Sura 12 · dakika 9 za kusoma
Imani Ipokeayo
“Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo na kuyataka, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.”—Marko 11:24
Ahadi ilioje hii! Kubwa kiasi hicho, tena ya Kimungu kiasi hicho, hata mioyo yetu midogo haiwezi kuiweza wala kuipokea kabisa, nayo kwa kila njia iwezekanayo hutafuta kuiwekea mipaka kulingana na tuonavyo kuwa salama au yawezekana; badala ya kuiacha, katika nguvu na uwezo wake uhuishao, kama vile alivyoitoa, iingie ndani, na kuipanua mioyo yetu hata kufikia kipimo cha kile ambacho upendo na uweza wake viko tayari kweli kututendea. Imani iko mbali sana na kuwa shime tu ya ukweli wa neno la Mungu, au hitimisho litokanalo na misingi fulani. Ni sikio lililomsikia Mungu akisema atakalolitenda, ni jicho lililomwona akilitenda, na kwa hiyo, palipo na imani ya kweli, haiwezekani jibu lisije. Kama tukiangalia tu kwamba twatenda lile jambo moja atutakalo tunapoomba: AMINI ya kwamba mmekwisha kupokea; yeye ataangalia kwamba anatenda lile alilolaidi: “Yatakuwa yenu.” Sauti kuu ya maombi ya Sulemani (2 Mambo ya Nyakati 6:4), “Na ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, aliyenena na baba yangu Daudi kwa kinywa chake, naye ametimiza kwa mikono yake yale aliyoyanena kwa kinywa chake,” ndiyo sauti kuu ya maombi yote ya kweli: kumwabudu kwa furaha Mungu ambaye mkono wake sikuzote huhakikisha utimilifu wa kile kinywa chake kilichonena. Basi, kwa roho hii na tusikilize kwa makini ahadi ile anayoitoa Yesu; kila sehemu yake ina ujumbe wake wa Kimungu unaostahili kusikilizwa.
“Yo yote mtakayo.” Katika neno hili la kwanza hekima yetu ya kibinadamu mara moja huanza kutia shaka na kuuliza: Je, hakika hili haliwezi kuwa kweli kihalisi kabisa? Lakini kama sivyo, kwa nini Bwana alilinena, akitumia usemi wenye nguvu kuliko yote aliouweza kuupata: “Yo yote mtakayo.” Wala si kana kwamba ni mara hii tu aliponena hivi; je, si yeye pia aliyesema, “Ukiweza kuamini, YOTE yanawezekana kwake yeye aaminiye;” “Kama mkiwa na imani, HAKUNA lisilowezekana kwenu.” Imani ni kazi ya Roho wa Mungu kabisa kwa njia ya neno lake katika moyo uliotayarishwa wa mwanafunzi aaminiye, hata haiwezekani utimilifu usije; imani ni rehani na mtangulizi wa jibu lijalo. Naam, “YO YOTE MTAKAYO katika maombi mkisali huku mkiamini, mnapokea.” Mwelekeo wa akili ya kibinadamu ni kuingilia hapa, na kwa vishazi fulani vya masharti, “ikiwa yafaa,” “ikiwa ni kulingana na mapenzi ya Mungu,” kuvunja nguvu ya kauli ionekanayo kuwa ya hatari. Ee, na tujihadhari kutenda hivi na maneno ya Bwana. Ahadi yake ni kweli kihalisi kabisa. Anataka “YO YOTE” yake aliyoirudia mara nyingi iingie mioyoni mwetu, na kutufunulia jinsi nguvu ya imani ilivyo kuu, jinsi Kichwa kinavyowaita viungo kushiriki naye katika uweza wake, jinsi Baba yetu anavyouweka uweza wake wote mikononi mwa mtoto amtumainiye kwa moyo wote. Katika “yo yote” hii imani itapata chakula na nguvu zake: tunapoidhoofisha, tunaidhoofisha imani. “YO YOTE” haina masharti: sharti pekee ni lile lililomo katika kuamini. Kabla hatujaweza kuamini ni lazima tuvumbue na kujua mapenzi ya Mungu ni yapi; kuamini ni zoezi la nafsi iliyojisalimisha na kujitoa chini ya uvutano wa Neno na Roho; lakini mara tuaminipo hakuna litakalokuwa lisilowezekana. Mungu na akatae tusijaribu kuyashusha “YOTE” yake hata kufikia kipimo cha kile tuonacho kuwa yawezekana. Sasa na tuchukue tu “YO YOTE” ya Kristo kama kipimo na tumaini la imani yetu: ni neno-mbegu ambalo, likichukuliwa kama vile alivyolitoa na kutunzwa moyoni, litajifunua na kuota mizizi, kuijaza maisha yetu kwa utimilifu wake, na hatimaye kuzaa matunda tele.
