Hata Ajapo
Kuzimia na Kuhuishwa Miguuni pa Kristo

Sura 22 · dakika 15 za kusoma

Kuzimia na Kuhuishwa Miguuni pa Kristo

HOTUBA ILIYOTOLEWA MWISHONI MWA MMOJAWAPO WA MIKUTANO YA CHUO CHA WACHUNGAJI. “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu akiniambia, Usiogope; mimi ni wa kwanza na wa mwisho; mimi ni yeye aliye hai, nami nalikuwa nimekufa; na tazama, ni hai hata milele na milele, Amina; nami ninazo funguo za kuzimu na za mauti.”—Ufunuo 1:17, 18.

KUZIMIA NA KUHUISHWA MIGUUNI PA KRISTO.

SASA hatuna la kulifikiri ila Bwana wetu. Twamjia yeye ili atusaidie kuwasahau wengine wote. Hatupo hapa kama wahudumu, tuliolemewa na huduma nyingi, bali sasa twaketi miguuni pake pamoja na Mariamu, au twaegemea kifuani pake pamoja na Yohana. Bwana mwenyewe atupa neno letu la siri tunapoukusanya msafara wetu kwa kusanyiko la mwisho. “Nikumbukeni” ndilo agizo lake la upendo. Twamsihi aijaze kumbukumbu yetu yote kama vile jua lijazavyo mbingu na nchi kwa nuru. Imetupasa kumfikiri Yesu peke yake, naye peke yake ndiye nitakayemnena. Laiti tungeguswa na kaa la moto litokalo kwake yeye aliye Madhabahu yetu na pia Dhabihu yetu!

Andiko langu lapatikana katika maneno ya Yohana, katika sura ya kwanza ya Ufunuo, mstari wa kumi na saba na wa kumi na nane:—

“Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akiniambia, Usiogope; mimi ni wa kwanza na wa mwisho; mimi ni yeye aliye hai, nami nalikuwa nimekufa; na tazama, ni hai hata milele na milele, Amina; nami ninazo funguo za kuzimu na za mauti.”

Yohana alikuwa, kuliko watu wote, aliyefahamiana zaidi na Yesu, wala Bwana wake hakuhitaji kamwe kumwambia, “Wanipenda mimi?” Nadhani, kama kungekuwa na mtu ye yote awezaye kusimama wima mbele za Mwokozi aliyetukuzwa, angekuwa yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda. Upendo huturuhusu kujichukulia uhuru mkubwa: mtoto atapanda goti la baba yake wa kifalme, wala hakuna mtu amshtakiye kwa ujuvi. Yohana alikuwa na upendo wa namna hiyo, na hata hivyo hata yeye hakuweza kuutazama uso wa Bwana wa utukufu bila kulemewa na hofu ya kicho. Angali mwilini, hata Yohana lazima azimie akijaliwa kupewa maono ya kabla ya wakati ya yule Mpendwa katika enzi yake. Tukiruhusiwa kumwona Bwana kabla ya miili yetu kufanyiwa mabadiliko yale ya ajabu ambayo kwayo twafanywa kama Yesu ili tumwone kama alivyo, tutaona kwamba maono hayo ni makuu kuliko tuwezavyo kuyastahimili. Kuuona wazi utukufu wa mbinguni wa Bwana wetu tungali hapa duniani hakungefaa, kwa maana isingetufaa sisi kulala daima tumezimia miguuni pa Mkombozi wetu, hali kuna kazi nyingi sana tunayopaswa kuifanya.

Niruhusuni, ndugu wapenzi, kulitoa andiko langu katika muktadha wake, na kulitumia kwetu sisi wenyewe, kwa kulishusha kutoka kile kiti cha enzi kule juu hata mezani hapa. Yamkini, nami nataraji itakuwa hivyo, kwamba tumwonapo Yesu hata hapa, tutaanguka pamoja na Yohana miguuni pake kama waliokufa. Hatutazimia, bali tutakufa kwa maana nyingine, kifo kitamu mno, hali uhai wetu umefichwa ndani yake. Baada ya kuyatafakari hayo, tutafikia yale andiko langu liyadokezayo: ndipo, na tuhuishwe pamoja na Yohana, kwa maana kama asingehuishwa asingaliweza kamwe kutuambia habari za kuzimia kwake. Hivyo tutakuwa na kifo pamoja na Kristo, na ufufuo ndani yake. Laiti tungepata kuonja kwa kina mambo yote mawili, kwa nguvu za Roho Mtakatifu!

