Mafundisho ya Msingi ya Imani ya Kikristo
Utakaso

Sura 12 · dakika 22 za kusoma · dakika 28 za kusikiliza

Utakaso

“Na Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nayo roho yenu, na nafsi yenu, na mwili wenu, mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.”—1 Wathesalonike 5:23.

Somo lililo mbele yetu sasa ni Utakaso. Somo hili ni la maana kubwa sana. Si kwamba tu kuna ujinga mwingi, na makosa, na mawazo potofu juu ya somo hili, bali, ajabu kusema, kuna pia ubishi mkali kupita kiasi juu yake. Ubishi juu ya somo hili ni mkali kiasi kwamba miaka kadhaa iliyopita palifanyika katika Chicago “makongamano ya utakatifu” mawili yaliyoshindana, wakati mmoja, katika kanisa lile lile, kwa saa tofauti za mchana; na uadui kati ya makundi hayo mawili ya “ndugu wa utakatifu” ulikuwa mkubwa mno hata mara moja walikaribia kupigana ngumi mbele ya madhabahu ya kanisa. Somo la Utakaso limezaa uchungu wa namna hiyo na mambo ya kupita kiasi ya namna hiyo mahali fulani hata wengi huogopa hata kulitumia neno “Utakaso.” Lakini neno hili si neno la Biblia tu, bali ni neno lenye maana nzito, neno lililojaa maana ya thamani; wala haingekuwa busara kwetu kuliacha neno hili jema la Biblia kwa sababu tu neno hilo hutumiwa vibaya mara nyingi. Siku moja mtu mmoja aliniambia katika Chuo cha Biblia cha Chicago, “Je, huogopi utakatifu?” Bila shaka alichokusudia mtu yule ni kwamba, je, siogopi baadhi ya sura za kile kiitwacho “fundisho la utakatifu.” Nilimjibu kwamba siuogopi utakatifu hata kidogo kama ninavyouogopa kutokuwa mtakatifu. Mafundisho ya Biblia juu ya somo hili ni wazi kabisa na ya thamani sana. Tutakayoyasema asubuhi hii yatakuwa chini ya vichwa vitatu. Kwanza, Utakaso ni Nini: 2. Jinsi ya Kutakaswa; 3. Utakaso Hutukia Lini.

I. UTAKASO NI NINI

Kwanza, basi, tufikirie Utakaso ni nini.

1. Kwanza kabisa niweke wazi kwamba Utakaso si “Ubatizo katika Roho Mtakatifu.” Mambo haya mawili huchanganywa daima. Kuna uhusiano wa karibu kati ya hayo mawili, lakini si kitu kimoja hata kidogo; na kuchanganya mambo mawili ambayo Mungu ameyatenganisha hakuwezi kuzaa kitu ila machafuko na mawazo potofu. Ya kwamba Utakaso si ubatizo katika Roho Mtakatifu, na kwamba ubatizo katika Roho Mtakatifu si Utakaso, itakuwa wazi kadiri tunavyoendelea na kugundua kutokana na kujifunza Biblia Utakaso ni nini hasa.

