Ukaaji wa Bwana Ndani Yetu ·Chanzo cha Nguvu Katika Maombi

Sura 12 · dakika 10 za kusoma

Chanzo cha Nguvu Katika Maombi

Warumi 8:26-27.—Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu; kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Naye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.

Hapa tunapata mafundisho ya Mungu kuhusu msaada wa Roho Mtakatifu katika maombi. Nusu ya kwanza ya sura hii ina umuhimu mkubwa kuhusiana na mafundisho ya neno la Mungu kuhusu Roho. Katika Warumi 6 tunasoma juu ya kuwa wafu kwa dhambi na hai kwa Mungu, na katika Warumi 7 juu ya kuwa wafu kwa sheria na kuolewa na Kristo, na pia juu ya kushindwa kwa mtu asiyezaliwa mara ya pili kuyatenda mapenzi ya Mungu. Haya ni maandalizi tu ya kutuonyesha jinsi tulivyo wanyonge; kisha katika sura ya nane inakuja kazi ya baraka ya Roho, iliyoelezwa hasa kwa maneno haya: “Kwa maana sheria ya Roho wa uzima ulio katika Kristo Yesu imekuweka huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.” Warumi 8:2. Roho hutuweka huru na nguvu ya dhambi, hutufundisha na kutuongoza ili tuenende kwa kufuata Roho.

Katika hali yetu ya ndani, twaweza kuwa na nia ya kiroho na kuwezeshwa kuyafisha matendo ya mwili. Roho Mtakatifu huusaidia udhaifu wetu. Maombi ndilo jambo la lazima kuliko yote katika maisha ya kiroho. Lakini hatujui jinsi ya kuomba wala tuombee nini kama itupasavyo. Roho, kama Paulo anavyotuambia, huomba kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Tena anatuambia kwamba mara nyingi sisi wenyewe hatujui Roho anatenda nini ndani yetu, bali yuko mmoja, Mungu, aichunguzaye mioyo. Maneno mara nyingi hufunua mawazo yangu na matakwa yangu, lakini si kile kilicho ndani sana ya moyo wangu; naye Mungu huja na kuuchunguza moyo wangu, na huko ndani kabisa, kilichofichika, kile nisichoweza kukiona na kilichokuwa kwangu shauku isiyoweza kutamkwa, Mungu hukipata.

Maombi yenye nguvu! Kukiri kwa kutokujua! Ndugu zangu, mara nyingi mimi mwenyewe kama mhudumu naogopa kwamba naomba kwa urahisi mno. Nimekuwa nikiomba kwa miaka hii arobaini au hamsini, na kimekuwa, kwa upande wa mwanadamu, kitu rahisi kuomba. Sisi sote tumefundishwa kuomba, na tunapoombwa, twaweza kuomba, lakini kunakuwa rahisi mno, nami naogopa kwamba twadhani tunaomba mara nyingi hali kuna maombi kidogo ya kweli. Basi kama tutakuwa na maombi ya Roho Mtakatifu ndani yetu, kitu kimoja kinahitajika; ni lazima tuanze kwa kuhisi, “Siwezi kuomba.” Mtu anapovunjika na kushindwa kuomba, na kuna moto unaowaka moyoni mwake, na mzigo umemlemea, kuna kitu kinachomvuta kwa Mungu. “Sijui niombe nini.” Hatutambui kutokujua kwetu vya kutosha. Abrahamu alitoka bila kujua aendako; hicho kilikuwa kipengele cha kutokujua na pia kipengele cha imani (Tazama Waebrania 11:8).

Yesu aliwaambia wanafunzi wake walipokuja na ombi lao kuhusu kiti cha enzi, “Hamjui mnaloliomba.” Mathayo 20:22. Paulo asema, “Hakuna ayajuaye mambo ya Mungu ila Roho wa Mungu.” 1 Wakorintho 2:11. Wewe wasema, “Kama sitaomba maombi ya zamani niliyojifunza kwa mama yangu au kwa mwalimu wangu chuoni au kwa uzoefu wangu wa jana na juzi, niombe nini?” Nakujibu, omba maombi mapya, na upande juu zaidi katika utajiri wa Mungu.