I. Tukiruhusiwa kumwona Kristo katika kumbukumbu zile rahisi na zenye kufundisha zilizo sasa juu ya meza, tutaanguka, kwa maana iliyobarikiwa, miguuni pake kama waliokufa.

Kwa maana, kwanza, hapa twaona maandalizi ya kuondolewa kwa dhambi zetu, na hivyo twakumbushwa juu yake. Hapa kuna mkate uliomegwa kwa sababu tumeivunja sheria ya Mungu, nasi tungalivunjwa milele kama asingekuwapo Mwokozi aliyejeruhiwa. Katika divai hii twaona ishara ya damu ambayo kwayo lazima tusafishwe, ama sivyo tuwe vitu vichafu vya kutupwa katika moto wa Tofethi, kwa sababu ni chukizo machoni pa Mungu. Kwa kuwa tuna mbele yetu kumbukumbu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi, yatukumbusha kifo chetu katika dhambi ambamo tungalidumu hata sasa kama isingekuwa ile neema iliyotunena tukaingia katika uzima na wokovu. Je, wazidi kuwa mkuu? Kuwa mdogo tena utakapoona kwamba wewe si kitu ila mtumwa aliyekombolewa. “Wahuru wa Bwana” ndiyo cheo chako halisi bado. Je, waanza kufikiri kwamba, kwa kuwa umetakaswa, huhitaji sana kusafishwa kila siku? Sikia neno lile, “Tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi,” na hata hapo “damu yake Yesu Kristo, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.” Twatenda dhambi hata tukiwa katika ushirika ulio wa juu kabisa na wa kimungu zaidi, nasi bado twaihitaji ile damu isafishayo. Jinsi hili litunyenyekezavyo mbele za Bwana! Imetupasa kuwa washindaji wa wenye dhambi, na hata hivyo sisi wenyewe tungali wenye dhambi, tukiuhitaji Mkate wa uzima kwa kweli kama vile wale tuwahudumiao.

Ah! na baadhi yetu tumekuwa wenye dhambi wa pekee sana; na kwa hiyo, kama twapenda sana, ni kwa sababu tumesamehewa mengi. Tumekosa tangu tulipomjua Mwokozi, na hiyo ni aina ya udhambi iliyo na uchungu mwingi mno; tumetenda dhambi tangu tulipoingia katika hali ya juu kabisa ya furaha ya kiroho, na kuwa pamoja naye juu ya mlima mtakatifu, na kuutazama utukufu wake! Hili huzaa haya takatifu. Twaweza kabisa kuanguka miguuni pa Yesu, ijapokuwa hujidhihirisha kwetu katika mkate na divai tu, kwa maana hivi hutuletea hisia ya udhambi wetu, hali vikitukumbusha jinsi Bwana wetu alivyoikabili dhambi yetu, akaiondoa.

Humu twaanguka chini kabisa kama waliokufa. Kiko wapi kile “Mimi”? Kuko wapi kujitukuza? Je, umebakiwa na cho chote mbele za Mwokozi aliyesulubiwa? Uilapo mwili wake na kuinywa damu yake kwa roho, je, waweza kujisifu katika mwili wako mwenyewe, au kuhisi kiburi cha damu na uzazi? Ole wetu kama pana chembe ya kiburi ichanganyikayo na huduma yetu, au doa la kujisifu pamoja na mafanikio yetu! Tumwonapo Yesu, Mwokozi wetu, Mwokozi wa wenye dhambi, hakika nafsi itazama, na unyenyekevu utaanguka miguuni pake. Tufikiripo Gethsemane na Kalvari, na maumivu yote na dhiki ya Mkombozi wetu mkuu, hakika, kwa Roho Mtakatifu, kujitukuza, kujitafutia, na kujitakia lazima kuanguke kama kwaliochinjwa kwa jeraha la mauti. “Nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa.”

