Sura 15 · dakika 14 za kusoma
Yesu Amelala Usingizi juu ya Mto
Yesu Amelala Usingizi juu ya Mto
BWANA wetu aliwachukua wanafunzi wake pamoja naye ndani ya mashua ili awafundishe somo la vitendo. Ni jambo moja kuzungumza na watu juu ya kuwa kwetu kitu kimoja nao, na juu ya jinsi wanavyopaswa kutumia imani wakati wa hatari, na juu ya usalama wao halisi katikati ya hatari inayoonekana; lakini ni jambo lingine, na lililo bora zaidi, kuingia ndani ya mashua pamoja nao, kuwaacha wasikie hofu yote ya dhoruba, kisha kuinuka, na kuukemea upepo, na kuiambia bahari, “Nyamaza, utulie.” Bwana wetu aliwapa wanafunzi wake somo la aina ya chekechea, mahubiri yaliyotendeka, ambamo kweli iliwekwa wazi mbele yao waione. Mafundisho kama hayo yalileta matokeo ya ajabu katika maisha yao. Na sisi pia na tufundishwe nayo!
Katika andiko letu kuna shwari kuu mbili; ya kwanza ni ile shwari iliyokuwa moyoni mwa Mwokozi, na ya pili ni ile shwari aliyoiumba kwa neno moja juu ya bahari iliyotikiswa na dhoruba.
I. Ndani ya Bwana kulikuwa na shwari kuu, na ndiyo sababu punde si punde kukawa na shwari kuu kumzunguka; kwa maana kilicho ndani ya Mungu hutoka kwa Mungu. Kwa kuwa kulikuwa na shwari ndani ya Kristo kwa ajili yake mwenyewe, baadaye kukawa na shwari nje kwa ajili ya wengine. Ilikuwa shwari ya ndani ya ajabu kama nini! “Alikuwa katika sehemu ya nyuma ya mashua, amelala usingizi juu ya mto.”
Alikuwa na tumaini kamili katika Mungu kwamba yote yalikuwa mema. Mawimbi yangeweza kunguruma, pepo zingeweza kuvuma, lakini hakufadhaishwa hata kidogo na ghadhabu yao. Alijua ya kuwa maji yalikuwa mikononi mwa Baba yake, na ya kuwa kila upepo haukuwa ila pumzi ya kinywa cha Baba yake; na hivyo hakutaabika; la, hakuwa hata na wazo la wasiwasi, alikuwa na raha kama vile katika siku ya jua. Nia yake na moyo wake vilikuwa huru kutoka kila aina ya masumbufu, kwa maana katikati ya dhoruba iliyokuwa ikikusanyika alijilaza kwa makusudi, akalala kama mtoto aliyechoka. Alikwenda sehemu ya nyuma ya mashua, mahali palipo mbali zaidi na mnyunyizo wa mawimbi; akatwaa mto, akauweka chini ya kichwa chake, na kwa nia thabiti akajitayarisha kusinzia. Kulala usingizi katika dhoruba lilikuwa tendo lake mwenyewe; hakuwa na kitu cha kumfanya akae macho, ndivyo tumaini lake katika Baba mkuu lilivyokuwa safi na kamili. Huu ni mfano ulioje kwetu! Hatuna hata nusu ya tumaini katika Mungu tunalopaswa kuwa nalo, hata walio bora kati yetu. Bwana anastahili imani yetu isiyo na mipaka, tumaini letu lisilo na shaka, kutegemea kwetu kusikofadhaishwa. Ee, laiti tungemtolea kama Mwokozi alivyofanya!