Unajua tunavyomwaza mwanafunzi aendaye chuoni akijidhania kwamba anajua kila kitu. Hatajifunza mengi. Sir Isaac Newton alisema, “Sijui ninavyoonekana kwa ulimwengu; lakini kwangu mimi mwenyewe, naonekana kuwa nimekuwa kama mvulana tu achezaye ufukweni na kujifurahisha kwa kupata kokoto laini zaidi au kombe zuri zaidi kuliko kawaida mara kwa mara, hali bahari kuu ya kweli ilikuwa mbele yangu bila kugunduliwa yote.” Na vivyo hivyo kuhusu kanisa: Twataka kuchukua nafasi yetu kama washiriki wa kanisa la Kristo katika nchi hii; na kwa kuwa wa mwili ule mkuu, kusema, “Bwana Mungu, je, hakuna lolote liwezalo kufanywa ili kulibariki kanisa la nchi hii na kulihuisha na kulitoa katika hali yake ya kidunia na katika udhaifu wake?”

Twaweza kushauriana pamoja na kuhitimisha bila imani, “La, hatujui la kufanywa; hatuna uvutano wala nguvu juu ya wahudumu hawa wote na makanisa yao.” Lakini kwa upande mwingine, ni baraka iliyoje kumjia Mungu na kusema, “Bwana, hatujui la kuomba. Wewe wajua la kutoa.” Roho Mtakatifu angeweza kuomba mara mia zaidi ndani yetu kama tungekuwa tu na utambuzi wa kutokujua kwetu, kwa sababu ndipo tungehisi kumtegemea kwetu.

Hapo ndipo wazo la kwanza: kutokujua kwetu. “Kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo;” lakini “Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.” Warumi 8:26. Mara nyingi twasikia juu ya kazi ya Mungu Baba na Mwana na Roho Mtakatifu katika kuutimiza na kuukamilisha ukombozi mkuu, nasi twajua kwamba Mungu alipofanya kazi katika uumbaji wa ulimwengu, hakuchoka, na hata hivyo twasoma neno lile la ajabu katika kitabu cha Kutoka kuhusu siku ya Sabato, “Akapumzika.”Mwanzo 2:2. Alistarehe, siku ya Sabato ilikuwa starehe kwake. Mungu ilimpasa kufanya kazi na Kristo ilimpasa kufanya kazi, na sasa Roho Mtakatifu afanya kazi, na mahali pake pa siri pa kufanyia kazi, mahali ambapo kazi yote lazima ianzie, ni moyoni ambapo huja kumfundisha mtu jinsi ya kuomba.

Mtu anapoanza kupata ufahamu wa kile kinachohitajika, kile kilichoahidiwa, na kile Mungu anachongoja kutimiza, anahisi kuwa kinapita fikira zake; ndipo wakati atakapokuwa tayari kusema, “Siwezi kumwekea mipaka yule Mtakatifu wa Israeli kwa mawazo yangu; najitoa katika imani kwamba Roho Mtakatifu aweza kuwa akiniombea kwa kuugua, kwa shauku, zisizoweza kutamkwa.” Yatumie hayo katika maombi yako.

Kuna nyanja mbalimbali za maombi. Kuna ibada, ambapo mtu huinama tu kumsujudia Mungu mkuu. Hatuchukui muda wa kuabudu. Twahitaji kuabudu kwa siri, ili tu kujiweka uso kwa uso na Mungu wa milele, apate kutufunika kwa uvuli wake na kutufunika na kutujaza upendo wake na utukufu wake. Ni Roho Mtakatifu awezaye kufanya ndani yetu shauku kama hiyo hata tuache anasa zetu na hata sehemu ya shughuli zetu, ili tupate kukutana na Mungu wetu mara kwa mara.

Nyanja inayofuata ya maombi ni ushirika. Katika maombi, hakuna ibada ya mfalme peke yake bali pia ushirika kama wa mtoto na Mungu. Wakristo huchukua muda mchache mno katika ushirika. Hudhani maombi ni kuja tu na maombi yao. Kama Kristo atanifanya kuwa kile nitakachokuwa, ni lazima nidumu katika ushirika na Mungu. Kama Mungu ataruhusu upendo wake uingie na kuangaza na kuwaka moyoni mwangu, ni lazima nichukue muda wa kuwa naye.

