Sura 2 · dakika 22 za kusoma
Tunda la Roho ni Upendo
Nataka kuutazama ukweli wa maisha yaliyojaa Roho Mtakatifu zaidi kwa upande wa vitendo, na kuonyesha jinsi maisha haya yatakavyojidhihirisha katika mwenendo na matendo yetu ya kila siku.
Chini ya Agano la Kale unajua Roho Mtakatifu mara nyingi aliwajilia watu kama Roho wa kimungu wa ufunuo ili kufunua siri za Mungu, au kwa nguvu za kuifanya kazi ya Mungu. Lakini wakati ule hakukaa ndani yao. Sasa, wengi wanataka tu kipawa cha Agano la Kale cha nguvu kwa ajili ya kazi, lakini wanajua kidogo sana kuhusu kipawa cha Agano Jipya cha Roho akaaye ndani, ahuishaye na kuyafanya upya maisha yote. Mungu anapotoa Roho Mtakatifu, kusudi lake kuu ni kuumbwa kwa tabia takatifu. Ni kipawa cha nia takatifu na hali ya kiroho, na kile tunachokihitaji kuliko kitu kingine chote, ni kusema:
“Ni lazima niwe na Roho Mtakatifu akiutakasa uhai wangu wote wa ndani kama kweli nitaishi kwa ajili ya utukufu wa Mungu.”
Waweza kusema kwamba Kristo alipowaahidi wanafunzi Roho, alifanya hivyo ili wapate nguvu za kuwa mashahidi. Ni kweli, lakini ndipo walipompokea Roho Mtakatifu kwa nguvu na uhalisi wa mbinguni kiasi kwamba aliumiliki utu wao wote mara moja na hivyo akawaandaa kama watu watakatifu kwa kuifanya kazi kwa nguvu kama walivyopaswa kuifanya. Kristo aliwaeleza wanafunzi juu ya nguvu, lakini ni Roho aliyeujaza utu wao wote ndiye aliyezitenda nguvu hizo.
Sasa nataka kukaa juu ya andiko lipatikanalo katika Wagalatia 5:22:
“Tunda la Roho ni upendo.”
Twasoma kwamba “Upendo ndio utimilifu wa sheria” (Warumi 13:10), na shauku yangu ni kunena juu ya upendo kama tunda la Roho kwa kusudi la namna mbili. Moja ni kwamba neno hili liwe taa itafutayo ndani ya mioyo yetu, na kutupa kipimo cha kuyapima mawazo yetu yote juu ya Roho Mtakatifu na uzoefu wetu wote wa maisha matakatifu. Na tujipime wenyewe kwa neno hili. Je, hii imekuwa desturi yetu ya kila siku, kutafuta kujazwa Roho Mtakatifu kama Roho wa upendo? “Tunda la Roho ni upendo.” Je, imekuwa uzoefu wetu kwamba kadiri tunavyozidi kuwa na Roho Mtakatifu ndivyo tunavyozidi kuwa na upendo? Katika kudai Roho Mtakatifu yatupasa kufanya hili kuwa lengo la kwanza la matarajio yetu. Roho Mtakatifu huja kama Roho wa upendo.
Laiti hili lingekuwa kweli katika Kanisa la Kristo, hali yake ingekuwa tofauti kama nini! Mungu na atusaidie kuushika ukweli huu rahisi, wa mbinguni kwamba tunda la Roho ni upendo udhihirikao katika maisha, na kwamba kadiri Roho Mtakatifu anavyoumiliki uhai kweli kweli, ndivyo moyo utakavyojazwa upendo halisi, wa kimungu, wa watu wote.
Moja ya sababu kuu zinazomfanya Mungu ashindwe kulibariki Kanisa lake ni kukosekana kwa upendo. Mwili unapogawanyika, hakuwezi kuwa na nguvu. Katika kipindi cha vita vyao vikuu vya kidini, wakati Uholanzi ilipojisimamia kwa uungwana dhidi ya Uhispania, mojawapo ya kauli mbiu zao ilikuwa: “Umoja hutoa nguvu.” Ni pale tu watu wa Mungu wanaposimama kama mwili mmoja, mmoja mbele za Mungu katika ushirika wa upendo, mmoja kwa mwenzake katika mapenzi ya ndani, mmoja mbele ya ulimwengu katika upendo ambao ulimwengu waweza kuuona—ndipo tu watakapokuwa na nguvu za kupata baraka waiombayo kwa Mungu. Kumbuka kwamba ikiwa chombo kinachopaswa kuwa kimoja kizima kimepasuka vipande vingi, hakiwezi kujazwa. Waweza kuchukua kigae, sehemu moja ya chombo, na kuteka maji kidogo ndani yake, lakini kama wataka chombo kijae, sharti chombo kiwe kizima. Hilo ni kweli kabisa juu ya Kanisa la Kristo, na kama kuna jambo moja tunalopaswa kuendelea kuliombea, ni hili: Bwana, tuyeyushe pamoja tuwe mmoja kwa nguvu za Roho Mtakatifu; Roho Mtakatifu, aliyewafanya wote kuwa na moyo mmoja na roho moja siku ya Pentekoste, na afanye kazi yake yenye baraka kati yetu. Ahsante Mungu, twaweza kupendana kwa upendo wa kimungu, kwa maana “tunda la Roho ni upendo.” Jitoeni kwa upendo, na Roho Mtakatifu atakuja; mpokeeni Roho, naye atakufundisha kupenda zaidi.
