Ukaaji wa Bwana Ndani Yetu ·Ili Mungu Awe Yote Katika Yote

Sura 13 · dakika 14 za kusoma

Ili Mungu Awe Yote Katika Yote

1 Wakorintho 15: 24-28.—“Ndipo mwisho, atakapomkabidhi Mungu Baba ufalme, atakapokuwa amebatilisha utawala wote na mamlaka yote na nguvu. Kwa maana lazima yeye atawale hata awaweke adui zake wote chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti. Kwa maana “Alivitia vitu vyote chini ya miguu yake.” Lakini isemapo, “Vitu vyote vimetiwa chini yake,” ni dhahiri ya kuwa yule aliyemtiisha vitu vyote hakuhesabiwa katika hayo. Na vitu vyote vitakapotiishwa chini yake, ndipo Mwana mwenyewe naye atatiishwa chini yake yeye aliyemtiisha vitu vyote, ili Mungu awe yote katika yote.”

Huu utakuwa mwisho mtukufu wa tamthilia kuu ya historia ya ulimwengu na wa ukombozi wa Kristo. Utakuja siku—utukufu wake ni mkubwa hata hatuwezi kuufikiria, siri yake ni ndefu hata hatuwezi kuielewa, lakini inakuja siku ambayo Mwana atakabidhi Ufalme ambao Baba alimpa, na ambao aliushinda kwa damu yake, na ambao ameuweka imara na kuukamilisha kutoka katika kiti cha enzi cha utukufu wake. “Humkabidhi Mungu Baba ufalme”. 1 Wakorintho 15:24.

Mwana mwenyewe naye atatiishwa chini ya Baba, “ili Mungu awe yote katika yote.” Siwezi kulielewa jambo hili—Mwana aliyebarikiwa milele aliye sawa na Mungu, tangu milele, na milele yote; Mwana aliyebarikiwa milele aliye juu ya kiti cha enzi atatiishwa chini ya Baba; na kwa namna ambayo kabisa iko juu ya ufahamu wetu, hapo ndipo itakapodhihirishwa, kama ambavyo haijapata kutokea, ya kuwa Mungu ni yote katika yote.

Ni kwa ajili ya hili Kristo amekuwa akitenda kazi; ni kwa ajili ya hili anatenda kazi leo ndani yetu; ni kwa ajili ya hili aliona ni jambo la maana kutoa damu yake; ni kwa ajili ya hili moyo wake unatamani ndani ya kila mmoja wetu; hii ndiyo asili hasa na utukufu wa Ukristo, “ili Mungu awe yote katika yote.” Na sasa, ikiwa hili ndilo lijazalo moyo wa Kristo; ikiwa hili laonyesha lengo moja la kazi ya Kristo, basi, nikitaka kuwa na roho ya Kristo ndani yangu, kauli-mbiu ya maisha yangu lazima iwe: Kila kitu kitiishwe, na kumezwa ndani yake, “ili Mungu awe yote katika yote.” Ushindi ulioje ungekuwa kama Kanisa lingekuwa likipigana kweli na bendera hiyo ikipepea juu yake! Maisha yalioje yangeweza kuwa yetu kama hiyo ingekuwa kweli bendera yetu! Kumtumikia Mungu kwa ukamilifu, kwa utimilifu, kwake tu, kumfanya kuwa yote katika yote! Jinsi yangeivika heshima, na kuiongeza, na kuichochea nafsi yetu yote! Ninatenda kazi, ninapigana, “ili Mungu awe yote katika yote;” ili siku ya utukufu iharakishwe. Ninaomba, na Roho Mtakatifu hufanya mashindano yake ndani yangu kwa tamaa isiyoelezeka, “ili Mungu awe yote katika yote.” Je, sisi Wakristo tungetambua ni kwa habari ya jambo kubwa jinsi gani tunavyotenda kazi na kuomba; kwamba tungekuwa na fahamu fulani ya Ufalme jinsi gani tulio washiriki wake, na udhihirisho wa Mungu jinsi gani tunaoutengenezea njia?