2. Pili, niseme kwamba Utakaso si kung’olewa kabisa kwa asili ya mwili. Tutaliona hili tutakapofika kuichunguza fasili ya Mungu ya Utakaso; kwa maana Mungu ameeleza waziwazi kabisa Utakaso ni nini na hutukia lini. Wale wanaofundisha “kung’olewa kabisa kwa asili ya mwili” wanaifikia kweli kuu na ya thamani, lakini wameieleza kweli hiyo kwa namna isiyo sahihi kabisa, ya kusikitisha, na isiyo ya kimaandiko, na namna hii ya kuieleza huzaa kutoelewa kukubwa, na makosa, na matumizi mabaya. Ubishi wote juu ya “kung’olewa kabisa kwa asili ya mwili” hutokana na kutoelewa, na kutumia maneno ambayo hayana msingi wowote katika Biblia. Biblia haisemi mahali popote juu ya “asili ya mwili,” na kwa hakika basi haisemi juu ya “kung’olewa kabisa kwa asili ya mwili.” Kuna kitu kama asili ya mwili, lakini si kitu cha kimaada, si dutu, si kitu kiwezacho kung’olewa kama ung’oavyo jino au kuondoa kidole tumbo. “Asili ya mwili” ni asili inayotawaliwa na mwili. Kwa hakika ni haki ya mwaminio kuwa na asili isiyotawaliwa na mwili. Asili yetu inapaswa kuwa, na inaweza kuwa, chini ya utawala wa Roho Mtakatifu, na hapo si asili ya mwili tena; lakini haikung’olewa asili moja na asili nyingine kuwekwa mahali pake, bali asili yetu hutolewa chini ya utawala wa mwili na kuwekwa chini ya utawala wa Roho Mtakatifu. Zaidi ya hayo, ingawa ni haki yetu kuwa na asili yetu chini ya utawala wa Roho Mtakatifu na kuokolewa kutoka katika utawala wa mwili, bado tunao “mwili,” nasi tutakuwa nao mwili maadamu tungali katika mwili huu. Lakini tukiwa “tunaenenda kwa Roho,” basi “hatuzitimizi tamaa za mwili” (Wagalatia 5:16). Sura ya 8 ya Warumi inaeleza maisha ya ushindi, kama vile sura ya 7, mistari ya 9-24, inavyoeleza maisha ya kushindwa, watu wanapokuwa “wa mwilini, wameuzwa chini ya dhambi,” lakini ni katika sura ya 8, ambapo maisha “katika Roho” yanaelezwa (Warumi 8:9), tunapoambiwa kwamba bado tunao mwili, lakini kwamba ni haki yetu kutoishi “kwa kufuata mambo ya mwili,” bali “kwa Roho,” “kuyafisha matendo ya mwili.” Basi twaona kwamba mwili upo, lakini katika nguvu za Roho sisi, siku kwa siku, na (tukiishi kwa kadiri ya haki yetu) kila siku, na kila saa, na kila dakika, daima “tunayafisha matendo ya mwili.”

3. Hayo yatosha kuhusu Utakaso usivyo. Tutaona hasa ulivyo tukiitazama fasili ya Mungu ya Utakaso. Tutaona kwamba neno Utakaso linatumika katika Biblia kwa maana mbili.

(1) Maana ya kwanza ya Utakaso tutaiona katika Mambo ya Walawi 8:10-12, “Kisha Musa akayatwaa yale mafuta ya kutiwa, akaitia mafuta maskani na vyote vilivyokuwamo ndani yake, akavitakasa. Akayanyunyiza katika mafuta hayo juu ya madhabahu mara saba, akaitia mafuta madhabahu na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake, ili kuvitakasa. Akamimina katika mafuta hayo ya kutiwa juu ya kichwa cha Haruni, akamtia mafuta ili kumtakasa.” Basi ni wazi kabisa katika fungu hili kwamba kutakasa maana yake ni kutenga, au kuweka wakfu kwa ajili ya Mungu, na kwamba Utakaso ni tendo la kutenga, au hali ya kutengwa, kwa ajili ya Mungu. Neno Takasa linatumika kwa maana hii tena na tena. Mfano mwingine ni Mambo ya Walawi 27:14, 16. “Tena mtu atakapoitakasa nyumba yake iwe takatifu kwa Mungu, ndipo kuhani ataikadiria, kama ni njema au kama ni mbaya; kama kuhani atakavyoikadiria, ndivyo itakavyosimama . . . tena mtu akimtakasia BWANA sehemu ya shamba la milki yake, ndipo makadirio yatakuwa kwa kadiri ya mbegu zake za kupanda.” Hapa tena ni wazi kwamba kutakasa maana yake ni kutenga, au kuweka wakfu kwa ajili ya Mungu, na kwamba Utakaso ni tendo la kutenga, au hali ya kutengwa, kwa ajili ya Mungu. Mfano mwingine tena wa matumizi hayo hayo ya neno takasa unapatikana katika Hesabu 8:17, “Kwa kuwa wazaliwa wa kwanza wote katika wana wa Israeli ni wangu, wa wanadamu na wa wanyama pia; siku ile nilipowapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri niliwatakasa kwa ajili yangu.” Bila shaka hii haimaanishi kwamba Mungu, wakati alipowapiga wazaliwa wa kwanza katika Misri, aling’oa kabisa asili ya mwili kutoka kwa wazaliwa wa kwanza wa Israeli. Inamaanisha kwamba aliwatenga wazaliwa wa kwanza wote wawe mali yake ya pekee. Mfano mwingine wenye kufundisha sana wa matumizi hayo hayo ya neno hili unapatikana katika habari ya Yeremia, kama alivyoieleza yeye mwenyewe katika Yeremia 1:4, 5, “Neno la BWANA likanijia, kusema, Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua; na kabla hujatoka tumboni nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.” Hii maana yake ni wazi kwamba kabla hajazaliwa Mungu alimtenga Yeremia kwa ajili yake mwenyewe. Bado kungekuwa na upungufu mwingi na udhaifu ndani yake, lakini alikuwa ametengwa kwa ajili ya Mungu. Mfano mwingine wenye kufundisha wa matumizi hayo hayo ya neno Takasa unapatikana katika Mathayo 23:17, katika maneno ya Bwana wetu Yesu mwenyewe: “Enyi wapumbavu na vipofu; ipi iliyo kubwa, ile dhahabu, au lile hekalu lililoitakasa ile dhahabu?” Lakini labda mfano ulio dhahiri kuliko yote ni katika yale anayoyasema Bwana wetu juu ya kujitakasa kwake mwenyewe katika Yohana 17:19, “Na kwa ajili yao najitakasa mwenyewe, ili nao watakaswe katika kweli.” Hapa maana iliyo wazi ni kwamba Bwana wetu Yesu alijitenga mwenyewe kwa ajili ya kazi hii kwa Mungu, naye alifanya hivyo ili waaminio nao watengwe kwa ajili ya Mungu “katika kweli,” au “katika ile kweli.” Haya ndiyo matumizi ya mara nyingi zaidi ya neno takasa. Kuna mifano mingi yake katika Biblia. Basi kutakasa maana yake ni kutenga, au kuweka wakfu kwa ajili ya Mungu; na Utakaso ni tendo la kutenga, au hali ya kutengwa, kwa ajili ya Mungu. Hii ndiyo maana ya msingi ya maneno haya.

