Njia ya Kuingia Patakatifu pa Patakatifu ·Moyo Uliothibitishwa

Sura 35 · dakika 10 za kusoma

Moyo Uliothibitishwa

"Ni vyema moyo uthibitishwe kwa neema; si kwa vyakula, ambavyo havikuwafaa wale walioshughulika navyo." WAEBRANIA 13:9.

NI jambo jema kuwa na moyo uliothibitishwa. Kwa wengi wetu, maisha ya ndani ni ya kigeugeu na yasiyo thabiti. Nyakati nyingine tunapata siku za bidii kuu ya kidini, ambapo yaonekana haiwezekani kutumia muda mrefu sana katika maombi na ushirika na Mungu. Hewa iko safi kiasi kwamba twaweza kuona ng'ambo ya maji ya bahari itugawanyayo, hata kufikia mistari ya mwambao wa mbinguni. Lakini jambo dogo sana laweza kuharibu amani yetu, na kuleta pazia la ukungu juu ya nafsi zetu, likitufunika labda kwa majuma marefu. Ee, laiti tungekuwa na moyo uliothibitishwa!

Sasa kuna jambo moja ambalo halitaleta hali hii ya baraka ya uthibitisho. Nalo laonyeshwa kwa neno lile, "vyakula"; ambalo lasimama badala ya taratibu za kimatambiko za sheria ya Kiyahudi. Siku zote kuna mwelekeo ndani ya moyo wa mwanadamu kuelekea dini ya matambiko. Ni rahisi zaidi sana kushika maagizo ya ibada ya nje kuliko kuikaza nafsi katika imani na upendo na ibada ya kiroho. Mpe mtu mcha-Mungu mzunguko wa utunzaji wa nje, haidhuru ni wa ukali na uchunguzi kiasi gani madai yako, nao wote utatekelezwa kwa wakati na kwa utumwa, pamoja na hisia ya siri ya kuridhika kwa kuruhusiwa kufanya jambo fulani kuelekea kupata kukubaliwa na kupendelewa na Mungu.

Kuna ongezeko kubwa la utunzaji wa kimatambiko miongoni mwetu. Twashuhudia kwa mshangao mwelekeo wa nyakati zetu kuelekea kupiga magoti; ukali wa kufunga wa Kwaresima; utunzaji wa makini wa ibada ndefu zisizokoma; na madai yote ya taratibu kali. Watu wasioonyesha ushahidi wowote katika tabia au mwenendo wao wa dini ya kweli ndio wenye uangalifu mkuu katika matambiko haya ya nje ya kidini. Vijana watatuliza dhamiri zao kwa siku ya kuvunja Sabato kwa ibada ya mapema. Katika visa vingi mambo haya ni ufufuo wa desturi za kale za Kibabeli, zilizoingia katika Kanisa lidaialo kuwa la Kristo katika siku zake mbaya na za giza zaidi za historia yake. Lakini ufufuo wao waonyesha shauku kuu za kidini za asili ya mwanadamu, na uvutano unaotolewa na matambiko ya nje badala ya hali halisi za ndani.

Lakini "vyakula" haviwezi kamwe kuuthibitisha uhai wa ndani. Hata mfuasi mwenye bidii zaidi wa matambiko sharti akiri hisia ya kutoridhika na kutotulia kwa ndani, kwa maana nafsi yahukumiwa kutembea daima jangwa kame la utaratibu wa kuchosha, ambako haifiki kwenye malisho ya majani mabichi wala maji ya pumziko. "Havikuwafaa wale walioshughulika navyo."

Kizuizi kingine kwa moyo uliothibitishwa chatokana na udadisi ambao daima hukimbilia mafundisho mbalimbali ya kigeni. Katika vizazi vyote vya Kanisa, watu wameshika vipengele pekee vya kweli, wakivipotosha kutoka katika upatano wa Injili, na kuvichukua hadi kufikia kupita kiasi kwa hatari; na mara kweli yoyote inapotazamwa nje ya nafasi yake katika mizani ya Injili, huwa uzushi, ikiziongoza nafsi katika upotovu kwa udanganyifu wa taa za uwongo ambazo watekaji wa meli hutikisa kando ya ufuo. Na mara tunapoanza kufuata mawazo na dhana za waalimu wa kibinadamu, mbali na fundisho la Roho wa Mungu, twaingia katika hali isiyotulia, yenye wasiwasi, ambayo ni kinyume kabisa cha moyo uliothibitishwa.

