Hata Ajapo
Wimbo wa Kukumbukwa

Sura 14 · dakika 23 za kusoma

Wimbo wa Kukumbukwa

WIMBO WA KUKUMBUKWA. “Nao walipokwisha kuimba wimbo, wakatoka kwenda katika mlima wa Mizeituni.”—Mathayo 26:30.27

WIMBO WA KUKUMBUKWA.

Tukio ambalo maneno haya yalinenwa lilikuwa mlo wa mwisho ambao Yesu alikula pamoja na wanafunzi wake kabla hajaondoka kwao kwenda kwenye kesi yake ya aibu na mauti yake ya fedheha. Ilikuwa karamu yake ya kuaga kabla ya kutengana kuchungu, na hata hivyo hawana budi kuimba. Alikuwa ukingoni mwa kilindi kile kikuu cha taabu ambamo alikuwa karibu kutumbukia, na hata hivyo angependa waimbe “wimbo.” Ni jambo la ajabu kwamba aliimba, na kwa daraja la pili ni jambo la kustaajabisha kwamba nao waliimba. Tutayatafakari mambo haya mawili ya pekee.

I. Na tukae kitambo juu ya jambo hili kwamba Yesu aliimba wakati kama huu. Anatufundisha nini kwa jambo hili? Je, hasemi kwa kila mmoja wetu, wafuasi wake “Dini yangu ni ya furaha na shangwe; Mimi, Bwana wenu, kwa kielelezo changu ningewafundisha kuimba hata saa ile ya mwisho ya adhama itakapofika, na giza lote la mauti litakapowazingira? Hapa, mezani, mimi ni Mwalimu wenu wa Uimbaji, nami nawawekea masomo katika muziki, ambamo sauti yangu inayokufa itawaongoza: pamoja na huzuni zote zinazoulemea moyo wangu, nitakuwa kwenu Mwimbaji Mkuu, na Mwimbaji Mtamu wa Israeli”? Kama kamwe kulikuwa na wakati ambao ingekuwa jambo la asili na lenye kupatana na uzito wa tukio hilo kwa Mwokozi kuinamisha kichwa chake mezani, akibubujika machozi tele; au, kama kamwe kulikuwa na majira ambapo angeweza ipasavyo kujitenga na wote, na kuomboleza mapambano yake yajayo kwa kuugua na kulia, ilikuwa wakati ule ule. Lakini la; moyo ule shujaa utaimba “wimbo.” Yesu wetu mtukufu anajionyesha mwanamume kuliko watu wengine wote. Aliye hodari kuliko wana wote wa watu, harudi nyuma katika saa ya vita, bali huipatanisha sauti yake kwa nyimbo za sifa zilizo tukufu zaidi. Asili ya Ukristo ule ambao Yesu ndiye Kichwa na Mwanzilishi wake, shabaha yake, roho yake, na kusudi lake, ni furaha na shangwe, nao waupokeao waweza kuimba katika kinywa hasa cha mauti.

Maelezo haya, hata hivyo, ni ya daraja la pili kabisa kwa lile lifuatalo: kutimiza kikamili kwa Bwana wetu sheria ni jambo lenye kustahili zaidi uangalifu wetu. Ilikuwa ni desturi, Pasaka ilipoadhimishwa, kuimba, na hii ndiyo sababu kuu iliyomfanya Mwokozi afanye hivyo. Wakati wa Pasaka, ilikuwa kawaida kuimba Zaburi ya mia na kumi na tatu, na zile tano zifuatazo, ambazo ziliitwa “Halleli.” Ya kwanza yaanza, kama utakavyoona, katika tafsiri yetu, kwa “Msifuni Bwana!” au, “Haleluya!” Ya mia na kumi na tano, na zile tatu zifuatazo, kwa kawaida ziliimbwa kama wimbo wa kufunga Pasaka. Basi, Mwokozi wetu hangepunguza fahari ya ile ibada kuu ya Kiyahudi, ijapokuwa ilikuwa mara ya mwisho ambayo angeiadhimisha. La; kutakuwako uzuri mtakatifu na furaha ya nyimbo za sifa; hakuna kitu kitakachopunguzwa; “Halleli” itakuwa kamili na timilifu. Twaweza kuamini salama kwamba Mwokozi aliimba, au yamkini aliimba kwa mahadhi, Zaburi hizi zote sita; na moyo wangu wanambia kwamba hakuna aliyekuwako mezani aliyeimba kwa ibada zaidi au kwa uchangamfu zaidi kuliko Bwana wetu mbarikiwa. Kuna sehemu fulani za Zaburi ya mia na kumi na nane, hasa, zinazotugusa kama zilizosikika kwa fahari ya pekee, zilipobubujika kutoka midomoni mwake mibarikiwa. Angalia mistari ya 22, 23, 24. Hasa yaangalie maneno yale, karibu na mwisho wa Zaburi, na uwaze wamsikia Bwana Mwenyewe akiyaimba, “Bwana ndiye Mungu, naye ametuangazia nuru; ifungeni dhabihu kwa kamba, hata pembe za madhabahu. Wewe u Mungu wangu, nami nitakushukuru; Wewe u Mungu wangu, nitakutukuza. Mshukuruni Bwana, kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele.”