Ili kuonyesha ni jambo kubwa jinsi gani kuwa wa Ufalme wa Mungu, na wa Kanisa tukufu la Kristo duniani, John McNeill anasimulia jinsi alipokuwa mvulana wa miaka kumi na miwili, akifanya kazi katika njia ya reli na kupata mshahara mkubwa wa shilingi sita kwa juma, alivyokuwa akienda nyumbani kwa mama yake na dada zake, waliomthamini mno Johnnie wao mdogo, na kuwafurahisha kwa kuwaeleza cheo alichokuwa nacho. Alikuwa akisema kwa kiburi kikubwa, “Ee, kampuni yetu—inayo maelfu mengi ya pauni yanayopita mikononi mwake kila mwaka; inachukua mamia mengi ya maelfu ya abiria kila mwaka; nayo inayo maili nyingi za reli, na injini nyingi na mabehewa mengi; na maelfu mengi katika utumishi wake!”

Mama na dada zake walikuwa na fahari kubwa juu yake kwa sababu alikuwa mshirika katika biashara kubwa namna hiyo.

Enyi Wakristo, laiti tungejihimiza wenyewe kuamini ya kuwa sisi ni wa Ufalme ambao Kristo anautayarisha ili kumkabidhi Baba, ili Mungu awe yote katika yote, jinsi utukufu ungejaza mioyo yetu, na kufukuza kila kitu kilicho duni, dhalili, na cha kidunia! Jinsi tungechukuliwa mbele katika imani hii yenye baraka! Ninaishi kwa ajili ya hili: kwamba Kristo apate Ufalme wa kumkabidhi Baba. Ninaishi kwa ajili ya hili, nami siku moja nitamwona akitiishwa chini ya Baba, na ndipo Mungu awe yote katika yote. Ninaishi kwa ajili yake, nami nitakuwako si kama shahidi tu, bali nitakuwa na sehemu katika yote hayo. Ufalme ukikabidhiwa, Mwana akitiishwa, na Mungu awe yote katika yote! Nitakuwa na sehemu katika hilo, na katika ibada ya kuabudu nitashiriki utukufu na baraka.

Na tulichukue hili mpaka mioyoni mwetu, ili litawale katika maisha yetu—wazo hili moja, imani hii moja, lengo hili moja, furaha hii moja: Kristo aliishi, akafa, na anatawala; mimi ninaishi na kufa na katika nguvu zake, ninatawala; kwa ajili ya jambo hili moja tu, “ili Mungu awe yote katika yote.” Na liimiliki mioyo yetu yote na maisha yetu. Twawezaje kufanya hili? Ni swali zito, ambalo napenda kukupa majibu machache ya rahisi. Nami nasema, kwanza kabisa: Mruhusu Mungu ashike nafasi yake katika moyo wako na maisha yako. Luther mara nyingi aliwaambia watu, walipokuja kumsumbua kwa habari ya matatizo, “Mwache Mungu awe Mungu.” Ee, mpe Mungu nafasi yake. Nayo ni nafasi gani? “Ili Mungu awe yote katika yote.” Mwache Mungu awe yote katika yote kila siku, tangu asubuhi hata jioni. Mungu atawale nami nitii. Ah, baraka ya kusema, “Mungu na mimi!” Pendeleo lililoje kuwa na mshirika namna huyo! Mungu kwanza, kisha mimi! Na bado kunaweza kuwa na kujitukuza kwa siri katika kujiunganisha na Mungu. Nami napata katika Biblia neno la thamani zaidi hata. Ndilo, “Mungu wala si mimi.” Si, “Mungu kwanza, nami wa pili;” Mungu ni yote, nami si kitu. Paulo alisema, “Nilijitaabisha zaidi kuliko wote, walakini si mimi.” Ndugu, na tujaribu kumpa Mungu nafasi yake—tuanze katika chumba chetu cha faragha, katika ibada yetu, na katika maombi. Nguvu ya maombi kwa kiasi kikubwa hutegemea kabisa ufahamu wetu wa yeye ninayesema naye. Ni jambo la maana sana, kama tunao nusu saa tu ya kuomba, kwamba tutumie muda kupata kumwona Mungu huyu mkuu, katika nguvu zake, katika upendo wake, katika ukaribu wake, akingoja tu kutubariki. Hili ni la maana zaidi sana kuliko kutumia nusu saa yote katika kumimina maombi yasiyohesabika na kuomba ahadi zisizohesabika.

