Sura 18 · dakika 9 za kusoma
Niseme Nini Zaidi?
“Nami niseme nini zaidi? Kwa maana wakati hautanitosha kuwasimulia habari za Gideoni, na Baraka, na Samsoni, na Yeftha; na Daudi, na Samweli, na manabii - ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto, waliokoka makali ya upanga, walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni.
Wanawake waliwapokea wafu wao kwa ufufuo. Wengine waliteswa hata kufa, wasikubali kufunguliwa, ili wapate ufufuo ulio bora zaidi. Wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, na kwa vifungo na kutiwa gerezani. Walipigwa mawe, walikatwa vipande viwili kwa msumeno, waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wamevaa ngozi za kondoo na za mbuzi; walikuwa wahitaji, wenye dhiki, wateswao - ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao - wakitangatanga katika jangwa na milimani, na katika mapango na katika mashimo ya nchi. Na hawa wote, ingawa walishuhudiwa kuwa wema kwa imani yao, hawakuipokea ile ahadi; kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora zaidi, ili wao wasikamilishwe pasipo sisi” (Waebrania 11:32-40).
Mistari tisa inayohitimisha sura hii inathibitisha wazi hoja yangu. Kwa imani, wengi walitenda matendo makuu na kuona miujiza mikuu; kwa imani, wengine walipitishwa katika maumivu na dhiki kuu. Hakika hii haikuwa kwa sababu waliamini, bali kwa sababu ilikuwa nia njema ya Mungu kwamba hata kupitia mateso Yeye angetukuzwa katika watu wake. Walikuwa tayari kwa sababu walikuwa na ushuhuda wa ndani wa uhalisia ambao haukuwaacha waukwepe huzuni na maumivu. Wangeweza kuyakwepa, kama wangemkana Bwana wao kama watesi wao walivyodai.
Mwandishi mtakatifu ameshafikisha hoja yake katika mifano ya awali ya sura hii. Sasa anakusanya tu majina mengi pamoja, hata si kwa mpangilio wa nyakati, lakini hilo halitawasumbua wasomaji wake kwa maana wanazijua vyema historia za kila jina jipya lililoandikwa. Sisi twaweza kupoteza uzito wa majina na matendo haya yanavyorushwa kwetu kwa haraka namna hii, lakini kwa Wayahudi, kila fungu la maneno lingeleta kumbukumbu iliyo hai.
Yosefo, mwanahistoria wa zamani, alitumia fungu lile lile la maneno ya Kiyunani kama mwandishi wetu alipoeleza jinsi Daudi alivyo‘shinda milki za wafalme.’
Septuaginta - tafsiri ya Kiyunani ya Agano letu la Kale - inatumia maneno yale yale kueleza jinsi Daudi alivyo‘tenda haki,’ jinsi imani ilivyo‘funga vinywa vya simba’ kwa ajili ya Danieli, na jinsi imani ilivyo‘zima moto uwakao’ kwa ajili ya Shadraka, Meshaki, na Abednego.
Taswira ya ‘kuokoka makali ya upanga’ ingegeuza fikira za wasomaji kuelekea kuokolewa kwa Eliya na Elisha kutoka kwa Yezebeli na Washami. Mifano mingine zaidi imetolewa kutoka maisha ya waaminifu ambayo hayakuandikwa katika Agano letu la Kale, lakini yawezekana ilijulikana vyema kwa wasomaji wa vitabu vya apokrifa, hasa kitabu cha pili cha Wamakabayo. Bila shaka, mafungu ya maneno ‘kuwa hodari katika vita’ na ‘kukimbiza majeshi ya wageni’ yangewafanya mara moja wakumbuke fahari zisizosahaulika za siku za Wamakabayo.
Hata hivyo, hadithi za imani si za ushindi sikuzote zionekanapo kwa macho ya kibinadamu. Kama sura hii ingeishia mstari wa 34, tungeshawishika kuamini kwamba mambo mema tu ndiyo yanayowapata wale wenye imani katika Mungu: afya, utajiri na ufanisi, lakini badala yake, mauti, mateso na dhiki. Je, haya yaweza kuwa kwa imani? Ndiyo! Ndiyo! Ndiyo! Ikiwa Mungu atatukuzwa ndani yake, ndiyo! Naye ametukuzwa kupitia mateso ya watu wake.
Nisomapo Injili ya Yohana, naona mara nyingi Yesu akinena juu ya utukufu wake ujao. Wewe hufikiria nini usomapo neno, “utukufu?” Nimejaribu kulifafanua na hatimaye nikahitimisha kuwa ni ukamilifu wa Mungu, uliofunuliwa. Yesu alisema katika Yohana 17:1, “Baba, saa imekwisha kufika; mtukuze Mwanao, ili Mwana apate kukutukuza wewe” naye akaenda msalabani. Kwa kweli, kila mara utukufu unapotajwa katika injili ya Yohana unahusishwa na mauti ya Yesu! Utukufu huja kupitia mateso!