Basi, kwa kuwa ilikuwa desturi iliyothibitika ya Israeli kuzisoma au kuziimba Zaburi hizi, Bwana wetu Yesu Kristo alifanya vivyo hivyo; kwa maana hangeacha kitu chochote bila kutimizwa. Kama vile, aliposhuka ndani ya maji ya ubatizo, aliposema, “Ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote,” ndivyo alivyoonekana kusema, alipoketi mezani, “Ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote; basi na tumwimbie Bwana, kama watu wa Mungu walivyofanya katika vizazi vilivyopita.” Wapenzi, na tuutazame kwa mshangao mtakatifu ukamilifu wa utii wa Mwokozi kwa mapenzi ya Baba yake, na tujitahidi kufuata nyayo zake, katika mambo yote, tukitaka kuwa watii kwa Neno la Bwana katika mambo madogo kama vile katika makubwa.

Je, hatuwezi kuthubutu kupendekeza sababu nyingine na yenye kina zaidi? Je, kuimba “wimbo” wakati wa karamu hakukuonyesha kuzama kwa nafsi ya Mwokozi kikamili katika mapenzi ya Baba yake? Kama, mpenzi, ungejua kwamba saa—tuseme saa nne usiku wa leo—ungechukuliwa mbali ili udhihakiwe, na kudharauliwa, na kupigwa mijeledi, na kwamba jua la kesho lingekuona ukishtakiwa kwa uongo, ukining’inia, mhalifu uliyehukumiwa, ili ufe msalabani, je, wadhani ungeweza kuimba usiku wa leo, baada ya mlo wako wa mwisho? Nina hakika usingeweza, isipokuwa kwa ujasiri na unyenyekevu unaozidi wa kidunia nafsi yako ingeweza kusema, “Ifungeni dhabihu kwa kamba, hata pembe za madhabahu.” Ungeimba kama roho yako ingekuwa kama roho ya Mwokozi; kama, kama yeye, ungeweza kupaza sauti, “Si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe;” lakini kama kungebaki ndani yako ubinafsi wowote, tamaa yoyote ya kuepushwa uchungu wa mauti, usingeweza kuimba “Halleli” pamoja na Bwana. Yesu mbarikiwa, jinsi ulivyojitoa kabisa! jinsi ulivyowekwa wakfu kikamilifu! hata kwamba, hali watu wengine huimba wanapoelekea kwenye furaha zao, Wewe uliimba njiani kuelekea mautini; hali watu wengine hupaza sauti zao za shangwe heshima inapowangoja, Wewe ulikuwa na wimbo shujaa na mtakatifu midomoni pako wakati aibu, na kutemewa mate, na mauti vilipokuwa fungu lako.

Kuimba huku kwa Mwokozi kunatufundisha pia moyo mzima wa Bwana katika kazi ile aliyokuwa karibu kuifanya. Shujaa-mzalendo huimba akiharakia vitani; kwa vuma za muziki wa kivita husonga mbele kukutana na adui; na hata vivyo hivyo moyo wa Bingwa wetu mtukufu wote humpatia wimbo hata katika saa ile ya kutisha ya uchungu wake wa upweke. Auangalia vita, lakini hauogopi; ingawa katika mashindano nafsi yake itakuwa na “huzuni nyingi hata kufa,” lakini kabla yake, yeye ni kama farasi wa vita wa Ayubu, “husema kati ya baragumu, Aha, aha; naye husikia harufu ya vita toka mbali.” Anao ubatizo wa kubatizwa nao, naye anasongwa hata utakapotimizwa. Bwana haendi kwenye uchungu bustanini kwa roho iliyoshtuka na kutetemeka, iliyoinama yote na kupondwa mavumbini; bali husonga mbele kuelekea mapambano kama mtu aliye na nguvu zake kamili juu yake—akitolewa kuwa dhabihu (kama naweza kutumia mfano huu), si kama maksai aliyechoka aliyebeba nira muda mrefu, bali kama mzaliwa wa kwanza wa ng’ombe, katika utimilifu wa nguvu zake. Huenda kuchinjwa, akiwa na roho yake tukufu isiyoogopa imara na thabiti ndani yake, akifurahi kuteseka kwa ajili ya watu wake na kwa utukufu wa Baba yake.

“Kwa kuwa hapo mwanzo mtazamo Wako uenea kila mahali

Uliona toka kifua cha Baba Yako hata kuzimu,

Ukipima kwa utulivu wa unabii

Ushukaji usio na mwisho;

Vivyo hivyo hata mwisho, ingawa sasa umefanywa mrithi

Wa maumivu ya kufa, na kuvuliwa utukufu Wako kwa muda,

Kwa jicho lisilogeuka

Wakabili dhoruba yote.”

