Ukaaji wa Bwana Ndani Yetu ·Kuingia Katika Pumziko

Sura 4 · dakika 11 za kusoma

Kuingia Katika Pumziko

Waebrania 4: 1.—Kwa hiyo, kwa kuwa ahadi ya kuingia katika pumziko lake ingaliko, na tuogope isije ikaonekana kwamba ye yote miongoni mwenu amepungukiwa kulifikia.

Waebrania 4: 11.—Basi na tujitahidi kuingia katika pumziko lile, ili mtu ye yote asianguke kwa mfano ule ule wa kuasi.

Nataka, kwa njia iliyo rahisi kupita zote, kujibu swali hili: “Mtu huingiaje katika pumziko lile?” na kuonyesha hatua rahisi azichukuazo, zote zikiwa zimefungamana katika tendo lile moja la kujisalimisha na imani. Nami nadhani hatua ya kwanza ni hii: kwamba mtu hujifunza kusema, “Naamini, kwa moyo wangu wote, kwamba kuna pumziko katika maisha ya imani.”

Israeli walipita katika hatua mbili. Jambo hili limeelezwa vizuri sana katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati: “Naye alitutoa huko, ili atulete huku”—sehemu mbili za kazi ya Mungu ya ukombozi—“Naye alitutoa huko, ili atulete huku, na kutupa nchi aliyowaapia baba zetu.” Kumbukumbu la Torati 6:23. Na jambo hili lawahusu waaminio wote. Wakati wa kuongoka kwako, Mungu alikutoa katika Misri, na Mungu yule yule mwenye uweza wote anatamani sana kukuingiza katika maisha ya Kanaani.

Unajua jinsi Mungu alivyowatoa Waisraeli, lakini hawakumruhusu awaingize, hata ikawalazimu kutanga-tanga miaka arobaini jangwani—huu ndio mfano wa Wakristo wengi mno. Mungu huwatoa katika kuongoka, lakini hawamruhusu awaingize katika yote aliyowaandalia. Kwa mtu aniulizaye, “Nawezaje kuingia katika pumziko?” nasema, kwanza kabisa, nena neno hili, “Naamini kwamba kuna pumziko ambamo Yesu, Yoshua wetu, aweza kumleta nafsi imwaminiyo.” Nawe kama ungependa kujua tofauti iliyoko kati ya maisha yale mawili—maisha uliyokuwa ukiishi, na maisha unayotaka kuyaishi sasa—tazama tu jangwa na Kanaani. Tofauti zake ni zipi? Jangwani, wakitanga-tanga miaka arobaini, mbele na nyuma; katika Kanaani, pumziko kamili katika nchi aliyowapa Mungu. Hiyo ndiyo tofauti kati ya maisha ya Mkristo aliyeingia Kanaani na yule ambaye hajaingia.

Katika kutanga-tanga mbele na nyuma; kuufuata ulimwengu, kisha kurudi na kutubu; kupotoshwa na majaribu, na kurudi ili tu kwenda tena; maisha ya kupanda na kushuka. Lakini katika Kanaani, ni maisha ya pumziko, kwa sababu nafsi imejifunza kutumaini: “Mungu hunilinda kila saa kwa uweza wake mkuu.” Kuna tofauti ya pili: maisha jangwani yalikuwa maisha ya uhitaji; katika Kanaani, maisha ya wingi. Jangwani hapakuwa na kitu cha kula; mara nyingi hapakuwa na maji. Mungu, kwa neema, aliwapa mahitaji yao kwa mana na maji kutoka mwambani. Lakini, hawakuridhika na hayo, na maisha yao yalikuwa ya uhitaji na manung'uniko. Bali katika Kanaani, Mungu aliwapa mashamba ya mizabibu wasiyoyapanda, na nafaka za zamani za nchi zikiwa zinawangoja; nchi ijaayo maziwa na asali; nchi iliyoishi kwa mvua ya Mbinguni na kutunzwa na Mungu Mwenyewe.