Jambo kuu ni kuhisi ya kuwa tunaweka maombi yetu katika kifua cha Upendo wenye uweza wote. Kabla ya na zaidi ya kila kitu, na tutumie muda tuombapo kuutambua utukufu na uwepo wa Mungu. Mpe Mungu nafasi yake katika kila ombi. Nasema, mruhusu Mungu awe na nafasi yake. Siwezi kumpa Mungu nafasi yake juu ya kiti cha enzi—kwa maana fulani naweza, nami napaswa kujaribu. Lakini jambo kuu ni mimi kuhisi ya kuwa siwezi kutambua ni nafasi gani ile, bali Mungu atazidi kujidhihirisha mwenyewe na nafasi aishikayo. Nawezaje kujua neno lolote juu ya jua?

Kwa sababu jua huangaza, na katika nuru yake, naona jua ni nini. Jua ni ushahidi wa nafsi yake. Hakuna mwanafalsafa ambaye angeweza kuniambia juu ya jua kama jua lisingeangaza.

Hakuna nguvu ya kutafakari na kufikiri iwezayo kuufikia uwepo wa Mungu. Kuwa kimya, ukitumaini, na ukipumzika, na Mungu wa milele ataangaza ndani ya moyo wako, na kujidhihirisha mwenyewe. Na ndipo, kwa asili ile ile kama ninavyofurahia nuru ya jua, na kwa asili kama ninavyoziangalia kurasa za kitabu nikijua ya kuwa naweza kuyaona maandishi kwa sababu nuru inaangaza; kwa asili ile ile Mungu atajidhihirisha mwenyewe kwa nafsi ingojayo, na kuufanya uwepo wake kuwa ni jambo halisi. Mungu atashika nafasi yake kama Mungu mbele ya mtoto wake, hata kwamba kabisa na kwa hakika jambo kuu katika moyo wa mtoto litakuwa: “Mungu yuko hapa, Mungu hujifanya kujulikana.”

Mpendwa, je, hili silo unalolitamani—ya kwamba Mungu atashika nafasi ambayo hajapata kuwa nayo kamwe; na ya kwamba Mungu atakujia katika ukaribu ambao hujapata kuuhisi bado; na, zaidi ya yote, ya kwamba Mungu atakujia katika ushirika udumuo na usiovunjika? Mungu aweza kushika nafasi yake mbele yako mchana kutwa. Narudia lile nililolitaja hapo awali kwa sababu Mungu amenifundisha somo kwalo: Kama vile Mungu alivyoifanya nuru ya jua kuwa laini, na tamu, na angavu, na ya wote, na isiyokoma, hata kamwe hainingharimu taabu ya dakika moja kuifurahia; vivyo hivyo, na kwa uhalisi zaidi sana kuliko nuru iniangazayo, ukaribu wa Mungu wangu waweza kudhihirishwa kwangu kama fungu langu la kudumu. Na sote tuombe “ili Mungu awe yote katika yote,” katika maisha yetu ya kila siku.