Na tujifunze, enyi warithi-wenzangu wa wokovu, kuimba wakati saa yetu ya mateso ijapo, wakati majira yetu ya kazi ngumu yanapokaribia; naam, na tumwage wimbo wa furaha wenye kina, wa fumbo, wenye utamu wa raha, wakati saa yetu ya kufa ikaribiapo! Uwe hodari, ndugu! Maji ni baridi; lakini hofu haitapunguza kwa vyovyote vitisho vya mto. Uwe hodari, ndugu! Mauti ni kazi ya adhama; lakini kuwa mwoga hakutayafanya kuwa madogo. Toa tarumbeta ya fedha; midomo yako na iukumbuke muziki uliopendwa siku nyingi, na sauti ziwe wazi na kali unapotia miguu yako Yordani: “Naam, nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya; kwa maana Wewe upo pamoja nami; gongo lako na fimbo yako vyanifariji.” Wapendwa, kumbukumbu la nyimbo za chumba kile cha juu na liende nanyi kesho katika biashara zenu; na kama mnatazamia jaribu kuu, na mnaogopa kwamba hamtaweza kuimba baada yake, basi imbeni kabla halijaja. Kamilisheni kazi yenu takatifu ya sifa kabla ya dhiki kuuharibu wimbo. Jazeni hewa kwa muziki mngali mwaweza. Wakati bado kuna mkate mezani, imbeni, ijapokuwa njaa yaweza kutisha; wakati bado mtoto anakimbia akicheka nyumbani, wakati bado wekundu wa afya u shavuni mwako, wakati bado mali zenu zimehifadhiwa, wakati bado moyo wako u mzima na salama, pazeni wimbo wenu wa sifa kwa Mungu Aliye Juu Sana; na Bwana wenu, Mwokozi aimbaye, awe katika hili kielelezo chenu chema na chenye faraja.

Kuna mengi zaidi ambayo yangeweza kusemwa kuhusu wimbo mtamu wa Bwana wetu wa kuaga, lakini hakuna haja ya kusonga wazo moja nje kwa jingine; nafasi yenu itatumika vyema katika kutafakari mada yenye kuzaa matunda kama hii.

II. Sasa tutalitazama kuimba kwa wanafunzi. Waliungana katika “Halleli”—kama Wayahudi wa kweli, walijiunga katika wimbo wa taifa. Israeli alikuwa na sababu njema ya kuimba wakati wa Pasaka, kwa maana Mungu alikuwa amewatendea watu wake yale ambayo hakuwa amelitendea taifa lingine lolote juu ya uso wa dunia. Kila Mwebrania hakika alihisi nafsi yake ikiinuliwa na kufurahi katika usiku ule wa Pasaka. Alikuwa “raia wa mji usio mdogo,” na ukoo aliouangalia nyuma ulikuwa ni ule ambao, ukilinganishwa nao, wafalme na wakuu walikuwa wa jana tu.

Wakikumbuka jambo lililoadhimishwa na karamu ya Pasaka, Israeli angeweza kufurahi ipasavyo. Waliimba juu ya taifa lao katika utumwa, likikanyagwa chini ya mguu wa kidhalimu wa Farao; walianza Zaburi kwa huzuni kubwa, walipofikiria zile tofali zilizofanywa bila majani, na tanuru ya chuma; lakini wimbo mara ukapanda kutoka besi ya kina, na kuanza kupanda ngazi, walipoimba juu ya Musa mtumishi wa Mungu, na juu ya Bwana kumtokea katika kile kichaka kilichowaka moto. Waliikumbuka ile fimbo ya fumbo, iliyokuwa nyoka, na iliyozimeza fimbo za waganga; muziki wao ulisimulia mapigo na maajabu ambayo Mungu alikuwa ameyatenda juu ya Soani; na juu ya usiku ule wa kutisha ambapo wazaliwa wa kwanza wa Misri walianguka mbele ya upanga wa kisasi wa malaika wa mauti, hali wao wenyewe, wakila mwana-kondoo aliyekuwa amechinjwa kwa ajili yao, na ambaye damu yake ilinyunyizwa juu ya kizingiti na juu ya miimo ya mlango, walikuwa wamehifadhiwa kwa neema. Kisha wimbo ukapaa juu kuhusu saa ile ambapo Misri yote ilinyenyekezwa miguuni pa Yehova, hali kwa watu wake, aliwaongoza nje kama kondoo, kwa mkono wa Musa na Haruni, nao walikwenda kwa njia ya bahari, naam bahari ya Shamu. Wimbo ukapanda juu zaidi walipoimba wimbo wa Musa, mtumishi wa Mungu, na wa Mwana-Kondoo. Kwa shangwe waliimba juu ya Bahari ya Shamu, na juu ya magari ya Farao yaliyoshuka katikati yake, na vilindi vikawafunika hata hakubaki hata mmoja wao. Ulikuwa wimbo mtukufu kweli walipoimba juu ya Rahabu aliyekatwa vipande, na juu ya joka lililojeruhiwa baharini, kwa mkono wa kuume wa Aliye Juu Sana, kwa ukombozi wa watu wateule.

