Pamoja na Kristo katika Shule ya Maombi
Siri ya Maombi ya Imani

Sura 13 · dakika 8 za kusoma

Siri ya Maombi ya Imani

‘Yesu akajibu, akawaambia, Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia, Ye yote asiyeona shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yatatukia; atakuwa nayo. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo na kutaka, aminini ya kwamba mmeyapokea, nayo yatakuwa yenu.’—Marko 11:22-24.

AHADI ya kujibiwa maombi iliyokuwa somo letu la jana ni miongoni mwa ahadi za ajabu kuliko zote katika Maandiko yote. Katika mioyo mingapi imezusha swali hili: Ni jinsi gani nitaifikia imani inayojua kwamba inapokea yote iombayo?

Ni swali hili ambalo Bwana wetu angependa kulijibu leo. Kabla hajawapa wanafunzi wake ahadi ile ya ajabu, alinena neno lingine, ambamo anaonyesha mahali imani ya kujibiwa maombi inakoanzia, na inakopata daima nguvu zake. MWAMININI MUNGU: neno hili linatangulia lile lingine, Iaminini ahadi ya kujibiwa maombi. Uwezo wa kuamini ahadi hutegemea kabisa, na tena tu, imani katika mwenye kuahidi. Kumwamini mtu huzaa kuliamini neno lake. Ni pale tu tunapoishi na kushirikiana na Mungu katika uhusiano wa binafsi, wenye upendo, pale ambapo MUNGU MWENYEWE ndiye kila kitu kwetu, pale ambapo utu wetu wote unafunuliwa daima na kuwekwa wazi kwa nguvu kuu zitendazo kazi mahali Uwepo wake Mtakatifu unapodhihirishwa, ndipo uwezo utakapokua wa kuamini kwamba yeye hutoa lo lote tuombalo.

Uhusiano huu kati ya imani katika Mungu na imani katika ahadi yake utakuwa dhahiri kwetu tukifikiri imani ni nini hasa. Mara nyingi hulinganishwa na mkono au kinywa, ambacho kwacho twapokea na kujitwalia kile kinachotolewa kwetu. Lakini ni jambo la maana tuelewe kwamba imani pia ni sikio ambalo kwalo nasikia kile kilichoahidiwa, na jicho ambalo kwalo naona kile kinachotolewa kwangu. Juu ya hili uwezo wa kupokea hutegemea. Lazima nimsikie yule anipaye ahadi: sauti yake yenyewe hunipa ujasiri wa kuamini. Lazima nimwone: katika nuru ya jicho lake na uso wake hofu yote juu ya haki yangu ya kupokea hutoweka. Thamani ya ahadi hutegemea mwenye kuahidi: ni juu ya ujuzi wangu wa jinsi mwenye kuahidi alivyo ndipo imani katika ahadi hutegemea.

Ni kwa sababu hii kwamba Yesu, kabla hajatoa ahadi ile ya ajabu ya maombi, kwanza asema, ‘MWAMININI MUNGU.’ Yaani, jicho lako na liwe wazi kwa Mungu aliye hai, na umtazame yeye, ukimwona yeye asiyeonekana. Ni kwa jicho ndipo najisalimisha kwa nguvu ya kile kilicho mbele yangu; naiacha tu iingie, itende nguvu yake, na iache alama yake akilini mwangu. Basi kumwamini Mungu ni kumtazama tu Mungu na jinsi alivyo, kumruhusu adhihirishe uwepo wake, kumpa muda na kuutoa utu wote upokee alama kamili ya jinsi alivyo kama Mungu, nafsi ikifunuliwa ipokee na kufurahi katika kivuli cha upendo wake. Naam, imani ni jicho ambalo kwalo Mungu huonyesha alivyo na atendavyo: kwa imani nuru ya uwepo wake na matendo ya nguvu zake kuu humiminika ndani ya nafsi. Kama vile kile ninachokiona kikaavyo ndani yangu, vivyo hivyo kwa imani Mungu akaa ndani yangu pia.

Na vivyo hivyo imani pia ni sikio ambalo kwalo sauti ya Mungu husikiwa sikuzote na ushirika naye kudumishwa. Ni kwa njia ya Roho Mtakatifu ndipo Baba asema nasi; Mwana ni Neno, kiini cha kile anenacho Mungu; Roho ndiye sauti iliyo hai. Hii mtoto wa Mungu anaihitaji imwongoze na kumwelekeza; sauti ile ya siri kutoka mbinguni lazima imfundishe, kama ilivyomfundisha Yesu, la kunena na la kutenda. Sikio lililofunuliwa kumwelekea Mungu, yaani, moyo uaminio unaomngoja, upate kusikia asemalo, litamsikia akinena. Maneno ya Mungu hayatakuwa maneno ya Kitabu tu, bali, yakitoka kinywani mwa Mungu, yatakuwa roho na kweli, uzima na nguvu. Yataleta kwa tendo na kwa uzoefu ulio hai vile ambavyo kwingineko ni mawazo tu. Kwa sikio hili lililofunuliwa nafsi hukaa chini ya nguvu ya uzima na uweza wa Mungu mwenyewe. Kama vile maneno niyasikiayo yaingiavyo akilini na kukaa na kutenda kazi humo, vivyo hivyo kwa imani Mungu huingia moyoni, na kukaa na kutenda kazi humo.