Mungu Ni Upendo
Basi, kwa nini tunda la Roho ni upendo? Kwa sababu Mungu ni upendo (1 Yohana 4:8).
Na hilo lina maana gani?
Ni asili na hali halisi ya Mungu kufurahia kujitoa mwenyewe. Mungu hana ubinafsi, Mungu hajiwekei kitu chochote. Asili ya Mungu ni kutoa daima. Katika jua na mwezi na nyota, katika kila ua unaliona, katika kila ndege wa angani, katika kila samaki wa baharini. Mungu huwapa viumbe vyake uhai. Na malaika walio kando ya kiti chake cha enzi, maserafi na makerubi walio miali ya moto—utukufu wao watoka wapi? Ni kwa sababu Mungu ni upendo, naye huwagawia mng’ao wake na heri yake. Nasi, watoto wake waliokombolewa—Mungu hufurahia kumimina upendo wake ndani yetu. Na kwa nini? Kwa sababu, kama nilivyosema, Mungu hajiwekei chochote. Tangu milele Mungu alikuwa na Mwanawe pekee, naye Baba akampa vitu vyote, wala hakuna kitu Mungu alichokuwa nacho kilichozuiliwa. “Mungu ni upendo.”
Mmoja wa mababa wa Kanisa la kale alisema kwamba hatuwezi kuufahamu Utatu vizuri zaidi ila kama ufunuo wa upendo wa kimungu—Baba, yule apendaye, Chemchemi ya upendo; Mwana, yule mpendwa, Birika la upendo, ambamo upendo ulimiminwa; na Roho, upendo ulio hai uliowaunganisha wote wawili kisha ukafurika hata katika ulimwengu huu. Roho wa Pentekoste, Roho wa Baba, na Roho wa Mwana ni upendo. Na Roho Mtakatifu ajapo kwetu na kwa watu wengine, je, atakuwa Roho wa upendo pungufu kuliko alivyo katika Mungu? Haiwezekani; hawezi kuibadili asili yake. Roho wa Mungu ni upendo, na “tunda la Roho ni upendo.”
Wanadamu Wanahitaji Upendo
Kwa nini ni hivyo? Hilo ndilo lililokuwa hitaji kuu moja la wanadamu, hilo ndilo jambo ambalo ukombozi wa Kristo ulikuja kulitimiza: kuurudisha upendo katika ulimwengu huu.
Mwanadamu alipotenda dhambi, kwa nini alitenda dhambi? Ubinafsi ulishinda—alijitafuta nafsi badala ya Mungu. Na tazama tu! Adamu mara moja aanza kumshtaki mwanamke kwa kumpotosha. Upendo kwa Mungu ulikuwa umeondoka, upendo kwa mwanadamu ulipotea. Tazama tena: kati ya watoto wawili wa kwanza wa Adamu mmoja anakuwa muuaji wa ndugu yake.
Je, hilo halitufundishi kwamba dhambi ilikuwa imeunyang’anya ulimwengu upendo? Ah! historia ya ulimwengu imekuwa ushahidi ulioje wa upendo kupotea! Huenda kukawa na mifano mizuri ya upendo hata miongoni mwa wapagani, lakini kama mabaki kidogo tu ya kile kilichopotea. Mojawapo ya mabaya makubwa dhambi iliyomtendea mwanadamu ni kumfanya awe mbinafsi, kwa maana ubinafsi hauwezi kupenda.
Bwana Yesu Kristo alishuka kutoka Mbinguni kama Mwana wa upendo wa Mungu. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee” (Yohana 3:16). Mwana wa Mungu alikuja kuonyesha upendo ni nini, naye aliishi maisha ya upendo hapa duniani katika ushirika na wanafunzi wake, katika huruma juu ya maskini na wenye taabu, katika upendo hata kwa adui zake, naye akafa kifo cha upendo. Na alipokwenda Mbinguni, alimtuma nani hapa chini? Roho wa upendo, aje kuufukuza ubinafsi na wivu na kiburi, na kuuleta upendo wa Mungu ndani ya mioyo ya watu. “Tunda la Roho ni upendo.”