Pia pamoja na imani yake kwa Baba palikuwa pamechanganyika tumaini tamu la Uana wake mwenyewe. Hakutia shaka kwamba yeye alikuwa Mwana wa Aliye Juu. Mimi naweza nisiitilie shaka nguvu ya Mungu ya kuokoa, lakini nyakati nyingine naweza kutilia shaka haki yangu ya kutarajia ukombozi; na ikiwa ni hivyo, faraja yangu hutoweka. Bwana wetu hakuwa na mashaka ya namna hii. Tangu zamani alikuwa amesikia neno lile, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye;” alikuwa ameishi na kuenenda na Mungu kiasi kwamba ushuhuda uliokuwa ndani yake haukukoma, hivyo hakuwa na swali lolote juu ya upendo wa Baba kwake yeye kama Mwanawe mwenyewe. “Nikibembeshwa katika kitanda cha vilindi,” Baba yake akimlinda,—ni jambo gani jema zaidi mtoto angeweza kufanya kuliko kulala usingizi katika hali ya furaha kama hiyo? Na ndivyo afanyavyo. Wewe na mimi, pia, twahitaji uhakikisho kamili zaidi wa uana wetu kama tungependa kuwa na amani kubwa zaidi na Mungu. Shetani analijua hilo, na kwa hiyo atatujia kwa dokezo lake la kunong’oneza, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu.” Kama tuna Roho wa kufanywa wana ndani yetu, tutamshinda mshtaki mara moja, kwa kukabili swali lake la nje kwa Ushuhuda ulio ndani. Ndipo tutakapojazwa shwari kuu, kwa sababu tuna tumaini katika Baba yetu, na uhakikisho wa uana wetu.
Kisha alikuwa na namna tamu—Bwana wetu huyu mbarikiwa—ya kumwachia Mungu yote. Hakai macho kwa kesha, hafanyi wasiwasi; bali huenda kulala. Lolote lijalo, ameyaacha yote mikononi mwa Mlinzi mkuu; na kitu gani zaidi chahitajika? Kama mlinzi angewekwa kuilinda nyumba yangu, ningekuwa mpumbavu ikiwa nami ningekesha kwa hofu ya wevi. Kwa nini kuwa na mlinzi ikiwa siwezi kumwamini alinde? “Umtwike Bwana mzigo wako;” lakini utakapokwisha kufanya hivyo, uuache kwa Bwana, wala usijaribu kuubeba mwenyewe. Kufanya hivyo ni kumdhihaki Mungu, kuwa na jina la Mungu, lakini si uhalisia wa Mungu. Weka chini kila masumbuko, kama vile Yesu alivyofanya alipokwenda kwa utulivu sehemu ya nyuma ya mashua, na kwa kimya akatwaa mto, akaenda kulala.
Lakini nadhani namsikia mtu akisema, “Ningeweza kufanya hivyo kama masumbuko yangu yangehusu nafsi yangu tu.” Ndiyo, labda ungeweza; walakini huwezi kumtwika Mungu mzigo wa kuwahangaikia watoto wako. Lakini Bwana wako alimwamini Baba juu ya wale waliokuwa wapenzi kwake. Je, hudhani kwamba wanafunzi wa Kristo walikuwa wa thamani kwake kama watoto wetu walivyo kwetu? Kama mashua ile ingevunjika, Petro angekuwaje? Angekuwaje “yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda”? Bwana wetu aliwaangalia kwa upendo mkuu wale aliowachagua na kuwaita, ambao walikuwa pamoja naye katika majaribu yake, lakini aliridhika kabisa kuwaacha wote katika ulinzi wa Baba yake, na kwenda kulala.
Wajibu, “Ndiyo, lakini kuna duara pana zaidi la watu wanaotazama kuona litakalonipata mimi, na litakaloipata kazi ya Kristo ambayo nimeshikamana nayo. Nalazimika kuhangaika, nikipenda nisipende.” Je, basi, hali yako ni ngumu kuliko ya Bwana wako? Je, wasahau kwamba “palikuwa pamoja naye na mashua nyingine ndogo nyingi”? Dhoruba ilipokuwa ikiitikisa mashua yake, mashua zao ndogo zilikuwa hatarini hata zaidi; naye aliwajali wote. Alikuwa Amiri Mkuu wa Ziwa la Genesareti usiku ule. Mashua nyingine zilikuwa kikosi chini ya ulinzi wake, na moyo wake mkuu uliwaelekea wote. Lakini alienda kulala, kwa sababu alikuwa ameziacha katika ulinzi wa Baba yake hata zile hangaiko za huruma na upendo wake. Sisi, ndugu zangu, tulio dhaifu sana kuliko yeye, tutapata nguvu kwa kufanya vivyo hivyo.
