Sura 20 · dakika 10 za kusoma
Utakatifu na Ufufuo
‘Mwana wa Mungu, aliyezaliwa katika uzao wa Daudi kwa jinsi ya mwili, aliyedhihirishwa kuwa Mwana wa Mungu kwa uweza, kwa jinsi ya Roho wa utakatifu, kwa ufufuo wa wafu.’—Warumi 1:4.
Maneno haya yanazungumza juu ya kuzaliwa mara mbili kwa Kristo. Kwa jinsi ya mwili, alizaliwa katika uzao wa Daudi. Kwa jinsi ya Roho, alikuwa mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu. Kama vile alivyokuwa Mwana wa Daudi kwa sababu ya kuzaliwa kwake kwa njia ya mwili, vivyo hivyo alidhihirishwa kuwa Mwana wa Mungu kwa uweza, kwa sababu ya kuzaliwa kwake katika ufufuo kwa njia ya Roho wa utakatifu. Kama vile uzima aliopokea kwa kuzaliwa kwake kwa kwanza ulivyokuwa uzima ndani ya mwili na kwa jinsi ya mwili pamoja na udhaifu wake, vivyo hivyo uzima mpya aliopokea katika ufufuo ulikuwa uzima katika nguvu za Roho wa utakatifu.
Msemo huu, Roho wa utakatifu, ni wa pekee. Si neno la kawaida linalotumika kwa Utakatifu wa Mungu kama lilivyotumika katika Waebrania 12:10, likieleza utakatifu kwa ujumla kama sifa ya kitu, bali ni neno lingine (linalotumika pia katika 2 Wakorintho 7:1 na 1 Wathesalonike 3:13) linaloeleza tabia ya utakatifu katika utendaji wake—utakatifu wa vitendo au uadilifu mtakatifu. Paulo alilitumia neno hili, kwa sababu alitaka kusisitiza wazo kwamba ufufuo wa Kristo ulikuwa wazi wazi tunda la ule uzima wa utakatifu na wa kujitakasa uliofikia kilele chake katika kifo chake. Ilikuwa ni roho ya ule uzima wa utakatifu aliouishi, ambao kwa nguvu zake alifufuliwa tena. Anatufundisha kwamba ule uzima na kifo cha kujitakasa, ambacho ndani yake peke yake utakaso wetu unasimama, kilikuwa shina na msingi wa ufufuo wake, na wa tangazo lake kwamba alikuwa Mwana wa Mungu kwa uweza, mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu. Ufufuo ulikuwa tunda alilolizaa ule Uzima wa Utakatifu.
Na hivyo ule Uzima wa Utakatifu unakuwa mali ya wote walio washiriki wa ufufuo. Uzima wa Ufufuo na Roho wa Utakatifu haviwezi kutenganishwa. Kristo alijitakasa mwenyewe katika kifo, ili sisi wenyewe tupate kutakaswa katika kweli: alipofufuliwa kutoka kwa wafu kwa nguvu ya Roho wa utakatifu, ile Roho wa utakatifu ilithibitishwa kuwa ndiyo nguvu ya Uzima wa Ufufuo, na Uzima wa Ufufuo kuwa ni Uzima wa Utakatifu.
Kama mwamini una sehemu katika huu Uzima wa Ufufuo. Umekwisha ‘zaliwa mara ya pili kwa ufufuo wa Yesu Kristo katika wafu.’ Wewe ‘umefufuliwa pamoja na Kristo.’ Umeamriwa ‘kujihesabu kuwa u hai kwa Mungu katika Kristo Yesu.’ Lakini uzima huo waweza kutenda kazi kwa nguvu tu kadiri unavyotafuta kuujua, kuujitolea kwake, kuuacha uwe na umiliki na utawala kamili. Na kama utatenda hivi, mojawapo ya mambo muhimu zaidi kwako kutambua ni kwamba, kama vile ilivyokuwa kwa nguvu ya Roho wa utakatifu ndipo Kristo alipofufuliwa, vivyo hivyo Roho wa utakatifu ule ule sharti iwe ndani yako alama na nguvu ya uzima wako. Jitahidi kuujua na kuumiliki Roho wa utakatifu kama ulivyoonekana katika uzima wa Bwana wako.