Na maandalizi ya ile ahadi ya Roho Mtakatifu yalikuwa nini? Waijua ahadi hiyo kama ipatikanavyo katika sura ya kumi na nne ya Injili ya Yohana. Lakini kumbuka lililotangulia katika sura ya kumi na tatu. Kabla Kristo hajaahidi Roho Mtakatifu, alitoa amri mpya, na juu ya amri hiyo mpya alisema mambo ya ajabu. Jambo moja lilikuwa: “Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo.” Kwao upendo wake wa kufa ulipaswa kuwa sheria pekee ya mwenendo na maingiliano yao kila mmoja na mwenzake. Ujumbe ulioje kwa wale wavuvi, kwa wale watu waliojaa kiburi na ubinafsi! “Jifunzeni kupendana,” akasema Kristo, “kama vile nilivyowapenda ninyi.” Na kwa neema ya Mungu walifanya hivyo. Pentekoste ilipofika, walikuwa na moyo mmoja na roho moja. Kristo aliwatendea hivyo.
Na sasa anatuita tukae na kuenenda katika upendo. Anadai kwamba ijapokuwa mtu akuchukia, bado umpende. Upendo wa kweli hauwezi kushindwa na kitu chochote Mbinguni wala juu ya nchi. Kadiri chuki inavyozidi, ndivyo upendo unavyozidi kushinda katika yote na kuonyesha asili yake ya kweli. Huu ndio upendo ambao Kristo aliwaamuru wanafunzi wake kuutenda.
Alisema nini zaidi? “Kwa hili watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yohana 13:35).
Nyote mnajua maana ya kuvaa alama. Na Kristo aliwaambia wanafunzi wake kwa maana hii: “Nawapa alama, na alama hiyo ni upendo. Hiyo ndiyo iwe ishara yenu. Ndicho kitu pekee Mbinguni au duniani ambacho kwa hicho watu waweza kunijua.”
Je, hatuanzi kuogopa kwamba upendo umeukimbia ulimwengu? Kwamba kama tungeuuliza ulimwengu: “Je, mmetuona tukivaa alama ya upendo?” ulimwengu ungesema: “Hapana; tuliyosikia juu ya Kanisa la Kristo ni kwamba hakuna mahali pasipo na ugomvi na mafarakano.” Na tumwombe Mungu kwa moyo mmoja tupate kuivaa alama ya upendo wa Yesu. Mungu aweza kuitoa.
Upendo Hushinda Ubinafsi
“Tunda la Roho ni upendo.” Kwa nini? Kwa sababu hakuna kitu ila upendo kiwezacho kuufukuza na kuushinda ubinafsi wetu.
Nafsi ni laana kuu, iwe katika uhusiano wake na Mungu, au na wenzetu wanadamu kwa jumla, au na Wakristo wenzetu, tukijifikiria wenyewe na kutafuta mambo yetu wenyewe. Nafsi ni laana yetu kubwa kuliko zote. Lakini, ahsante Mungu, Kristo alikuja kutukomboa na nafsi. Nyakati fulani twanena juu ya wokovu kutoka katika maisha ya nafsi—na Mungu asifiwe kwa kila neno liwezalo kunenwa juu yake ili kutusaidia—lakini nachelea kwamba watu wengine hudhani wokovu kutoka katika maisha ya nafsi maana yake ni kwamba sasa hawatakuwa tena na taabu yoyote katika kumtumikia Mungu; nao husahau kwamba wokovu kutoka katika maisha ya nafsi maana yake ni kuwa chombo kifurikacho upendo kwa kila mtu mchana kutwa.
Na hapo ndipo una sababu inayowafanya watu wengi kuomba nguvu za Roho Mtakatifu, nao hupata kitu, lakini ah, kidogo mno! kwa sababu waliomba nguvu kwa ajili ya kazi, na nguvu kwa ajili ya baraka, lakini hawakuomba nguvu za wokovu kamili kutoka katika nafsi. Hilo lamaanisha si nafsi yenye haki tu katika maingiliano na Mungu, bali pia nafsi isiyo na upendo katika maingiliano na watu. Na kuna wokovu. “Tunda la Roho ni upendo.” Nawaletea ahadi tukufu ya Kristo kwamba yeye aweza kuijaza mioyo yetu upendo.