Baada ya kumwachia Baba yake kila kitu, Bwana wetu alifanya jambo lililokuwa la busara kupita yote. Alifanya sawasawa na saa ile ilivyodai. “Kwa nini,” wasema, “alienda kulala!” Hilo lilikuwa jambo bora zaidi Yesu angeweza kufanya; na nyakati nyingine ndilo jambo bora zaidi tuwezalo kufanya. Kristo alikuwa amechoka na kuchakaa; na mtu awaye yote akiwa amechoka, ni wajibu wake kwenda kulala kama awezavyo. Mwokozi ilimpasa kuamka tena asubuhi, akihubiri na kufanya miujiza, na kama hakulala, hangefaa kwa wajibu wake mtakatifu; ilimpasa kujiweka tayari kwa utumishi wake. Akijua ya kuwa wakati wa kulala umefika, Bwana hulala, naye afanya vema kwa kulala. Mara nyingi, tulipokuwa tukihangaika na kufadhaika, tungemtukuza Mungu zaidi sana kama tungelikwenda kulala kihalisi. Kumtukuza Mungu kwa kulala si vigumu kama wengine wawezavyo kudhani; walau, kwa Bwana wetu lilikuwa jambo la kawaida. Hapa umehangaika, una huzuni, umechoka; tabibu akuandikia dawa; dawa yake haikufai kitu; lakini ee! kama utaingia katika amani kamili na Mungu, na kwenda kulala, utaamka ukiwa umeburudishwa bila kipimo kuliko kwa dawa yoyote. Usingizi ambao Bwana humpa mpendwa wake ni wa kutuliza kweli kweli. Uutafute kama Yesu alivyoutafuta. Nenda kitandani, ndugu, nawe utamwiga Bwana wako vizuri zaidi kuliko kwa kujitia katika hasira, na kuwasumbua watu wengine.
Kuna usingizi wa kiroho ambao katika huo twapaswa kumwiga Yesu. Mara ngapi nimeitaabisha akili yangu maskini juu ya kanisa langu kubwa, hata niliporudiwa na fahamu zangu, ndipo nikajiambia mwenyewe, “Wewe u mpumbavu kama nini! Je, huwezi kumtegemea Mungu? Je, si kazi yake kuliko yako?” Ndipo nikauchukua mzigo wangu katika maombi, nikamwachia Bwana. Nimesema, “Kwa jina la Mungu, jambo hili halitanihangaisha kamwe tena,” nami nimemwachia hangaiko langu la haraka, nikalimaliza milele. Nimeyatoa kwa makusudi mengi mno mashaka mazito mikononi mwa Bwana kiasi kwamba, rafiki zangu walipokuwa wakiniambia, “Je, jambo fulani laendeleaje?” nimejibu tu, “Sijui, wala sina tena hamu ya kujua. Bwana ataingilia kati kwa namna moja au nyingine, lakini sitajitaabisha nalo tena.” Hakuna madhara yaliyowahi kuja kwa njia ya jambo lolote nililoliacha katika ulinzi wa Mungu. Kuzuia mkono wangu kumekuwa hekima. “Simameni, mkauone wokovu wa Mungu” ni agizo la Mungu mwenyewe. Hapa na tumfuate Yesu. Akiwa na tumaini la mtoto katika Baba mkuu, hujiondoa hadi shetri ya mashua, huchagua mto, hujilaza juu yake kwa makusudi, na huenda kulala; na ijapokuwa mashua inajaa maji, na kuyumba na kupwaya, yeye hulala tu. Hakuna kiwezacho kuvunja amani ya nafsi yake tulivu. Kila baharia aliyomo huyumbayumba huku na huku, na kupepesuka kama mtu mlevi, na kufikia ukomo wa akili zake; lakini Yesu hakufikia ukomo wa akili zake, wala hapepesuki, kwa maana hupumzika katika hali ya kutokuwa na hatia kamili, na tumaini lisilofadhaishwa. Moyo wake una furaha katika Mungu, na kwa hiyo hukaa katika utulivu. Ee, laiti tungepata neema ya kumwiga!