Imani inapokuwa sasa katika utendaji kamili kama jicho na sikio, kama kipawa cha nafsi ambacho kwacho twamwona na kumsikia Mungu, ndipo itakapoweza kutumia nguvu zake kamili kama mkono na kinywa, ambavyo kwavyo twajitwalia Mungu na baraka yake. Uwezo wa kupokea utategemea kabisa uwezo wa utambuzi wa kiroho. Kwa sababu hii Yesu alisema, kabla hajatoa ahadi kwamba Mungu angeyajibu maombi ya imani: ‘MWAMININI MUNGU.’ Imani ni kujisalimisha tu: najisalimisha kwa alama ambayo habari nizisikiazo huiacha juu yangu. Kwa imani najisalimisha kwa Mungu aliye hai. Utukufu wake na upendo wake hujaza moyo wangu, na huutawala uzima wangu. Imani ni ushirika; najitoa kwa nguvu ya rafiki anipaye ahadi, na kuunganishwa naye kwayo. Na ni tupatapo kuingia katika ushirika huu ulio hai na Mungu mwenyewe, katika imani imwonayo na kumsikia yeye daima, ndipo yawapo rahisi na ya asili kuiamini ahadi yake juu ya maombi. Imani katika ahadi ni tunda la imani katika mwenye kuahidi: maombi ya imani yamefungamana katika maisha ya imani. Na kwa njia hii imani iombayo kwa mafanikio kwa kweli ni kipawa cha Mungu. Si kama kitu ambacho yeye hukitoa au kukimimina mara moja, bali kwa maana iliyo na kina zaidi na kweli zaidi, kama hali au tabia iliyobarikiwa ya nafsi ambayo hufanyizwa na kukua ndani yetu katika maisha ya ushirika naye. Bila shaka kwa yeye amjuaye Baba yake vema, na aishiye katika ushirika wa daima wa karibu naye, ni jambo rahisi kuiamini ahadi kwamba yeye atafanya mapenzi ya mtoto wake aishiye katika muungano naye.

Ni kwa sababu wengi mno wa watoto wa Mungu hawaelewi uhusiano huu kati ya maisha ya imani na maombi ya imani ndipo uzoefu wao wa nguvu ya maombi umepungua hivyo. Wanapotamani kwa bidii kupata jibu kutoka kwa Mungu, hukaza moyo wao wote juu ya ahadi, na kujitahidi kwa uwezo wao wote kuishika ahadi ile kwa imani. Wasipofaulu, huwa tayari kukata tamaa; ahadi ni kweli, lakini imepita uwezo wao kuishika kwa imani. Sikilizeni somo ambalo Yesu atufundisha siku hii: MWAMININI MUNGU, Mungu aliye hai: imani na imtazame Mungu kuliko kile kilichoahidiwa: ni upendo wake, nguvu yake, uwepo wake ulio hai utakaoiamsha na kuitenda imani. Tabibu angemwambia yule aombaye njia fulani ya kupata nguvu zaidi mikononi na katika viganja vyake ili ashike na kukamata, kwamba mwili wake wote lazima ujengwe na kutiwa nguvu. Vivyo hivyo dawa ya imani dhaifu hupatikana tu katika kutiwa nguvu kwa maisha yetu yote ya kiroho kwa ushirika na Mungu. Jifunze kumwamini Mungu, kumshika Mungu, kumruhusu Mungu autwae uzima wako, nayo itakuwa rahisi kuishika ahadi. Yeye amjuaye na kumtumaini Mungu huona rahisi kuiamini ahadi pia.

