Mawazo kwa Saa ya Utulivu
Desemba

Sura 12 · dakika 10 za kusoma

Desemba

Desemba 1

Pasipo Kristo. Efe. 2:12.

Pasipo tumaini la kutuchangamsha, Nahodha wa kutuongoza, Rafiki wa kutushauri, neema ya kututegemeza, mbingu za kutukaribisha, na Mungu wa kututuliza!—Selected.

Desemba 2

Ninapokuwa dhaifu, ndipo nilipo na nguvu. 2 Kor. 12:10.

Hii ndiyo njia ya Mungu. Twasonga mbele kwa kurudi nyuma, twapata nguvu kwa kuwa dhaifu, twapata hekima kwa kuwa wapumbavu.—F. Whitfield.

Desemba 3

Watu watakatifu wa Mungu walinena wakiongozwa na Roho Mtakatifu. 2 Pet. 1:21.

Biblia ni maandishi ya Mungu aliye hai. Kila herufi iliandikwa kwa kidole cha Mwenyezi. Kila neno lililomo lilidondoka kutoka midomo ya milele. Kila sentensi iliamriwa na Roho Mtakatifu. Ijapokuwa Musa alitumika kuandika historia zake kwa kalamu yake ya moto, Mungu aliiongoza kalamu ile. Yamkini Daudi aligusa kinubi chake, na kuacha zaburi tamu za wimbo zikidondoka kutoka vidoleni mwake; lakini Mungu aliisogeza mikono yake juu ya nyuzi hai za kinubi chake cha dhahabu. Sulemani aliimba nyimbo za mapenzi na kutoa maneno ya hekima kamili; lakini Mungu aliiongoza midomo yake, na kumfanya mhubiri kuwa fasaha. Nikimfuata Nahumu mwenye ngurumo, farasi zake wanapolima maji; au Habakuki, aonapo hema za Kushani katika taabu; nikimsoma Malaki, dunia iunguapo kama tanuru; nikigeukia ukurasa laini wa Yohana, anenaye juu ya upendo; au sura ngumu za Petro, anenaye juu ya moto ukiwateketeza adui za Mungu; nikigeukia Yuda, arushaye laana juu ya adui za Mungu—kila mahali namkuta Mungu akinena; ni sauti ya Mungu, si ya mwanadamu; maneno ni maneno ya Mungu; maneno ya Yeye aliye wa Milele, Asiyeonekana, Mwenyezi, Yehova wa vizazi vyote. Biblia hii ni Biblia ya Mungu; nami niionapo, nadhani nasikia sauti ikichipuka ndani yake, ikisema, “Mimi ni Kitabu cha Mungu. Ee mwanadamu, nisome. Mimi ni maandishi ya Mungu. Chunguza ukurasa wangu, kwa maana niliandikwa na Mungu. Nipende, kwa maana Yeye ndiye Mtungaji wangu, nawe utamwona akionekana na kudhihirika kila mahali.”—Spurgeon.

Desemba 4

Wote wakamwacha, wakakimbia. Marko 14:50.

Kutengana kamwe hakutoki upande wake.—J. Hudson Taylor.

Desemba 5

Mfalme Belshaza akafanya karamu kubwa. Dan. 5:1.

Kulikuwa na Mgeni mmoja asiyealikwa, lakini alikuja, na kazi ya kidole chake ikang’aa ukutani.—Selected.

Desemba 6

Anyweshaye atanyweshwa naye mwenyewe. Mith. 11:25.

Maisha yenye matokeo na maisha yapokeayo ni kitu kimoja. Hakuna pigo la mkono lifanyalo kazi fulani kwa Mungu ambalo halivuni pia zaidi ya kweli ya Mungu, na kuliingiza katika hazina ya uzima.—Phillips Brooks.

Desemba 7

Wakamjia, wakamletea mtu mwenye kupooza. Marko 2:3.

Kama isingekuwa kwa sababu ya kupooza, mtu huyu asingemwona Kristo kamwe!—Selected.

Desemba 8

Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, wala usisahau fadhili zake zote . . . akutiaye taji ya fadhili na rehema. Zab. 103:2, 4.

Twanena juu ya darubini ya imani, lakini nadhani twahitaji zaidi hadubini ya upendo makini na wenye shukrani. Tumia hili kwa vipande vidogo vya maisha yetu ya kila siku, katika nuru ya Roho, nayo yatokea kwa ajabu jinsi gani!—Frances Ridley Havergal.