Hapa, tena, twajifunza somo la pili. Yesu ameweka chakula juu ya meza hii. Mkate wadhihirisha yote yaliyo ya lazima, na kikombe yote yaliyo ya anasa: maandalizi kwa mahitaji yetu yote na kwa tamaa zetu zote zilizo halali, yote tuyahitajiyo kwa riziki na furaha. Basi, mimi ni nafsi maskini kama nini nisiyeweza hata kujipatia mkate! Kwa habari za faraja, sipaswi hata kuzifikiri; lazima nipewe ama sivyo sitaonja kamwe. Ndugu, sisi ni watu wa kawaida wategemeao ukarimu wa Jamaa yetu mkuu: twaijia meza yake kwa ajili ya matunzo yetu, hatuna miliki zetu wenyewe. Yeye awalishaye shomoro huzilisha nafsi zetu; katika mambo ya kiroho, sisi hatukusanyi ghalani kuliko hao ndege waliobarikiwa; Baba yetu wa mbinguni hutulisha kutoka katika ule “utimilifu wote” ambao amependezwa kutuwekea akiba katika Yesu. Tusingeweza kuishi hata saa moja kiroho pasipo yeye aliye si mkate tu, bali uzima; si divai ifurahishayo tu, bali faraja yenyewe. Uhai wetu wategemea Yesu; yeye ni Kichwa chetu na pia chakula chetu. Kamwe hatutaukua na kuuacha uhitaji wetu wa mkate wa asili, na kiroho kamwe hatutainuka juu ya uhitaji wetu wa Kristo aliyepo, bali zaidi tutahisi shauku iliyo kali zaidi na tamaa ya haraka zaidi kwake. Mtazame yule mtu mwenye ubatili kule. Ahisi ya kuwa yeye ni mtu mkuu, nawe wakiri kwamba yeye akuzidi wewe katika vipawa; lakini ni mdanganyifu kama nini, kiumbe mpumbavu kama nini kuota kwamba yeye ni mtu wa maana! Sasa ataonekana kuwa apungukiwa; kwa maana, kama sisi wenyewe, hatoshi hata kuwaza neno lo lote juu ya nafsi yake. Mwombaji ampasaye kuishi kwa sadaka, kula mkate wa kutegemea wengine, kupokea kikombe cha hisani,—ana la kujisifia nini? Yeye ndiye yule Mkuu atulishaye, atupaye yote tuyafurahiayo, aliye yote kwa yote kwetu; na kwa habari zetu sisi, sisi ni waombaji,—nakaribia kusema, wateja wa hisani,—jamii ya Ndugu Waombaji, tuliokufa kwa mali yote ya kiroho ya nafsi kama walivyokufa waliouawa huko Marathoni. Yule mtumwa mweusi angeweza angalao kudai pumzi yake mwenyewe, lakini sisi hatuwezi kudai hata hiyo. Roho wa Mungu lazima atupe pumzi ya kiroho, ama sivyo uhai wetu utakoma. Tufikiripo hili, hakika kumwona Kristo katika mkate huu na Divai hii, ijapokuwa ni maono hafifu yakilinganishwa na yale yaliyoiteka nyara moyo wa Yohana, kutatufanya tuanguke miguuni pa Mkombozi kama waliokufa.

Kile “Mimi” hakiwezi kuishi, kwa maana Bwana wetu hakuandaa chakula cho chote kwa ajili ya ule Ubinafsi wa ubatili, na ubwana wake. Ameandaa vyote kwa ajili ya haja, lakini hakuna kitu kwa ajili ya kujisifu. Ee, hisia iliyobarikiwa ya kujiangamiza nafsi! Tumeionja mara kadhaa juma hili walipotusomea ndugu zetu baadhi ya zile karatasi; na, zaidi ya hayo, tulinyauka kabisa katika mwako wa ile furaha ambayo Bwana wetu alitujalia. Nataraji kusanyiko hili lenye furaha na mazoezi yake ya mbinguni yameuyeyusha ule Ubinafsi ndani yetu, na kuufanya, kwa kitambo, utiririke kwa machozi. Kufa kwa nafsi ni hisia iliyobarikiwa. Na tuitambue sisi sote! Tunapokuwa dhaifu kabisa katika kifo cha nafsi tunachokitambua, ndipo tuko na nguvu hata utimilifu wa uweza. Tukizimia hata kufa kwa nafsi, na kupoteza utambuzi wote wa uwezo binafsi, twaingizwa katika kile kisicho na mwisho, na twaishi ndani ya Mungu.

II. Sasa na tutafakari jinsi tupatavyo uhai tena, na hivyo kumjua Bwana kuwa ndiye ufufuo na uzima. Yohana alihuishwa kweli, naye atuambia jinsi ilivyotokea. Asema juu ya yule Mbarikiwa Milele,—“Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akiniambia, Usiogope; mimi ni wa kwanza na wa mwisho; mimi ni yeye aliye hai, nami nalikuwa nimekufa; na tazama, ni hai hata milele na milele, Amina; nami ninazo funguo za kuzimu na za mauti.”