Ona tu jinsi jambo hili linavyodhihirika waziwazi kwa watakatifu wa zamani. Kila onyesho la pekee la nguvu ya imani lilikuwa tunda la ufunuo wa pekee wa Mungu. Litazame kwa Abrahamu: ‘neno la Bwana lilimjia Abramu, likisema, Usiogope, Abramu; mimi ni ngao yako. Naye Akamchukua nje, akasema . . . AKAMWAMINI BWANA.’ Na baadaye tena: ‘Bwana akamtokea, akamwambia Mimi ni Mungu Mwenyezi. Abramu akaanguka kifudifudi, na Mungu akazungumza naye, akisema, Mimi, tazama, agano langu li pamoja nawe.’ Ni ufunuo wa Mungu mwenyewe uliyoipa ahadi nguvu yake iliyo hai ili iingie moyoni na kuitenda imani. Kwa sababu walimjua Mungu, watu hawa wa imani hawakuweza kufanya lo lote ila kuiamini ahadi yake. Ahadi ya Mungu itakuwa kwetu kile Mungu mwenyewe alicho. Ni mtu aendaye mbele za Bwana, na kuanguka kifudifudi ili asikilize Mungu aliye hai anenapo naye, ndiye atakayeipokea ahadi kweli. Ingawa tunazo ahadi za Mungu katika Biblia, tukiwa na uhuru kamili wa kuzitwaa, nguvu ya kiroho hupungua, isipokuwa Mungu mwenyewe atuambiapo. Naye huwaambia wale waendao na kuishi pamoja naye. Kwa hiyo, MWAMININI MUNGU: imani na iwe jicho tupu na sikio, kujisalimisha ili Mungu aweke alama yake kamili, na kujidhihirisha kwa ukamilifu ndani ya nafsi. Ihesabu kuwa mojawapo ya baraka kuu za maombi kutumia imani katika Mungu, kama Mungu aliye hai na mwenye nguvu anayengoja kutimiza ndani yetu radhi yote ya mapenzi yake, na kazi ya imani kwa nguvu. Mwone yeye kuwa Mungu wa Upendo, ambaye furaha yake ni kubariki na kujitoa mwenyewe. Katika ibada hiyo ya imani katika Mungu nguvu itakuja upesi kuiamini ahadi pia: ‘YO YOTE MYAOMBAYO, AMININI YA KWAMBA MMEYAPOKEA.’ Naam, angalia kwamba kwa imani umfanye Mungu kuwa wako mwenyewe; ahadi itakuwa yako pia.

Mafunzo ya thamani ambayo Yesu anayo ya kutufundisha siku hii. Twatafuta vipawa vya Mungu: Mungu anataka kutupa YEYE MWENYEWE kwanza. Twafikiri maombi kuwa nguvu ya kuvuta vipawa vyema kutoka mbinguni; Yesu huyafikiri kuwa njia ya kujivuta juu kwa Mungu. Twataka kusimama mlangoni na kulia; Yesu angependa kwanza tuingie ndani na kutambua kwamba sisi ni rafiki na watoto. Na tukubali fundisho hili. Kila uzoefu wa udogo wa imani yetu katika maombi na utusukume kwanza kuwa na kutumia imani zaidi katika Mungu aliye hai, na katika imani hiyo kujisalimisha kwake. Moyo uliojaa Mungu una nguvu kwa maombi ya imani. Imani katika Mungu huzaa imani katika ahadi, na katika ahadi pia ya kujibiwa maombi.

Kwa hiyo, mtoto wa Mungu, tenga wakati, tenga wakati, wa kuinama mbele zake, wa kumngoja yeye ili ajidhihirishe mwenyewe. Tenga wakati, na nafsi yako kwa hofu takatifu na ibada itumie na kuidhihirisha imani yake katika yeye Asiye na Mwisho, na atakapojitoa mwenyewe na kukumiliki, maombi ya imani yataitawaza imani yako katika Mungu.

‘BWANA, UTUFUNDISHE KUOMBA.’

Ee Mungu wangu! Nakuamini wewe. Nakuamini wewe kama Baba, Usiye na Mwisho katika Upendo wako na Uweza wako. Na kama Mwana, Mkombozi wangu na Uzima wangu. Na kama Roho Mtakatifu, Mfariji na Mwongozi na Nguvu. Ee Mungu Mmoja katika Utatu, nina imani kwako. Najua na nina hakika kwamba yote uliyo, u hivyo kwangu, na kwamba yote uliyoahidi utayatimiza.

Bwana Yesu! ongeza imani hii. Nifundishe kutenga wakati, na kungoja na kuabudu katika Uwepo Mtakatifu mpaka imani yangu ipokee yote yaliyomo kwa Mungu wangu kwa ajili yangu. Iiache imwone yeye kuwa Chemchemi ya Uzima wote, akitenda kazi kwa Nguvu za Uweza wote ili kutimiza mapenzi yake ulimwenguni na ndani yangu. Iiache imwone yeye katika upendo wake akitamani kukutana na kutimiza haja zangu. Iiache imiliki moyo wangu na uzima wangu hata kwa imani Mungu peke yake akae humo. Bwana Yesu, nisaidie! kwa moyo wangu wote ningemwamini Mungu. Imani katika Mungu na inijaze kila dakika.

Ee Mwokozi wangu Mbarikiwa! laweza kanisa lako kukutukuza namna gani, laweza kutimiza namna gani kazi ile ya maombezi ambayo kwayo ufalme wako lazima uje, isipokuwa maisha yetu yote yawe IMANI KATIKA MUNGU. Ee Bwana Mbarikiwa! nena Neno lako, ‘MWAMININI MUNGU,’ hata vilindini mwa nafsi zetu.

Ukurasa 1 / 1 · 8 dakika zimebaki katika sura