Fikiria mbali huko Afrika Kusini yuko mwanamke ambaye mumewe amekwenda safari ndefu bara. Atakuwa mbali kwa miezi kadhaa mbali na posta zote. Mke ana shauku ya kupokea habari. Kwa majuma, hajapata barua wala habari kutoka kwake. Siku moja, akiwa amesimama mlangoni pake, aja Kafir mkubwa, mkali. Ana sura ya kutisha nao amebeba mikuki yake na ngao. Mwanamke anashtuka na kukimbilia ndani ya nyumba na kufunga mlango. Aja na kubisha hodi mlangoni, naye ana hofu. Anamtuma mtumishi wake, ambaye anarudi na kusema, “Mtu anasema lazima akuone.” Anakwenda, akiwa na hofu tele. Anatoa gazeti la zamani. Amekuja kwa safari ya mwezi mzima kwa miguu kutoka kwa mumewe, na ndani ya lile gazeti chafu mna barua kutoka kwa mumewe, ikimwambia habari ya hali yake njema. Jinsi mke yule anavyoifurahia barua ile! Anaisahau ile sura iliyomtisha. Na sasa majuma yanapopita tena, jinsi anavyoanza kumtamani yule mjumbe Kafir mbaya wa sura! Baada ya kungoja kwa muda mrefu aja tena, na wakati huu anakimbia nje kumlaki kwa sababu ndiye mjumbe atokaye kwa mumewe mpendwa, naye anajua ya kuwa pamoja na sura yake yote ya kuchukiza, yeye ni mchukuzi wa ujumbe wa upendo. Ee, jifunze kuikubali mapenzi ya Mungu katika kila jambo!

Kama Mungu awe yote katika yote katika moyo wako na maisha yako, nasema si tu, Mruhusu ashike nafasi yake, na kuyakubali mapenzi yake yote, bali, tatu, Tumaini katika nguvu zake. Rafiki wapendwa, ni “Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.” Ni “Mungu wa amani,” kwa mujibu wa fungu jingine, “awakamilishe katika kila neno jema mpate kuyafanya mapenzi yake, akitenda ndani yetu yapendezayo mbele zake” Wewe walalamika juu ya udhaifu, juu ya unyonge, juu ya utupu. Usijali; ndicho ulichoumbiwa—kuwa chombo kilichotupwa, ambamo ndani yake Mungu aweza kuweka utimilifu wake na nguvu zake. Basi jifunze somo hili. Najua si rahisi. Muda mrefu baada ya Paulo kuwa mtume, ilimbidi Bwana Yesu aje kwa namna ya pekee kabisa kumfundisha kusema, “Nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi zaidi” 2 Wakorintho 12:9. Paulo alikuwa katika hatari ya kujitukuza, kwa sababu ya mafunuo yaliyotoka Mbinguni, na Yesu akamjia, na kusema, “Neema yangu yakutosha, kwa maana uweza wangu hukamilishwa katika udhaifu” 2 Wakorintho 12:9.

Maisha ya Paulo yalibadilika tangu wakati ule katika jambo hili moja, naye akasema, “Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adhabu, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.” 2 Wakorintho 12:10.

Je, kweli unatamani Mungu awe yote katika yote? Tumia muda kusema kila siku uinamapo mbele za Mungu, “Nguvu ya Mungu Mwenyezi itendayo kazi katika jua, na mwezi, na nyota, na maua, inatenda kazi ndani yangu. Ni hakika kama vile ninavyoishi. Nguvu ya Mungu Mwenyezi inatenda kazi ndani yangu. Yanibidi tu kujinyenyekeza, na kuwa kimya; yanibidi kuwa mtiifu zaidi, na kujisalimisha kwa mapenzi yake; yanibidi kuwa na tumaini zaidi, na kumruhusu Mungu afanye nami atakavyo.” Mpe Mungu njia yake nawe, na umwache Mungu atende kazi, naye atatenda kwa nguvu. Utulivu ulio wa ndani zaidi mara nyingi umethibitika kuwa ndio chanzo cha tendo lililo kuu zaidi. Limeonekana katika uzoefu wa watakatifu wengi wa Mungu, nao ndio uzoefu tunaouhitaji,—ya kwamba katika utulivu wa kujisalimisha na imani, kutenda kazi kwa Mungu kumedhihirishwa.

Nne: Kama Mungu awe yote katika yote, toa kila kitu dhabihu kwa ajili ya ufalme wake na utukufu wake. “Ili Mungu awe yote katika yote.”

