Sura 39 · dakika 1 za kusoma · dakika 1 za kusikiliza
Mazungumzo ya ndani ya Kristo na roho mwaminifu
“NITASIKIA atakayonena Bwana Mungu ndani yangu.”
Heri roho imsikiayo Bwana akinena ndani yake, ipokeayo neno la faraja kutoka kinywani mwake. Heri masikio yanayodaka sauti za mnong’ono wa Kimungu, wala hayajali manung’uniko ya ulimwengu huu. Naam, heri masikio yasikilizayo, si sauti ivumayo nje, bali kweli ifundishayo ndani. Heri macho yaliyofumbwa kwa mambo ya nje na kukazwa kwa mambo ya ndani. Heri wale wapenyao ndani, wajitahidio kila siku kujiandaa zaidi na zaidi kuzielewa siri. Heri wale watamanio kumtolea Mungu wakati wao, na wanaojitenga na vizuizi vya ulimwengu.
Yatafakari mambo haya, ee roho yangu, ukafunge mlango wa hisi zako, ili upate kusikia anayonena Bwana Mungu wako ndani yako. “Mimi ni wokovu wako,” asema Mpendwa wako. “Mimi ni amani yako na uzima wako. Kaa Nami nawe utapata amani. Viache vitu vyote vipitavyo, uvitafute vya milele. Vitu vyote vya muda ni nini ila mitego? Na viumbe vyote vitaweza kukupa msaada gani ukiachwa na Muumba?” Basi, viache vitu hivi vyote, ujifanye mwenye kumpendeza na mwaminifu kwa Muumba wako, ili upate kufikia furaha ya kweli.