Wengi wetu nyakati fulani hujitahidi sana kupenda. Twajaribu kujilazimisha kupenda, wala sisemi hilo ni baya; ni bora kuliko kutokuwa na chochote. Lakini mwisho wake daima ni wa huzuni sana. “Nashindwa mfululizo,” ndivyo mtu wa namna hiyo apaswavyo kuungama. Na sababu ni nini? Sababu ni hii tu: Kwa sababu hawajapata kamwe kujifunza kuamini na kukubali ukweli kwamba Roho Mtakatifu aweza kumimina upendo wa Mungu ndani ya moyo wao. Andiko lile lenye baraka; mara nyingi limewekewa mipaka!—“Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu” (Warumi 5:5). Mara nyingi limefahamika kwa maana hii: Lamaanisha upendo wa Mungu kwangu. Ah, mpaka ulioje! Huo ni mwanzo tu. Upendo wa Mungu daima ni upendo wa Mungu katika ukamilifu wake, katika utimilifu wake kama nguvu ikaayo ndani, upendo wa Mungu kwangu unaomrukia yeye tena kwa upendo, na kufurika kwa wenzangu wanadamu kwa upendo—upendo wa Mungu kwangu, na upendo wangu kwa Mungu, na upendo wangu kwa wenzangu wanadamu. Hivyo vitatu ni kimoja; huwezi kuvitenganisha.
Aminini kwamba upendo wa Mungu waweza kumiminwa ndani ya moyo wako na wangu ili tupate kupenda mchana kutwa.
“Ah!” wasema, “ni kidogo kama nini nimekifahamu hicho!”
Kwa nini mwana-kondoo daima ni mpole? Kwa sababu hiyo ndiyo asili yake. Je, humgharimu mwana-kondoo taabu yoyote kuwa mpole? Hapana. Kwa nini? Ni mzuri na mpole hivyo. Je, mwana-kondoo huhitaji kujifunza ili kuwa mpole? Hapana. Kwa nini hilo humjia kwa urahisi hivyo? Ni asili yake. Na mbwa-mwitu—kwa nini haimgharimu mbwa-mwitu taabu yoyote kuwa mkatili, na kuyaingiza meno yake makali katika yule mwana-kondoo au kondoo maskini? Kwa sababu hiyo ndiyo asili yake. Hana haja ya kujipa ujasiri; asili ya mbwa-mwitu ipo pale.
Nami nawezaje kujifunza kupenda? Kamwe hata Roho wa Mungu atakapoujaza moyo wangu upendo wa Mungu, nami nianze kuutamani upendo wa Mungu kwa maana tofauti kabisa na jinsi nilivyokuwa nikiutafuta kwa ubinafsi, kama faraja na furaha na heri na anasa kwangu mimi mwenyewe; kamwe hata nitakapoanza kujifunza kwamba “Mungu ni upendo,” na kuudai, na kuupokea kama nguvu ikaayo ndani kwa ajili ya kujitoa nafsi; kamwe hata nitakapoanza kuona kwamba utukufu wangu, heri yangu, ni kufanana na Mungu na kufanana na Kristo, katika kuacha kila kitu ndani yangu kwa ajili ya wenzangu wanadamu. Mungu na atufundishe hilo! Ah, heri ya kimungu ya upendo ambao kwao Roho Mtakatifu aweza kuijaza mioyo yetu! “Tunda la Roho ni upendo.”
Upendo Ni Kipawa cha Mungu
Tena nauliza, Kwa nini ni lazima iwe hivyo? Na jibu langu ni: Bila hili hatuwezi kuishi maisha ya kila siku ya upendo.
Mara ngapi, tunaponena juu ya maisha yaliyowekwa wakfu, twalazimika kunena juu ya hasira, na watu wengine nyakati fulani wamesema:
“Mnaikuza hasira kupita kiasi.”
Sidhani twaweza kuikuza kupita kiasi. Fikiri kwa muda juu ya saa na maana ya mikono yake. Mikono huniambia kilicho ndani ya saa, na nikiona kwamba mikono imesimama tuli, au kwamba mikono inaonyesha vibaya, au kwamba saa imechelewa au imetangulia, nasema kwamba kitu fulani ndani ya saa hakifanyi kazi vizuri. Na hasira ni kama vile ufunuo ambao saa hutoa juu ya kilicho ndani. Hasira ni ushahidi kama upendo wa Kristo unaujaza moyo, au sivyo. Wangapi walioko ambao huona rahisi zaidi kanisani, au katika mkutano wa maombi, au katika kazi ya Bwana—kazi ya bidii, ya moyo—kuwa watakatifu na wenye furaha kuliko katika maisha ya kila siku pamoja na mke na watoto; rahisi zaidi kuwa watakatifu na wenye furaha nje ya nyumba kuliko ndani yake! Uko wapi upendo wa Mungu? Katika Kristo. Mungu ametuandalia ukombozi wa ajabu katika Kristo, naye atamani kutufanya kitu kilicho juu ya maumbile. Je, tumejifunza kuutamani, na kuuomba, na kuutarajia katika utimilifu wake?
Kisha kuna ulimi! Nyakati fulani twanena juu ya ulimi tunapozungumza juu ya maisha bora, na maisha ya raha, lakini fikiri tu uhuru ambao Wakristo wengi huipa ndimi zao. Wao husema:
“Nina haki ya kufikiri nipendavyo.”