Kuna msingi mmoja tu usiotikisika kamwe, hali moja isiyobadilika kamwe. "Ni vyema moyo uthibitishwe kwa neema." Kwanza kabisa, bila shaka, moyo uliothibitishwa ni zawadi ya Mungu. "Yeye anayetuthibitisha sisi pamoja nanyi katika Kristo ni Mungu." "Bwana atakuthibitisha uwe taifa takatifu kwake mwenyewe." "Mungu wa neema yote na awakamilishe, awathibitishe, awatie nguvu, awaimarishe." Kwa hiyo twahitaji kumwomba yeye atupe moyo uliothibitishwa katika neema. Lakini kuna masharti fulani pia yaliyoonyeshwa katika muktadha huu ambayo yafaa tuyatii.

SHARTI TULE KRISTO. Kule kukanusha kwenyewe kwa mstari wa kumi kwathibitisha kwamba kuna madhabahu ambayo sisi tuna haki ya kula juu yake. Si Wayahudi peke yao, bali Wakristo pia, hukazia kula; lakini ah, jinsi kilivyo tofauti chakula kifanyacho mlo wao! Katika mfumo ule wa kale ambao Wakristo hawa Waebrania walikuwa wametoka humo, makuhani walikula sehemu kubwa ya dhabihu ambazo watu waliziletea juu ya madhabahu ya Mungu. Hii ilikuwa njia ya kujikimu kwao. Kwa kuwa walitengwa kabisa kwa ajili ya utumishi wa Mungu, na hawakuwa na urithi katika nchi, "waliishi kwa madhabahu." Lakini sisi, tulio makuhani kwa haki ya kiungu zaidi, tumeacha nyuma yetu Hema, pamoja na taratibu zake na dhabihu zake, na hatuwezi kula vyakula hivi vya nje bila kuisaliti hali ya kiroho ya dini takatifu tuidaiyo.

Madhabahu yetu ni msalaba. Dhabihu yetu ni Mwokozi anayekufa. Chakula chetu ni kuula mwili wake. "Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni, mtu akila katika hicho asife." "Chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu."

Kula huhusisha hatua tatu: kupokea, kutafuna, na kuyeyusha; na kila moja ya hizi ina mfano wake wa kiroho katika kule kula Kristo ambako ndiko uhai hasa wa uhai wetu. Sisi pia, sharti tumpokee, kwa kusoma kwa makini Neno la Mungu. Neno limo katika maneno. Maneno yake ni roho na uzima. Hatuhitaji kuwa tukiyasoma daima, kama vile tusivyopaswa kuwa tukila daima. Lakini kama vile mlo mzuri utakavyoendelea kutulisha muda mrefu baada ya kuula, naam hata tunapoacha kuufikiria, vivyo hivyo funzo refu la maombi la Neno la Mungu litazilisha nafsi zetu kwa muda mrefu baadaye.

Sisi pia, sharti tutimize hatua ya pili ya kula kwa kutafakari kwa muda mrefu na kwa fikira juu ya yote yaliyofunuliwa kwetu katika Neno kuhusu nafsi na kazi ya Bwana Yesu. Ni kwa kuiacha tu mioyo na akili zetu ikae ikitafakari juu ya mambo haya matakatifu ndipo yanapokuwa halisi kiasi cha kutulisha. Ni afadhali kusoma kidogo na kutafakari zaidi, kuliko kusoma sana na kutafakari kidogo.

Sisi pia sharti tumyeyushe Kristo ndani yetu, hata awe sehemu ya nafsi zetu hasa, nasi tuanze kuishi, lakini si sisi, kwa sababu Kristo aishi ndani yetu, naye amekuwa uhai wetu hasa. Bwana wetu aliwaambia wanafunzi wake kwamba aliishi kwa Baba; na akasema kwamba, kama wangetaka kuishi katika hali ile ile ya kumtegemea yeye, sharti "wamle yeye" (Yohana 6:57). Katika hali yake mwenyewe Kristo, kuwako kwake kulikuwa kumefikia kilele kikubwa cha muungano na Baba yake kiasi kwamba kumwona au kumsikia au kumjua yeye kulikuwa kumwona na kumsikia na kumjua Mungu. Na kama tungetumia tu muda zaidi peke yetu naye katika ushirika wa maombi na wa upendo, badiliko kubwa lingetupita sisi pia, nasi tungegeuzwa kuwa mfano wake katika hatua zifuatanazo za utukufu juu ya utukufu.