Lakini, wapenzi, kama nimesema kwamba Israeli angeweza kuimba ipasavyo hivyo, niseme nini juu ya wale kati yetu tulio waliokombolewa kiroho na Bwana? Tumewekwa huru kutoka utumwa mbaya kuliko ule wa Misri: “kwa mkono wenye nguvu na kwa mkono ulionyoshwa,” Mungu ametuokoa. Damu ya Yesu Kristo, Mwana-Kondoo wa Pasaka ya Mungu, imenyunyizwa juu ya mioyo na dhamiri zetu. Kwa imani twaishika Pasaka, kwa maana tumehifadhiwa; tumetolewa Misri; na ingawa dhambi zetu zilitupinga hapo zamani, zote zimezama katika Bahari ya Shamu ya damu ya upatanisho ya Yesu: “vilindi vimewafunika, hakuna hata mmoja wao aliyebaki.” Kama Myahudi angeweza kuimba “Halleli kuu”, “Halleli” yetu yapasa kuwa yenye kung’aa zaidi; na kama kila nyumba katika “nchi ya furaha ya Yudea” ilijaa muziki wakati watu walipokula karamu ya Pasaka, tuna sababu zaidi sana ya kujaza kila moyo kwa uimbaji mtakatifu usiku wa leo, tunapomla Yesu Kristo, aliyechinjwa, na ametukomboa kwa Mungu kwa damu yake.

III. Sasa wakati umefika kwangu kusema jinsi ninavyotamani kwa bidii mwimbe “wimbo.”

Sikusudii kuwaomba mtumie sauti zenu, bali mioyo yenu na ijae kiini cha sifa. Kila mara tunapoiendea meza ya Bwana, inayotuwakilisha Pasaka, haitupasi kuijia kama kuijia mazishi. Na tuchague nyimbo za adhama, lakini si nyimbo za maombolezo. Na tuimbe kwa upole, lakini si kwa furaha kidogo. Hizi si karamu za mazishi; hizo si mikate ya mazishi ilalayo juu ya meza hii, na kitambaa kile cheupe kizuri cha kitani si sanda. “Huu ni mwili wangu,” alisema Yesu, lakini mwili uliowakilishwa hivyo haukuwa maiti, twamla Kristo aliye hai. Damu inayoonyeshwa na divai ile ni damu-uhai mpya ya Mfalme wetu asiyekufa. Hatuutazami mwili wa Bwana wetu kama nyama iliyopoa kama udongo, iliyotobolewa kwa vidonda, bali kama uliotukuzwa mkono wa kuume wa Baba. Twaadhimisha sikukuu ya furaha tunapomega mkate siku ya kwanza ya juma. Hatuji hapa tukitetemeka kama watumwa, tukipiga magoti kama vijakazi wanyonge waliohukumiwa kula kwa magoti; twaikaribia kama watu huru kwenye karamu ya Bwana wetu, kama mitume wake, kuegemea au kuketi kwa raha; si kula mkate tu ambao waweza kuwa wa wenye huzuni nyingi, bali kunywa divai iliyo ya watu ambao nafsi zao zina furaha. Na tuutambue wema, naam, wajibu wa uchangamfu katika karamu hii ya ukumbusho; na, kwa hiyo, na tuimbe “wimbo.”

Tukiisha kuridhika juu ya jambo hili, labda mwauliza, “Tutaimba wimbo gani?” Aina nyingi za nyimbo ziliimbwa zamani za kale: angalia orodha, na hutapata karibu hata mmoja ambao hauwezi kutufaa sasa.

Mmojawapo wa nyimbo za kwanza za dunia ulikuwa wimbo wa vita. Waliimba zamani wimbo kwa mshindi, aliporudi kutoka vitani. “Sauli amewaua elfu zake, na Daudi makumi elfu yake.” Wanawake walichukua matari yao, na kufurahi katika kucheza shujaa aliporudi kutoka vitani. Hata vivyo hivyo zamani watu wa Mungu walimtukuza kwa matendo yake makuu, wakiimba kwa sauti kuu pamoja na matoazi yenye sauti kubwa: “Mwimbieni Bwana, kwa maana ametukuka kwa fahari . . . Bwana ni shujaa wa vita; Bwana ndilo jina lake.” Ndugu zangu, na tupaze wimbo wa vita usiku wa leo! Kwa nini isiwe hivyo? “Ni nani huyu ajaye kutoka Edomu, mwenye mavazi ya rangi kutoka Bosra? huyu aliye mtukufu katika mavazi yake, asafiriye katika ukuu wa nguvu zake? Ni mimi ninenaye kwa haki, mwenye uwezo wa kuokoa.” Njoni, na tumsifu Imanueli wetu, tunapokiona kichwa cha adui yetu mkononi mwake wa kuume; tunapomwona akiuongoza mateka utumwani, akipaa juu, kwa sauti ya furaha ya baragumu, na tuimbe wimbo wa ushindi; na tupaze wimbo wa vita, “Io Triumphe!” Tazama, aja, mtukufu wote kutoka vitani: tunapokusanyika kwenye meza hii ya karamu, inayotukumbusha vita vyake na ushindi wake pia, na tumsalimu kwa zaburi ya ushindi wa shangwe, ambayo itakuwa ni utangulizi tu wa wimbo tutakaotazamia kuuimba tutakapopanda juu—

“Ambapo waimbaji wote hukutana.”

Namna nyingine ya kwanza ya wimbo ilikuwa ile ya kichungaji. Wachungaji walipoketi kati ya kondoo, walizipatanisha filimbi zao, na kupaza nyimbo laini na tamu zilizopatana na utulivu wa mashambani. Kila upande palikuwa shwari na kimya; jua liling’aa sana, na ndege walikuwa wakitunga nyimbo kati ya matawi yenye majani. Je, nitaonekana mwenye kuwaza-waza nikisema, na tuungane katika wimbo wa kichungaji usiku wa leo? Tukiketi kuzunguka meza, kwa nini tusiimbe, “Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza”? Kama kuna mahali chini ya nyota ambapo mtu angeweza kuhisi raha na utulivu kamili, hakika ni kwenye meza ya Bwana. Hapa, basi, na tumwimbie Mchungaji wetu mkuu wimbo wa kichungaji wa furaha. Sauti ya kondoo na iwe masikioni mwetu tunapomkumbuka Mchungaji Mwema aliyeutoa uhai wake kwa ajili ya kundi lake.