Wanaponena kila mmoja juu ya mwenzake, wanaponena juu ya jirani zao, wanaponena juu ya Wakristo wengine, mara ngapi kuna maneno makali! Mungu na anilinde nisiseme neno lolote ambalo lingekuwa bila upendo; Mungu na aufunge mdomo wangu kama sitanena kwa upendo mwororo. Lakini ninalolisema ni jambo la kweli. Mara ngapi hupatikana miongoni mwa Wakristo walioungana pamoja katika kazi, uchambuzi mkali, hukumu kali, maoni ya haraka, maneno yasiyo na upendo, dharau ya siri kila mmoja kwa mwenzake, hukumu ya siri kila mmoja kwa mwenzake! Ah, kama vile upendo wa mama uwafunikavyo watoto wake na kuwafurahia na kuwa na huruma iliyo mwororo kabisa juu ya udhaifu au makosa yao, vivyo hivyo yapasa kuwe katika moyo wa kila mwamini upendo wa kimama kwa kila ndugu wa kiume na wa kike katika Kristo. Je, umelenga hilo? Je, umelitafuta? Je, umewahi kuliombea? Yesu Kristo alisema: “Mpendane kama vile nilivyowapenda ninyi” (Yohana 13:34). Naye hakuliweka hilo miongoni mwa amri nyingine, bali alisema kwa maana hii:
“Hiyo ni amri mpya, amri ile moja: Mpendane kama vile nilivyowapenda ninyi” (Yohana 13:34).
Ni katika maisha na mwenendo wetu wa kila siku ambamo tunda la Roho ni upendo. Kutoka humo hutoka neema na fadhila zote ambamo upendo hudhihirishwa: furaha, amani, uvumilivu, upole, wema; hakuna ukali wala ugumu katika sauti yako, hakuna ukosefu wa fadhili wala ubinafsi; unyenyekevu mbele za Mungu na mwanadamu. Waona kwamba hizi zote ni fadhila zilizo pole zaidi. Mara nyingi nimefikiri nisomapo maneno yale katika Wakolosai, “Jivikeni basi, kama wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu” (Wakolosai 3:12), kwamba kama sisi tungeliyaandika haya, tungeziweka mbele fadhila za kiume, kama vile bidii, ujasiri, na juhudi; lakini twahitaji kuona jinsi fadhila zilizo pole, zilizo za kike zaidi zinavyohusiana hasa na kumtegemea Roho Mtakatifu. Hizi kweli ni neema za mbinguni. Hazikupatikana kamwe katika ulimwengu wa kipagani. Kristo alihitajika aje kutoka Mbinguni kutufundisha. Heri yako ni uvumilivu, upole, fadhili; utukufu wako ni unyenyekevu mbele za Mungu. Tunda la Roho ambalo aliliteremsha kutoka Mbinguni kutoka moyoni mwa Kristo aliyesulubiwa, na ambalo hulitoa ndani ya moyo wetu, kwanza kabisa ni—upendo.
Wajua asemavyo Yohana: “Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote. Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu” (1 Yohana 4:12). Yaani, siwezi kumwona Mungu, lakini kama fidia naweza kumwona ndugu yangu, na nikimpenda, Mungu hukaa ndani yangu. Je, hilo ni kweli kabisa? Kwamba siwezi kumwona Mungu, lakini ni lazima nimpende ndugu yangu, naye Mungu atakaa ndani yangu? Kumpenda ndugu yangu ndiyo njia ya ushirika wa kweli na Mungu. Wajua asemavyo Yohana zaidi katika kipimo kile kizito kabisa, “Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezije kumpenda Mungu ambaye hakumwona?” (1 Yohana 4:20). Yuko ndugu, mtu asiyependeka kabisa. Anakusumbua kila mara mkutanapo. Ana tabia iliyo kinyume kabisa na yako. Wewe u mfanyabiashara mwangalifu, nawe wapaswa kushughulika naye katika biashara yako. Yeye ni mchafu mno, asiye na mpangilio wa kibiashara. Wasema:
“Siwezi kumpenda.”
Ah, rafiki, hujajifunza fundisho ambalo Kristo alitaka kulifundisha kuliko yote. Mtu na awe vyovyote atakavyo, wewe wapaswa kumpenda. Upendo unapaswa kuwa tunda la Roho mchana kutwa na kila siku. Naam, sikiliza! Kama mtu hampendi ndugu yake ambaye amemwona—kama humpendi yule mtu asiyependeka ambaye umemwona, wawezaje kumpenda Mungu ambaye hukumwona? Waweza kujidanganya kwa mawazo mazuri juu ya kumpenda Mungu. Ni lazima uuthibitishe upendo wako kwa Mungu kwa upendo wako kwa ndugu yako; hicho ndicho kipimo kimoja ambacho kwacho Mungu atauhukumu upendo wako kwake. Kama upendo wa Mungu umo moyoni mwako utampenda ndugu yako. Tunda la Roho ni upendo.