Ee, Mkristo, njoo useme leo, “Naamini kuna uwezekano wa badiliko kama hilo, kutoka katika maisha yale ya mauti ya kiroho, na giza, na huzuni, na malalamiko, ambayo mara nyingi nimeishi, kuingia katika nchi ipatiayo kila hitaji; ambamo neema ya Yesu huthibitika kuwa yatosha kila siku, kila saa.”

Sema leo: “Naamini uwezekano kwamba kuna nchi kama hiyo ya pumziko kwa ajili yangu.” Kisha, tofauti ya tatu: Jangwani, hapakuwa na ushindi. Walipojaribu, baada ya kutenda dhambi huko Kadeshi, kupanda kupigana na adui zao, walishindwa. Katika nchi ile waliwashinda adui wote; tokea Yeriko na kuendelea, walikwenda toka ushindi hata ushindi. Na hivyo Mungu angoja, na Kristo angoja, na Roho Mtakatifu angoja, kutoa ushindi kila siku; si kuondolewa majaribu; la, si hivyo; bali katika muungano na Kristo nguvu iwezayo kusema, “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.” “Katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.”

Wafilipi 4:13. Mungu na amsaidie kila moyo kusema hivyo.

Kisha huja hatua ya pili. Nataka useme si tu, “Naamini kuna maisha kama hayo,” bali, pili, “Sijayapata bado.” Sema hivyo. “Sijawahi kuyapata hayo bado.” Wengine waweza kusema, “Nimeyatafuta;” na wengine waweza kusema, “Sijawahi kusikia habari zake;” wengine waweza kusema, “Mara kwa mara nilidhani nimeyapata, lakini nikayapoteza tena.” Kila mmoja na awe mnyofu mbele za Mungu. Na sasa, je, wote ambao bado hawajayapata kwa unyofu, wataanza kusema, “Bwana, hata sasa sijawahi kuyapata”? Na kwa nini ni jambo la maana hivyo kunena hivyo? Kwa sababu, ndugu wapendwa, watu wengine hutaka kuingia katika maisha haya ya pumziko taratibu; na kwa kimya kabisa kujiingiza, lakini Mungu hataki hivyo. Maisha yako jangwani hayakuwa maisha ya huzuni kwako mwenyewe tu bali ya dhambi na kumvunjia Mungu heshima.

Kila kuingia kwa ndani zaidi katika wokovu lazima siku zote kuwe kwa njia ya toba na kuungama. Kwa hiyo, kila Mkristo na awe radhi kusema: “Sikuishi maisha yale, nami nina hatia; nimemvunjia Mungu heshima; nimekuwa kama Israeli; nimemchochea hasira kwa kutokuamini na kuasi kwangu. Ee Mungu, unirehemu!”

Ee, na lipande mbele za Mungu—ungamo la siri: “Sijayapata; ole wangu! Sikumtukuza Mungu kwa maisha katika nchi ya pumziko.”

Kisha huja neno la tatu nataka ulinene, nalo ni: “Ashukuriwe Mungu, maisha hayo ni kwa ajili yangu.” Wengine husema, “Naamini kuna maisha kama hayo, lakini si kwa ajili yangu.” Kuna watu ambao daima husema: “Ee, tabia yangu si thabiti kabisa; nia yangu kwa asili ni dhaifu sana; hali yangu ya moyo ni ya wasiwasi na ya kuchochewa upesi, haiwezekani kwangu kuishi daima bila wasiwasi, nikipumzika katika Mungu.” Ndugu mpendwa, usiseme hivyo. Wasema hivyo kwa sababu moja tu: Hujui atakalokutendea Mungu wako. Anza kuiacha nafsi, ukamtazame Mungu. Lichukue neno hilo la thamani: “Naye alitutoa huko, ili atulete huku.” Mungu aliyewapitisha katika Bahari ya Shamu ndiye Mungu aliyewapitisha katika Yordani hata Kanaani. Mungu aliyekuongoa ndiye Mungu awezaye kukupa kila siku ya maisha haya yaliyobarikiwa.