Hili ni lengo tukufu, lenye fahari, takatifu namna hiyo hata Kristo akasema, “Kwa ajili ya hili nitatoa uhai wangu. Kwa ajili ya hili, nitatoa vyangu vyote, hata kufa kwa msalaba. Kwa ajili ya hili, nitajitoa mwenyewe.” Kama lilikuwa la thamani hiyo kwa Kristo, je, halina thamani kwako?

Kama mtu angemwuliza Yesu wa Nazareti, “Mwili ni kwa ajili ya nini; matumizi ya juu kabisa ya mwili wako ni yapi?” Angesema, “Matumizi na utukufu wa mwili wangu ni ya kwamba naweza kuutoa dhabihu kwa Mungu. Hilo ndilo kila kitu.” Kuna faida gani ya kuwa na akili; na kuna faida gani ya kuwa na fedha; na kuna faida gani ya kuwa na watoto? Ni kwamba naweza kuwatoa kwa Mungu; kwa maana Mungu lazima awe yote katika yote katika kila kitu. Namwomba Mungu atupe mtazamo namna huo wa ufalme wake, na utukufu wake, hata kila kitu kingine kitoweke. Ndipo, kama ungekuwa na maisha elfu kumi, ungesema, “Huu ndio uzuri na thamani ya maisha, ‘ili Mungu awe yote katika yote’ kwangu, na kwamba niweze kuwathibitishia watu ya kuwa Mungu ni zaidi ya kila kitu, ya kuwa maisha yana thamani ya kuishi tu kadiri yanavyotolewa kwa Mungu kuyajaza”.

Na tutoe kila kitu dhabihu kwa ajili ya ufalme wake na utukufu wake. Anza kuishi siku baada ya siku kwa maombi haya, “Mungu wangu, nimejitoa kwako. Uwe wewe yote katika yote yangu.” Wasema, “Je, naweza kulitambua hilo?” Naam, kwa njia hii: Mwache Roho Mtakatifu akae ndani yako; mwache Roho Mtakatifu awake ndani yako kama moto, na kuwaka ndani yako kwa kuugua kusikoelezeka, akimlilia Mungu mwenyewe adhihirishe uwepo wake na mapenzi yake ndani yako. Katika sura ya nane ya Warumi, Paulo alinena juu ya kuugua kwa viumbe vyote.

Na viumbe vyote vinaugulia nini? Vinaugulia ukombozi, ule uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu (Tazama Warumi 8:19). Nasadiki hilo ndilo Paulo alilomaanisha aliponena juu ya kuugua kwa Roho Mtakatifu—kule kuugua kusikoelezeka kwa ajili ya wakati ujao wa utukufu ambapo Mungu atakuwa yote katika yote. Enyi Wakristo, toeni muda wenu dhabihu; toeni mambo yenu dhabihu; toeni nguvu bora za mioyo yenu dhabihu katika kuomba, kutamani, na kulia kwamba “Mungu awe yote katika yote.”

Na mwisho: kama Mungu awe yote katika yote, mngoje yeye daima mchana kutwa. Hoja yangu ya kwanza ilihusu kumpa Mungu nafasi yake, lakini nataka kulieleza hili kwa uwazi zaidi katika kuhitimisha. Mngoje Mungu daima mchana kutwa. Kama utafanya hivyo, ni lazima uishi sikuzote katika uwepo wake. Mahali patakatifu ambapo tutakaa mbinguni ni uwepo wa Mungu ulio karibu kabisa. Uwepo wa Mungu udumuo bila shaka ni urithi wa kila mtoto wa Mungu, kama vile jua liangazavyo. Baba kamwe hamfichi mtoto wake uso wake. Dhambi huuficha, na kutokuamini huuficha, lakini Baba huuacha upendo wake uangaze mchana kutwa juu ya nyuso za watoto wake. Jua linaangaza mchana na usiku. Jua lako halitatua kamwe. Anza kulitafuta hili. Njoo uishi katika uwepo wa Mungu. Kwa kweli pako mahali pa kudumu katika uwepo wake, katika siri ya hema yake, ambapo mtu fulani ameimba kwa uzuri sana: Pamoja nami, popote niendako, Uwepo ule mkuu waenda; Ile furaha isiyoelezeka, Pumziko lisilosumbuliwa.

