Mtakatifu katika Kristo ·Utakatifu na Imani

Sura 19 · dakika 11 za kusoma

Utakatifu na Imani

‘Ili wapate msamaha wa dhambi, na urithi kati ya wale waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu.’—Matendo 26:18.

Kadiri tunavyozidi kuichunguza Maandiko katika nuru ya Roho Mtakatifu, au kuishi maisha ya Kikristo kwa nguvu zake, ndivyo inavyozidi kupata kina hakika yetu juu ya nafasi ya pekee na kuu ambayo imani inayo katika mpango wa Mungu wa wokovu. Nasi tunajifunza pia kuona kwamba ni haki na sawa iwe hivyo: asili yenyewe ya mambo yadai hivyo. Kwa sababu Mungu ni Kiumbe cha Kiroho na Asiyeonekana, kila ufunuo wa nafsi yake, ikiwa katika kazi zake, neno lake, au Mwanawe, wadai imani. Imani ni hisi ya kiroho ya nafsi, ikiwa kwake kile ambacho hisi ni kwa mwili; kwa hiyo peke yake twaingia katika mawasiliano na kugusana na Mungu.

Imani ni unyenyekevu ule wa nafsi unaongoja kwa utulivu kusikia, kuelewa, kukubali yale Mungu asemayo; kupokea, kushika, kumiliki yale Mungu atoayo au atendayo. Kwa imani twamruhusu, twamkaribisha Mungu mwenyewe, yule Nafsi Aliye Hai, aingie ili afanye makao yake kwetu, awe uzima wetu hasa. Hata tukidhani kwamba twaijua vema kiasi gani, sikuzote yatupasa kuijifunza kweli hii upya, ili tuitumie kwa kina zaidi na kwa ukamilifu zaidi, kwamba katika maisha ya Kikristo imani ndilo jambo la kwanza, jambo lile pekee limpendezalo Mungu, na kutuletea baraka. Na kwa sababu Utakatifu ni utukufu wa Mungu ulio juu kuliko yote, na baraka iliyo kuu kuliko zote aliyo nayo kwa ajili yetu, ni hasa katika maisha ya utakatifu ndipo tunapohitaji kuishi kwa imani peke yake.

Bwana wetu hapa anena juu ya ‘wale waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu.’ Yeye mwenyewe ni Utakaso wetu kama vile alivyo Kuhesabiwa Haki kwetu: kwa hili kama kwa lile ni imani ambayo Mungu aidai, na yote mawili hutolewa sawasawa mara moja. Kitenzi-nomino kilichotumika hapa si cha wakati uliopo, kinachoashiria mwendo au kazi inayoendelea kutendwa, bali ni cha wakati ulioisha, kinachoonyesha tendo lililotendwa mara moja kwa ajili ya siku zote. Tumwaminipo Kristo, twampokea Kristo mzima, kuhesabiwa haki kwetu na utakaso wetu: mara hiyohiyo twakubaliwa na Mungu kuwa wenye haki ndani yake, na kuwa watakatifu ndani yake. Mungu atuhesabu na atuita, kile tulicho hasa, watu waliotakaswa katika Kristo. Ni tunapoongozwa kuona yale Mungu ayaonayo, imani yetu inavyoshika kwamba maisha matakatifu ya Kristo ni yetu katika kumiliki halisi, ili yakubaliwe na yatwaliwe kwa matumizi ya kila siku, ndipo tutakapoweza kweli kuishi maisha yale Mungu anayotuitia, maisha ya watakatifu katika Kristo Yesu. Ndipo tutakapokuwa katika hali ile ipasayo ambapo kile kiitwacho utakaso wetu unaoendelea waweza kutimizwa. Utakuwa ni kukubali na kutumia katika maisha ya kila siku nguvu za maisha matakatifu yaliyotayarishwa ndani ya Yesu, ambayo katika muungano naye yamekuwa milki yetu ya sasa na ya kudumu, na yatendayo kazi ndani yetu kwa kadiri ya imani yetu.