Mhunzi huweka fimbo yake ya chuma motoni. Akiiacha humo kwa muda mfupi haiwi nyekundu kwa moto. Aweza kuitoa ili afanye jambo nayo na baada ya muda aiweke tena kwa dakika chache, lakini wakati huu haiwi nyekundu kwa moto. Katika mchana kutwa, aweza kuiweka fimbo hiyo motoni mara nyingi na kuiacha humo dakika mbili au tatu kila mara, lakini kamwe haipati moto barabara. Akichukua muda na kuiacha fimbo hiyo dakika kumi au kumi na tano motoni, chuma chote kitakuwa nyekundu kwa moto ule ulio motoni. Basi kama tutakuwa na moto wa utakatifu wa Mungu, na upendo, na nguvu, ni lazima tuchukue muda zaidi na Mungu katika ushirika. Ndicho kilichowapa watu kama Abrahamu na Musa nguvu zao. Walikuwa watu waliotengwa kwa ajili ya ushirika na Mungu, naye Mungu aliye hai aliwafanya kuwa hodari. Laiti tungetambua tu maombi yanavyoweza kufanya!

Nyanja nyingine, na iliyo muhimu kuliko zote, ya maombi ni maombezi. Ni kazi iliyoje Mungu aliyoifungua kwa ajili ya wale walio makuhani wake—waombezi! Twapata neno la ajabu katika unabii wa Isaya; Mungu asema, “Na washike ulinzi wangu” Isaya 27:5, na tena, “Wala hakuna aitaye jina lako, ajitahidiye ili akushike wewe.” Isaya 64:7. Katika mafungu mengine, Mungu awataja waombezi kwa ajili ya Israeli. Je, umewahi kumshika Mungu? Ashukuriwe Mungu, baadhi yetu tumefanya hivyo; lakini ndugu zangu, wawakilishi wa kanisa la Kristo katika United States, kama Mungu angetuonyesha kuna kiasi gani cha maombi ya bidii kwa ajili ya uamsho katika kanisa, kiasi gani cha kukiri kwa moyo mweupe dhambi za kanisa, kiasi gani cha kumsihi Mungu na kutompa raha hata aifanye Yerusalemu kuwa utukufu duniani, nadhani sote tungeona aibu. Twahitaji kuitoa mioyo yetu kwa Roho Mtakatifu, ili apate kutuombea na kuomba ndani yetu kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.

Nifanye nini ili niwe na Roho Mtakatifu huyu ndani yangu? Roho hutaka muda na nafasi moyoni; hutaka nafsi nzima. Hutaka shauku yangu yote na uvutano wangu wote uende kwa ajili ya heshima na utukufu wa Mungu; hutaka nijitoe. Rafiki mpendwa, hujui ungeweza kufanya nini kama ungejitoa kwa maombezi. Maombezi ni kazi ambayo mgonjwa aliyelala kitandani mwaka baada ya mwaka aweza kuifanya kwa nguvu. Ni kazi ambayo maskini asiye na hata senti ya kutoa kwa chama cha wamisionari aweza kuifanya siku kwa siku. Ni kazi ambayo msichana mdogo aliye katika nyumba ya baba yake na anayepaswa kusaidia katika utunzaji wa nyumba aweza kuifanya kwa Roho Mtakatifu. Watu mara nyingi huuliza: Kanisa la siku zetu lafanya nini kuwafikia umati? Huuliza ingawa huuliza kwa kutetemeka, kwa maana huhisi kutokuwa na msaada: Twaweza kufanya nini dhidi ya utu wa mali na kutokuamini katika mahali kama London, Berlin, New York, na Paris? Tumekata tamaa kama kwamba hakuna tumaini. Laiti wanaume na wanawake wangeitwa nje ili wajiunge pamoja kumshika Mungu! Sisemi juu ya umoja wowote wa maombi au wakati wowote wa maombi uliotengwa maalum, bali kama Roho angeweza kuwapata wanaume na wanawake watakaotoa maisha yao kumlilia Mungu, Roho hakika kabisa angekuja.

Si ubinafsi wala si furaha tupu tunayoitafuta tunapozungumza juu ya amani na pumziko na baraka ambayo Kristo aweza kutoa. Mungu atutaka, Kristo atutaka, kwa sababu ana kazi ya kufanya; kazi ya Calvary yapaswa kufanywa mioyoni mwetu, twapaswa kudhabihu maisha yetu ili kumsihi Mungu kwa ajili ya wanadamu. Basi na tujitoe siku kwa siku na kumwomba Mungu kwamba impendeze kumruhusu Roho wake Mtakatifu afanye kazi ndani yetu.

