Sura 16 · dakika 11 za kusoma
Furaha ya Utii
Wakati mmoja nilisoma maneno haya: “Utii mkamilifu ungeleta furaha kamili, kama tungekuwa na tumaini kamili katika nguvu ile tuliyoitii.” Yalinigusa moyo. Yalinifunulia njia iwezekanayo, ambayo sikuwahi kuiwaza, ya kuwa na furaha. Baadaye, ijapokuwa uasi wangu, msemo huo uliendelea kuninginia moyoni. Uliahidi pumziko na njia ya kukua. Ulituliza na kuutosheleza moyo wangu wenye shauku.
Ni lazima niseme, nimelipata pumziko hili, si kama maono, bali kama uhalisi. Nimemwona Bwana Yesu, Bwana wetu. Twaweza kujitoa kwake na kulichukua nira lake juu yetu ili tupate pumziko kamili. Wewe, nafsi ipendwayo, isitasitayo, hujui furaha unayoikosa. Bwana amejidhihirisha kwako. Anataka ujisalimishe kwake kabisa. Wewe warudi nyuma na kusitasita. Kiasi fulani cha kujisalimisha u tayari kukitoa, nawe wafikiri kwamba ni sawa na inafaa ukitoe. Lakini waonekana kudhani kwamba kujitoa kabisa, bila kubakiza cho chote, ni jambo kubwa mno kuombwa. Waliogopa. Lahusisha mengi mno, wafikiri, nalo ni kazi kubwa mno. Kuwa mtii kwa kiasi ndiyo shauku yako; wazo la kuwa mtii kabisa lakutisha.
Wewe wawaona pia nafsi nyingine. Zaenenda kwa dhamiri zisizohangaika katika njia iliyo pana kuliko ile uliyowekewa wewe. Wajiuliza, kwa nini ni hivi? Laonekana jambo la ajabu, na labda gumu, kwamba wewe wapaswa kutenda yale wao wasiyopaswa kutenda. Tena, wapaswa kuacha bila kutenda yale wao walio na uhuru wa kuyatenda. Ah! Mkristo mpendwa, tofauti hii hasa iliyopo kati yenu ndiyo pendeleo lako, ijapokuwa bado hulijui. Bwana wako asema, “Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, ndiye anipendaye. Naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.”(Yohana 14:21) Wewe unazo amri zake; wale uwaoneao wivu, hawana. Wajua nia ya Bwana wako katika mambo mengi, ambayo, hata sasa, wao waenenda gizani. Je, hili si pendeleo? Je, ni jambo la kusikitikia kwamba nafsi yako iko karibu hivyo na Bwana wako? Yeye aweza kukuambia mambo ambayo walio mbali zaidi hawayajui. Je, hutambui ni kiwango gani cha urafiki wa ndani chenye upole hili likionyeshacho?
Mahusiano mengi ya maisha yahitaji kujitoa kwa kiasi tu kutoka pande zote mbili. Twaweza kuwa na urafiki mkubwa.
Lakini, twatumia sehemu kubwa ya maisha yetu katika shughuli zilizotengana, zilizo tofauti. Tunapokuwa pamoja, twaweza kufurahia ushirika wa mmoja na mwenzake. Twaweza kuona mambo mengi tunayoshiriki pamoja. Lakini, hatuhuzunishwi na kutengana. Urafiki mwingine ulio wa karibu zaidi hauingiliani nao. Twapungukiwa na upendo wa kutosha kuwa na haki au shauku ya kushiriki mambo yetu ya faragha kabisa. Kiasi fulani cha kujizuia na cha umbali ndicho kifaacho, twahisi hivyo. Lakini kuna mahusiano mengine maishani ambapo haya yote yabadilika. Urafiki huwa upendo. Mioyo miwili hujitoa mmoja kwa mwenzake, ili isiwe tena miwili bali mmoja.
Umoja wa nafsi hutokea, ambao hufanya vyote alivyo navyo mmoja kuwa mali ya mwenzake. Mambo yaliyotengana na njia zilizotengana za maisha haziwezekani tena. Mambo yaliyokuwa halali hapo awali sasa si halali. Ni kwa sababu ya ukaribu wa kifungo kifungacho. Kujizuia na umbali vifaavyo kwa urafiki tu huwa vyenye kuua katika upendo. Upendo hutoa vyote, na sharti upokee vyote kwa kubadilishana. Matakwa ya mmoja humfunga mwenzake.
Kila moyo watamani kuyajua matakwa ya siri ya mwenzake. Wataka kuruka juu ya upepo ili kuyatimiza.
Je, watu wa namna hii huhisi kulemewa na mzigo ambao upendo huweka juu yao? Je, huwaonea wivu urafiki ule wa baridi na wa utulivu wauonao? Je, hujuta ukaribu walio nao na mpendwa wao kwa sababu ya wajibu uzaao?