Na ulikuwa katika nini? Siri yake, twaambiwa, ilikuwa: ‘Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako, Ee Mungu.’ ‘Katika mapenzi hayo,’ kama yalivyotimizwa na Kristo, ‘tumetakaswa kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja.’ Huku ndiko Kristo kujitakasa mwenyewe, katika uzima na katika kifo; hiki ndicho Roho wa utakatifu alichokifanya ndani yake; hiki ndicho Roho yule yule, Roho wa uzima ndani ya Kristo Yesu, atakachokifanya ndani yetu: uzima ulio katika mapenzi ya Mungu ni uzima wa utakatifu. Tafuta kwa bidii kulishika hili waziwazi. Kristo alikuja kufunua utakatifu wa kweli utakavyokuwa katika hali za uzima wa mwanadamu na udhaifu. Alikuja akulitendee, ili apate kukupa kwa njia ya Roho wake. Usipolifahamu kwa akili na kulikubali kwa moyo wote, Roho hawezi kulitenda ndani yako. Tafuta kwa moyo wako wote kulishika: mapenzi ya Mungu yakikubaliwa bila kusita, ndiyo nguvu ya utakatifu.
Ni katika hili ndipo jitihada yoyote ya kuwa mtakatifu kama Kristo alivyo mtakatifu, pamoja naye na katika Utakatifu wake, sharti ipate mwanzo wake. Wengi hutafuta kuchukua sehemu chache za uzima au sura ya Kristo kwa kuiga, na hata hivyo hushindwa sana katika nyingine. Hawajaona kwamba kujikana, ambako Yesu anaita, kwa kweli kunamaanisha kuikana nafsi, katika maana kamili ya neno hilo. Katika jambo hata moja mapenzi ya nafsi hayapaswi kutendwa: Yesu, kama alivyoyafanya mapenzi ya Baba peke yake, sharti atawale, wala si nafsi. Ku ‘simama mkamilifu na kutimilika katika mapenzi yote ya Mungu’ sharti kuwe kusudi, ombi, na tumaini la mwanafunzi. Hapana haja ya kuogopa kwamba haiwezekani kuyajua mapenzi ya Baba katika kila jambo. ‘Mtu ye yote akipenda kuyatenda, atajua.’ Baba hatamwacha mtoto anayependa katika kutokuyajua mapenzi yake. Kadiri kujisalimisha kwa Roho wa utakatifu, kwa Yesu na kwa mamlaka ya uzima wake mtakatifu, kunavyozidi kuwa rahisi, dhambi na hiari ya nafsi zitagunduliwa, ufahamu wa kiroho utafunguliwa, na sheria iliyoandikwa katika sehemu za ndani itakuwa dhahiri na yenye kueleweka. Hapana haja ya kuogopa kwamba haiwezekani kuyatenda mapenzi ya Baba yanapojulikana. Mara ile huzuni ya kushindwa na dhambi imwongozapo mwamini katika hali ya Warumi 7, na ile ‘furaha katika sheria ya Mungu kwa utu wa ndani’ ikiisha thibitisha bidii yake katika kilio, ‘Ole wangu, maskini mimi,’ wokovu utakuja kwa njia ya Yesu Kristo. Roho hatendi kazi ya kutaka tu bali na kutenda; pale ambapo mwamini angeweza tu kulalamika, ‘Kutenda lililo jema sikupati,’ yeye humpa nguvu na wimbo, ‘Kwa maana sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.’
Katika imani hii, kwamba inawezekana kuyajua na kuyatenda mapenzi ya Mungu katika mambo yote, pokea kutoka kwake, ambaye ndani yake peke yake u mtakatifu, kama kanuni ya uzima wako; ‘Nimekuja niyafanye mapenzi yako, Ee Mungu.’ Ndiyo kanuni ya uzima wa ufufuo: pasipo hiyo Yesu asingefufuliwa kamwe. Ndiyo kanuni ya uzima mpya ndani yako. Ikubali; itafakari; itambue; itende. Waamini wengi wamegundua kwamba maneno mepesi ya kujiweka wakfu, yanayoonyesha kusudi la kuyafanya mapenzi ya Mungu katika kila jambo, yamekuwa mlango wa kuingia katika furaha na nguvu ya uzima wa ufufuo ambao hapo awali haukujulikana. Mapenzi ya Mungu ni ufafanuzi kamili wa ukamilifu wake wa kimaadili, Utakatifu wake wa Kimungu. Kuchukua nafasi ya mtu katikati ya mapenzi hayo, kuyaishi, kuchukuliwa na kutegemezwa nayo, ndiyo iliyokuwa nguvu ya ule uzima wa Yesu ambao usingeweza kushikwa na mauti, ambao haukuweza ila kupasuka katika utukufu wa ufufuo. Kama ulivyokuwa kwa Yesu, ndivyo utakavyokuwa kwetu.