Kisha inakuja wazo la mwisho, kwamba Mungu mwenyewe huja kuutazama kwa furaha mwelekeo wa mtoto wake.

Labda mtu yule maskini hajui kwamba anaomba; labda anaona aibu kwa maombi yake. Ni afadhali zaidi hivyo. Labda anahisi kulemewa na kukosa raha, lakini Mungu husikia, Mungu hugundua nia ya Roho ilivyo, naye atajibu. Ee, fikiri siri hii ya ajabu, Mungu Baba juu ya kiti cha enzi tayari kutupa baraka zake kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake; Kristo kuhani mkuu mwenye uweza wote akisihi mchana na usiku. Na tuifungue na kuipanua mioyo yetu na kumwambia Mungu, “Ee, laiti ningekuwa kuhani, ili niwe mbele za Mungu daima na kumshika Mungu na kuteremsha baraka kwa wanadamu wenzangu wanaopotea!”

Mungu hutamani kuona maombezi ya Yesu yakionekana katika mioyo ya watoto wake, na pale ayapatapo, ni furaha kwake. Naye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu. Neno la Mungu hutujia daima kuomba kwa ajili ya wote na tusiridhike na nafsi zetu. Fikiri juu ya mamia ya washiriki wa kanisa katika nchi hii, makutano wasiozaliwa mara ya pili, makutano waliozaliwa mara ya pili sasa hivi, lakini bado wa kidunia na wazembe. Fikiri juu ya maelfu ya Wakristo wa jina—Wakristo kwa jina, lakini wanaomwibia Mungu! Nasi twaweza kuwa na furaha? Kama tunaubeba mzigo wa roho za watu, twaweza kuwa na amani na furaha hii? Mungu hukupa amani na furaha bila kusudi lingine ila kwamba uwe hodari kuubeba mzigo wa roho za watu katika furaha ya wokovu wa Kristo.

Hatutaki kusema, “Najitahidi kuwa mtakatifu kadiri niwezavyo; nina nini nami na watu wale wa kidunia walio karibu nami?” Kama kuna ugonjwa mbaya mkononi mwangu, mwili wangu hauwezi kusema, “Sina lolote nami.” Watu walipokuwa wametenda dhambi, Ezra alirarua mavazi yake, akainama mavumbini na kufanya kukiri. Alitubu kwa niaba ya watu.

Nehemia, taifa lilipotenda dhambi, alifanya kukiri, na kujitupa mbele za Mungu, akiiombolezea kutotii kwao kwa Mungu wa baba zao. Danieli alifanya vivyo hivyo. Nawe wadhani kwamba sisi kama waaminio hatuna kazi kubwa ya kufanya?

Tuseme tungekuwa bila dhambi hata moja; tuseme tu hivyo; je, ndipo tungeweza kufanya kukiri? Mtazame Kristo, asiye na dhambi! Alishuka katika maji ya ubatizo pamoja na wenye dhambi; alijifanya kuwa mmoja nao. Mungu amesema nasi ili kutuuliza kama twatambua tulivyo. Sasa hutuuliza kama sisi ni wa kanisa la nchi hii na kama tumeubeba mzigo wa dhambi zilizotuzunguka. Na tumwendee Mungu, naye kwa Roho Mtakatifu na aijaze mioyo yetu mzigo usioweza kutamkwa kwa ajili ya kanisa, na Mungu na atupe neema ya kuomboleza mbele zake. Nasi tutakapoanza kukiri dhambi za kanisa, tutaanza kuzihisi dhambi zetu wenyewe kama hatujawahi. Katika nyaraka tano kati ya zile kwa makanisa saba ya Asia, sauti kuu ilikuwa “Tubuni.” Halikuwepo wazo lolote la kushinda na kupata baraka isipokuwa wangetubu. Na tutubu kwa niaba ya kanisa la Kristo, naye Mungu atatupa ujasiri wa kuhisi kwamba ataihuisha kazi yake.

Yaliyomo

Ukaaji wa Bwana Ndani Yetu Andrew Murray

Ukurasa 1 / 1 · 10 dakika zimebaki katika sura