Sura 23 · dakika 8 za kusoma
Neno na Maombi
‘Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lo lote, nanyi mtatendewa.’—Yohana 15:7.
KUUNGANA huku kwa lazima kati ya neno na maombi ni mojawapo ya masomo rahisi na ya kwanza kabisa katika maisha ya Kikristo. Kama vile yule mpagani aliyeongoka karibuni alivyosema: Ninaomba—ninasema na baba yangu; ninasoma—Baba yangu ananisemesha. Kabla ya kuomba, ni neno la Mungu linalonitayarisha kwa kunifunulia jambo ambalo Baba ameniamuru kuliomba. Katika kuomba, ni neno la Mungu linalonitia nguvu kwa kuipa imani yangu hoja na haki yake ya kuomba. Na baada ya kuomba, ni neno la Mungu linaloniletea jibu nikiisha kuomba, kwa maana ndani yake Roho hunijalia kuisikia sauti ya Baba. Maombi si mazungumzo ya upande mmoja bali ni mazungumzo ya pande mbili; sauti ya Mungu ikijibu yangu ndiyo sehemu yake ya muhimu zaidi. Kuisikiliza sauti ya Mungu ndiyo siri ya uhakika kwamba yeye ataisikiliza yangu. ‘Tega sikio lako, usikie;’ ‘Nitegee sikio;’ Isikie sauti yangu;’ ni maneno ambayo Mungu humwambia mwanadamu kama vile mwanadamu amwambiavyo Mungu. Kusikia kwake kutategemea kusikia kwetu; jinsi maneno yake yanavyopata nafasi ndani yangu, ndivyo kitakavyopimwa kiasi cha nguvu ya maneno yangu kwake. Maneno ya Mungu yalivyo kwangu, ndio kipimo cha jinsi yeye mwenyewe alivyo kwangu, na hivyo cha unyofu wa shauku yangu kwake katika maombi.
Ni uhusiano huu kati ya neno lake na maombi yetu ndio Yesu anaouonyesha asemapo, ‘Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lo lote, nanyi mtatendewa.’ Umuhimu mkuu wa ukweli huu unadhihirika tukiona usemi ule mwingine ambao huu umeuchukua nafasi yake. Zaidi ya mara moja Yesu alikuwa amesema, “Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu.’ Kukaa kwake ndani yetu kulikuwa ukamilisho na taji ya kukaa kwetu ndani yake. Lakini hapa, badala ya ‘Ninyi ndani yangu nami ndani yenu,’ asema, ‘Ninyi ndani yangu na maneno yangu ndani yenu.’ Maneno yake kukaa ni sawa na yeye mwenyewe kukaa.
Ni mtazamo gani mkubwa unaofunuliwa hapa kuhusu nafasi ambayo maneno ya Mungu katika Kristo yanapaswa kuwa nayo katika maisha yetu ya kiroho, na hasa katika maombi yetu. Katika maneno ya mtu hujifunua mwenyewe. Katika ahadi zake hujitoa mwenyewe, hujifunga kwa yule anayeipokea ahadi yake. Katika amri zake huweka wazi mapenzi yake, hutafuta kujifanya bwana juu ya yule anayedai utii wake, ili amwongoze na amtumie kana kwamba ni sehemu yake mwenyewe. Ni kwa njia ya maneno yetu ndipo roho hushirikiana na roho, ndipo roho ya mtu mmoja huvuka na kujihamishia kwa mwingine. Ni kwa njia ya maneno ya mtu, yaliyosikiwa na kukubaliwa, na kushikwa sana na kutiiwa, ndipo aweza kujitoa mwenyewe kwa mwingine. Lakini haya yote kwa maana finyu na yenye mipaka sana.
Lakini Mungu, yeye Mwenye kutokuwa na mwisho, ambaye ndani yake kila kitu ni uzima na nguvu, roho na kweli, kwa maana ya ndani kabisa ya maneno hayo,—Mungu ajisemapo mwenyewe katika maneno yake, kwa hakika hujitoa YEYE MWENYEWE, Upendo wake na Uzima wake, Mapenzi yake na Nguvu yake, kwa wale wanaoyapokea maneno haya, katika hali halisi ipitayo ufahamu. Katika kila ahadi hujiweka Mwenyewe mkononi mwetu ili tumshike na tumiliki; katika kila amri hujiweka Mwenyewe mkononi mwetu ili tushiriki naye Mapenzi yake, Utakatifu wake, Ukamilifu wake. Katika Neno la Mungu, Mungu hutupa SISI YEYE MWENYEWE; Neno lake si kitu pungufu ya Mwana wa Milele, Kristo Yesu. Na hivyo maneno yote ya Kristo ni maneno ya Mungu, yamejaa uzima na nguvu ya Kimungu yenye kuhuisha. ‘Maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.’