Na sababu ni nini kwamba Roho Mtakatifu wa Mungu hawezi kuja kwa nguvu? Je, haiwezekani?
Wakumbuka ule ulinganisho niliouutumia niliponena juu ya chombo. Naweza kuteka maji kidogo katika kigae, kipande cha chombo; lakini kama chombo kitajaa, sharti kisiwe kilichovunjika. Na watoto wa Mungu, popote wakutanapo, wa kanisa au utume au chama chochote wawe, sharti wapendane kwa nguvu, ama sivyo Roho wa Mungu hawezi kuifanya kazi yake. Twanena juu ya kumhuzunisha Roho wa Mungu kwa mambo ya kidunia na taratibu za nje na desturi na kosa na kutojali, lakini, nawaambia, jambo moja lililo juu ya yote linalomhuzunisha Roho wa Mungu ni huku kukosekana kwa upendo. Kila moyo na ujichunguze wenyewe, na kuomba kwamba Mungu auchunguze.
Upendo Wetu Huonyesha Nguvu za Mungu
Kwa nini tunafundishwa kwamba “tunda la Roho ni upendo”? Kwa sababu Roho wa Mungu amekuja ili kuyafanya maisha yetu ya kila siku kuwa dhihirisho la nguvu za kimungu na ufunuo wa yale Mungu awezayo kuwatendea watoto wake.
Katika sura ya pili na ya nne ya Matendo twasoma kwamba wanafunzi walikuwa na moyo mmoja na roho moja. Katika miaka ile mitatu waliyotembea na Kristo hawakuwahi kamwe kuwa katika roho hiyo. Mafundisho yote ya Kristo hayakuweza kuwafanya kuwa na moyo mmoja na roho moja. Lakini Roho Mtakatifu alikuja kutoka Mbinguni na kuumimina upendo wa Mungu ndani ya mioyo yao, nao wakawa na moyo mmoja na roho moja. Roho Mtakatifu yule yule aliyeuleta upendo wa Mbinguni ndani ya mioyo yao ni lazima atujaze sisi pia. Kilicho pungufu ya hicho hakitatosha. Kama vile Kristo alivyofanya, mtu aweza kuhubiri upendo kwa miaka mitatu kwa ulimi wa malaika, lakini hilo halingemfundisha mtu yeyote kupenda isipokuwa nguvu za Roho Mtakatifu zimjilie ili kuuleta upendo wa Mbinguni ndani ya moyo wake.
Fikiri juu ya kanisa kwa ujumla. Migawanyiko iliyoje! Fikiri juu ya vyama mbalimbali. Chukua swali la utakatifu, chukua swali la damu itakasayo, chukua swali la ubatizo wa Roho—tofauti zilizoje zisababishwazo miongoni mwa waamini wapendwa na maswali kama hayo! Kwamba kuna tofauti za maoni halinisumbui. Hatuna umbile na tabia na nia moja. Lakini mara ngapi chuki, uchungu, dharau, mafarakano, ukosefu wa upendo husababishwa na kweli zilizo takatifu kabisa za Neno la Mungu! Mafundisho yetu, kanuni zetu za imani, zimekuwa za maana zaidi kuliko upendo. Mara nyingi twadhani sisi ni mashujaa kwa ajili ya kweli nasi twaisahau amri ya Mungu ya kuinena kweli katika upendo. Na ilikuwa hivyo katika kipindi cha Matengenezo kati ya makanisa ya Kilutheri na ya Kikalvini. Uchungu ulioje uliokuwako wakati ule kuhusu Meza Takatifu, iliyokusudiwa kuwa kifungo cha muungano miongoni mwa waamini wote! Na hivyo, katika vizazi vyote, kweli za Mungu zilizo tamu kabisa zimekuwa milima iliyotutenganisha.
Kama twataka kuomba kwa nguvu, na kama twataka kutarajia Roho Mtakatifu ashuke kwa nguvu, na kama kweli twataka kwamba Mungu amwage Roho wake, ni lazima tuingie agano na Mungu kwamba tutapendana kwa upendo wa mbinguni.
Je, uko tayari kwa hilo? Ni ule tu upendo ulio wa kweli ulio mkubwa vya kutosha kuwapokea watoto wote wa Mungu, walio bila upendo na wasiopendeka kabisa, na wasiostahili, na wasiovumilika, na wanaosumbua. Kama nadhiri yangu—kujisalimisha kabisa kwa Mungu—ilikuwa ya kweli, basi ni lazima imaanishe kujisalimisha kabisa kwa upendo wa kimungu unijaze; kuwa mtumishi wa upendo nimpende kila mtoto wa Mungu aliye kandokando yangu. “Tunda la Roho ni upendo.”