(2) Lakini neno hili, kama linavyotumika katika Biblia, lina pia maana ya pili inayohusiana kwa karibu na maana hii ya msingi. Mfano wa maana hii ya pili utaonekana katika 2 Mambo ya Nyakati 29:5, “Nisikilizeni, enyi Walawi; jitakaseni sasa, mkaitakase nyumba ya BWANA, Mungu wa baba zenu, mkautoe uchafu katika patakatifu.” Tukikumbuka ile “sambamba” (parallelism) ambayo ndiyo sifa kuu ya ushairi wa Kiebrania, ni wazi kwamba kutakasa hapa ni sawa na maneno “Mkautoe uchafu katika patakatifu” yanayopatikana katika sehemu ya mwisho ya mstari huo. Basi kutakasa hapa maana yake ni kutenga na unajisi wa kiibada au wa kimaadili, kusafisha; na Utakaso ni tendo la kutenga, au hali ya kutengwa, na unajisi wa kiibada au wa kimaadili. Matumizi hayo hayo ya neno hili yanapatikana katika Mambo ya Walawi 11:44, “Kwa kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wako; basi jitakaseni, mwe watakatifu; kwa kuwa mimi ni mtakatifu; wala msijitie unajisi kwa kitu cho chote kitambaacho kiendacho juu ya nchi.” Hapa tena ni wazi kwamba “jitakaseni” ni sawa na “mwe watakatifu,” nalo linalinganishwa kinyume na “kujitia unajisi,” na maana yake ni kutenga na unajisi wa kiibada au wa kimaadili, kusafisha; na Utakaso ni tendo la kutenga, au hali ya kutengwa, na unajisi wa kiibada au wa kimaadili. Maana hiyo hiyo ya utakaso inapatikana katika Agano Jipya katika 1 Wathesalonike 5:23, “Na Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nayo roho yenu, na nafsi yenu, na mwili wenu, mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.” Hapa twaona uhusiano wa karibu kati ya utakaso kamili na kuhifadhiwa kamili, bila lawama, na kutakasa hapa maana yake ni wazi kutenga na unajisi wa kimaadili, na utakaso hapa tena ni tendo la kutenga, au hali ya kutengwa, na unajisi wa kimaadili. Jambo hilo hilo ni dhahiri katika sura ya 4 ya waraka huo huo, mstari wa 7 (1 Wathesalonike 4:7), “Kwa maana Mungu hakutuita kwa uchafu, bali katika utakaso.” “Utakaso” wetu hapa umewekwa kinyume kabisa na “uchafu,” na kwa hiyo ni dhahiri kwamba utakaso hapa maana yake ni hali ya kutengwa na unajisi wote wa kimaadili. Jambo hilo hilo ni dhahiri katika mstari wa 3 wa sura hiyo hiyo, “Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, ndio kutakaswa kwenu, mjiepushe na uasherati.” Hapa tena ni dhahiri kwamba Utakaso maana yake ni kutengwa na uchafu, au unajisi wa kimaadili. Basi, maana mbili za Utakaso ni hizi: tendo la kutenga, au kuweka wakfu, au hali ya kutengwa, au kuwekwa wakfu, kwa ajili ya Mungu; na tendo la kutenga, au hali ya kutengwa, na unajisi wa kiibada au wa kimaadili. Maana hizi mbili za neno hili zinahusiana kwa karibu—mtu hawezi kutengwa kweli kwa ajili ya Mungu bila kutengwa na dhambi.