Anza kusema, kwa mianzo ya imani dhaifu, hata kabla hujayadai, anza hata kwa akili kusema: “Ni kwa ajili yangu; naamini hivyo. Mungu hamnyimi urithi mwana wake ye yote. Atoacho ni kwa ajili ya kila mmoja. Naamini maisha yale yaliyobarikiwa yananingoja. Yamekusudiwa kwa ajili yangu. Mungu anangoja kuyatoa na kuyafanya kazi ndani yangu. Litukuzwe jina lake lililobarikiwa! Nafsi yangu yasema ni kwa ajili yangu pia.” Ee, lichukue neno hilo dogo “mimi,” na kwa kuutazama uso wa Mungu wenyewe uthubutu kusema: “Hazina hii isiyokadirika ni kwa ajili yangu; ni kwa ajili yangu.” Je, umesema hivyo? Sema sasa: “Maisha haya yawezekana kwangu mimi pia.”

Kisha huja hatua ifuatayo, nayo ni: “Siwezi kamwe, kwa juhudi yangu yo yote, kuyashika; ni Mungu ndiye lazima anipe.” Nataka uwe hodari sana kusema, “Ni kwa ajili yangu.” Lakini kisha nataka ujiangushe chini kabisa useme, “Siwezi kuyakamata; siwezi kujitwalia mimi mwenyewe.” Basi wawezaje kuyapata? Ashukuriwe Mungu, akiisha kukushusha chini katika utambuzi wa kutokuwa na msaada kabisa na kukata tamaa ya nafsi, ndipo huja wakati ambapo aweza kukukaribia na kukuuliza, “Je, utamwamini Mungu wako aifanye kazi hii ndani yako?” Wakristo wapendwa sana, sema moyoni mwako: “Siwezi kamwe, kwa juhudi yo yote, kumshika Mungu, wala kujitwalia hili mimi mwenyewe; ni kipawa cha Mungu.” Uithamini hali hii ya kutokuwa na uwezo iliyobarikiwa.

Ni Yeye aliyetutoa, ndiye Mwenyewe lazima atuingize.

Watu hushangaa wanaposikia mahubiri mengi hivyo juu ya imani, na maombi ya bidii hivyo ya kuamini, nao huuliza kwa nini wao hawawezi kuamini. Kuna jibu moja tu: Ni nafsi. Nafsi inafanya kazi; inajaribu, na kujitahidi, nayo lazima ishindwe. Lakini utakapofika mwisho wa nafsi na kuweza tu kulia, “Bwana, unisaidie! Bwana, unisaidie!”, ndipo wokovu u karibu; amini hilo. Ni Mungu aliyewaingiza watu. Ni Mungu atakayekuingiza wewe.

Mtu apaswa kuwa radhi, kwa ajili ya pumziko hili, kuacha kila kitu. Neema ya Mungu ni ya bure kabisa. Hutolewa pasipo fedha na pasipo thamani. Na bado, kwa upande mwingine, Yesu alisema kwamba kila mtu atakaye lulu ile ya thamani kubwa lazima atoe sadaka ya vyote alivyo navyo, lazima auze vyote alivyo navyo ili aununue lulu ile.

Haitoshi kuuona uzuri, na uvutio, na utukufu, na kwa karibu kuionja furaha na shangwe ya maisha haya ya ajabu kama yalivyowekwa mbele yako. Lazima uwe mmiliki, mwenye shamba. Yule mtu aliyeliona shamba lenye hazina, na yule mtu aliyeiona lulu ile kubwa, wote walifurahi; lakini walikuwa bado hawajaipata. Walikuwa wameipata kwa kuiona, wameitazama, wameitamani, wamefurahi kwayo, lakini walikuwa bado hawajaimiliki. Hata walipokwenda na kuuza vyote, kuacha kila kitu, na kununua ile ardhi, na kununua ile lulu.

Ndugu, kuna mengi sana yapasayo kuachwa: ulimwengu, anasa zake, upendeleo wake, na maoni yake mema.

Wapaswa kusimama mbele ya ulimwengu katika hali ile ile aliyosimama Yesu. Ulimwengu ulimkataa na kumtupa nje, nawe wapaswa kuishika nafasi ya Bwana wako, ambaye wewe u wake, na kufuatana na Kristo aliyekataliwa. Wapaswa kuacha kila kitu. Wapaswa kuacha yote yaliyo mema ndani yako na kunyenyekezwa katika mavumbi ya mauti.