Ah, Mungu alifanya jambo la ajabu alipompa Kristo, aliye mkono wake wa kuume, Roho Mtakatifu ashuke kutoka moyoni mwa Baba na upendo wake wa milele. Na jinsi tulivyomshusha Roho Mtakatifu hata kuwa nguvu tu ambayo kwayo yatupasa kuifanya kazi yetu! Mungu na atusamehe! Ah, laiti Roho Mtakatifu angeheshimiwa kama nguvu ya kutujaza uhai wenyewe na asili ya Mungu na ya Kristo!
Kazi ya Kikristo Yahitaji Upendo
“Tunda la Roho ni upendo.” Nauliza tena, Kwa nini ni hivyo? Na jibu huja: Hiyo ndiyo nguvu pekee ambayo kwayo Wakristo waweza kweli kuifanya kazi yao.
Naam, ndicho tunachokihitaji. Twataka si upendo tu wa kutufunga kila mmoja kwa mwenzake, bali twataka upendo wa kimungu katika kazi yetu kwa ajili ya waliopotea walio kandokando yetu. Ah, je, mara nyingi hatuchukui kazi nyingi, kama vile watu wachukuavyo kazi ya kutenda mema, kutokana na roho ya asili ya huruma kwa wenzetu wanadamu? Je, mara nyingi hatuchukui kazi ya Kikristo kwa sababu mchungaji wetu au rafiki yetu anatuita tuifanye? Na je, mara nyingi hatuifanyi kazi ya Kikristo kwa bidii fulani lakini bila kuwa tumepata ubatizo wa upendo?
Watu mara nyingi huuliza: “Ubatizo wa moto ni nini?”
Nimejibu zaidi ya mara moja: Sijui moto kama moto wa Mungu, moto wa upendo wa milele uliyoiteketeza dhabihu pale Kalvari. Ubatizo wa upendo ndio Kanisa liuhitajio, na ili kuupata ni lazima tuanze mara moja kusujudu nyuso zetu chini mbele za Mungu katika kuungama, na kusihi:
“Bwana, acha upendo kutoka Mbinguni utiririke chini ndani ya moyo wangu. Ninaitoa nafsi yangu niombe na niishi kama mtu aliyejitoa kwa ajili ya upendo wa milele ukae ndani yake na kumjaza.”
Ah, naam, kama upendo wa Mungu ungekuwako ndani ya mioyo yetu, ungeleta tofauti kama nini! Wako waamini mamia wasemao:
“Ninamfanyia Kristo kazi, nami nahisi ningeweza kufanya kazi kwa bidii zaidi, lakini sina kipawa. Sijui jinsi au wapi pa kuanza. Sijui niwezalo kufanya.”
Ndugu wa kiume, ndugu wa kike, mwombe Mungu akubatize kwa Roho wa upendo, na upendo utaipata njia yake. Upendo ni moto utakaoteketeza kila ugumu. Waweza kuwa mtu mwenye haya, asitasitaye, asiyeweza kunena vyema, lakini upendo waweza kuteketeza kila kitu. Mungu na atujaze upendo! Twauhitaji kwa ajili ya kazi yetu.
Umesoma hadithi nyingi zenye kugusa moyo za upendo uliodhihirishwa, nawe umesema, Nzuri kama nini! Nilisikia moja si muda mrefu uliopita. Mwanamke mmoja alikuwa ameombwa kuhutubu katika Nyumba ya Uokozi ambako kulikuwa na idadi ya wanawake maskini. Alipofika pale na kuufikia dirisha pamoja na mlezi, aliona nje kiumbe duni kikiwa kimeketi, akauliza:
“Yule ni nani?”
Mlezi akajibu: “Ameshaingia nyumbani mara thelathini au arobaini, na daima amekwenda zake tena. Hakuna liwezalo kufanywa naye, ni duni na mgumu hivyo.”
Lakini yule mwanamke akasema: “Ni lazima aingie ndani.”
Ndipo mlezi akasema: “Tumekuwa tukikungoja, na mkutano umekusanyika, nawe una saa moja tu kwa ajili ya hotuba.”
Yule mwanamke akajibu: “Hapana, hili ni la maana zaidi”; naye akaenda nje mahali yule mwanamke alipokuwa ameketi, akasema:
“Ndugu yangu, kuna nini?”
“Mimi si ndugu yako,” likawa jibu.
Ndipo yule mwanamke akaweka mkono wake juu yake, akasema: “Naam, mimi ni ndugu yako, nami nakupenda”; na hivyo akanena hata moyo wa yule mwanamke maskini ukaguswa.