II. JINSI WATU WANAVYOTAKASWA

Sasa tunafika kwenye swali la pili, Watu hutakaswaje? Jibu kamili la swali hili lina sehemu kadhaa.

1. Sehemu ya kwanza ya jibu inapatikana katika andiko letu la sura hii, 1 Wathesalonike 5:23, “Na Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nayo roho yenu, na nafsi yenu, na mwili wenu, mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.” Inaonekana kutokana na mstari huu kwamba Mungu ndiye huwatakasa watu, na Utakaso ni kazi ya Mungu. Kutengwa kwa watu na dhambi na kutengwa kwao kwa ajili ya Mungu, vyote viwili ni kazi ya Mungu. Kama vile katika agano la kale alikuwa ni Mungu aliyewatenga wazaliwa wa kwanza wa Israeli kwa ajili yake mwenyewe, vivyo hivyo katika agano jipya ni Mungu anayemtenga mwaminio kwa ajili yake mwenyewe na kumtenga na dhambi. Kimsingi Utakaso si kazi yetu bali ni kazi ya Mungu.

2. Sehemu ya pili ya jibu inapatikana katika Waefeso 5:25, 26, “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase, akilisafisha kwa maji katika neno.” Hapa tunafundishwa kwamba Kristo hulitakasa kanisa na kwamba Utakaso ni kazi ya Kristo. Bila shaka swali linazuka, Kristo hulitakasa kanisa kwa maana gani? Jibu linapatikana katika Waebrania 10:10, “Na kwa mapenzi hayo tumetakaswa, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.” Hapa inaonekana kwamba Yesu Kristo hulitakasa kanisa kwa kujitoa mwenyewe kuwa dhabihu kwa ajili yake. Kwa kujitoa hivyo kwa ajili yake kuwa dhabihu, Kristo hulitenga Kanisa kwa ajili ya Mungu. Kama vile damu ya Mwana-kondoo wa Pasaka, katika sura ya 11 na ya 12 ya Kutoka, ilivyoweka tofauti kati ya Israeli na Wamisri, vivyo hivyo Bwana wetu Yesu, kwa kuutoa mwili wake mwenyewe, ameweka tofauti ya milele kati ya mwaminio ndani yake na ulimwengu, naye amemtenga kila mwaminio milele kwa ajili ya Mungu. Msalaba wa Kristo unasimama kati ya mwaminio na ulimwengu. Damu ya Kristo iliyomwagika humtenga mwaminio na ulimwengu, humnunua kwa ajili ya Mungu, na hivyo humfanya kuwa mali ya Mungu.