Kwa vipindi vya kawaida twakutana kuizunguka meza ya Bwana kula mkate na kunywa divai. Lakini kule kumla yeye kwapaswa kuwa mara kwa mara kama milo yetu ya kawaida ya kila siku.

Kwa nini tuilishe roho kwa uchache kuliko tuulishavyo mwili? Ole! jinsi tuutunzavyo huu kwa anasa, na kuiacha ile na njaa, hata tunapopita hisia ya kutamani! Twaharibu hamu yetu ya kula kwa kuilisha kwa peremende na vipande vitamu vya hisia. Twaridhika kuishi kama vimelea juu ya maji-maji ya wengine, badala ya kupata lishe moja kwa moja sisi wenyewe. Ni ajabu gani basi kwamba twachukuliwa huku na huku na kila upepo wa mafundisho, na kupungukiwa na moyo uliothibitishwa? Na labda hakungekuwa na jambo bora zaidi kwa sisi sote watu wa Kikristo kuliko ufufuo wa funzo la Biblia, wakfu mpya wa saa ya asubuhi, na utunzaji wa kawaida na wa mpangilio wa nyakati za ushirika mrefu na Bwana na Mkuu wetu.

KAMA TUNGETAKA KULA KRISTO, SHARTI TUENDE NJE YA KAMBI. Katika taratibu takatifu za Siku kuu ya Upatanisho iliamriwa kwamba miili ya wanyama wote waliopatwa na mauti kama sadaka za dhambi, na ambao damu yao ilikuwa imenyunyizwa mbele ya kiti cha rehema, ichomwe moto Nje ya kambi (Mambo ya Walawi 16:27). Na katika ubainisho huu wa ajabu, kweli mbili yamkini zilifananishwa: kwanza, kwamba katika utimilifu wa wakati, Yesu, sadaka ya kweli ya dhambi ya ulimwengu, angeteseka nje ya lango la mji; na pili, kwamba watu sharti waziache nyuma kanuni na matambiko ya mifumo ya kidunia, kama wangetaka kuutambua baraka wote wa kukubaliwa na Mungu kwa njia ya dhabihu ya Kristo.

Basi, kama tungetaka kumpata Yesu kuwa chakula chetu, furaha yetu, uhai wetu, hatupaswi kutarajia kumpata katika kambi zilizopigwa na watu wa ulimwengu huu. Sharti tutoke kutoka katika kambi zote kama hizo; kutoka katika kambi ya udini wa ulimwengu vilevile kama kutoka katika ile ya ufisadi wake; kutoka katika mahema ya utaratibu wake na utambiko wake, vilevile kama kutoka katika yale ya ubatili wake.

Sera ya kutoka nje ya kambi ndiyo njia pekee salama kwetu sisi wenyewe, kama vile ilivyo njia pekee yenye msaada kwa ulimwengu wenyewe. Wako wengi wanaobisha kwamba sera yenye hekima zaidi ni kubaki ndani ya kambi, wakitafuta kuinua maadili yake. Hawatambui kwamba, kama tukiifuata shauri yao, sharti tubaki humo peke yetu; kwa maana Bwana wetu tayari ameondoka. Bila shaka haifai kwamba tupate makao mahali ambapo yeye ametupwa nje. Kuna nini ndani yetu kinachotufanya tukaribishwe hivyo, hali Bwana wetu alitupwa nje kwa hukumu ya wahalifu walio wa chini kabisa? Zaidi ya hayo, haitachukua muda mrefu kabla hatujagundua kwamba, badala ya sisi kuiathiri kambi kwa wema, hewa ya kambi itatuambukiza kwa uovu wake. Badala ya sisi kuinua, itatushusha.

Kanuni pekee ya kuusogeza ulimwengu ni kumwiga Arkimede katika kupata mahali pa kusimama nje yake. Watu wote walioacha alama katika kuinua nyakati zao wamelazimika kujiunga na jeshi la wasafiri liendelealo daima kupita katika malango ya mji, na kuchukua msimamo wao kando ya msalaba ambao Yesu alikufa juu yake. Tukitazama nyuma mahali pale pa kukumbukwa, twaonekana kupaona pakiwa na wingi wa mitume, wafia-dini, wanamatengenezo, na manabii wa kila kizazi, wanaotualika tujiunge nao. Yabaki kwetu kusema kama tutakawia katikati ya anasa na uvutano vinavyotushawishi kuelekea kambini; au kama tutathubutu kuuchukua msalaba wetu, na kumfuata Bwana wetu kando ya Via Dolorosa, tukiuchukua ushutumu wake. Ah, mioyo michanga, wanafunzi wa siri, mnaosita-sita kati ya maoni mawili, tokeo la uchaguzi kama huo haliwezi kuwa na shaka! Kwa kilio, Deus vult, mtajiunga na vita hivi vitakatifu vya msalaba, na kuchukua msimamo wenu pamoja na Yesu, mahali pa kukutania pa msalaba wake.

