewe unaamini?” “Basi wewe ni nini?” Huenda itachukua kulirudia mara mbili au tatu kabla hajaliona, na anapojibu “Nimehesabiwa haki,” mwambie amshukuru Mungu kwa kumhesabia haki na amkiri Kristo, nawe uhakikishe kwamba anafanya hivyo. Watafutaji wengi wa kundi hili hujikwaa juu ya ukweli kwamba hawana ushuhuda wa Roho Mtakatifu. Waonyeshe kutoka 1 Yohana 5:10 kwamba ushuhuda wa neno juu ya kukubaliwa kwao unatosha, na kwamba, wasipouamini ushuhuda huu wa Mungu katika neno lake, wanamfanya kuwa mwongo. Waonyeshe zaidi kutoka Waefeso 1:13, kwamba ni baada ya kuuamini ushuhuda wa neno ndipo tunapopata “kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu.” Mpangilio wa asili katika uhakika ni huu: Kwanza, uhakika wa kuhesabiwa kwetu haki, uliosimama juu ya “Neno la Mungu.” Pili, kumkiri Kristo hadharani, “kwa kinywa,” Warumi 10:10. Tatu, ushuhuda wa Roho Mtakatifu. Shida ya wengi ni kwamba wanataka kuupindua mpangilio huu, wawe na ushuhuda wa Roho Mtakatifu kabla hawajamkiri Kristo kwa kinywa. Kutoka Mathayo 10:32, 33, tunajifunza kwamba tunapomkiri Kristo mbele ya watu, ndipo yeye anatukiri mbele za Baba. Hatuwezi kwa busara kutazamia ushuhuda wa Roho kutoka kwa Baba mpaka tumekiriwa mbele za Baba. Kwa hiyo kumkiri Kristo, kwa mantiki, hutangulia ushuhuda wa Roho.
Ni muhimu sana, unapotumia mafungu haya, kuweka wazi imani iokoayo ni nini; kwa sababu wengi wanaweza kusema kwamba wanaamini wakati hawaamini, kwa maana ya mafungu haya, na hivyo kupata uhakika wa uongo na kuwa na matumaini ya uongo, wasipate kamwe kuwekwa huru. Kuna uzembe mwingi katika kuwashughulikia wale wasio na uhakika. Watendakazi wana hamu kubwa mno ya kuwaona watafutaji wakisimama waziwazi, hata wanawasukuma kufikia uhakika wakati hawana haki ya kuwa na uhakika wa wokovu, kwa kuwa hawajampokea Kristo kweli.
Yohana 1:12, na 2 Timotheo 1:12, yanaweka wazi kabisa kuamini ni nini—kumpokea Yesu au kujikabidhi kwa Yesu. Warumi 10:10, litatimiza kusudi kama hilo kwa kuonyesha kwamba “ni kwa moyo mtu huamini hata kupata haki.”
2. Wale wasio na uhakika kwa sababu ya dhambi. Shida ya wale wasio na uhakika, mara nyingi, ni kwamba kuna dhambi fulani au desturi yenye mashaka ambayo wanapaswa kuiungama na kuiacha. Yohana 8:12; Isaya 55:7; Mithali 28:13; Zaburi 32:1‒5, ni mafungu yanayofaa katika kuwashughulikia watu wa kundi hili, kwa kuwa yanaonyesha kwamba ni pale dhambi inapoungamwa na kuachwa, nasi tukamfuata Kristo, ndipo tunapopokea msamaha, nuru na uhakika. Mara nyingi ni vema, mtu anapokosa uhakika, kumwuliza swali waziwazi: “Je, unajua dhambi yo yote unayoishikilia, au jambo lo lote maishani mwako ambalo dhamiri yako inakusumbua juu yake?”