3. Sehemu ya tatu ya jibu la swali, watu hutakaswaje, inapatikana katika 2 Wathesalonike 2:13 na katika mafungu mengine, “Lakini imetupasa sisi kumshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu, ndugu, mpendwao na Bwana, kwa sababu Mungu amewachagua ninyi tangu mwanzo mpate wokovu, katika kutakaswa na Roho na kuiamini kweli.” Inaonekana kutokana na fungu hili, kama ilivyo katika mafungu mengine ya Biblia, kwamba ni Roho Mtakatifu anayemtakasa mwaminio, na kwamba Utakaso ni kazi ya Roho Mtakatifu. Hapa swali linazuka, Roho Mtakatifu humtakasa mwaminio kwa maana gani? Kwa maana hii: kama vile katika kielelezo cha Agano la Kale maskani, madhabahu na kuhani vilitengwa kwa ajili ya Mungu kwa mafuta ya kutiwa (Mambo ya Walawi 8:10-12), vivyo hivyo katika utimizo wake katika Agano Jipya, mwaminio, aliye maskani na kuhani pia, hutengwa kwa ajili ya Mungu kwa kutiwa mafuta na Roho Mtakatifu. Zaidi ya hayo, ni kazi ya Roho Mtakatifu moyoni inayoushinda mwili na unajisi wake, na hivyo kumtenga mwaminio na dhambi na kumvika neema za Kimungu za tabia, na kumfanya astahili kuwa mali ya Mungu mwenyewe. Kama Paulo anavyosema katika Wagalatia 5:22, 23, “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi.” Kinyume na kazi hii ya Roho Mtakatifu, tunasoma katika mistari iliyotangulia mara moja “matendo ya mwili” ni nini, orodha ya kutisha ya uovu na dhambi, nasi tunaambiwa katika mstari wa 16, “Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.”

4. Sehemu ya nne ya jibu la swali, tunatakaswaje, inapatikana katika Waebrania 13:12, “Kwa hiyo Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa nje ya lango.” Ni wazi kutokana na fungu hili kwamba waaminio hutakaswa kwa damu ya Yesu Kristo. Hapa swali linazuka, Damu ya Yesu hutakasa kwa maana gani? Jibu ni wazi: Damu ya Yesu Kristo hutusafisha na hatia yote ya dhambi, na hivyo hututenga na umati wa wanadamu walio chini ya laana ya sheria iliyovunjwa, na kututenga kwa ajili ya Mungu (taz. 1 Yohana 1:7, 9). Katika kipindi cha Agano la Kale damu ya dhabihu iliwasafisha Waisraeli na hatia ya makosa ya kiibada na kuwatenga kwa ajili ya Mungu; katika utimizo wake katika Agano Jipya damu ya Kristo humsafisha mwaminio na hatia ya makosa ya kimaadili na kumtenga kwa ajili ya Mungu.

5. Sehemu ya tano ya jibu la swali, watu hutakaswaje, inapatikana katika Yohana 17:17, “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.” Hapa Bwana wetu Yesu katika maombi yake anaonyesha kwamba sisi tunatakaswa katika kweli, na kwamba kweli ni Neno la Mungu. Neno la Mungu hutakasa kwa maana gani? Swali hili linajibiwa waziwazi katika sehemu mbalimbali za Neno la Mungu, ambapo tunafundishwa kwamba Neno la Mungu husafisha mbali kuwapo kwa dhambi, na hivyo hututenga nayo na kututenga kwa ajili ya Mungu. (Zaburi 119:9, 11; Yohana 15:3.) Tunapoyaleta maisha yetu katika kugusana kila siku na Neno, dhambi na upungufu wa maisha yetu na mioyo yetu hufunuliwa na kuondolewa, na hivyo tunazidi kutengwa na dhambi kwa ajili ya Mungu. (taz. Yohana 13:10.)

6. Sehemu ya sita ya jibu la swali, watu hutakaswaje, inapatikana katika 1 Wakorintho 1:30, “Bali kwa yeye ninyi mmo katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakaso, na ukombozi.” Katika fungu hili tunafundishwa kwamba Yesu Kristo alifanywa kwetu utakaso utokao kwa Mungu. Maana yake hasa ni nini? Ni hii tu: kwamba kutengwa na dhambi na kutengwa kwa ajili ya Mungu tumewekewa tayari katika Kristo Yesu, na kwa kumtwaa Yesu Kristo tunaupata utakaso huo tuliowekewa tayari. Kadiri tunavyomtwaa Kristo kikamilifu zaidi, ndivyo tunavyotakaswa kikamilifu zaidi. Lakini utakaso mkamilifu tumewekewa tayari ndani yake, kama vile hekima kamilifu imewekwa tayari ndani yake (Wakolosai 2:3). Tunatwaa hekima, au utakaso, au kitu kingine cho chote tulichowekewa tayari katika Kristo, kwa kipimo kinachozidi kuongezeka daima. Kwa Kristo akaaye ndani yetu, tunayeonyeshwa na Roho katika Neno, tunafanywa kufanana na Kristo na kuzaa matunda.