Mazungumzo yalidumu kwa muda, na mkutano ulikuwa ukingoja kwa saburi. Hatimaye yule mwanamke akamleta yule mwanamke ndani ya chumba. Alikuwapo yule kiumbe maskini, duni, aliyedhalilika, aliyejaa aibu. Hakukubali kuketi juu ya kiti, bali aliketi juu ya kigoda kando ya kiti cha mnenaji, naye akamwacha aegemee kwake, huku mikono yake ikiuzunguka shingo ya yule mwanamke maskini, alipokuwa akiwanena watu waliokusanyika. Na upendo ule uligusa moyo wa yule mwanamke; alikuwa amempata mtu aliyempenda kweli kweli, na upendo ule ukatoa nafasi ya kuufikia upendo wa Yesu.
Msifuni Mungu! kuna upendo juu ya nchi ndani ya mioyo ya watoto wa Mungu; lakini ah, laiti kungekuwa na zaidi!
Ee Mungu, wabatize wachungaji wetu kwa upendo mwororo, na wamisionari wetu, na wasomaji wetu wa Biblia, na watumishi wetu, na vyama vyetu vya vijana wa kiume na vijana wa kike. Ah, laiti Mungu angeanza nasi sasa, na kutubatiza kwa upendo wa mbinguni!
Upendo Huchochea Maombezi
Tena mara nyingine. Ni upendo tu uwezao kutuandaa kwa ajili ya kazi ya maombezi.
Nimesema kwamba upendo ni lazima utuandae kwa ajili ya kazi yetu. Je, wajua ni kazi gani iliyo ngumu kuliko zote na ya maana kuliko zote ipasayo kufanywa kwa ajili ya ulimwengu huu wenye dhambi? Ni kazi ya maombezi, kazi ya kwenda kwa Mungu na kuchukua muda wa kumshika.
Mtu aweza kuwa Mkristo mwenye bidii, mchungaji mwenye bidii, na mtu aweza kutenda mema, lakini ole! mara ngapi hulazimika kuungama kwamba anajua kidogo tu maana ya kukaa na Mungu. Mungu na atupe kipawa kikuu cha roho ya maombezi, roho ya kuomba na kusihi! Na niwaombe kwa jina la Yesu msiache siku ipite bila kuwaombea watakatifu wote, na watu wote wa Mungu.
Naona wako Wakristo wanaolidharau hilo. Naona kuna vyama vya maombi ambako huwaombea wanachama, wala si waamini wote. Nawasihi, tumieni muda kuliombea Kanisa la Kristo. Ni haki kuwaombea wapagani, kama nilivyokwisha kusema. Mungu na atusaidie kuwaombea zaidi. Ni haki kuwaombea wamisionari na kazi ya uinjilisti, na wasioongoka. Lakini Paulo hakuwaambia watu wawaombee wapagani wala wasioongoka. Paulo aliwaambia wawaombee waamini. Fanyeni hili kuwa ombi lenu la kwanza kila siku: “Bwana, wabariki watakatifu wako kila mahali.”
Hali ya Kanisa la Kristo iko chini kwa kiasi kisichoelezeka. Waombeeni watu wa Mungu ili awajilie, ombeaneni kila mmoja na mwenzake, waombeeni waamini wote wanaojaribu kumfanyia Mungu kazi. Upendo na uujaze moyo wako. Mwombe Kristo aumimine upya ndani yako kila siku. Jaribu kuuingiza ndani yako kwa Roho Mtakatifu wa Mungu: Nimetengwa kwa ajili ya Roho Mtakatifu, na tunda la Roho ni upendo. Mungu na atusaidie kulielewa.
Mungu na ajalie kwamba tujifunze siku kwa siku kumngoja yeye kwa utulivu zaidi. Msimngoje Mungu kwa ajili yetu wenyewe tu, ama sivyo nguvu za kufanya hivyo zitapotea upesi; bali na tujitoe kwa huduma na upendo wa maombezi, na kuwaombea zaidi watu wa Mungu, watu wa Mungu walio kandokando yetu, roho ya upendo ndani yetu na ndani yao, na kazi ya Mungu tuliyoshikamana nayo; na jibu litakuja bila shaka, na kumngoja kwetu Mungu kutakuwa chemchemi ya baraka na nguvu zisizoelezeka. “Tunda la Roho ni upendo.”
Je, una upungufu wa upendo wa kuungama mbele za Mungu? Basi ungama na useme mbele zake, “Ee Bwana, upungufu wa moyo wangu, upungufu wa upendo wangu—naukiri.” Na kisha, uutupapo upungufu huo miguuni pake, amini kwamba damu yakutakasa, kwamba Yesu aja kwa nguvu zake zenye uweza, zitakasazo, ziokoazo ili kukuokoa, na kwamba atatoa Roho wake Mtakatifu.
“Tunda la Roho ni upendo.”