Historia ya Wamakabayo ilikuwa imejaa kumbukumbu za mateso na kufa kishahidi kwa Wayahudi waaminifu wakati wa siku mbaya za Mshami, Antioko Epifane. Hizi ni hadithi ambazo wasomaji Waebrania wangeweza kuzihusianisha vyema na mafungu ya maneno hapo juu, na historia ya kanisa tangu nyakati za mitume na mwandishi wa Waebrania, ina masimulizi mengi yanayofanana.
Tungeweza kuandika, “Kwa imani Stefano aliuawa, akilia, ‘Baba, usimhesabie dhambi hii!’” Kwa tendo hili la imani, alimfungua Sauli wa Tarso kutoka katika hukumu ya Mungu, na hivyo kufungua njia kwa Mungu kumwita Sauli aingie katika huduma yake kuu kama Paulo Mtume. Kama Stefano angeitikia dhiki yake kwa kuiombea ghadhabu ya Mungu imshukie Sauli (kama, nakiri, ningeshawishika kufanya!), najiuliza kama Sauli angewahi kuwa mtume yule mkuu.
Kwa imani Paulo alifungwa gerezani Rumi ili apate wakati wa kuandika nyaraka zile kuu ambazo zimekuwa chemchemi ya kutia moyo na mwongozo kwa waaminio wasiohesabika.
Kwa imani waamini wa kwanza waliteswa ili injili ienee katika ulimwengu wote wa Kirumi walipowakimbia watesi wao.
Kwa imani, Cranmer, Ridley, na Latimer walichomwa motoni katikati ya karne ya kumi na sita ili “taa iwashwe katika Uingereza ambayo kamwe haitazimwa” (Hugh Latimer).
Kwa imani wamishonari waliamriwa watoke Uchina katikati ya karne ya ishirini ili kanisa safi la waamini lipate kukua ndani ya utamaduni wa Kichina - si nakala ya kanisa la kimagharibi. Hilo ni jambo gumu kwa wengi wetu tulio na mtazamo potofu kwamba dhana ya kimagharibi ya kanisa peke yake ndiyo inayokubalika kwa Mungu. Katika safari zangu nimekaribia kufikia msimamo wa kejeli kwamba kanisa letu la ‘kimagharibi’ ndilo lisilokubalika zaidi kwa Mungu!
Wengine hawatakubali kwamba kanisa la Uchina limekua hadi mamilioni mengi tangu wamishonari walipoondoka. Niongeze hapa, nisije nikaeleweka vibaya, kwamba naamini kwa dhati katika umishonari na wamishonari. Hata hivyo, wakati mwingine naona njia zetu na ukosefu wetu wa umoja ni vigumu kuvikubali. Ashukuriwe Bwana, jambo hili linazidi kupungua katika historia ya hivi karibuni ya umishonari.
Kwa imani vijana watano wa Kimarekani walifia katika misitu ya Ekwado tarehe 8 Januari, 1956 ili Wahindi wa Auka nao wapate kuwa warithi pamoja nasi wa utajiri wa Injili. Tahariri za ulimwengu ziliita hii kuwa upotevu mkubwa wa maisha ya vijana wa Kimarekani, lakini kama mmoja wao, Jim Elliott, alivyokuwa ameandika katika shajara yake saa chache kabla ya kifo chake, “Si mpumbavu yeye atoaye kile asichoweza kukishika, ili apate kile asichoweza kukipoteza!” (Jim Elliot). Hiyo yapaswa kuwa kauli-mbiu ya wote watakaoenenda kwa imani.
Majina ya Pete Fleming, Roger Youderian, Ed McCully, Nate Saint, na Jim Elliott, pamoja na ya wake zao, yanajulikana vyema mbinguni na kuzimuni pia. Kwa maana kupitia kifo na dhiki waliyoiteseka, ufa mpana ulifanywa katika kuta za gereza zilizokuwa zimewaweka Wahindi wa Auka katika utumwa wa dhambi.
Leo, twaweza kufurahi kwamba maelfu mengi ya watu hao wa thamani wameingia katika uhuru unaopatikana katika Kristo peke yake.
Kama msomaji wangu hajui tukio hili, nakuhimiza usome, “Through Gates of Splendour” kilichoandikwa na Elizabeth Elliott, mjane wa Jim.
Kweli twaweza kukubaliana na kauli isemayo kwamba kifo cha mashahidi kimekuwa uhai wa kanisa. Leo, katika karne ya ishirini, huenda kuna kufa kishahidi kwingi zaidi na mateso mengi zaidi kuliko wakati wowote katika historia, lakini kanisa halikushindwa nalo linaendelea kukua kwa kasi kubwa mno.
Wengine kupitia maji, wengine kupitia gharika, Wengine kupitia moto, lakini wote kupitia damu; Wengine kupitia huzuni kuu lakini Mungu hutoa wimbo, wakati wa usiku na mchana kutwa.
(G.A.Young) Je, tusiweze pia kuandika kwamba kwa imani, (jina lako) aliingia katika bonde jipya la maumivu kwa sababu Baba anataka kumfanya afanane zaidi na Mwanawe mwingine, Yesu?