Wale waliojifunza kuhusu viziwi na mabubu hutuambia jinsi uwezo wa kusema unavyotegemea sana uwezo wa kusikia, na jinsi kupoteza kusikia kwa watoto kunavyofuatwa na kupoteza kusema pia. Jambo hili ni kweli kwa maana pana zaidi: kama tunavyosikia, ndivyo tusemavyo. Jambo hili ni kweli kwa maana ya juu kabisa katika mawasiliano yetu na Mungu. Kutoa ombi—kutamka matakwa fulani na kukumbusha ahadi fulani—ni jambo rahisi, nalo laweza kujifunzwa kutoka kwa mwanadamu kwa hekima ya kibinadamu. Lakini kuomba katika Roho, kunena maneno yanayomfikia na kumgusa Mungu, yanayoathiri na kuongoza nguvu za ulimwengu usioonekana,—kuomba huko, kunena huko, kwategemea kabisa kusikia kwetu sauti ya Mungu. Kwa kadiri tunavyoisikiliza sauti na lugha anayosema Mungu, na katika maneno ya Mungu kupokea mawazo yake, nia yake, uzima wake, mioyoni mwetu, ndivyo tutakavyojifunza kusema kwa sauti na lugha ambayo Mungu husikia. Ni sikio la mwanafunzi, lililoamshwa asubuhi kwa asubuhi, ndilo litayarishalo ulimi wa aliyefundishwa, kusema na Mungu vile vile na wanadamu, kama ipasavyo (Isaya 50:4).
Kuisikia huku sauti ya Mungu ni jambo kubwa kuliko kujifunza Neno kwa uangalifu tu. Yaweza kuwako mafunzo na maarifa ya Neno, ambamo mna ushirika mdogo tu wa kweli na Mungu aliye hai. Lakini kunako pia kusoma Neno, mbele za uso wenyewe wa Baba, na chini ya uongozi wa Roho, ambako ndani yake Neno hutujia kwa nguvu iliyo hai kutoka kwa Mungu mwenyewe; kwetu sisi ni sauti yenyewe ya Baba, ushirika halisi wa binafsi naye. Ni sauti iliyo hai ya Mungu iingiayo moyoni, iletayo baraka na nguvu, na kuamsha itikio la imani iliyo hai ifikiayo moyo wa Mungu tena.
Ni juu ya kuisikia huku sauti ndipo nguvu ya kutii na ya kuamini vyote hutegemea. Jambo kuu si kujua ni nini Mungu amesema tunapaswa kufanya, bali kwamba Mungu mwenyewe anatuambia. Si sheria, wala si kitabu, wala si kujua lililo sawa, kunakofanya utii, bali ni uvutano wa binafsi wa Mungu na ushirika wake ulio hai. Na hata vivyo hivyo si kujua ni nini Mungu ameahidi, bali ni uwepo wa Mungu mwenyewe akiwa Mwenye kuahidi, ndio uamshao imani na tumaini katika maombi. Ni katika uwepo kamili wa Mungu peke yake ndipo kutotii na kutokuamini vinakuwa jambo lisilowezekana.
‘Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lo lote, nanyi mtatendewa.’ Twaona maana yake. Katika maneno hayo Mwokozi hujitoa mwenyewe. Ni lazima tuwe na maneno hayo ndani yetu, yakiingizwa katika utashi wetu na maisha yetu, yakidhihirika katika tabia na mwenendo wetu. Ni lazima tuyawe nayo yakikaa ndani yetu: maisha yetu yote yakiwa ufafanuzi mmoja unaoendelea wa maneno yaliyo ndani, na kutujaza; maneno yakidhihirisha Kristo ndani, na maisha yetu yakimdhihirisha nje. Ni maneno ya Kristo yanapoingia ndani ya moyo wetu wenyewe, na kuwa maisha yetu na kuyaathiri, ndipo maneno yetu yataingia moyoni mwake na kumwathiri. Maombi yangu yatategemea maisha yangu; maneno ya Mungu yalivyo kwangu na ndani yangu, ndivyo maneno yangu yatakavyokuwa kwa Mungu na ndani ya Mungu. Nikifanya asemalo Mungu, Mungu atafanya nisemalo mimi.
Jinsi watakatifu wa Agano la Kale walivyouelewa vyema uhusiano huu kati ya maneno ya Mungu na yetu, na jinsi kwao maombi yalivyokuwa kweli itikio la upendo kwa yale waliyokuwa wamemsikia Mungu akiyanena! Kama neno lilikuwa ahadi, walimtegemea Mungu kufanya kama alivyokuwa amenena. ‘Fanya kama ulivyosema;’ ‘Kwa maana wewe, Bwana, umelinena;’ ‘Sawasawa na ahadi yako;’ ‘Sawasawa na neno lako;’ katika misemo kama hiyo walionyesha kwamba yale Mungu aliyonena katika ahadi yalikuwa shina na uzima wa yale waliyonena katika maombi. Kama neno lilikuwa amri, wao walifanya tu kama Bwana alivyokuwa amenena: ‘Basi Abramu akaenda kama Bwana alivyokuwa amemwambia.’ Maisha yao yalikuwa ushirika na Mungu, kubadilishana neno na wazo. Aliyoyanena Mungu waliyasikia na kuyafanya; waliyoyanena wao Mungu aliyasikia na kuyafanya. Katika kila neno analolinena kwetu, Kristo mzima hujitoa mwenyewe ili alitimize kwa ajili yetu. Kwa kila neno hataki pungufu ya sisi kumtoa mtu mzima ili alishike neno hilo, na kupokea utimilifu wake.