II. Waliorudi Nyuma. Kuna makundi mawili ya waliorudi nyuma, nayo yapasa kushughulikiwa kwa njia tofauti.
1. Waliorudi nyuma wasiojali; wale wasio na hamu kubwa ya kumrudia Mwokozi. Kwa watu wa namna hiyo tumia Yeremia 2:5, ulikaze swali hili moyoni mwao, “Umeona uovu gani kwa Bwana?” Waonyeshe ukosefu mbaya wa shukrani na upumbavu wa kumwacha Mwokozi na Rafiki wa namna hiyo. Yamkini wametangatanga mbali kwa sababu ya kutendewa vibaya na watu wanaojiita Wakristo, lakini washikilie palepale kwenye jambo la jinsi Bwana alivyowatendea na jinsi wao wanavyomtendea sasa. Tumia pia Yeremia 2:13, uwaonyeshe ni nini walichokiacha na kwa ajili ya nini. Waache wausome mstari huo, kisha uwaulize, “je, mstari huo si kweli? Ulipomwacha Bwana, je, hukuiacha ‘chemchemi ya maji ya uzima’ ukageukia ‘mabirika yaliyovunjika, yasiyoweza kuweka maji?’” Ufafanue mstari huo kwa kuonyesha jinsi ambavyo ingekuwa upumbavu kugeuka kutoka kwenye chemchemi ya maji safi ya uzima na kuyaendea mabirika yaliyovunjika au madimbwi ya matope. Mungu ameuheshimu sana mstari huu katika kuwarudisha kwake waliorudi nyuma. Tumia Yeremia 2:19. Wakiisha kuusoma, waulize kama hawajaona kwamba ni “neno baya na chungu” kumwacha Bwana, Mungu wao. Mithali 14:14; 1 Wafalme 11:9, na Luka 15:13‒17, mara nyingi yanaweza kutumiwa kwa matokeo mazuri kwa aliyerudi nyuma asiyetubu, kumwonyesha matokeo ya kutangatanga kwake. Nina rafiki mmoja ambaye siku zote hutumia Amosi 4:11-12, na mara nyingi kwa matokeo mazuri.
2. Waliorudi nyuma ambao wamechoshwa na kutangatanga kwao na dhambi yao, nao wanatamani kumrudia Bwana. Hawa labda ni kundi rahisi kushughulikiwa kama lo lote tunalokutana nalo. Yeremia 3:12, 13, na 22, yatawaonyesha jinsi Bwana alivyo tayari kuwapokea tena, na kwamba anachowaomba tu ni kwamba waikiri dhambi yao na kumrudia. Hosea 14:1‒4, limejaa mwaliko mororo kwa waliorudi nyuma wanaotubu, tena linaonyesha njia ya kumrudia Mungu. Isaya 43:22, 24, 25, na Isaya 44:20‒22; Yeremia 29:11‒13; Kumbukumbu la Torati 4:28‒31; 2 Nyakati 7:14; 1 Yohana 1:9; 2:1‒2, yanadhihirisha upendo wa Mungu usiokoma kwa aliyerudi nyuma, na utayari wake wa kumpokea tena. Marko 16:7; 2 Nyakati 15:4; 33:1‒9, 12, 13, yanatoa mifano ya watu waliorudi nyuma sana waliomrudia Bwana, na jinsi alivyowapokea kwa upendo, 1 Yohana 1:9; Yeremia 3:12‒13; 2 Nyakati 15:12, 15; 7:14, yanaonyesha hasa ni hatua gani aliyerudi nyuma anapaswa kuchukua ili amrudie Bwana na arudishwe katika kibali chake, yaani: ajinyenyekeze, aziungame dhambi zake, na aiache dhambi yake. Luka 15:11‒24, labda ndilo fungu lifaalo kuliko yote katika kumshughulikia aliyerudi nyuma anayetaka kurudi, kwa kuwa lina mambo yote mawili: hatua ambazo aliyerudi nyuma anapaswa kuchukua, na aina ya mapokezi atakayoyapata.
Aliyerudi nyuma akiisha kurudi, sikuzote apewe maelekezo juu ya jinsi ya kuishi ili asirudi nyuma tena. Maelekezo ya kutolewa yatapatikana katika Sura 12, sehemu 15.