7. Sehemu ya saba ya jibu la swali, watu hutakaswaje, inapatikana katika Waebrania 12:14, “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao.” Hapa tunafundishwa kwamba tunayo sehemu yetu wenyewe katika utakaso, na kwamba kama tutatakaswa kwa maana kamili kabisa, utakaso ni kitu tunachopaswa kukifuatia, au kukitafuta kwa bidii, kama tutakipata. Ingawa utakaso ni kazi ya Mungu, sisi tunayo sehemu yetu ndani yake, yaani, kuufanya kuwa shabaha ya shauku yetu ya dhati na ya kuufuatia kwetu kwa bidii.

8. Sehemu ya nane ya jibu la swali, tunatakaswaje, inapatikana katika Warumi 6:19, 22, “Kama vile mlivyovitoa viungo vyenu kuwa watumwa wa uchafu na wa uasi mpate kuasi, vivyo hivyo sasa vitoeni viungo vyenu kuwa watumwa wa haki mpate kutakaswa. . . . Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru na dhambi, na kufanywa watumwa wa Mungu, mnayo faida yenu hata utakaso.” Maana ya maneno haya ni wazi, na mafundisho yake ni ya maana na ya kutumika maishani. Hapa tunafundishwa kwamba tunaufikia utakaso kwa kuvitoa viungo vyetu kuwa watumishi (watumwa, yaani watu walio mali kamili ya bwana wao) wa haki, na kwa kujifanya wenyewe kuwa watumwa wa Mungu. Kwa maneno mengine, kama tunataka kuufikia utakaso tunapaswa kuutoa mwili wetu wote na kila kiungo chake kwa Mungu, viwe watumishi wake, mali yake kabisa, nasi tunapaswa kujitoa wenyewe kwa Mungu kama watumishi wake, tuwe mali yake kamili. Hii ndiyo njia ya vitendo ya kuufikia utakaso, njia iliyo wazi kwa kila mmoja wetu hapa leo, hata kama tu dhaifu namna gani ndani yetu wenyewe.

9. Sehemu ya tisa na ya mwisho ya jibu la swali, tunatakaswaje, inapatikana katika Matendo 26:18, “Uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu, ili wapate msamaha wa dhambi na urithi kati ya wale waliotakaswa kwa imani iliyo ndani yangu.” Hapa tunaambiwa kwamba tunatakaswa kwa imani katika Kristo. Utakaso, sawa na kuhesabiwa haki, kuzaliwa upya, na kufanywa wana, unategemea imani. Imani ni mkono unaojitwalia baraka ya utakaso ambayo Mungu ametuwekea tayari kwa njia ya Mwanawe Yesu Kristo, kwa kifo chake msalabani, na kwa njia ya nguvu za Roho Mtakatifu atendaye kazi ndani yetu. Nasi tunaudai utakaso kwa imani rahisi katika Yeye aliyemwaga damu yake, na kwa kujisalimisha chini ya utawala wa Roho Mtakatifu, ambaye Yesu Kristo humtoa.

III. UTAKASO HUTUKIA LINI

Sasa tunafika kwenye swali ambalo juu yake pamekuwa na majadiliano mengi kuliko yote, tofauti za maoni nyingi kuliko zote, ubishi mwingi kuliko wote. Utakaso hutukia lini? Tukienda kwenye Biblia zetu kupata jibu la swali hili, hakuna haja ya kuwa na tofauti ya maoni. Jibu lina sehemu tatu.