Hamhitaji kukumbushwa kwamba watu wa kale walipenda sana nyimbo za sherehe. Walipokusanyika kwenye sikukuu zao kuu, wakiongozwa na wanamuziki wao wateule, waliimba kwa shangwe kubwa, kwa furaha ya kelele. Waache wale watakao kusema kwa sifa ya divai, nafsi yangu itaisifu damu ya thamani ya Yesu; waache watakao kusifu nafaka na mafuta, mazao tajiri ya mavuno, moyo wangu utaimba juu ya Mkate ule uliokuja kutoka mbinguni, ambao, mtu akiula, hataona njaa kamwe. Mwanena juu ya karamu za kifalme, na uimbaji unaostahili sikio la mfalme? Yetu ni sikukuu tukufu zaidi, na wimbo wetu ni mtamu zaidi sana. Hapa kuna nafasi kwenye meza hii usiku wa leo kwa ushairi na muziki wote wa dunia, kwa maana mahali hapa panastahili nyimbo zenye kung’aa zaidi kwa furaha, zenye kumeta zaidi kwa vito vya shangwe takatifu, kuliko wowote ambao watu wa kale wangeweza kuuwaza.

“Sasa kwa wimbo wa sifa tukufu

Kwa Mwana sawa na Yehova mkuu!

Amka, sauti yangu, katika nyimbo za mbinguni

Simulia maajabu makuu aliyoyatenda!”

Wimbo wa upendo hatuna budi kuukumbuka, kwa maana huo ndio wimbo wa pekee wa jioni hii. “Sasa nitamwimbia Mpenzi wangu wimbo.” Upendo wake kwetu ni mada isiyokufa; na kama upendo wetu, ukipepewa na pumzi ya mbinguni, unavyowaka moto mkali, twaweza kuimba, naam, nasi tutaimba kati ya nyinyoro, wimbo wa mapenzi.

Katika Agano la Kale, twakuta Zaburi nyingi zilizoitwa kwa jina, “Wimbo wa Kupanda.” “Wimbo wa Kupanda” huu hudhaniwa na wengine kuwa uliimbwa watu walipopanda ngazi za hekalu, au walipofanya hija kwenye mahali patakatifu. Wimbo mara nyingi hubadilika, mara ni wa huzuni, na tena ni wa furaha; wakati mmoja, sauti ni ndefu zilizovutwa na nzito, wakati mwingine, ni za uchangamfu na shangwe. Tutaimba “Wimbo wa Kupanda” usiku wa leo. Tutaomboleza kwamba tulimchoma Bwana, nasi tutafurahi katika msamaha uliolipiwa kwa damu. Wimbo wetu lazima ubadilike-badilike tunapoongea juu ya dhambi, tukihisi uchungu wake, na kuuomboleza, na kisha juu ya msamaha, tukifurahi katika utimilifu wake mtukufu.

Daudi aliandika Zaburi nyingi kiasi alizoziita, “Maskili,” ambazo zaweza kuitwa kwa Kiingereza, “Zaburi za mafundisho.” Wapi, wapenzi, tutapata mafundisho yaliyo tajiri zaidi kuliko kwenye meza ya Bwana wetu? Yeye aelewaye siri ya kufanyika mwili na ya kubadilishwa dhabihu, ni bingwa katika theolojia ya Kimaandiko. Kuna mafundisho mengi zaidi katika mwili wa Mwokozi na katika damu ya Mwokozi kuliko katika ulimwengu wote pia. Enyi mnaotaka kujifunza njia ya faraja, na jinsi ya kuikanyaga njia ya kifalme kuelekea hekima ya mbinguni, njoni msalabani, mkamwone Mwokozi akiteseka, na kumwaga damu ya moyo wake kwa ajili ya dhambi ya mwanadamu!

Baadhi ya Zaburi za Daudi huitwa, “Mikitami”, ambayo maana yake ni “Zaburi ya dhahabu.” Hakika ni lazima tuimbe mmojawapo wa hizi. Zaburi zetu lazima ziwe za dhahabu tunapoimba juu ya Kichwa cha Kanisa, aliye kama dhahabu safi. Ya thamani zaidi kuliko fedha au dhahabu ni ile gharama isiyokadirika aliyoilipa kwa fidia yetu. Naam, enyi wana wa upatano wa muziki, leteni nyimbo zenu zenye mahadhi mazuri zaidi hapa, na Mwokozi wenu na apate Zaburi zenu za dhahabu!

Zaburi fulani katika Agano la Kale zimeitwa, “Juu ya Shoshanimu,” yaani, “Juu ya nyinyoro.” Enyi nafsi za mabikira, ambao mioyo yao imeoshwa katika damu, na imefanywa nyeupe na safi, leteni vinanda vyenu vya wimbo:-

“Basi hapa, leteni muziki wenu,

Pigeni kwa sauti kila uzi wa furaha!”