Kwa mtazamo huu ni dhahiri kwamba imani ina kazi ya namna mbili. Imani ni bayana ya mambo yasiyoonekana, ingawa yaliyoko sasa hasa, ni uthibitisho wa mambo yatarajiwayo, lakini bado hayajawapo. Yashughulika na yaliyopo yasiyoonekana, pia na yajayo yasiyoonekana. Kama bayana ya mambo yasiyoonekana, yafurahia katika Kristo utakaso wetu ulio kamili, kama milki iliyopo sasa. Kwa imani mimi natazama tu kile Kristo alicho, kama kilivyofunuliwa katika Neno na Roho Mtakatifu. Nikidai yote alivyo kuwa yangu, najua kwamba Utakatifu wake, asili yake takatifu na uzima wake, ni vyangu; mimi ni mtakatifu: kwa imani ndani yake nimetakaswa. Hii ndiyo sura ya kwanza ya utakaso: yatazama kile kilicho jambo kamili na lililotimizwa, hali halisi kabisa. Kama uthibitisho wa mambo yatarajiwayo, imani hii yajinyosha katika uhakika wa tumaini kuelekea yajayo, kuelekea mambo nisiyoyaona wala kuyaonja bado, nayo yadai, siku kwa siku, kutoka kwa Kristo utakaso wetu, kile inachohitaji kwa ajili ya utakatifu wa vitendo, ‘kuwa watakatifu katika kila namna ya kuishi.’ Hii ndiyo sura ya pili ya utakaso: mimi namtegemea Yesu anipatie, katika uzoefu wa nafsi, hatua kwa hatua na bila kukoma, kwa mahitaji ya kila dakika, kile kilichowekwa akiba katika ukamilifu wake. ‘Kwa yeye ninyi mmo katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu utakaso na Mungu.’ Chini ya sura yake ya kwanza imani husema, najua mimi ni ndani yake, na Utakatifu wake wote ni wangu; katika sura yake ya pili yanena, namtumaini yeye kwa ajili ya neema na nguvu ninazohitaji kila dakika ili kuishi maisha matakatifu.

Na bado, si lazima kusemwa, hawa wawili ni mmoja. Ni Yesu mmoja aliye utakaso wetu, tuutazameapo katika nuru ya kile alichofanywa kwa ajili yetu mara moja kwa ajili ya siku zote, au kile ambacho, kama tunda la hilo, anakuwa katika uzoefu wetu siku kwa siku. Na hivyo ni imani moja ambayo, kadiri inavyozidi kumchunguza na kumwabudu na kumfurahia Yesu kama aliyefanywa na Mungu kuwa utakaso wetu, kama yeye ambaye ndani yake tumetakaswa, huzidi kuwa jasiri zaidi kutazamia kutimizwa kwa kila ahadi kwa ajili ya maisha ya kila siku, na kuwa na nguvu zaidi kudai ushindi juu ya kila dhambi. Imani katika Yesu ndiyo siri ya maisha matakatifu: mwenendo wote mtakatifu, matendo yote yaliyo matakatifu kweli, ni tunda la imani katika Yesu kama utakatifu wetu.