Mafuriko yote ya uhai wa nafsi zetu yatatiririka kwa nguvu mpya kama, kwanza kabisa, tukiletwa katika kugusana na Yesu: “Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu.” Uvumilivu wa ajabu kwamba hauweki mguu wake juu yetu, na kutukanyaga kama matope ya njiani! Nimelala miguuni pake kama aliyekufa, na kama angenidharau kuwa nimechafuliwa kwa uozo, nisingeweza kuipinga haki yake. Lakini hapa hakuna neno lo lote juu ya mguu wake! Mguu huo umetobolewa kwa ajili yetu, wala haiwezekani kwamba mguu ambao umekaziwa misumari msalabani kwa ajili ya watu wake ungewakanyaga wakati wo wote katika ghadhabu yake. Sikia maneno haya, “Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu.” Mkono wa kuume wa nguvu zake na wa utukufu wake auweka juu ya mtumishi wake aliyezimia. Ulikuwa mkono wa mwanadamu. Ni mkono wa kuume wa yule ambaye, katika dhiki zetu zote, aliteswa, aliye Ndugu aliyezaliwa kwa ajili ya taabu. Kwa hiyo, kila kitu juu ya mkono wake kina nguvu ya kuhuisha. Maneno ya huruma, ndugu zangu, mara nyingi hayana matendo, na kwa hiyo ni dhaifu mno kumhuisha aliyezimia; kugusa kwa huruma kwafaa zaidi sana. Mnaikumbuka ile hadithi ya kufurahisha ya yule mtoto mweusi wa porini ambaye hakuweza kupatikana kamwe hata yule bibi mdogo alipoketi karibu naye, na kuuweka mkono wake juu yake. Eva alimshinda Topsy maskini kwa kugusa huko kwa upole. Ulimi ulishindwa, lakini mkono ndio uliopata ushindi. Ndivyo ilivyokuwa kwa Bwana wetu apendezaye. Alituonyesha kwamba yeye ni mfupa wa mifupa yetu na nyama ya nyama yetu; alijileta katika kugusana nasi, akatufanya tuutambue uhalisi wa upendo wake kwetu, ndipo akawa mshindi mkuu juu yetu.

Hivyo, tulihisi kwamba yeye si jambo la kubuni, bali ni Kristo halisi, kwa maana mkono wake ulikuwapo, nasi tuliuhisi ule mkazo wa upole. Kuwekwa kwa mkono wa kuume wa Bwana kumeleta uponyaji kwa wagonjwa, kuona kwa vipofu, na hata uhai kwa waliokufa, wala si jambo geni kwamba kungemrudisha mwanafunzi aliyezimia. Na muhisi ninyi nyote wakati huu huu katika nguvu yake yote ihuishayo! Na kutiririke kutoka katika mkono wa kuume wa Bwana, si huruma yake tu, kwa sababu ni mwanadamu kama sisi, bali kadiri ya nguvu za uungu wake kadiri ziwezavyo kuingizwa katika mwanadamu, ili tujazwe utimilifu wote wa Mungu! Hilo lawezekana wakati huu hasa. Meza ya Bwana yawakilisha kutolewa kwa mwili mzima wa Kristo kwetu, ili uingie ndani yetu kuwa chakula; hakika, tukiingia katika maana yake ya kweli, twaweza kutumaini kuhuishwa na kupewa uhai; kwa maana hapa tuna zaidi ya kuguswa tu na mkono, ni Kristo mzima aingiaye ndani yetu kiroho, na hivyo aja katika kugusana na utu wetu wa ndani kabisa. Naamini “uwepo halisi”: je, wewe huamini? Uwepo wa kimwili ni jambo jingine: huo hata hatuutamani. Bwana Yesu, uje katika kugusana kwa mikono mingi nasi sasa kwa kukaa ndani yetu, na sisi ndani yako!