Je, hawajivunii katika wajibu huu hasa? Tena, kwa furaha ya upole na yenye shangwe, huwahurumia hao maskini walio mbali wasiothubutu kukaribia hivyo? Je, kila ufunuo mpya wa nia za mmoja kwa mwenzake si furaha? Tena, je, kuna njia yo yote iliyo ngumu ambayo upendo wao huwalazimisha kuiendea? Ah! Nafsi wapendwa, kama mmelijua hili, hata kwa saa chache; kama mmewahi kumpenda mtu kiasi cha kupata furaha katika kujitoa sadaka kwa ajili yake; kama mmewahi kutamani kuutoa utashi wenu kwa mwingine kama pendeleo tamu, basi, kwa upendo wote wa Bwana wenu wa mbinguni, nawasihi mfanye vivyo hivyo kwa ajili ya Mungu!
Yeye akupenda kwa upendo ulio zaidi ya upendo wa urafiki. Kama bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi wake, ndivyo Yeye akufurahiavyo wewe. Ni kujisalimisha kamili tu kutakakomtosheleza. Amekupa vyote, naye ataka vyote kwa kubadilishana. Kujizuia kwa kidogo kabisa kutamhuzunisha moyoni. Hakujizuia nafsi yake, basi wewe wawezaje kujizuia nafsi yako? Kwa ajili yako, alitoa vyote alivyokuwa navyo. Kwa ajili yake, wewe wapaswa kufanya vivyo hivyo. Ee, uwe mkarimu katika kujisalimisha kwako! Ipokee ari yake isiyopimika kwa ajili yako, kwa ari isiyopimika kwake Yeye. Uwe na furaha na hamu ya kujitupa kabisa katika mikono yake mipendwa, na kumkabidhi hatamu za utawala. Cho chote kilicho chako, mwache akipate chote. Achana milele na kila kitu kilichotengana naye. Nauacha uhuru wangu wa kuchagua. Nafurahia umoja wetu. Wafanya kujitoa kwangu kuwe si jambo liwezekanalo tu, bali la lazima.
Je, hukuwahi kutamani kumpenda mtu aliye mbali? Hukuwa karibu vya kutosha kwa ukaribu wa ndani zaidi. Je, hukuhisi shauku iwakayo ya kujisalimisha kwake? Lakini, hukuwa na mtu ye yote ambaye ungeweza kumpa upendo huo. Je, mikono yako haikujaa vidamu vya thamani sana vya marhamu, vya alabasta? Hukuwahi kuwa karibu vya kutosha na moyo wo wote ili kuvimimina. Kama ukiisikia sauti tamu ya Bwana wako, Yeye akuita kwenye mahali pa ukaribu naye Mwenyewe. Lataka kutengana na kila kitu kinginecho. Litafanya kujitoa kwako kuwe si jambo liwezekanalo tu, bali la lazima. Je, utarudi nyuma au utasitasita?
Je, utaona ni vigumu kwamba Yeye akufunulia zaidi ya nia yake kuliko awafunuliavyo wengine? Hatakuacha uwe na furaha katika jambo lo lote likutenganishalo naye Mwenyewe. Je, wataka kwenda mahali ambapo Yeye hawezi kwenda pamoja nawe, au kuwa na shughuli ambazo Yeye hawezi kuzishiriki?
La! La, mara elfu, la! Utaruka nje kuyalaki mapenzi yake mapendwa kwa furaha yenye hamu. Hata takwa lake dogo kabisa litakuwa sheria ikufungayo, ambayo kuivunja kungekuvunja moyo kabisa. Utafurahia wembamba wa njia akuwekeayo. Utawahurumia, kwa huzuni isiyo na kikomo, hao maskini walio mbali waliokosa furaha hii. Wajibu wa upendo utakuwa ndiyo mapendeleo yake matamu kupita yote. Haki yako ya kumpa Bwana wako vyako vyote itahisiwa kama kuinuliwa kwenye ulimwengu wa utukufu usioelezeka. Furaha kamili itatoka katika utii mkamilifu. Ndipo utakapoyajua kidogo ya yale Yesu aliyoyamaanisha aliposema, “ Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; naam, sheria yako imo moyoni mwangu.”( Zaburi 40:8 ) Nawe je, wadhani furaha iliyomo katika hili yote itakuwa upande wako? Je, Bwana hana furaha katika wale ambao wamejisalimisha hivyo kwake, na ambao hupenda kumtii? Ah, rafiki zangu, hatustahili kunena juu ya hili. Lakini Maandiko hufunua mianya ya ile furaha, kuridhika, na shangwe ambayo Bwana wetu anayo ndani yetu. Huiteka nafsi kwa vidokezo vyake vya ajabu vya heri. Kwamba sisi twamhitaji Yeye ni rahisi kufahamu; lakini kwamba Yeye atuhitaji sisi laonekana lisiloweza kufahamika. Ni jambo la asili kumtamani Yeye. Lakini kwamba Yeye atutamani sisi ni gumu kuamini. Lakini, mara kwa mara, Yeye alisema hivyo, nasi tuwezaje ila kumwamini?