Desemba 9

Upitapo katika maji nitakuwa pamoja nawe. Isa. 43:2.

Uwepo wa Mungu katika jaribu ni bora zaidi kuliko kuepushwa na jaribu. Huruma ya moyo wake pamoja nasi ni tamu zaidi sana kuliko nguvu za mkono wake kwa ajili yetu.—Selected.

Desemba 10

Ndipo mtakapopambanua kati ya mwenye haki na mwovu. Mal. 3:18.

Anne wa Austria akamwambia Kardinali Richelieu: “Mungu halipi mwishoni mwa kila juma, lakini hulipa mwishoni!”—Selected.

Desemba 11

Uzima wenu ni nini? Maana ni ukungu utokeao kwa kitambo kidogo, kisha hutoweka. Yak. 4:14.

“Maisha ni moja tu; karibu yatapita—
Na kilichofanywa kwa Kristo tu ndicho kitakachodumu.”—Selected.

Desemba 12

Yeye (Yesu) . . . akatazama juu mbinguni. Marko 6:41.

Katika kumtumikia Mungu, kwanza tazama mbinguni. Ni mpango mtukufu. Mara kwa mara Bwana wetu Yesu Kristo alitazama mbinguni na kusema, “Baba.” Na tumwige Yeye; ingawa twasimama duniani, na tuwe na mwenendo wetu mbinguni. Kabla hujatoka nje, kama ungetaka kuulisha ulimwengu, kama ungetaka kuwa baraka katikati ya ukame na njaa ya kiroho, inua kichwa chako kuelekea mbinguni. Ndipo uso wako wenyewe utang’aa, mavazi yako yenyewe yatanukia manemane na uudi na mdalasini kutoka majumba ya pembe za ndovu ambako umekuwa pamoja na Mungu na Mwokozi wako. Utatiwa muhuri wa heshima na nguvu za utumishi wa Mungu Aliye Juu Sana.—McNeil.

Desemba 13

Wanafunzi waliitwa Wakristo kwa mara ya kwanza huko Antiokia. Mdo. 11:26.

Jina hili ladokeza kwamba dalili iliyo dhahiri itokezwayo na tabia yetu, vilevile na kwa maneno yetu, iwe ni kwamba sisi ni mali ya Yesu Kristo. Yeye apaswa waziwazi kuwa kitovu na kiongozi, msukumo na kielelezo, nguvu na thawabu, za maisha yetu. Sisi ni Wakristo. Hilo lapaswa kuwa dhahiri kwa watu wote waone, tukinena au tukinyamaza.

Je, ndivyo ilivyo kwako?—Alex. McLaren.

Desemba 14

Basi kwa kuwa tuna ahadi hizi. 2 Kor. 7:1.

Misitu katika siku za kiangazi imejaa viota vya ndege. Vimefichwa kati ya majani. Ndege wadogo wanajua vilipo; na dhoruba iinukapo, au usiku ukaribiapo, huruka, kila mmoja kwenda kiota chake mwenyewe. Vivyo hivyo ahadi za Mungu zimefichwa katika Biblia, kama viota katika misitu mikubwa; nako huko tunapaswa kukimbilia katika hatari au tisho lolote, tukijificha humo katika kiota cha nafsi yetu hata dhoruba ipite. Hakuna ngome katika ulimwengu huu zisizoweza kushindwa kama maneno ya Kristo.—J. R. Miller.

Desemba 15

Sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; lakini lililo kuu kuliko hayo ni upendo. 1 Kor. 13:13. (R. V.)

Upendo ndilo jambo kuu kuliko yote ambalo Mungu aweza kutupa: kwa maana Yeye mwenyewe ni Upendo; nalo ndilo jambo kuu kuliko yote tuwezalo kumpa Mungu: kwa maana litajitoa sisi wenyewe, na kuchukua pamoja nalo yote yaliyo yetu.—Jeremy Taylor.

Desemba 16

Yeye (Tomaso) . . . akasema, Nisipoona . . . mimi sisadiki. . . . Yesu . . . akasema . . . Usiwe asiyeamini, bali aaminiye. Yoh. 20:25, 27.

Kila shaka iliyo moyoni mwa Mkristo ni dharau ifanyiwayo Neno la Mungu, na dhabihu ya Kristo.—Selected.

Desemba 17

Lutu . . . akapiga hema yake kuelekea Sodoma. Mwa. 13:12.

Na punde si punde Lutu akahamia Sodoma; na kabla ya muda mrefu Sodoma ikahamia ndani yake.—Theodore Cuyler.