KAMA TUKIENDA NJE YA KAMBI, SHARTI TUUCHUKUE USHUTUMU WAKE. Yasimuliwa juu ya Charles Simeon mwema, wa Cambridge, kwamba, mwanzoni mwa kazi yake kama mchungaji wa kiinjili huko Cambridge, alikutana na matukano na upinzani mkali kiasi kwamba roho yake ilionekana kuwa karibu kuvunjwa. Akiligeukia Neno la Mungu kwa mwongozo na kitia-moyo, jicho lake lilitua juu ya fungu lifuatalo: "Nao walipokuwa wakitoka, wakamwona mtu wa Kirene, jina lake Simoni; huyo wakamlazimisha auchukue msalaba wake." Kufanana kwa jina na lake mwenyewe kulimshtua, naye alichochewa kupata ujasiri mpya kwa wazo la umoja wake na mateso ya Yesu. Ndivyo ilivyo kwetu sote. Kama tukitukanwa kwa ajili ya jina la Yesu, heri sisi; nasi twapaswa kufurahi, kwa kadiri tulivyo washiriki wa mateso ya Kristo, ili kwamba, utukufu wake utakapofunuliwa, sisi pia tupate kufurahi kwa furaha kuu mno.

Ni jambo la ajabu kama nini kujifunza ukaribu wa vifungo ambavyo kwavyo twafungwa na watakatifu wa zamani! Tunapotukanwa kwa kuwa Wakristo, twajua kidogo kile alichohisi Musa alipodhihakiwa katika jumba la kifalme la Misri kwa asili yake ya Kiebrania; lakini "aliuhesabu ushutumu wa Kristo kuwa utajiri mkuu kuliko hazina zote za Misri, kwa maana aliyaelekeza macho yake kwenye thawabu."

LAKINI TUKIWA TWAUCHUKUA USHUTUMU WA KRISTO, TUTAUPATA MJI PEKEE UDUMUO. Ni jambo la kushangaza sana kwamba, tunapojing'oa kutoka katika lango la mji, na kuaga kile kilichoonekana kuwa ishara ya majengo yenye kudumu zaidi ya udumu wa kidunia, kwa kweli twatoka nje ya mambo yapitayo na yasiyo halisi ili kuwa raia wa Mji pekee udumuo na uendeleao.

Miji mikubwa zaidi ya ukuu wa kibinadamu haikudumu. Babeli, Ninawi, Thebesi, miji yenye nguvu ya Meksiko-yote imepita. Imezikwa katika vilima, ambavyo juu yake majani hukua kwa wingi; hali wanyama wa mwituni hutambaa kupitia mabaki yanayooza ya wakati uliopita. Lakini, katikati ya yote, wainuka kizazi hadi kizazi jengo la kudumu, Mji uendeleao, muungano ukusanyikao kumzunguka Mwokozi asiyebadilika, wala haujawa na kipengele chochote cha kuoza. Je, twaishi kiasi cha kutosha katika Mji huu katika uzoefu wetu wa kawaida? Yawezekana kuzikanyaga barabara zake za dhahabu tunapoendelea kwa taabu katika njia kuu za miji mikubwa ya dunia; kuchangamana katika makundi yake ya baraka, na kushiriki mazoezi yake matakatifu, ingawa kwa kuonekana twatumia siku zetu katika ofisi za mji zenye giza, na katikati ya wenzetu wapendao fedha. Msafiri wa kweli aendaye Mjini kwa kweli aishi Mjini. Haitachukua muda mrefu, nao hautakuwa tu shabaha ya imani na maono ya kiroho, utadhihirika. Tazama, waja! waja! Mji mtakatifu ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukimetameta kwa nuru yake, ukilia kwa wimbo, makao ya watakatifu, mji mkuu wa dunia iliyokombolewa, Bibi-arusi wa Mwana-Kondoo, ambaye kwa ajili yake ulimwengu ulifanywa.

Yaliyomo

Njia ya Kuingia Patakatifu pa Patakatifu F. B. Meyer

Ukurasa 1 / 1 · 10 dakika zimebaki katika sura