II. Lakini hapa angalieni, ndugu wapenzi, tofauti kati ya Bwana na wanafunzi wake; kwa maana wakati yeye alipokuwa katika shwari kuu, wao walikuwa katika dhoruba kuu. Hapa oneni kushindwa kwao. Walikuwa kama vile sisi tulivyo, na sisi mara nyingi tu kama vile walivyokuwa.
Walishindwa na hofu. Waliogopa sana kwamba mashua ingezama, na kwamba wote wangeangamia. Kwa kuikubali hivyo hofu, walizisahau sababu imara za ushujaa zilizokuwa karibu nao; kwa maana, kwa kweli, walikuwa salama vya kutosha. Kristo yumo ndani ya chombo kile, na kama mashua ikizama, atazama pamoja nao. Baharia yule wa kipagani alijipa moyo wakati wa dhoruba kwa kuwa Kaisari alikuwamo ndani ya mashua iliyokuwa ikitikiswa na pepo za dhoruba; na je, wanafunzi wasingejihisi salama Yesu akiwa ndani? Msiogope, mnamchukua Yesu na kazi yake! Yesu alikuwa amekuja kufanya kazi, na wanafunzi wake wangeweza kujua ya kuwa hawezi kuangamia kabla ya kazi ile kutimizwa. Je, wasingeweza kumwamini? Walikuwa wamemwona akizidisha mikate na samaki, na kutoa pepo, na kuponya maradhi ya kila namna; je, wasingeweza kumwamini kuituliza dhoruba? Kutokuamini kusiko na akili! Imani katika Mungu ni busara ya kweli, bali kumtilia Mungu shaka ni jambo lisilo na akili. Ni kilele cha upuuzi na upumbavu kuutilia shaka upendo wenye uweza wote.
Na wanafunzi walikuwa wapumbavu kiasi cha kumtendea Bwana jambo baya sana. Alikuwa amechoka kwa kusikitisha, na alihitaji sana usingizi; lakini wakamwendea haraka, wakamwamsha kwa namna iliyokuwa na ukatili kidogo na isiyo na heshima. Walikuwa wazito kufanya hivyo, lakini hofu yao iliwasukuma; na kwa hiyo wakamwamsha, wakisema maneno yasiyo na ukarimu wala upendo: “Mwalimu, hujali sisi kuwa tunaangamia?” Aibu iwe juu ya midomo iliyouliza swali gumu namna hiyo! Je, walipofikiri hawakujilaumu wenyewe sana? Hakuwa amewapa sababu ya maneno magumu kama hayo; na, zaidi ya hayo, ilikuwa haifai kwao kumwita “Mwalimu,” kisha kumwuliza, “Hujali sisi kuwa tunaangamia?” Je, ashtakiwe kwa ugumu wa moyo namna hiyo hata awaache wanafunzi wake waaminifu waangamie hali ana uweza wa kuwaokoa? Ole wetu, sisi pia, tumekuwa na hatia ya makosa kama hayo! Nadhani nimewajua baadhi ya wanafunzi wa Kristo walioonekana kutia shaka hekima au upendo wa Bwana wao. Hawakusema waziwazi kwamba alikosea, bali walisema kwamba alienenda kwa njia ya ajabu; hawakulalamika waziwazi kwamba hakuwa na fadhili kwao, bali walinong’ona kwamba hawakuweza kupatanisha matendo yake na upendo wake usio na mwisho. Ole wetu, Yesu amevumilia mengi kutokana na kutokuamini kwetu! Picha hii na itusaidie kuona madoa yetu, na upendo wa Bwana wetu mpenzi na uyaondoe!