“Na hawa wote, ingawa walishuhudiwa kuwa wema kwa imani yao, hawakuipokea ile ahadi; kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora zaidi, ili wao wasikamilishwe pasipo sisi” (Waebrania 11:39-40).
Wanaume na wanawake hawa wote wa imani wameandikwa kuwa mfano kwetu. Hawakupokea thawabu yoyote katika maisha haya kwa ajili ya uaminifu wao. Walikuwa na imani katika Mungu. Walimwamini na kulitii neno alilolinena kwao na ndani yao; hata hivyo, hawakuwa wamekipokea kile “kitu kilicho bora zaidi” kilicho chetu leo.
Thawabu ya uaminifu wao inapatikana katika Mwokozi, Kristo, atakayempa kila mtu kama anavyostahili - si kwa ukuu wake machoni pa ulimwengu au kanisa, bali kwa imani yake. Zaidi ya hayo, tumepewa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu, aliye ahadi ya Baba (Matendo 1:4), “Kristo ndani yetu, tumaini la utukufu” atakayetuongoza katika kweli. Ni ushuhuda wake wa ndani unaotuwezesha kuenenda katika imani tunapojisalimisha kwa ufunuo wake wa ndani. Ni Yeye aliyetuleta katika imani iokoayo, naye atazaa tunda la imani ndani yetu tunaposimama kando ya vijito vya maji yaliyo hai. Tunapokunywa sana kutoka mito ya maji yaliyo hai, tutazaa tunda kwa wakati wake.
Ee Bwana, natamani kuenenda katika mapenzi yako. Kama vile ayala aoneavyo shauku vijito vya maji, ndivyo moyo wangu unavyokutamani wewe. Uniongoze katika mapenzi yako. Siombi kujua mapenzi yako wala kuwa na furaha ndani yake. Kama utaniongoza kupitia mabonde marefu niko tayari kwenda, kwa maana wewe utakuwa mfariji wangu hata katika bonde la uvuli wa mauti. Najua jinsi niwezavyo kuwa mpumbavu na mkaidi, hivyo wakati wowote nitakapotoka nje ya mapenzi yako, nakupa ruhusa kamili unirudishe mstarini kwa fimbo. Ninachoomba tu ni kwamba mwishoni mwa safari hii, nitakusikia ukisema, “vema, mtumishi mwema na mwaminifu!”
Picha niliyo nayo ya imani ni kwamba mimi ni mtoto tu niliyeshika mkono wa Baba yangu wa mbinguni.
Sijui kama leo atanipeleka mahali pa furaha kama ‘duka la peremende’ la maisha, au badala yake katika maumivu ya ‘daktari wa meno.’ Ninachojua ni kwamba itamlazimu anipeleke mahali pa pili kama nitakwenda mara kwa mara mahali pa kwanza!
Sijui kama kesho ataniongoza katika bonde refu, lakini najua kwamba, katika maisha yangu yaliyopita, mabonde kama hayo daima yamekuwepo kabla hajanipeleka vilele vya milima pamoja Naye.
Sijui mapenzi yake kwangu ni yapi (isipokuwa yale Maandiko yanayotufunulia sote), lakini najua kwamba Yeye anaijua njia iliyo mbele.
Sijui kesho ina nini, lakini namjua yeye aishikaye kesho, naye ameshika mkono wangu!
“Nataka maisha yangu yajae sifa kwako, Bwana wangu wa thamani wa kimungu Uliyekufa kwa ajili yangu.
Mapenzi yangu yote na yawe yako, yakiongozwa na upendo wa kimungu, Uishi ndani yangu uzima wako, Ee Mwokozi mwenye enzi.
Kiitikio: Mapenzi yako ya thamani ya kimungu, kwa furaha nayafanya yangu, Moyo wangu utakuwa kiti chako cha enzi, na chako peke yako.
Chagua wewe njia niiendeayo, na kokote niongozwako, Nisaidie kuendelea kufuata, Ee Mwokozi mwenye enzi.
Msafiri aliyezaliwa upya, mgeni apitaye, Mimi si wa ulimwengu huu kwa kuwa mimi ni wako.
Nikiachishwa maonyesho yake yapitayo, nikibadilishwa nijue upendo wako, Ushike mkono wangu ndani ya wako, Ee Mwokozi mwenye enzi.
Adui waovu washambuliapo na karibu washinde, Katika saa ile ya giza uwe wewe nguvu yangu na ngao yangu.
Basi nipe kumbatio lako lenye nguvu, unitegemeze kwa neema yako, Katika udhaifu uwe nguvu yangu, Ee Mwokozi mwenye enzi.
Naam, nichagulie njia, ijapokuwa siwezi kuona, Sababu upendayo kuniongoza hivyo.
Najua njia yenye taabu itaniongoza hadi nchi za mchana, Ambako nitakaa pamoja nawe, Ee Mwokozi mwenye enzi.”
(H.Tee) - ruhusa yaombwa.
MWISHO