Mioyo yenu, itakapokuwa katika hali yake bora, itakapokuwa safi zaidi, na kutakaswa zaidi kutoka takataka za kidunia, na impe Yesu utukufu wake na ubora wake.

Kisha kuna Zaburi nyingine zilizowekwa wakfu “Kwa wana wa Kora.” Kama kisio hili ni sahihi, sababu tunayoipata jina hili, “Kwa wana wa Kora”—“wimbo wa mapenzi,”—lazima iwe hii: kwamba Kora, Dathani, na Abiramu walipomezwa, wana wa Dathani na Abiramu walimezwa pia; lakini wana wa Kora hawakuangamia. Kwa nini hawakuangamizwa, hatuwezi kusema. Labda ni kwamba neema kuu iliwahurumia wale ambao haki ingeweza kuwahukumu; na “wana wa Kora” tangu wakati ule wakafanywa waimbaji watamu wa patakatifu; na kila mara palipokuwa na “wimbo wa mapenzi” maalum, ulikuwa daima ukiwekwa wakfu kwao. Ah! tutakuwa na mmojawapo wa nyimbo hizo za upendo usiku wa leo, kuzunguka meza, kwa maana sisi pia, tumeokolewa kwa neema ipendelezayo. Tutaimba juu ya Mpenzi wa mbinguni, na maji mengi ambayo hayangeweza kuuzima upendo wake.

“Upendo, mkubwa hata kiasi kwamba hakuna kiwezacho kuufunga;

Upendo, wenye kina mno usioweza kupimwa na fikira

Upendo, uliomfanya Bwana wa vyote

Kunywa pakanga na nyongo.

“Upendo, uliomwongoza msalabani,

Akichukua huko hasara isiyoelezeka;

Upendo, uliomleta hata gizani

Mwa kaburi lenye baridi na giza.

“Upendo, uliomfanya toka hapo afufuke

Juu sana ya mbingu zenye nyota,

Huko kwa utunzaji wa upole na wa upendo,

Kushiriki huzuni za watu wake wote.

“Upendo, usiotaka kumwacha apumzike

Hata wateule wake wote wabarikiwe;

Hata wote ambao kwa ajili yao alikufa

Waishi wakifurahi ubavuni pake.”

Hatujaimaliza hata nusu ya orodha, lakini ni wazi kwamba, tukiketi kwenye meza ya Bwana, hatutakosa nyimbo za sifa zinazofaa. Labda hakuna wimbo mmoja utakaokidhi kabisa hisia za wote; na ingawa hatungewaandikia wimbo, tungemwomba Roho Mtakatifu aandike sasa roho ya sifa juu ya mioyo yenu, ili, mkiketi hapa, mpate “baada ya kula” kuimba “wimbo.”

IV. Kwa dakika moja au mbili na tuulize—“wimbo utakuwa wa sauti gani?” Lazima uwe wa pekee, kwa maana kama tutaimba “wimbo” usiku wa leo, kuzunguka meza, sauti lazima iwe na sehemu zote za muziki. Yule mwamini kule ana moyo mzito kwa sababu ya huzuni nyingi, misiba, na kukesha kando ya wagonjwa. Ampenda Bwana wake, na angependa kumsifu, lakini nafsi yake yakataa kutumia mbawa zake. Ndugu, tutakuwa na sauti ambayo waweza kuungana nayo, nawe utaongoza besi. Utaimba juu ya ushirika wako na Mpenzi wako katika mateso yake; jinsi yeye, pia, alivyompoteza rafiki; jinsi alivyotumia usiku mzima bila usingizi; jinsi nafsi yake ilivyokuwa na huzuni nyingi. Lakini sauti isiwe yote besi, au isingetufaa baadhi yetu usiku wa leo, kwa maana twaweza kufikia noti iliyo juu zaidi. Tumemwona Bwana, na roho yetu imefurahi katika Mungu Mwokozi wetu. Twataka kupaza kwaya juu; naam, kuna mioyo ya kweli hapa ambayo nyakati nyingine imejaa furaha hata itataka muziki maalum uandikwe kwa ajili yao. “Kama ni katika mwili, sijui; au kama ni nje ya mwili, sijui:” alisema Paulo, na hivyo wamesema wengine tangu wakati ule, Kristo alipokuwa pamoja nao. Ah! ndipo wamelazimika kupanda hata noti zilizo juu zaidi, hata upeo wa juu kabisa wa wimbo.

Kumbukeni, wapenzi, kwamba Mwokozi yule yule atakayekubali makelele ya furaha ya wenye nguvu, atapokea pia sauti za huzuni za wanyonge na waliao. Enyi wadogo, enyi watoto wachanga katika neema, mwaweza kupaza sauti, “Hosana,” na Mfalme hatawanyamazisha; nanyi enyi wenye nguvu, kwa nguvu zenu zote za imani, mwaweza kupaza sauti, “Haleluya!” na sauti zenu zitakubaliwa pia.