III. Nimewaambia juu ya shwari ya Bwana na juu ya kushindwa kwa wanafunzi; sasa na tuutafakari ule shwari kuu Yesu aliouumba. “Kukawa shwari kuu.”
Sauti yake ndiyo iliyoiumba. Wasema ya kuwa mafuta yakimwagwa juu ya maji yatakuwa laini, nami nadhani kuna kweli fulani katika maneno hayo; lakini kuna kweli yote katika hili, ya kuwa Mungu akinena, dhoruba hutulia na kuwa shwari, hata mawimbi ya bahari yanyamaza. Yatosha tu Bwana wetu Yesu kunena ndani ya moyo wa yeyote miongoni mwetu, na mara ile amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itatumiliki. Hata ukiwa na huzuni ya namna gani nzito, wala kukata tamaa kwa kutisha kiasi gani, Bwana aweza mara moja kuumba shwari kuu ya tumaini. Ni mlango wa tumaini ulioje huu unaowafungulia wote walio katika taabu! Kama ningeweza kumfanya maskini kuwa tajiri kwa kunena tu, na mgonjwa kuwa mzima, nina hakika ningefanya hivyo mara moja; lakini Yesu ni bora bila kipimo kuliko mimi, na kwa hiyo najua ya kuwa atanena amani kwa moyo uliojaribiwa na kutaabika.
Angalia, pia, ya kuwa shwari hii ilikuja mara moja. “Yesu akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu.” Mara tu Yesu aliponena, kila kitu kilinyamaza. Nimekutana na watu wengi mno waliokuwa katika taabu ya akili, nami nimewaona wachache waliotoka polepole kuingia katika nuru na uhuru; lakini mara nyingi zaidi ukombozi umekuja ghafula. Lango la chuma limejifungua lenyewe, na mfungwa ameingia katika uhuru wa papo hapo. “Mtego umevunjika, na sisi tumeokoka.” Ni furaha iliyoje kujua ya kuwa pumziko liko karibu hivyo hata wakati dhoruba inavuma kwa ukali kupita kiasi!
Angalia, pia, ya kuwa Mwokozi aliunganisha pumziko hili na imani, kwa maana aliwaambia wanafunzi mara tu shwari ilipokuja, “Mbona mwaogopa hivi? Mbona hamna imani?” Imani na shwari huenda pamoja. Ukiamini, utapumzika; ukijitupa tu juu ya Mungu wako, ukijisalimisha kabisa kwa mapenzi yake, utapata rehema, na furaha, na nuru. Hata kama hatuna imani, Bwana nyakati nyingine atatupa baraka tunayoihitaji, kwa maana hufurahia kututendea zaidi ya vile tulivyo na haki ya kutarajia kwake; lakini kwa kawaida sheria ya ufalme wake ni, “Iwe kwenu kama imani yenu ilivyo.”
Shwari hii kuu inafurahisha mno, na kuhusu hili nataka kutoa ushuhuda wangu binafsi. Nanena kwa kujua kwangu mwenyewe nisemapo kwamba yapita akili zote. Nilikuwa nimeketi, usiku ule mmoja, nikitafakari rehema na upendo wa Mungu, ghafula nikakuta ndani ya moyo wangu mwenyewe hisia tamu kupita zote ya amani kamili. Nilikuwa nimefika nchi ya Beula, ambako jua huangaza pasipo wingu. “Kukawa shwari kuu.” Nilihisi kama vile mabaharia wawezavyo kuhisi ambao wametupwatupwa katika maji yaliyochafuka, na ghafula, wasijue kwa nini, bahari inakuwa tulivu kama kioo, na ndege wa baharini huja na kuketi katika miduara ya furaha juu ya maji. Nilihisi kuridhika kikamilifu, naam, furaha isiyogawanyika. Hakuna wimbi la taabu lililopiga ufuoni mwa moyo wangu, na hata mbali baharini katika vilindi vya nafsi yangu kila kitu kilikuwa kimya. Sikujua tamaa isiyotimizwa, wala shauku isiyotoshelezwa. Sikuweza kuvumbua sababu ya wasiwasi, wala kisa cha hofu. Hakukuwa na kitu kilichokaribia ushabiki katika hisia zangu, wala hata kitu cha mshtuko: nafsi yangu ilikuwa ikimngoja Mungu, na kujifurahisha katika yeye peke yake. Ee, heri ya pumziko hili katika Bwana! Ni pepo iliyoje hii! Ni lazima niruhusiwe kusema kidogo juu ya kisiwa hiki cha zambarau katika bahari ya maisha yangu: hakikuwa kingine ila kipande cha mbinguni. Mara nyingi twanena juu ya dhoruba zetu kuu za kiroho, mbona tusinene juu ya shwari zetu kuu? Kama tukiingia katika taabu, twafanya kelele iliyoje juu yake! Mbona tusiimbe juu ya ukombozi wetu?