‘Maneno yangu yakikaa ndani yenu;’ sharti ni rahisi na wazi. Katika maneno yake mapenzi yake yanafunuliwa. Kadiri maneno yakaavyo ndani yangu, mapenzi yake huniongoza; utashi wangu huwa chombo kitupu ambacho mapenzi yake huyajaza, chombo chenye hiari ambacho mapenzi yake huyatumia; yeye huujaza utu wangu wa ndani. Katika kutenda utii na imani utashi wangu huzidi kuwa na nguvu, nao huletwa katika upatano wa ndani zaidi naye. Yeye aweza kuutumaini kabisa kwamba hautaki jambo lo lote ila lile alitakalo yeye; hana hofu kuitoa ahadi, ‘Maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lo lote, nanyi mtatendewa.’ Kwa wote waaminio hivyo, na kutenda kwa kadiri yake, atalitimiza neno hilo kihalisi kabisa.
Enyi wanafunzi wa Kristo! je, halizidi kuwa wazi zaidi na zaidi kwetu kwamba wakati tumekuwa tukitoa udhuru kwa maombi yetu yasiyojibiwa, kwa uzembe wetu katika maombi, kwa kudai kunyenyekea kwa hekima na mapenzi ya Mungu, sababu halisi imekuwa ni kwamba maisha yetu dhaifu ndiyo yaliyosababisha maombi yetu dhaifu? Hakuna kiwezacho kufanya watu kuwa na nguvu ila neno litujialo kutoka kinywani mwa Mungu: kwa hilo yatupasa kuishi. Ni neno la Kristo, lipendwalo, lililoishiwa ndani yake, likikaa ndani yetu, likiwa kwa njia ya utii na tendo sehemu ya utu wetu, ndilo litufanyalo kuwa kitu kimoja na Kristo, litustahilishalo kiroho kumgusa, kumshika Mungu. Yote yaliyo ya ulimwengu hupita; bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele. Ee na tuutoe moyo na uhai kwa maneno ya Kristo, maneno ambayo ndani yake yeye hujitoa YEYE MWENYEWE sikuzote, Mwokozi aliye hai, wa binafsi, nayo ahadi yake itakuwa uzoefu wetu wenye utajiri: ‘Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lo lote, nanyi mtatendewa.’
‘BWANA, UTUFUNDISHE KUOMBA!’
——0———
Ee Bwana mbarikiwa! Somo lako siku ya leo limenifunulia tena upumbavu wangu. Naona jinsi ilivyo kwamba maombi yangu hayakuwa na imani na nguvu zaidi. Nilikuwa nimeshughulika zaidi na kusema kwangu kwako kuliko kusema kwako kwangu. Sikuelewa kwamba siri ya imani ni hii: haiwezi kuwako imani ila kwa kadiri lilivyo Neno lililo hai likikaa nafsini.
Na neno lako lilikuwa limenifundisha waziwazi hivi: Kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, si mwepesi wa kusema; wala moyo wako usiharakishe kutoa neno lo lote mbele za Mungu. Bwana, nifundishe kwamba ni kwa neno lako lililoingizwa katika maisha yangu tu ndipo maneno yangu yaweza kupokelewa moyoni mwako; kwamba neno lako, likiwa nguvu iliyo hai ndani yangu, litakuwa nguvu iliyo hai kwako; kile ambacho kinywa chako kimekinena mkono wako utakitenda.
Ee Bwana! niokoe na sikio lisilotahiriwa. Nipe sikio lililofunguliwa la mwanafunzi, lililoamshwa asubuhi kwa asubuhi ili kuisikia sauti ya Baba. Kama vile wewe ulivyonena tu uliyoyasikia, maneno yangu na yawe mwangwi wa kunena kwako kwangu. ‘Musa alipoingia ndani ya hema ya kukutania ili anene naye, aliisikia sauti ikinena naye kutoka juu ya kiti cha rehema.’ Bwana, na iwe hivyo kwangu mimi pia. Maisha na tabia inayochukua alama moja, ya kwamba maneno yako yanakaa na kuonekana ndani yake, na yawe matayarisho ya baraka kamili: ‘Ombeni mtakalo lo lote, nanyi mtatendewa.’ Amina.
Sura ya 23 imekamilika
Neno na Maombi