Njoni, basi, na tuwe na sauti ambayo sote twaweza kuungana nayo; lakini ah! hatuwezi kufanya moja itakayowafaa wafu—wafu, namaanisha, “katika makosa na dhambi”—na kuna baadhi kama hao hapa. Oh, Mungu na aifungue vinywa vyao, na kuifungua ndimi zao; lakini kwa habari ya sisi tulio hai kwa Mungu, na tuchangie, tunapoijia meza, kila mmoja fungu lake la muziki, na hivyo kufanya wimbo wa upatano uliochanganyika, wenye sehemu nyingi, wimbo mmoja mkuu wa sifa ulioungana kwa Yesu Bwana wetu!

Hatupaswi kuchagua sauti kwa meza ya ushirika ambayo si laini sana. Hizi si mada za kelele ambazo tunazoshughulika nazo tunapokaa hapa. Mwokozi anayevuja damu, aliyevikwa vazi lililotiwa rangi kwa damu—hii ni mada ambayo lazima uishughulikie kwa upole wa upendo, kwa maana kila kilicho kikali ni kisichofaa hapa. Ingawa sauti ni laini, lazima pia iwe tamu. Nyamazeni, enyi mashaka; kaeni kimya, enyi hofu; tulieni, enyi masumbufu! Kwa nini mwaja hapa? Muziki wangu lazima uwe mtamu na laini nimwimbapo yeye. Lakini oh! lazima pia uwe na nguvu; lazima kuwe na mvumo kamili katika sifa yangu. Vuteni vibonye, na kinanda kivume kwa sauti kuu! Kwa utimilifu mvumo wake wa upatano wa radi na upae mbinguni; kila noti na ipigwe kwa sauti yake kubwa zaidi. “Msifuni kwa matoazi yaliayo, kwa matoazi yenye sauti kubwa; kwa kinubi chenye sauti ya adhama.” Laini, tamu, na yenye nguvu, muziki na uwe.

Ole! walalamika kwamba nafsi yako haipo katika sauti nzuri. Basi mwombe Bwana azipange nyuzi za moyo. Zile “Sela” tunazozikuta mara nyingi katika Zaburi hudhaniwa na wasomi wengi kumaanisha, “Panga nyuzi za kinubi katika sauti nzuri:” kweli twahitaji “Sela” nyingi, kwa maana mioyo yetu daima haipangwi vizuri. Oh, laiti usiku wa leo Bwana angemwezesha kila mmoja wetu kutoa ile sala yenye mahadhi ambayo mara nyingi tuimbayo,—

“Nifundishe wimbo fulani wenye mahadhi,

Uimbwao na ndimi za moto huko juu:

Sifu mlima—oh, niimarishe juu yake,

Mlima wa upendo wa Mungu usiobadilika!”

V. Twafunga kwa kuuliza,—ni nani atakayeuimba wimbo huu?

Tukiketi kuzunguka meza ya Baba, tutapaza wimbo wa furaha, lakini ni nani atakayeufanya? “Mimi,” asema mmoja; “na sisi,” wasema wengine. Ni sababu gani inayowafanya wengi wawe tayari kuungana? Sababu yaonekana katika ule mstari tuliokuwa tukiuimba sasa hivi,—

“Wakati Yeye ni mada ya wimbo,

Ni nani awezaye kukataa kuimba?”

Nini! Mkristo anyamaze wakati wengine wanamsifu Bwana wake? La; lazima aungane katika wimbo. Shetani hujaribu kuwanyamazisha watu wa Mungu, lakini hawezi, kwa maana Bwana hana mtoto aliyefungwa ulimi katika jamaa yake yote. Wote waweza kunena, na wote waweza kulia, hata kama wote hawawezi kuimba, nami nadhani kuna nyakati ambapo wote waweza kuimba; naam, ni lazima, kwa maana mwaijua ile ahadi, “Ndipo ulimi wa bubu utakapoimba.” Hakika, Yesu aongozapo wimbo, kama pakiwa na wanyamavu wowote katika jamaa ya Bwana, ni lazima waanze kulisifu jina la Bwana. Baada ya kichwa cha Jitu Kata-Tamaa kukatwa, Kristiana na Bwana Moyo-Mkuu, na wote wengine, walitoa vyakula vyao vizuri zaidi, na kufanya karamu, na Bwana Bunyan asema kwamba, walipokwisha kula karamu, walicheza. Katika mchezo palikuwa na mchezaji mmoja wa ajabu, yaani, Bwana Tayari-Kuchechemea. Basi, Bwana Tayari-Kuchechemea kwa kawaida alitembea kwa magongo, lakini kwa mara moja aliyaweka kando. “Nami,” asema Bunyan, “nawahakikishieni alicheza vyema kwa miguu yake!” Hii kwa njia ya kimzaha yatuonyesha kwamba, nyakati nyingine, hata wale wenye huzuni sana, akina Tayari-Kuchechemea, wanapoona kichwa cha Jitu Kata-Tamaa kikikatwa, wanapoona mauti, kuzimu, na dhambi vikiongozwa mateka kwa ushindi katika magurudumu ya gari la ushindi la Kristo, wahisi kwamba hata wao lazima kwa mara moja wajiingize katika wimbo wa furaha. Basi, niulizapo swali usiku wa leo, “Ni nani atakayeimba?” nategemea kwamba Tayari-Kuchechemea ataahidi, “Mimi.”