Lakini, kulikuwa na kitu kingine kilichohitajika, kwa maana Bwana wetu Yesu, baada ya kugusa, alitoa lile neno: “Usiogope; mimi ni wa kwanza na wa mwisho.” Asema nini? Je, asema, “Wewe ndiwe”? Fungueni Agano zenu, mkaone. Je, apaza sauti, “Usiogope; wewe ndiwe mwanafunzi mpendwa, Yohana mtume na mwanateolojia”? Sipati kitu cha namna hiyo. Hakumwelekeza mtumishi wake ajitazame mwenyewe, bali amkumbuke yule Mimi Niko mkuu, Mwokozi wake, na Bwana. Faraja ya uzima ya kila mtoto wa Mungu aliyezimia, ya kila mtu atambuaye jeraha la mauti kwa kile “Mimi” cha asili, iko katika kile “Mimi” chenye enzi, ambaye yeye peke yake aweza kusema “Mimi Niko.” Waishi kwa sababu yuko “Mimi Niko” aliye na uzima ndani yake mwenyewe, naye anao uzima huo kwa ajili yako.

“Mimi ni wa kwanza.” “Nimekutangulia, na kuitengeneza njia yako; nilikupenda kabla hujanipenda mimi; niliuamuru mwendo wako wote wa maisha kabla hujakuwako. Katika kila kazi ya neema kwa ajili yako na ndani yako, mimi ni wa kwanza. Kama umande utokao kwa Bwana, sikumngoja mtu, wala sikukawia kwa ajili ya wanadamu. Nami pia ni wa mwisho, nikikamilisha yale yakuhusuyo, na kukuhifadhi hata mwisho. Mimi ni Alfa na Omega kwako, na herufi zote zilizo katikati; nilianza nawe, nami nitaisha nawe, kama mwisho waweza kuwaziwa. Naenenda mbele ya jeshi, nami nauleta mkia nyuma. Kuhifadhiwa kwako mwisho kwatoka kwangu kama vile mwanzo wako uliojaa tumaini.” Ndugu, je, hofu yainuka juu ya saa ile ya giza itishayo kufika karibuni? Ni saa gani hiyo? Yesu ajua, naye atakuwa nawe usiku kucha, hata kutakapopambazuka. Kama Yesu ndiye mwanzo na mwisho kwetu, kuna nini kingine? Tunacho cha kuogopa nini isipokuwa vile vitu vichafu vya kutobuni kwa kutoamini kwetu, vile vipuuzi vya uovu vijifanyavyo kuwa kutokuamini, na mashaka, na mawazo yasiyo ya wema? Kristo hufunga nje kila kitu kiwezacho kutudhuru, kwa maana afunika wakati wote, na nafasi yote; yuko juu ya vilele, na chini ya vilindi; na kila mahali yeye ni Upendo.

Endelea kusoma,—“Mimi ni yeye aliye hai.” “Kwa sababu mimi ni hai, ninyi nao mtakuwa hai; hakuna mauti ya kweli itakayokupata, kwa maana mauti haina tena mamlaka juu yangu,—Kichwa chako, Uzima wako.” Maadamu yuko Kristo aliye hai mbinguni, hakuna mwamini atakayeiona mauti kamwe: atalala usingizi katika Yesu, na ndiyo yote, kwa maana hata hapo atakuwa “pamoja na Bwana milele.”

Endelea kusoma,—“nami nalikuwa nimekufa.” “Kwa hiyo, ujapokufa, hutashuka chini kuliko nilikoshuka mimi; nawe utainuliwa tena kama vile mimi nilivyorudi kutoka kaburini.” Mfikirie Yesu kuwa amepita katika ufalme wa uvuli wa mauti, nawe hutaogopa kufuata katika nyayo zake. Viungo vinavyokufa vipumzike wapi ila juu ya kitanda kile kile pamoja na Kichwa chao kilichokufa zamani?

“Na tazama, ni hai hata milele na milele.” Naam, itazame, wala usiache kamwe kuitazama: twamtumikia Bwana aliye hai milele. Ndugu, rudini nyumbani kutoka mkutano huu katika nguvu za usemi huu mtukufu! Mtoto mpendwa aweza kuugua, au mke mpenzi aweza kuchukuliwa nyumbani; lakini Kristo asema, “Ni hai hata milele na milele.” Moyo uaminio hauwezi kamwe kuwa mjane, kwa maana Mume wake ni Mungu aliye hai. Bwana wetu Yesu hatatuacha yatima, atakuja kwetu. Basi hii ndiyo furaha yetu: si ndani yetu wenyewe, bali katika ukweli kwamba yu hai daima ili kutimiza mapenzi mema ya Baba ndani yetu na kwa ajili yetu. Songeni mbele, askari wa msalaba, kwa maana Kiongozi wetu asiyekufa aongoza njia.