1. Sehemu ya kwanza ya jibu inapatikana katika 1 Wakorintho 1:2, “Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, wale waliotakaswa katika Kristo Yesu, walioitwa kuwa watakatifu, pamoja na wote walitajao jina la Bwana wetu Yesu Kristo kila mahali, Bwana wao na wetu.” Hapa Roho Mtakatifu, akinena kwa kinywa cha Mtume Paulo, anatangaza waziwazi kwamba washiriki wote wa kanisa la Mungu tayari wametakaswa katika Kristo Yesu. Utakaso kwa maana hii si kitu tunachopaswa kukitazamia wakati ujao; ni kitu kilichokwisha kutukia. Dakika ile mtu ye yote anapokuwa mshiriki wa Kanisa la Mungu kwa imani rahisi katika Kristo Yesu—kwa maana wote walio na imani katika Kristo Yesu ni washiriki wa Kanisa la Mungu—dakika ile ile mtu huyo ametakaswa. Kila mwanamume na mwanamke aliyeokoka katika jengo hili asubuhi hii, kila mmoja aliye na imani hai katika Yesu Kristo, ametakaswa. Utakaso wetu umo ndani ya wokovu wetu. Lakini ni kwa maana gani sisi, yaani, waaminio wote, tumekwisha kutakaswa? Jibu la swali hili linapatikana katika fungu la Maandiko ambalo tumekwisha kulitaja, Waebrania 10:10, 14, “Na kwa mapenzi hayo tumetakaswa, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu. . . . Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa.” Maana yake ni wazi. Kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu juu ya Msalaba wa Kalvari kuwa upatanisho mkamilifu kwa ajili ya dhambi, kila mwaminio amesafishwa milele na hatia ya dhambi. “Tumekamilishwa milele” kwa habari ya msimamo wetu mbele za Mungu, nasi tumetengwa kwa ajili ya Mungu. Dhabihu ya Kristo haihitaji kurudiwa kama zilivyorudiwa dhabihu za Kiyahudi (V. I). Kazi imefanyika mara moja tu, dhambi imeondolewa, tena imeondolewa milele (Waebrania 9:26; taz. Wagalatia 3:13), nasi tumetengwa milele kuwa milki ya Mungu ya pekee na ya milele. Mtu ye yote akikuuliza kama umetakaswa, ikiwa wewe ni mwaminio katika Yesu Kristo, yaani, ikiwa una imani hai katika Yesu Kristo, unayo haki ya kusema, “Ndiyo, nimetakaswa.” Kila mwaminio katika Kristo ni mtakatifu, mtakatifu si kwa maana ambayo neno hilo hutumiwa mara nyingi siku hizi, bali kwa maana ya Biblia, yaani, kwa kuwa ametengwa kwa ajili ya Mungu, na ni wa Mungu, na ni mali ya pekee ya Mungu. Lakini kuna maana nyingine ambayo kwayo kila mwaminio anaweza kutakaswa kikamilifu leo. Hii inapatikana katika Warumi 12:1, “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.” Katika fungu hili twaona kwamba ni haki ya mwaminio ya sasa na yenye baraka, na wajibu wake wa maana na mzito, kuutoa mwili wake kwa Mungu kuwa dhabihu iliyo hai—si sehemu fulani au sehemu kadhaa za mwili, bali mwili wote pamoja na kila kiungo chake na kila uwezo wake. Na tunapoutoa hivyo mwili wetu wote kwa Mungu kuwa dhabihu iliyo hai, hapo tumetakaswa kabisa. Toleo kama hilo humpendeza Mungu sana. Kama vile Mungu katika Agano la Kale alivyoonyesha kupendezwa kwake na toleo kwa kushusha moto ili kulitwaa kwake mwenyewe, vivyo hivyo mwili wote unapotolewa hivyo kwa Mungu, Mungu atashusha moto tena, moto wa Roho Mtakatifu, na kujitwalia kile kilichotolewa hivyo. Dakika ile mwaminio anapojitoa hivyo kuwa dhabihu iliyo hai kwa Mungu, basi, kwa kadiri ya mapenzi yake, yaani kusudi linaloyatawala maisha yake, kiini hasa cha utu wake, yeye ni wa Mungu kabisa, au “ametakaswa kikamilifu.” Bado anaweza, na bado atagundua kila siku, anapojifunza Neno la Mungu na kuangaziwa na Roho Mtakatifu, matendo yake, mazoea ya maisha, namna za kuhisi, za kusema na za kutenda, yasiyopatana na kusudi hili kuu la mapenzi yake; na hayo lazima yaungamwe kwa Mungu kuwa ya kulaumiwa na kuondolewa, na sehemu hii ya utu wake na ya maisha yake iletwe, kwa Roho wa Mungu na kwa Kristo akaaye ndani, katika kupatana na mapenzi ya Mungu kama yalivyofunuliwa katika Neno lake. Ushindi katika eneo hili jipya lililogunduliwa ambalo bado halijadaiwa unaweza kuwa wa papo hapo. Kwa mfano, naweza kugundua ndani yangu hasira ya haraka ambayo ni dhahiri haimpendezi Mungu. Naweza kwenda kwa Mungu, kuiungama, kuikana, kisha papo hapo, si kwa nguvu zangu mwenyewe, bali kwa kumtazama Yesu na kuudai uvumilivu wake na upole wake, kuishinda, na kamwe nisishindwe tena upande huo. Na ndivyo ilivyo kwa kila dhambi nyingine na kila udhaifu mwingine katika maisha yangu ninaoletwa kuona kwamba haumpendezi Mungu.