Desemba 18

Unitakase na makosa ya siri. Zab. 19:12.

Ulimwengu wahitaji watu walio huru na makosa ya siri. Watu wengi ni huru na makosa makubwa ya waziwazi.—Selected.

Desemba 19

Msikiaji wa neno . . . mtendaji wa kazi. Yak. 1:23, 25.

Dini yaweza kujifunzwa siku ya Jumapili, lakini yaishi katika kazi ya siku za juma. Mwenge wa dini waweza kuwashwa kanisani, lakini hufanya kuwaka kwake dukani na barabarani. Dini hutafuta uhai wake katika maombi, lakini huishi uhai wake katika matendo. Hupandwa chumbani cha faragha, lakini hufanya kukua kwake huko nje ulimwenguni. Hujipamba mbawa kwa kuruka katika nyimbo za sifa, lakini kuruka kwake halisi kuko katika kazi za upendo. Huazimia na kutafakari juu ya uaminifu isomapo somo lake la Kikristo katika Kitabu cha Kweli, lakini “mwaminifu ni yule afanyaye kwa uaminifu.” Huvaa silaha zake katika misaada na vitegemezo vyote vya patakatifu kama chumba chake cha kuvalia, lakini hupigana kwa ajili ya lililo haki, tukufu, na jema katika shughuli zote za maisha halisi, na uwanja wake wa vita ni shamba pana lote la maisha.—John Doughty.

Desemba 20

Hamjui litakalokuwa kesho. Yak. 4:14.

“Kesho” ni mshirika mkuu wa shetani—Goliathi hasa ambaye kwake anatumaini ushindi. “Sasa” ni kijana aliyetumwa dhidi yake. . . . Ulimwengu utakubali kwa hiari kuwa Wakristo kesho iwapo Kristo atawaruhusu kuwa wa kidunia leo.—William Arnot.

Desemba 21

Bahari ilizidi kuchafuka na kuwa na dhoruba. Yona 1:11.

Dhambi katika nafsi ni kama Yona katika merikebu. Hugeuza maji tulivu kabisa kuwa bahari yenye dhoruba.—Selected.

Desemba 22

Msiwe na shaka, bali wafuasi wa wale ambao kwa imani na uvumilivu wanazirithi ahadi. Ebr. 6:12.

Mungu hutoa ahadi. Imani huiamini. Tumaini hulitazamia. Uvumilivu hulingoja kwa utulivu.—Selected.

Desemba 23

Nenda ukaketi mahali pa mwisho. Luka 14:10.

Yeye aliye radhi kuchukua mahali pa chini kabisa siku zote atapata nafasi ya kuketi; hakuna msongamano mkubwa wa kugombania mahali pabaya zaidi. Hakuna kusukumana nyuma kama kulivyo mbele; basi kama tungetaka kustarehe, twafanya vema kukaa nyuma.—Thomas Champness.

Desemba 24

Dumuni katika maombi. Kol. 4:2.

Maombi yetu mara nyingi hufanana na hila za kifisadi za watoto wa mjini, wanaogonga milango ya majirani zao kisha kukimbia; mara nyingi twagonga mlango wa mbinguni kisha kukimbilia katika roho ya ulimwengu; badala ya kungoja kuingizwa na kujibiwa, twatenda kana kwamba twaogopa maombi yetu yasije yakajibiwa.—Williams.

Desemba 25

Wingi wa jeshi la mbinguni wakimsifu Mungu, na kusema, Atukuzwe Mungu juu mbinguni. Luka 2:13, 14.