Soma tena mara moja zaidi,—“nami ninazo funguo za kuzimu na za mauti.” Nilipoyatafakari maneno haya, nilistaajabia umaskini na unyonge wa habari za uovu; kwa maana mkuu wake, ibilisi, hana funguo za nyumba yake mwenyewe; hawezi kuaminiwa nazo; zinaning’inia mshipini mwa Kristo. Hakika mimi sitakwenda kuzimu kamwe, kwa maana Bwana wangu Yesu aliufunga ufunguo dhidi ya kuingia kwangu tangu zamani. Milango ya kuzimu ilifungwa kwa ajili yangu alipokufa kwa niaba yangu. Nilimwona akiufunga mlango, na, zaidi ya hayo, nilimwona akining’iniza ufunguo mshipini mwake, nao uko hapo hata leo. Kristo anazo funguo za kuzimu; basi, wakati wo wote apendapo, aweza kumfunga kizimbani yule simba alaye, na kuizuia nguvu yake ya uovu. Ee, laiti siku ile ingekuja! Inakuja, kwa maana yule joka ana ghadhabu kuu, akijua ya kuwa wakati wake ni mfupi. Tusiende peke yetu kupigana na adui huyu wa kutisha; na tumwambie Mshindi wake habari zake, na kumsihi aifupishe mnyororo wake. Nayapenda maneno yenye nguvu ya mwanamke aliyekuwa akifa aliyoyasema kwa mtu aliyemwuliza afanyalo alipojaribiwa na ibilisi kwa sababu ya dhambi yake. Alijibu, “Ibilisi hanijaribu sasa; alinijia kitambo kidogo kilichopita, wala hanipendi vya kutosha hata aje tena!” “Kwa nini?” “Naam, aliondoka kwa sababu nilimwambia, Teule, teule!” “Ulimaanisha nini kwa hilo?” “Je, hukumbuki jinsi ilivyosemwa katika Maandiko, ‘Bwana na akukemee, Ee Shetani; naam, Bwana aliyeuchagua Yerusalemu na akukemee’?” Andiko la yule mwanamke mzee lilifaa vema, naye adui alijua vema ule ukemeo uliomo ndani yake. Yoshua, kuhani mkuu, alipovaa mavazi machafu, akasimama mbele ya malaika, Shetani alisimama mkono wake wa kuume ili kumpinga, lakini alinyamazishwa kwa kuambiwa juu ya uteule wa Mungu: “Bwana aliyeuchagua Yerusalemu na akukemee.” Ah, ndugu, mkono wa kuume wa Kristo ukiwa juu yetu, yule mwovu huondoka! Ajua vema mno uzito wa mkono huo wa kuume.

Umalize mstari,—“na za mauti.” Bwana wetu anazo funguo za mauti, na hili litakuwa jambo la furaha kwetu saa zetu za mwisho zitakapofika. Tukimwambia, “Bwana, naenda wapi?” ajibu, “Ninazo funguo za mauti na za ulimwengu wa roho. Je, hatutajibu, “Twajihisi na uhakika kabisa kwenda po pote utakapotuongoza, Ee Bwana”? Ndipo tutafuata nyayo zake tukiwa pamoja naye. Miili yetu itashuka katika kile watu wakiitacho nyumba ya mifupa, ingawa kwa kweli ni chumba cha kuvua mavazi cha watakatifu, ukumbi wa mbinguni, kabati la mavazi yetu ambako yatasafishwa na kukamilishwa. Tuna mavazi ya kiroho yanayofaa kwa kipindi hicho cha kati, lakini twatazamia kwamba miili yetu itafufuka tena kwa mfano wa “Bwana atokaye mbinguni.” Tutakuwa wapataji kama nini tutakapoyachukua tena yale mavazi tuliyoyavua, na kuyakuta yamebadilishwa kwa utukufu mwingi, na kufanywa yatufaa kuyavaa hata mbele za Bwana wetu! Basi, kama hofu iliyo mbaya zaidi ikupatayo ingetimia, nawe ukafa kihalisi miguuni pa Bwana wako, hakuna sababu ya kuogopa, kwa maana hakuna adui awezaye kukudhuru, kwa kuwa ule mkono wa kuume wa kimungu umeahidiwa kukuokoa hata mwisho. Na tumpe yule Mpendwa sifa iliyo ya ibada na yenye juhudi zaidi tunaposhiriki sasa karamu hii ya kifalme. Mfalme aketi mezani pake, na nardo yetu itoe harufu yake iliyo tamu zaidi.

Ukurasa 1 / 1 · 15 dakika zimebaki katika sura