Na si hayo tu. Maisha yako ya dini yaliyopita na uzoefu na mafanikio—wapaswa kuyaacha yote na kuwa si kitu, ili Mungu peke yake apate utukufu. Mungu amekutoa katika kuongoka; yalikuwa maisha ya Mungu Mwenyewe aliyokupa: lakini uliyanajisi kwa kuasi na kutokuamini. Yaache yote. Acha hekima yako yote, na mawazo yako mwenyewe juu ya kazi ya Mungu.

Tazama jinsi ilivyo vigumu kwa mhudumu wa Injili kuacha hekima yake yote, na kuiweka miguuni pa Yesu, kuwa mpumbavu na kusema: “Bwana, sijui neno lo lote kama inipasavyo kulijua. Nimekuwa nikihubiri Injili, na jinsi nilivyoona kidogo utukufu wa nchi iliyobarikiwa na maisha yaliyobarikiwa!” Kwa nini Roho aliyebarikiwa hawezi kutufundisha kwa ufanisi zaidi? Hakuna sababu ila hii: hekima ya mwanadamu huizuia; hekima ya mwanadamu huizuia nuru ya Mungu isiangaze ndani. Na hivyo twaweza kusema mambo mengine; acha yote. Wengine waweza kuwa na dhambi ya pekee ya kuiacha. Aweza kuwapo Mkristo mwanamume aliye na hasira na ndugu yake. Aweza kuwapo Mkristo mwanamke aliyegombana na jirani yake. Waweza kuwapo marafiki wasioishi kama ipasavyo. Waweza kuwapo Wakristo washikao sana kitu fulani kidogo cha shaka, wasio radhi kujisalimisha na kuacha nyuma yote ya maisha na tamaa ya jangwani. Ee, mpenzi, ichukue hatua hii useme: “Niko tayari kuacha kila kitu ili niwe na lulu hii ya thamani kubwa; wakati wangu, uangalifu wangu, biashara yangu, nayahesabu yote kuwa ya chini kuliko pumziko hili la Mungu kama jambo la kwanza katika maisha yangu; nayatoa yote ili nitembee katika ushirika mkamilifu na Mungu.”

Huwezi kupata hilo na kuishi kila siku katika ushirika mkamilifu na Mungu, bila kutoa wakati kwa ajili yake. Hutoa wakati kwa kila jambo. Ni saa ngapi kwa siku ambazo msichana ametumia kwa miaka na miaka ili aweze kuwa hodari wa kupiga kinanda? Ni miaka mingapi ambayo kijana husoma ili ajitayarishe kwa kazi ya sheria au tiba? Saa, siku, majuma, miezi, na miaka, aliyotoa kwa furaha ili ajikamilishe kwa kazi yake. Nawe je, watazamia kwamba dini ni rahisi hivyo kiasi kwamba pasipo kutoa wakati waweza kupata ushirika wa karibu na Mungu? Huwezi. Lakini, ee, ndugu zangu wanaume na wanawake, lulu ile ya thamani kubwa yastahili kila kitu. Mungu astahili kila kitu.

Kristo astahili kila kitu. Ee, njoo leo, useme, “Bwana, kwa gharama yo yote, unisaidie; nataka sana kuishi maisha haya.”

Nawe kama ukiona ni vigumu kusema hivyo, na kama kuna vita ndani ya moyo, usijali; mwambie Mungu, “Bwana, nilidhani nilikuwa radhi, lakini naona kuna kutokuwa radhi kwingi kiasi gani; njoo uvumbue ubaya ulio bado moyoni.” Kwa neema yake, ukikubali kulala miguuni pake na kumtumaini, wokovu utakuja.