Huna faraja nyingi nyumbani, labda; kwa kazi ngumu sana wapata kile kidogo. Jumapili kwako ni siku ya pumziko la kweli, kwa maana wafanyishwa kazi kwa ukatili juma zima. Mashavu yako hayo, maskini msichana, yanazidi kupauka, na ni nani ajuaye kama zile mistari ya kusikitisha ya Hood yaweza kuwa kweli juu yako?—

“Shona, shona, shona,

Katika umaskini, njaa, na uchafu,

Ukishona kwa mara moja, kwa uzi maradufu,

Sanda na shati pia.”

Lakini, dada yangu, waweza hakika kufurahi usiku wa leo licha ya haya yote. Yaweza kuwa kidogo duniani, lakini kuna mengi mbinguni. Yaweza kuwa faraja ndogo kwako hapa mbali na Kristo; lakini oh! utakapopanda, kwa imani, katika utukufu wake, nafsi yako yafurahi. Utakuwa tajiri kama walio matajiri zaidi usiku wa leo kama Roho Mtakatifu atakuleta tu mezani, na kukuwezesha kumla Bwana na Mwalimu wako. Labda umekuja hapa usiku wa leo wakati ambao haikupasa kufanya hivyo. Tabibu angekuambia ubaki kitandani mwako, lakini uling’ang’ania kuja katika nyumba ambako Bwana amekutana nawe mara nyingi sana. Nategemea kwamba tutaisikia sauti yako katika wimbo. Yaonekana palikuwa katika siku za Daudi na mambo mengi ya kunyamazisha sifa ya Mungu, lakini Daudi alikuwa mmoja ambaye angeimba. Napenda usemi wake ule, ambapo shetani aonekana kuja juu, na kuweka mkono wake kinywani pake, na kusema, “Nyamaza.” “La,” asema Daudi, “nitaimba.” Tena shetani ajaribu kumnyamazisha, lakini Daudi hanyamazishwi, kwa maana mara tatu alisema, “Nitaimba, naam, nitamwimbia Bwana sifa.” Bwana na akufanye uazimie usiku huu kwamba utamsifu Bwana Yesu kwa moyo wako wote!

Ole! kuna wengi kati yenu hapa usiku wa leo ambao nisingeweza kuwaalika kwenye karamu hii ya wimbo, na ambao hamngeweza kweli kuja kama mngealikwa. Dhambi zenu hazijasamehewa; nafsi zenu hazijaokolewa; hamjamwamini Kristo; bado mko katika giza la asili, bado katika uchungu wa nyongo, na katika vifungo vya uovu. Je, itakuwa hivyo daima? Je, mtajiangamiza wenyewe? Je, mmefanya mapatano na mauti, na agano na kuzimu? Rehema yavuta subira! Uvumilivu waendelea! Yesu asubiri! Kumbukeni kwamba alitundikwa msalabani kwa ajili ya wenye dhambi kama vile mlivyo ninyi, na kwamba kama mkimwamini sasa, mtaokolewa. Tendo moja la imani, na dhambi zote mlizozitenda zafutwa. Mtazamo mmoja tu wa jicho la imani kwenye vidonda vya Masihi, na mzigo wenu wa uovu wavingirishwa hata vilindini vya bahari, nanyi mmesamehewa kwa dakika moja!

“Oh!” asema mmoja, “laiti Mungu angenijalia niweze kuamini!” Nafsi maskini, Mungu na akusaidie kuamini sasa! Mungu alijitwalia mwili wetu; Kristo alizaliwa kati ya watu, na kuteswa kwa sababu ya hatia ya mwanadamu, akifanywa kuteswa “yeye Mwenye haki kwa ajili ya wasio haki, ili atulete kwa Mungu.” Kristo aliadhibiwa katika nafasi, mahali, na badala ya kila mwanamume na mwanamke atakayemwamini. Kama mkimwamini, aliadhibiwa kwa ajili yenu; nanyi hamtaadhibiwa kamwe. Madeni yenu yamelipwa, dhambi zenu zimesamehewa. Mungu hawezi kuwaadhibu, kwa maana amemwadhibu Kristo badala yenu, naye hataadhibu mara mbili kwa kosa moja. Kuamini ni kutumaini. Kama sasa mtaikabidhi nafsi yenu kwake kabisa, mmeokolewa, kwa maana aliwapenda, na kujitoa mwenyewe kwa ajili yenu. Mtakapojua hili, na kulihisi kuwa kweli, ndipo njoni kwenye meza ya Bwana, na kuungana nasi, tutakapoimba, baada ya kula, wimbo wetu,—

“‘Imekwisha!’—Oh, furaha iliyoje

Maneno haya yenye kupendeza yatoayo!

Baraka za mbinguni zisizo na kipimo

Zatujilia kutoka kwa Kristo Bwana:

‘Imekwisha!’

Watakatifu, yaandikeni maneno ya kufa.

“Pangeni upya vinubi vyenu, enyi maserafi,

Unganeni kuimba mada yenye kupendeza;

Wote waliomo duniani, na wote waliomo mbinguni,

Unganeni kumsifu jina la Imanueli!

Haleluya!

Utukufu kwa Mwana-Kondoo avujaye damu!”

Ukurasa 1 / 1 · 23 dakika zimebaki katika sura