Ameifanya mioyo yetu iweze kuuhisi upendo huu mkuu. Amejitoa Mwenyewe kuwa lengo lake. Ni jambo la thamani isiyo na kikomo kwake. Yeye asema, “Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, ndiye anipendaye.
Naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake”(Yohana 14:21). Yeye abisha hodi katika kila moyo, akitafuta kuwa upendo wake ulio mkuu. “Je, utanipokea?” humwambia mwaminiye, “ Ili niwe mpendwa wako, je, utanifuata katika mateso na upweke? Je, utavumilia taabu kwa ajili yangu? Usitake thawabu ila tabasamu na sifa yangu.
Je, utajitupa kwa kujitoa kabisa katika mapenzi yangu? Je, utanikabidhi mamlaka kamili juu ya nafsi yako na vyote ulivyo? Je, utaridhika na kunipendeza mimi, mimi peke yangu? Je, naweza kuwa na njia yangu ndani yako katika mambo yote? Je, utaingia katika umoja wa karibu hivyo nami hata kufanya kutengana na ulimwengu kuwe la lazima? Je, utanikubali kuwa Bwana wako wa pekee, na kuwaacha wengine wote, upate kushikamana nami peke yangu?” Kwa njia elfu, Yeye ahutolea kila mwaminiye toleo hili la umoja naye Mwenyewe. Lakini si wote wamwambiao, “Ndiyo.” Pendo nyingine na mambo mengine yaonekana kwao kuwa ya thamani mno hata kutupwa mbali.
Hawaikosi Mbingu kwa sababu ya hili. Lakini huikosa furaha isiyoelezeka.
Wewe, hata hivyo, si mmoja wa hawa. Tangu mwanzo kabisa nafsi yako imelia kwa hamu na furaha kwa matoleo yake yote, “Ndiyo, Bwana; ndiyo!” Wewe u tayari kupita kiasi kummiminia hazina zako zote zilizo bora za upendo na kujitoa. Ari yako ya kujisalimisha yaweza kuwasumbua baadhi ya Wakristo walio wa kadiri.
Upendo wako wafanya kutengana na ulimwengu kuwe la lazima, jambo ambalo upendo ulio duni hauwezi hata kuliwaza.
Sadaka na huduma zawezekana na ni tamu kwako. Zisingeweza kutoka katika moyo usiojitoa hivyo.
Maisha uliyoyaingia yakupa haki ya kumwaga kwa wingi vyako vyote juu ya Mpendwa wako. Huduma ambazo nafsi zilizo mbali zaidi hazizijui kamwe, sasa huwa pendeleo lako tamu kupita yote.
Bwana wako adai kwako, kwa sababu ya umoja wako naye, mengi zaidi kuliko adaiavyo kwao.
Yale yaliyo halali kwao, upendo umeyafanya kuwa si halali kwako. Kwako Yeye aweza kuzifunua siri zake, na kwako Yeye atazamia jibu la papo hapo kwa kila takwa la upendo wake. Ee, ni jambo la ajabu! Pendeleo lile tukufu, lisiloelezeka, uliloliingia! Haitakuwa na maana sana watu wakikuchukia. Waweza kukuepuka, kukushutumu, na kulitupa nje jina lako kama ovu kwa ajili yake! “Furahini siku ile, mkarukeruke kwa furaha. Thawabu yenu ni kubwa mbinguni. Kama mkishiriki mateso yake, mtashiriki pia utukufu wake.” Ndani yako Yeye aiona taabu ya nafsi yake, naye aridhika. Upendo wako na kujitoa kwako ndiyo thawabu yake ya thamani kwa yote aliyokutendea.
Ni jambo tamu lisiloelezeka kwake. Basi usiogope kujiachilia katika kujitoa kwa moyo wote kwa Bwana wako kusikovumilia kujizuia ko kote. Wengine waweza wasikubali, lakini Yeye atakubali, na hilo latosha. Usiupime utii wako wala huduma yako. Moyo wako na mkono wako uwe huru kumtumikia Yeye, kama vile moyo wake na mkono wake vilivyokuwa huru kukutumikia wewe. Mwache apate vyote ulivyo navyo, mwili, nafsi, na roho, wakati, vipawa, sauti, kila kitu. Yafunue maisha yako yote mbele zake ili apate kuyaongoza. Mwambie kila siku, “Bwana, nitaipangaje siku hii ili nikupendeze? Niende wapi? Nifanye nini? Nimtembelee nani? Niseme nini?” Ukabidhi akili yako mikononi mwake na useme, “Bwana, niambie jinsi ya kufikiri ili nikupendeze?” Mpe kusoma kwako, shughuli zako, urafiki wako. Kisha useme, “Bwana, nipe ufahamu wa kuyapima mambo haya kwa hekima yako.”” Usiache kuwe na siku wala saa ambayo humo huyafanyi mapenzi yake kwa akili, na kumfuata Yeye kikamilifu.