Utakatifu ni Uzima: huu ndio usemi rahisi zaidi wa kweli ile ambayo maandiko yetu yanaifundisha. Hauwezi kuwepo utakatifu hata kutakapopandwa uzima mpya. Uzima mpya hauwezi kukua na kupasuka katika nguvu ya ufufuo, hauwezi kuzaa matunda, ila kadiri unavyokua katika utakatifu. Maadamu mwamini anaishi uzima uliochanganyika, sehemu katika mwili na sehemu katika roho, pamoja na kiasi cha nafsi na kiasi cha Kristo, anautafuta utakatifu bure. Ni Uzima Mpya ndio uzima mtakatifu: kuufahamu kikamilifu kwa imani, kujisalimisha kwake kikamilifu katika mwenendo, ndiko kutakakokuwa njia kuu ya utakatifu. Yesu aliishi na kufa na kufufuka tena ili atuandalie asili mpya, itakayopokelewa siku baada ya siku katika utii wa imani: sisi ‘tumevaa utu mpya, ulioumbwa kwa mfano wa Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.’ Uzima wa ndani, uliofichwa pamoja na Kristo katika Mungu, uliofichwa pia ndani sana katika vilindi vya utu wetu wa ndani kabisa, na ukubaliwe, na usubiriwe, na ujitolewe kwake, nao utajitenda wenyewe katika uzuri wote wa utakatifu.
Kuna zaidi. Uzima huu si kama uzima wa asili, kanuni kipofu, isiyo na fahamu, itendayo lengo lake bila kukusudia katika utii usiopinga sheria ya asili yake. Kuna Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu—Roho wa utakatifu—Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu kama Nafsi ya Kimungu, akiingia katika ushirika nasi, na kutuongoza katika ushirika wa Kristo aliye Hai. Ni huu ndio uujazao uzima wetu tumaini na furaha. Mwokozi aliyefufuka aliwavuvia wanafunzi wake Roho Mtakatifu: Roho humleta Yule aliyefufuka uwanjani, mioyoni mwetu, kama rafiki wa binafsi, kama Kiongozi na Mtia-nguvu aliye Hai. Roho wa utakatifu ni Roho, na Uwepo, na Nguvu ya Kristo aliye Hai. Yesu alisema juu ya Roho, ‘Ninyi mnamjua.’ Je, si haja yetu kuu kumjua huyu Roho Mtakatifu, Roho wa Kristo, wa Utakatifu wake na wa wetu? Twawezaje ‘kuenenda kwa kufuata Roho’ na kufuata mwongozo wake, kama hatumjui yeye na sauti yake na njia yake?
Na tujifunze somo moja zaidi kutoka katika maandiko yetu. Ni kutoka katika kaburi la mwili na mapenzi ya nafsi ndipo Roho wa utakatifu apasukapo katika nguvu ya ufufuo. Sharti tukubali kufa kwa mwili, kufa kwa nafsi pamoja na kutaka kwake na kutenda kwake, kama mahali pa kuzaliwa kwa uzoefu wetu wa nguvu ya Roho wa utakatifu. Kwa kila pambano na dhambi, katika kila zoezi la imani au maombi, sharti tuingie katika kifo cha Yesu, kifo cha nafsi, na kama wale wasemao, ‘hatutoshi sisi wenyewe kufikiri neno lo lote kana kwamba latoka kwetu wenyewe,’ kwa imani ya utulivu tutazamie Roho wa Kristo kuifanya kazi yake. Roho atatenda kazi, akikutia nguvu sana katika utu wa ndani, na kujenga ndani yako hekalu takatifu kwa ajili ya Bwana. Na wakati utakuja, kama haujaja kwako bado, nao waweza kuwa karibu zaidi kuliko uthubutuvyo kutumaini, ambapo kukaa kwa Kristo moyoni mwako kwa kujua kwa njia ya imani, kufunuliwa kwake kikamilifu na kutawazwa kwake kuwa mtawala na mlinzi wa moyo na uzima, kutakuwa kumekuwa uzoefu wa binafsi. Kwa jinsi ya Roho wa utakatifu, kwa ufufuo kutoka kwa wafu, Mwana wa Mungu atadhihirishwa kwa uweza katika ufalme ulio ndani yako.
Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu.
Ee Bwana Mungu Mtakatifu Zaidi! twakusifu kwa kuwa ulimfufua Mwana wako kutoka kwa wafu na kumpa utukufu, ili imani yetu na tumaini letu viwe kwako. Uliufanya ufufuo wake kuwa nguvu ya uzima wa milele ndani yetu, na sasa, kama vile alivyofufuliwa, vivyo hivyo tuenende katika upya wa uzima. Kama vile Roho wa utakatifu alivyokaa na kutenda ndani yake, ndivyo akaavyo na kutenda ndani yetu, na kuwa ndani yetu Roho wa uzima.
Ee Mungu! twakusihi uikamilishe kazi yako ndani ya watakatifu wako. Wape hisia ya kina zaidi ya wito mtakatifu ambao umewaita katika Kristo, Yule aliyefufuka. Wape wote kuipokea Roho ya uzima wake hapa duniani, kufurahia mapenzi ya Mungu, kama roho ya uzima wao. Wale ambao bado hawajaipokea hii kikamilifu na waletwe kuifanya, na kwa imani ya nguvu ya uzima mpya waseme, Nayakubali mapenzi ya Mungu kuwa sheria yangu pekee. Roho wa utakatifu na awe roho ya maisha yao!
Baba! twakusihi, Kristo na afunuliwe hivyo mioyoni mwetu, katika uzoefu unaozidi kuongezeka wa nguvu ya ufufuo wake, kuwa Mwana wa Mungu, Bwana na Mtawala ndani yetu. Uzima wake wa ndani na uuvuvie uzima wote wa nje, ili nyumbani na katika jamii, katika fikira na usemi na tendo, katika dini na katika biashara, uzima wake upate kuangaza kutoka kwetu katika uzuri wa utakatifu. Amina.
1. Maandiko yanauangalia ufufuo katika pande mbili tofauti. Kwa mtazamo mmoja, ni hati ya uzima mpya, chanzo cha kuhesabiwa haki kwetu. (Warumi 4:25, 1 Wakorintho 15:17.) Kwa mwingine ni kuzaliwa upya kwetu, nguvu ya uzima mpya itendayo kazi ndani yetu, chanzo cha utakaso wetu. (Warumi 6:4; 1 Petro 1:3.) Msamaha na utakatifu haviwezi kutenganishwa; vina chanzo kimoja, kuungana na Kristo aliye Hai aliyefufuka.
2. Baraka kwa wanafunzi ya kumpata Kristo aliyefufuka ilikuwa hii: Yeye, waliyemdhania amekufa, akaja na kujidhihirisha mwenyewe kwao. Kristo yu hai ili ajidhihirishe mwenyewe kwako na kwangu; mngoje yeye, mtumaini kwa jambo hili. Atajidhihirisha mwenyewe kwako kuwa utakaso wako. Hakikisha kwamba unaye katika umiliki ulio hai, nawe unao Utakatifu wake.
3. Uzima wa Kristo ndio utakatifu wa Kristo. Sababu ya sisi kushindwa mara nyingi katika kufuatia utakatifu ni kwamba uzima wa kale, ule mwili, kwa nguvu zake wenyewe hutafuta utakatifu kama vazi zuri la kuvaa na kuingia nalo mbinguni. Ni kifo cha kila siku kwa nafsi ambapo kutoka humo uzima wa Kristo huinuka.
4. Kufa hivi, kuishi hivi katika Kristo, kuwa mtakatifu—twawezaje kukifikia? Yote huja ‘kwa jinsi ya Roho wa utakatifu.’ Uwe na Roho Mtakatifu ndani yako. Sema kila siku, ‘Namwamini Roho Mtakatifu.’
5. Mtakatifu katika Kristo. Kristo akaapo ndani yetu, na nia yake, kama ilivyopata kudhihirishwa katika maneno na kazi yake hapa duniani, iingiapo na kujaza hiari yetu na fahamu yetu binafsi, ndipo kuungana kwetu naye kunapokuwa vile alivyokusudia kuwe. Ni Roho ya mwenendo wake mtakatifu, Roho ya uadilifu wake mtakatifu, sharti iwe ndani yetu.