2. Lakini hili si jibu lote la swali, tunatakaswa lini. Sehemu ya pili ya jibu inapatikana katika 1 Wathesalonike 3:12, “Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote, kama sisi tulivyo kwenu.” Na katika sura ya 4 ya waraka huo huo, mstari wa 1 na wa 10, “Basi, zaidi ya hayo, ndugu, twawasihi na kuwaonya katika Bwana Yesu, kwamba kama mlivyopokea kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kama vile mnavyoenenda, mzidi sana zaidi na zaidi. . . . Kwa maana mnalitenda neno hilo kwa ndugu wote walio katika Makedonia yote. Lakini, ndugu, twawasihi mzidi sana zaidi na zaidi.” Na katika 2 Petro 3:18, “Bali kukueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo.” Na 2 Wakorintho 3:18, “Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiutazama utukufu wa Bwana kama katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama kwa Roho wa Bwana.” Na katika Waefeso 4:15, 16, “Bali tuishike kweli katika upendo, tukue hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, ndiye Kristo. Kutoka kwake yeye mwili wote, ukiungwa na kushikamanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, hukuza mwili hata ujijenge wenyewe katika upendo.” Kutokana na mafungu haya twaona kwamba kuna kazi ya Utakaso inayoendelea hatua kwa hatua, kuongezeka katika upendo, kuzidi zaidi na zaidi katika mwenendo wa utauwa na katika kumpendeza Mungu, kukua katika neema na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo, kubadilishwa kufanana na mfano wa Bwana wetu toka utukufu hata utukufu, kila kumtazama kwetu upya kukitufanya tufanane naye zaidi; kukua hata kumfikia Kristo katika mambo yote, mpaka tufikie kuwa mtu mkamilifu, hata kufikia kimo cha utimilifu wa Kristo. Hapa twaona kwamba kuna kazi ya Utakaso inayoendelea hatua kwa hatua.

3. Lakini hata sasa bado hatujapata jibu lote la swali, Watu Hutakaswa Lini. Tunaipata sehemu iliyobaki ya jibu la swali hili katika andiko letu, 1 Wathesalonike 5:23, likitafsiriwa kwa usahihi kama lilivyo katika Revised Version, “Na Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nayo roho yenu, na nafsi yenu, na mwili wenu, mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.” Hapa tunaambiwa waziwazi kwamba utakaso kamili wa waaminio, kamili kwa maana kamili kabisa, ni kitu cha kutafutwa katika maombi, nacho kitatimizwa na Mungu wakati ujao na kukamilishwa wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Wazo hilo hilo linapatikana katika kitabu hiki hiki, sura ya 3, mistari ya 12 na 13, “Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote, kama sisi tulivyo kwenu; ili awafanye imara mioyo yenu, iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wake wote.” Ni “wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wake wote” ndipo atakapoifanya imara mioyo yetu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu, na ndipo roho yetu na nafsi yetu na mwili wetu vitakapohifadhiwa kamili bila lawama. Wazo hilo hilo linapatikana katika 1 Yohana 3:2, “Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.” Si katika maisha haya ya sasa, wala si wakati wa kufa, tunapotakaswa kabisa, roho, nafsi, na mwili. Ni wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Hii ni mojawapo ya sababu nyingi kwa nini mwaminio aliyefundishwa vema hulia daima, “Amina; na uje, Bwana Yesu. Uje upesi.”