Kila mahali, ule utulivu wenye baraka Wa Mahali pale Patakatifu; Utulivu wa upendo uabuduo, Bubu mbele za uso wake.

Hili ndilo fungu la wale ambao ombi hili wamejaliwa—“Neno moja nimelitaka kwa BWANA, nalo nitalitafuta, nikae nyumbani mwa BWANA siku zote za maisha yangu, niutazame uzuri wa BWANA, na kutafakari hekaluni mwake.” Zaburi 27:4. “Maana atanisitiri katika banda lake.” Mst. 5. Mungu mwenyewe atakuchukua na kukuweka pale hata kazi yako yote itafanywa ndani ya Mungu. Mpendwa, mngoje Mungu daima. Huwezi kufanya hili usipokuwa katika uwepo wake. Ni lazima uishi katika uwepo wake. Ndipo utakapojifunza tabia ile yenye baraka ya kumngoja Mungu. Ugumu halisi wa kufika mahali pa kumngoja Mungu kwa kweli ni kwa sababu Wakristo wengi hawajatafuta kuutambua ukaribu wa Mungu na kumpa Mungu nafasi ya kwanza. Lakini na tujitahidi kuelekea hili, na tumtumaini Mungu atupe kwa neema yake, na tumngoje Mungu mchana kutwa. “Macho yangu,” asema mmoja, “yamekuelekea wewe daima.” Mngoje Mungu kwa uongozi, na Mungu, ukimngoja sana, atakupandisha katika nguvu mpya kwa ajili ya utumishi wake, katika furaha mpya katika ushirika wake. Atakuongoza uende katika tumaini kubwa zaidi kwake; atakuandaa kutazamia mambo mapya kutoka kwake. Mpendwa, hakuna ajuaye Mungu atakalomtendea mtu aliyejitoa kwake kabisa. Lisifiwe jina lake! Kila mmoja wetu na aseme, “Maisha yangu na yawe ni kuishi na kufa, kutaabika na kuomba daima kwa ajili ya jambo hili moja: ya kwamba ndani yangu, na kunizunguka, na katika kanisa; ya kwamba ulimwenguni kote,‘ Mungu awe yote katika yote ’.”

Mbegu ndogo ni mwanzo wa mti mkubwa. Mbegu ya haradali huwa mti ambao ndege wa angani waweza kutulia ndani yake. Ile siku kuu ambayo maandiko yanenayo, ambapo Kristo mwenyewe atatiishwa chini ya Baba, na kuukabidhi Ufalme kwa Baba, na Mungu atakuwa yote katika yote—huo ndio mti mkuu wa Ufalme wa Mungu ukifikia utimilifu wake mkamilifu na utukufu wake. Ee, na tuichukue mbegu ya utukufu huo mioyoni mwetu, na tuiname katika kujisalimisha na kunyenyekea, na tuseme,“Amina, Bwana; hili na liwe wazo langu moja. Hili na liwe maisha yangu—kunena na kutenda kazi, kuomba na kuwako ili tu wengine waletwe kumjua yeye pia. Haya ndiyo maisha yangu—kujitoa kwa tamaa zisizoelezeka za Roho Mtakatifu, ili nisipumzike, bali nizidi kuweka jicho langu juu ya siku ile—siku ya utukufu, ambapo kweli, Mungu atakuwa yote katika yote.”

Mungu na atusaidie kila mmoja wetu. Mungu atusaidie sote kujitoa kwake, na kwa Kristo, na kuyafanya kuwa maisha yetu ya kila siku; kwa ajili ya jina lake. Amina.

Ukaaji wa Bwana Ndani Yetu Andrew Murray

Ukurasa 1 / 1 · 14 dakika zimebaki katika sura