Kumtumikia Yeye kutayapa maisha yako mng’ao. Kutayapamba hata maisha yasiyopendeza kabisa kwa mng’ao wa kimbingu.
Je, umewahi kuhuzunika kwamba mvuto wa ujana hupotea upesi hivyo katika hali ngumu za ulimwengu? Mlete Mungu katika maisha yako na katika mambo yake madogo madogo. Furaha iliyo kuu zaidi itaitetemesha nafsi yako kuliko ile ambayo siku za ujana zilizong’aa zaidi zingeweza kuijua. Hakuna kitakachoonekana kigumu au kikali tena. Maisha yaliyo duni kabisa yatatukuzwa kwa hili. Nilipomtazama mwanamke maskini kwenye chombo chake cha kufulia, niliyawaza mambo ya kukatisha tamaa katika maisha yake. Nilijiuliza kwa nini maisha kama hayo lazima yawepo. Kisha, kwa mtetemo wa furaha, nilikumbuka kule kutukuzwa kwake kuwezekanako. Nilijiambia, hata maisha haya, yaliyoishiwa ndani ya Kristo na pamoja naye, yakimfuata Yeye po pote aongozapo, yangekuwa matukufu.
Kila saa yake yangejaa ari.
Nafarijika kujua kwamba baraka kuu za Mungu zakaa katika maisha yaliyo maskini na yaliyo manyenyekevu zaidi. “Kwa maana,” asema Bwana wetu Mwenyewe, “ye yote,” akiwa tajiri au maskini, mzee au kijana, mtumwa au huru.
Ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.
Tulia kitambo juu ya maneno haya yaliyo rahisi lakini ya ajabu. Ndugu yake, umbu lake, na mama yake! Ni nini tusingekitoa ili kuwa mmoja wa hawa! Ee, niache nikusihi, Mkristo mpendwa. Njoo, onja uone jinsi Bwana alivyo mwema. Yeye anayo mambo ya ajabu yaliyowekwa akiba kwa ajili ya wale “washikao amri zake, na kutenda yampendezayo machoni pake.” “Kama utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuzishika amri zake zote nikuagizazo leo, atakutukuza juu ya mataifa yote ya dunia. Kama utaisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, baraka hizi zote zitakujilia.”
“ Utabarikiwa mjini, na utabarikiwa mashambani. Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako, maongeo ya makundi yako ya ng’ombe, na wadogo wa makundi yako ya kondoo. Kikapu chako kitabarikiwa, na chombo chako cha kukandia unga. Utabarikiwa uingiapo, na utabarikiwa utokapo. Bwana atawafanya adui zako wakuoao washindwe mbele yako. Watakutokea kwa njia moja, nao watakukimbia kwa njia saba. (Kumbukumbu la Torati 28:3-7) “Bwana ataiamuru baraka ikae juu yako katika ghala zako, na katika kila utakalolitia mkono wako. Naye atakubariki katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako. Bwana atakuimarisha uwe taifa takatifu kwake, kama alivyokuapia, kama utazishika amri za Bwana, Mungu wako, na kwenda katika njia zake.” (Kumbukumbu la Torati 28:8-9) “ Na watu wote wa duniani wataona ya kuwa umeitwa kwa jina la Bwana, nao watakuogopa. Naye Bwana atakuzidishia mafanikio, katika uzao wa tumbo lako, na uzao wa wanyama wako, na uzao wa nchi yako, katika nchi ile Bwana aliyowaapia baba zako kukupa. Bwana atakufungulia hazina yake njema, mbingu, kuinyeshea nchi yako mvua kwa wakati wake, na kuibariki kila kazi ya mkono wako. Nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa. Naye Bwana atakufanya kuwa kichwa, wala si mkia; nawe utakuwa juu tu, wala hutakuwa chini; kama utazitii amri za Bwana, Mungu wako, nikuagizazo leo, kuzishika na kuzitenda,”(Kumbukumbu la Torati 28:10-13) Kwa Waisraeli, ilikuwa ya nje na ya muda. Kwetu sisi, ni ya ndani na ya kiroho. Tena, ni tukufu zaidi sana. Utashi wetu tuliojisalimisha na uruke nje kuukumbatia katika utimilifu wake wote!