Twajua jinsi imani itendavyo, na ni zipi vizuizi vyake vikuu, katika suala la kuhesabiwa haki. Ni vema tujikumbushe kwamba yako hatari zilezile katika kutumia imani itakasayo kama katika imani ihesabuyo haki. Imani kwa Mungu husimama kinyume na kutumainia nafsi: hasa kinyume na kutaka kwake na kutenda kwake. Imani huzuiwa na kila jitihada ya kutenda jambo sisi wenyewe. Imani humtazama Mungu atendaye kazi, na kujitoa kwa nguvu zake, kama zilivyofunuliwa katika Kristo kwa njia ya Roho; humruhusu Mungu atende kazi ya kutaka na ya kutenda pia. Imani lazima itende kazi; pasipo matendo imekufa, kwa matendo peke yake yaweza kukamilishwa; katika Kristo Yesu, kama Paulo asemavyo, hakuna kifaacho ila ‘imani itendayo kazi kwa upendo.’ Lakini matendo haya, ambayo imani katika kazi ya Mungu huyachochea na kuyatenda, ni tofauti sana na matendo ambayo mwamini mara nyingi hutumia bidii zake bora, ili tu kujikuta kwamba anashindwa. Maisha ya kweli ya utakatifu, maisha ya wale waliotakaswa katika Kristo, yana shina lake na nguvu zake katika hisi idumuyo ya kutokuwa na uwezo kabisa, katika pumziko lile la ndani limtumainiaye atendaye nguvu na uzima wa Kimungu, katika kujisalimisha kwa nafsi kabisa kwa Mwokozi mpenzi, katika imani ile ikubaliyo kuwa si kitu, ili yeye awe vyote. Yaweza kuonekana haiwezekani kutambua au kueleza tofauti kati ya utendaji utokao kwa nafsi na utendaji utokao kwa Kristo kwa njia ya imani: tukijua tu kwamba iko tofauti kama hiyo, tukijifunza kutojiamini wenyewe, na kumtegemea Kristo atendaye kazi, Roho Mtakatifu atatuongoza katika siri hii ya Bwana pia. Matendo ya imani ni matendo ya Kristo.

Na kama kwa jitihada, vivyo hivyo imani huzuiwa pia na tamaa ya kuona na kuhisi. ‘Ukiamini, utaona;’ Roho Mtakatifu ataitia imani yetu muhuri kwa uzoefu wa Kimungu; tutaona utukufu wa Mungu. Lakini hii ni kazi yake: yetu ni, wakati vyote vinapoonekana gizani na baridi, mbele ya yote ambayo asili au uzoefu hushuhudia, bado kila dakika kumwamini Yesu kama utakaso wetu utoshaye kwa yote, ambaye ndani yake twafanywa wakamilifu mbele za Mungu. Malalamiko juu ya kukosa hisia, juu ya udhaifu au ukavu, mara chache huleta faida: ni nafsi ile ikataayo kujishughulisha na nafsi yenyewe, ikiwa na udhaifu wake au nguvu za adui, bali yatazama tu kile Yesu alicho, na alichoahidi kutenda, ambayo kwake maendeleo katika utakatifu yatakuwa maandamano ya furaha kutoka ushindi hata ushindi. ‘Bwana mwenyewe atawapigania;’ wazo hili, lililorudiwarudiwa mara nyingi kuhusiana na Israeli kuimiliki nchi ya ahadi, ni chakula cha imani: katika udhaifu wa kujitambua, mbele ya adui wenye nguvu, huimba wimbo wa mshindi. Mungu aonekanapo kuwa hafanyi kile tuliyomtumainia, ndipo hasa wakati wa imani kujitukuza ndani yake.