Kisha huja hatua ifuatayo, nayo ni kusema: “Sasa najisalimisha mimi mwenyewe kwa Mungu mtakatifu na wa milele, ili aniongoze niingie katika pumziko hili kamili.” Ee, ndugu, tunapaswa kujifunza kukutana na Mungu uso kwa uso. Dhambi yangu imekuwa juu ya Mungu. Daudi alilihisi hilo aliposema, “Nimekutenda dhambi Wewe peke yako.” Ni Mungu aliye katika kiti cha hukumu ambaye uso wake utakutana nao wewe binafsi. Ni Mungu Mwenyewe, binafsi, aliyekutana nawe ili kuzisamehe dhambi zako. Njoo leo ujiweke mikononi mwa Mungu aliye hai. Mungu ni upendo. Mungu yu karibu. Mungu anangoja kukupa baraka yake. Moyo wa Mungu unakutamani wewe. “Mwanangu,” asema Mungu, “wewe wadhani unatamani pumziko; ni mimi ninayekutamani wewe kwa sababu natamani kupumzika moyoni mwako kama nyumbani kwangu, kama hekalu langu.” Wamhitaji Mungu wako.

Naam, lakini Mungu wako akuhitaji wewe, ili apate ukamilifu wa moyo wa Baba yake katika Kristo ndani yako. Njoo leo useme: “Sasa najisalimisha mimi mwenyewe kwa Kristo. Nimeamua. Katika jina la Yesu, nayapokea maisha yale ya pumziko kamili.’”

Kisha huja wazo langu la mwisho. Utakaposema hivyo, ongeza: “Na sasa, namtumaini Mungu ayafanye yote kuwa halisi kwangu katika uzoefu wangu. Kwamba nitaishi mwaka mmoja au miaka thelathini, nimesikia tena leo: ‘Mungu ni Yehova, YEYE ALIYEKO mkuu wa wakati ujao usio na mwisho, yule wa milele; na miaka thelathini kwake ni sawasawa kabisa na sasa;’ na kwamba Mungu hujitoa Mwenyewe kwangu, si kwa kadiri ya nguvu zangu za kumshika, bali kwa kadiri ya nguvu zake za upendo zenye uweza wote za kunishika mimi.” Je, utamtumaini Mungu leo kwa ajili ya wakati ujao? Ee, je, hutamtazama Mungu katika Kristo Yesu tena mara moja? Mara elfu umesikia, na kufikiri, na kushukuru—“Mungu ametupa Mwana wake;” lakini je, hutasema, “Atakosaje kutupa vitu vyote pamoja naye, kila dakika na kila siku ya maisha yangu?” Sema hivyo kwa imani. “Atakosaje Mungu kuwa radhi kunilinda katika nuru ya uso wake, katika uzoefu kamili wa nguvu ya Kristo ya kuokoa? Je, Mungu hakulifanya jua liangaze kwa fahari hivyo, na je, nuru si radhi hivyo kujimwaga katika kila pembe na kona ambako yaweza kupata mahali pa kuingilia? Na je, Mungu wangu, aliye upendo, hatakuwa radhi mchana kutwa kuangaza ndani ya moyo wangu huu, tokea asubuhi hata usiku, tokea mwisho wa mwaka hata mwisho wa mwaka?” Mungu ni upendo. Anatamani sana kujitoa Mwenyewe kwetu.

Ee, njoni, Wakristo, hata sasa mmeishi maisha katika nguvu zenu wenyewe. Je, hamtaanza leo? Je, hamtachagua maisha ambamo Mungu atakuwa yote, na ambamo mnapumzika katika yeye kwa yote? Je, hamtachagua maisha ambamo mtasema: “Ee, Mungu, nakuomba, nakutazamia, nakutumaini kwa ajili yake. Naingia leo katika pumziko la Mungu ili Mungu anilinde; ili Mungu anilinde kila saa. Naingia katika pumziko la Mungu.” Je, uko tayari kusema hivyo? Uwe na moyo mkuu; usiogope, waweza kumtumaini Mungu. Yeye huleta katika pumziko. Sikiliza neno la Mungu katika Manabii tena mara moja: “Angalia uwe mtulivu, usiogope, wala moyo wako usizimie.” Mtumaini tena upya leo: “Ee mpendwa, unichukue, uniingize nami nitakutumaini wewe, na ndani yako Baba.” Waweza kulitegemea hilo. Atakuchukua na kazi itafanyika.

Yaliyomo

Ukaaji wa Bwana Ndani Yetu Andrew Murray

Ukurasa 1 / 1 · 11 dakika zimebaki katika sura