Na tuzichunguze rehema zetu. Kila dhambi tuliyowahi kuitenda imesamehewa. “Damu yake Yesu Kristo, Mwanawe, yatusafisha dhambi yote.” Nguvu ya dhambi ndani yetu imevunjika; “haitawatawala ninyi, kwa maana hammo chini ya sheria, bali chini ya neema.” Shetani ni adui aliyeshindwa; ulimwengu umeshindwa na Bwana wetu Yesu, na mauti imebatilishwa naye. Maongozi yote hutenda kazi kwa faida yetu. Umilele hauna tisho kwetu, ndani ya siri zake haubebi kitu ila kutokufa na utukufu. Hakuna kiwezacho kutudhuru. Bwana ndiye ngao yetu, na thawabu yetu kubwa mno. Kwa hiyo, basi, mbona tuogope? Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ndiye kimbilio letu. Kwa mwamini, amani si kiburi: ana ruhusa ya kufurahia “amani kamilifu”—utulivu ulio na kina, na uliojengwa juu ya kweli, unaozunguka vitu vyote, na usiovunjwa na kimojawapo cha visababishi elfu kumi vya usumbufu ambavyo vinginevyo vingeweza kuzuia pumziko letu. “Utamlinda katika amani kamilifu yeye ambaye moyo wake umekutegemea; kwa kuwa anakutumaini.” Ee, kuingia katika shwari ile, na kukaa ndani yake hata tufike ulimwengu ule ambako hakuna tena bahari!
Shwari kama ile iliyotawala ndani ya Mwokozi wetu, tukibahatika kuifikia, itatupa kwa kadiri yetu uwezo wa kuyatuliza mambo ya nje. Aliye na amani aweza kufanya amani. Hatuwezi kufanya miujiza, walakini kazi zile Yesu alizozifanya nasi tutazifanya pia. Tukilala usingizi wake, tutaamka katika nguvu yake iliyopumzika, na kuyachukulia mawimbi na pepo kama vitu vilivyo chini ya nguvu ya imani, na kwa hiyo viwezavyo kuamriwa vinyamaze. Tutanena hata kuwafariji wengine: shwari yetu itatenda maajabu katika mashua ndogo ambazo wengine ni manahodha wake. Sisi, pia, tutasema, “Nyamaza! Utulie.” Tumaini letu litakuwa la kuambukiza, na wenye hofu watakuwa hodari: upendo wetu wa upole utajienea, na wagomvi watapoa hata kuwa na saburi. Ila tu jambo hilo lazima lianze ndani yetu wenyewe. Hatuwezi kuumba shwari hata tuwe katika shwari. Ni rahisi zaidi kutawala vitu vya asili kuliko kutawala ukaidi wa tabia yetu iliyopotoka. Neema itakapotufanya kuwa mabwana wa hofu zetu, hata tuweze kutwaa mto na kulala usingizi katikati ya tufani, ghadhabu ya dhoruba imekwisha. Yeye hutoa amani na usalama atoapo usingizi kwa mpendwa wake.
Sura ya 15 imekamilika
Yesu Amelala Usingizi juu ya Mto