Labda hakuna kitu kidhihirishacho tabia ya kweli ya imani kuliko furaha na sifa. Umpe mtoto ahadi ya zawadi kesho: mara hiyo asema, Asante, na kufurahi. Shukrani za furaha ni uthibitisho wa jinsi ahadi yako ilivyoingia moyoni kweli. Waambiwa na rafiki juu ya urithi mkubwa aliokuachia katika wosia wake: yaweza yasitimie kwa miaka mingi, lakini hata sasa yakufurahisha. Tumekwisha kuona jinsi furaha ilivyo sehemu ya utakatifu: ni hasa sehemu ya utakatifu kwa imani. Kila mara ninapoona kweli jinsi maandalizi ya Mungu yalivyo mazuri na yalivyo kamili, ambayo kwayo utakatifu wangu u ndani ya Yesu, na ambayo kwayo napaswa kumruhusu atende kazi ndani yangu, moyo wangu wapaswa kuinuka katika sifa na shukrani. Badala ya kuruhusu wazo kwamba, baada ya yote, ni maisha ya kufikiwa kwa shida namna hiyo na ya kujikana nafsi bila kukoma namna hiyo, maisha haya ya utakatifu kwa imani, twapaswa kumsifu mno kwa kuwa ameyafanya yawezekane na yawe ya hakika kwetu: twaweza kuwa watakatifu, kwa sababu Yesu, yule Mwenye Nguvu na Mwenye Upendo, ni utakatifu wetu. Sifa itaidhihirisha imani yetu; sifa itaithibitisha; sifa itaiimarisha. ‘Ndipo waliyaamini maneno yake, wakaimba sifa zake.’ Sifa itatuweka kwenye imani: tutaona kwamba tuna jambo moja tu la kutenda, kuendelea katika imani itumainiyo sikuzote na kusifu sikuzote. Ni katika kuambatana na Yesu kwa uzima na kwa upendo, kunakofurahia ndani yake, na kumsifu daima kwa yale alivyo kwetu, ndipo imani hujithibitisha yenyewe, na kupokea nguvu za utakatifu.

‘Waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu.’ Naam, ‘kwa imani iliyo kwangu:’ ni Yesu aliye hai kinafsi ajitoaye mwenyewe, yeye mwenyewe katika utajiri wote wa Nguvu zake na Upendo wake, kama shabaha, nguvu, na uzima wa imani yetu. Yeye atwambia kwamba kama tungependa kuwa watakatifu, sikuzote na katika kila jambo watakatifu, ni lazima tuangalie jambo moja tu: kuwa sikuzote na kwa ukamilifu tumejaa imani ndani yake. Imani ni jicho la nafsi: nguvu ambayo kwayo twatambua kuwapo kwake Yule Asiyeonekana, ajapo kujitoa mwenyewe kwetu. Imani haioni tu, bali hutwaa na kuchukua kuwa yake: na tuzitulize nafsi zetu kabisa mbele ya Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu, ili aihuishe na kuiimarisha imani ile, ambayo kwa ajili yake ametolewa kwetu. Imani ni kujisalimisha: kwa kujitoa wenyewe kwa Yesu ili kumruhusu atende kazi yake ndani yetu, kwa kujikabidhi kwake ili aishi maisha yake na kutimiza mapenzi yake ndani yetu, tutamwona akijitoa mwenyewe kabisa kwetu, na kutwaa umiliki kamili. Hivyo imani itakuwa nguvu: nguvu ya utii wa kutenda mapenzi ya Mungu: ‘imani yetu iliyo takatifu kupita zote,’ ‘imani waliyokabidhiwa watakatifu.’ Nasi tutaelewa jinsi ilivyo rahisi, kwa mwenye moyo mmoja, siri ya utakatifu: ni Yesu tu. Sisi tu ndani yake, Utakaso wetu: yeye kinafsi ni Utakatifu wetu; na maisha ya imani ndani yake, yampokeayo na kummiliki, lazima yawe maisha ya utakatifu. Yesu asema, ‘Waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu.’

Kuweni watakatifu, kama mimi nilivyo mtakatifu.

Bwana mpendwa! tena nimeona, kwa mshangao wa kuabudu, kile ambacho u tayari kuwa kwangu. Ni ndani yako mwenyewe, na katika maisha ya ushirika hai nawe mwenyewe, ndipo nitakapokuwa mtakatifu. Ni katika maisha rahisi ya kuambatana kinafsi, ya kutumaini na upendo, ya kujisalimisha na kujiweka wakfu, ndipo wewe wawa vyangu vyote, na kunifanya mshiriki wa nafsi yako na Utakatifu wako.