Malaika walikuwa wamehudhuria katika matukio mengi matukufu, nao walikuwa wameungana katika kwaya nyingi za dhati kwa ajili ya sifa za Muumba wao Mwenyezi. Walikuwepo wakati wa uumbaji: “Nyota za asubuhi ziliimba pamoja, na wana wote wa Mungu wakapiga kelele kwa furaha.” Walikuwa wameona sayari nyingi zikifinyangwa kati ya viganja vya Yehova, na kuzungushwa kwa mikono yake ya milele katika ukubwa usio na mwisho wa anga. Walikuwa wameimba nyimbo za dhati juu ya ulimwengu mwingi ambao Yule Mkuu alikuwa ameuumba. Hatuna shaka, mara nyingi walikuwa wameimba, “Baraka na heshima, na utukufu, na fahari, na nguvu, na mamlaka, na uweza, viwe kwake Yeye aketiye juu ya kiti cha enzi,” akijidhihirisha katika kazi ya uumbaji. Wala sina shaka, kwamba nyimbo zao zilikuwa zimeongezeka nguvu katika vizazi vyote. Kama vile walipoumbwa kwanza, pumzi yao ya kwanza ilikuwa wimbo, vivyo hivyo walipomwona Mungu akiumba ulimwengu mpya, ndipo wimbo wao ulipopokea sauti nyingine; wakapaa juu kidogo zaidi katika daraja za ibada. Lakini wakati huu, walipomwona Mungu akiinama kutoka kiti chake cha enzi na kuwa mtoto mchanga aning’iniaye kifuani mwa mwanamke, waliinua sauti zao juu zaidi tena; na kufikia mwisho kabisa wa muziki wa kimalaika, wakapata sauti za juu kabisa za mizani ya kimungu ya sifa nao wakaimba, “Atukuzwe Mungu juu mbinguni,” kwa maana katika wema zaidi walihisi Mungu hangeweza kwenda juu zaidi. Hivyo sifa yao ya juu kabisa walimpa katika tendo lililo juu kabisa la Uungu wake.—Spurgeon.

Desemba 26

Hasha, nisione fahari isipokuwa katika msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Gal. 6:14.

Msalaba ni kitovu kikuu cha ulimwengu wa kimaadili wa Mungu! Kwa kitovu hiki Mungu daima alielekeza, na jicho la imani daima lilitazama mbele, hata Mwokozi alipokuja. Na sasa ni lazima daima tugeukie msalaba huo kama kitovu cha baraka zetu zote, na msingi wa ibada yetu yote, duniani na mbinguni pia—katika wakati huu na katika milele yote.

Desemba 27

Yeye yu hai daima. Ebr. 7:25.

Ni tumaini letu kwa ajili yetu wenyewe, na kwa ajili ya kweli yake, na kwa ajili ya wanadamu. Watu huja na kuondoka. Viongozi, waalimu, wafikiriji, hunena na kufanya kazi kwa kitambo, kisha hunyamaza na kuwa dhaifu. Yeye hudumu. Wao hufa, lakini Yeye huishi. Wao ni taa zilizowashwa, na kwa hiyo, mapema au baadaye huzimwa, bali Yeye ndiye Nuru ya kweli ambako wao huchota mng’ao wao wote, naye huangaza milele.—Alex. McLaren.

Desemba 28

Urafiki wa dunia ni uadui na Mungu. Yak. 4:4.

Ni kama mtambaazi ulivyo na mwaloni. Mtambaazi waweza kuupa mwaloni sura tukufu, nzuri, lakini wakati wote unakula uhai wake. Je, twafanya maridhiano na adui za Mungu? Je, twakumbatiwa na ulimwengu kwa heshima zake, anasa zake, sifa zake? Hili laweza kutuongezea machoni pa ulimwengu, lakini nguvu zetu zapotea.—Denham Smith.

Desemba 29

Yeye (Hana) . . . akamwomba Bwana, akalia sana . . . akanena moyoni mwake. 1 Sam. 1:10, 13.

Kwa shughuli ya kweli katika kiti cha rehema nipe ombi la kutengenezwa nyumbani, ombi litokalo katika vilindi vya moyo wangu, si kwa sababu niliizua, bali kwa sababu Mungu Roho Mtakatifu, aliliweka humo, na kulipa nguvu hai kiasi kwamba nisingeweza kujizuia kuliachilia litoke. Ijapokuwa maneno yako yamevunjika, na sentensi zako hazishikamani, kama tamaa zako ni za dhati, kama ni kama makaa ya mretemu, yakiwaka kwa mwali mkali, Mungu hatajali jinsi yanavyopata kutamkwa. Kama huna maneno, huenda utaomba vema zaidi bila hayo kuliko nayo. Kuna maombi yavunjayo migongo ya maneno; ni mazito mno kwa lugha yoyote ya kibinadamu kuyachukua.—Spurgeon.

Desemba 30

Nuhu akapata neema machoni pa Bwana. Mwa. 6:8.

Nuhu alipata neema kwa njia ile ile ambayo Paulo alipata rehema (1 Tim. 1:16), yaani, kwa rehema kumshika.—Selected.

Desemba 31

Tumaini hilo tunalo kama nanga ya nafsi. Ebr. 6:19.

Tia nanga kwenye kiti cha enzi cha Mungu, kisha ufupishe kamba!—Selected.

Ukurasa 1 / 1 · 10 dakika zimebaki katika sura