Bwana Yesu mbarikiwa! naamini kwako, unisaidie kutokuamini kwangu. Naungama kile kilichosalia cha kutokuamini, nami nategemea uwepo wako kukishinda na kukitupa nje. Nafsi yangu yazidi kufunuka daima ili kuona zaidi jinsi wewe mwenyewe ulivyo Uzima wangu na Utakatifu wangu. Wewe waupanua moyo wangu ili kufurahia ndani yako mwenyewe kama vyangu vyote, na kuhakikishiwa kwamba wewe mwenyewe watwaa umiliki na kulijaza hekalu la nafsi yangu kwa utukufu wako. Wanifundisha kuelewa kwamba, hata uzoefu ujapokuwa dhaifu na wa kibinadamu na wa kukatisha tamaa kiasi gani, Roho wako Mtakatifu ni nguvu ya imani yangu, akiniongoza kukua hata kufikia uhakika ulio na nguvu zaidi na mkubwa zaidi kwako wewe ambaye ndani yako mimi ni mtakatifu. Ee Mwokozi wangu! nalitwaa neno lako leo, ‘Waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu,’ kama ufunuo mpya wa upendo wako na kusudi lake kwangu. Ndani yako mwenyewe imo Nguvu ya utakatifu wangu; ndani yako imo Nguvu ya imani yangu. Libarikiwe jina lako kwa kuwa umenipa mimi pia nafasi kati ya wale unaowanena: ‘Waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu.’ Amina.

1. Na tukumbuke kwamba si ile imani tu ishughulikayo hasa na Kristo kwa ajili ya utakaso, bali imani yote iliyo hai, ndiyo yenye nguvu ya kutakasa. Kila kitu kimtupacho nafsi kabisa juu ya Yesu, kiitacho kutumaini kwa dhati na kwa unyofu, kiwe jaribu la imani, au maombi ya imani, au kazi ya imani, husaidia kutufanya watakatifu, kwa sababu chatuleta katika kugusana kwa uzima na yule Mtakatifu.

2. Ni kwa njia ya Roho Mtakatifu peke yake ambapo Kristo na Utakatifu wake hufunuliwa siku kwa siku na kufanywa vyetu katika kumiliki halisi. Na hivyo imani impokeayo yeye ni ya Roho pia. Jisalimishe kwa unyofu na kutumaini kwa kazi yake. Usiogope, kana kwamba huwezi kuamini: unayo ‘Roho ya imani’ ndani yako: unayo nguvu ya kuamini. Nawe waweza kumwomba Mungu akutie nguvu kwa uwezo kwa Roho wake katika utu wa ndani, kwa ajili ya imani impokeayo Kristo katika kukaa ndani kusikojua kikomo.

3. Nina imani kiasi tu kadiri nilivyo na Roho. Je, hili basi silo nihitajilo zaidi—kuishi kabisa chini ya uvutano wa Roho?

4. Kama vile jicho katika kuona lilivyo lenye kupokea, na hujitoa kuruhusu kitu kilichowekwa mbele yake kifanye chapa yake, vivyo hivyo imani ni chapa Mungu aifanyayo juu ya nafsi ajapokaribia. Je, imani ya Abrahamu haikuwa tunda la Mungu kukaribia na kusema naye, chapa Mungu aliyofanya juu yake? Na tutulie ili kulitazama fumbo la Kimungu la Kristo utakatifu wetu: Uwepo wake, ukingojewa na kuabudiwa, utaifanya imani. Yaani, Roho itokayo kwake na kuingia ndani ya wale wanaoshikamana naye, itakuwa imani.

5. Utakatifu kwa imani katika Yesu, si kwa jitihada yako mwenyewe,

Utawala wa dhambi umepondwa na kuvunjwa kwa nguvu ya neema peke yake,—

Utakatifu wa Mungu mwenyewe ndani yako, uzuri wake mwenyewe kipajini pako,—

Huu ndio utakuwa mng’ao wako wa msafiri, hii ni sehemu yako iliyobarikiwa sasa.

F. R. H.


Siku ya Kumi na Tisa.

Yaliyomo

Mtakatifu katika Kristo Andrew Murray

Ukurasa 1 / 1 · 11 dakika zimebaki katika sura