“Yo yote myaombayo na kuyataka.” Ni katika maombi ambapo “yo yote” hii huletwa kwa Mungu, kuombwa na kupokewa kutoka kwake. Imani ile ipokeayo vitu hivyo ni tunda la maombi. Kwa upande mmoja ni lazima iwepo imani kabla ya kuwepo maombi; kwa upande mwingine imani ni tokeo na ukuzi wa maombi. Ni katika uwepo wa binafsi wa Mwokozi, katika kushirikiana naye, ambapo imani huinuka kushika kile ambacho hapo kwanza kilionekana kuwa cha juu mno. Ni katika maombi ambapo twashikilia shauku yetu mbele ya nuru ya Mapenzi Matakatifu ya Mungu, ambapo nia zetu hujaribiwa, na ushahidi hutolewa kama kweli twaomba katika jina la Yesu, na kwa ajili ya utukufu wa Mungu peke yake. Ni katika maombi ambapo twangoja mwongozo wa Roho atuonyeshe kama twaomba jambo lililo sahihi na kwa roho iliyo sahihi. Ni katika maombi ambapo tunapata kujitambua upungufu wetu wa imani, ambapo twaongozwa kumwambia Baba kwamba twaamini, na kwamba twathibitisha uhalisi wa imani yetu kwa ujasiri ule ambao kwao twadumu. Ni katika maombi ambapo Yesu hufundisha na kuvuvia imani. Yeye angojaye kuomba, au akatishwaye tamaa katika maombi, kwa sababu bado hahisi imani inayohitajika kupata jibu, kamwe hatajifunza kuamini kwa kweli. Yeye aanzaye kuomba na kutaka atavumbua kwamba Roho wa imani hakuna mahali unapotolewa kwa hakika zaidi kama miguuni pa Kiti cha Enzi.
“Aminini ya kwamba mnayapokea.” Ni wazi kwamba tunachopaswa kuamini ni kwamba twapokea vilevile vitu tuombavyo. Mwokozi haashirii kwamba kwa kuwa Baba anajua kilicho bora huenda akatupa kitu kingine. Ule mlima ule ule ambao imani huuamuru uondoke hutupwa baharini kabisa. Kuna maombi ambayo, katika kila jambo, twadhihirisha haja zetu kwa maombi na dua, na thawabu yake ni amani tamu ya Mungu ilindayo moyo na akili. Haya ni maombi ya kutumaini tu. Yahusu vitu ambavyo hatuwezi kuvumbua kama Mungu atavitoa au la. Kama watoto twadhihirisha shauku zetu katika mambo yasiyohesabika ya maisha ya kila siku, na kumwachia Baba atoe au asitoe kama aonavyo kuwa bora. Lakini maombi ya imani ambayo Yesu anena juu yake ni jambo tofauti, jambo lililo juu zaidi. Wakati, ikiwa katika mambo makuu zaidi ya kazi ya Bwana, au katika mambo madogo ya maisha yetu ya kila siku, nafsi inapoongozwa kuona jinsi hakuna kitu kimheshimucho Baba kama imani iliyo na hakika kwamba atatenda alilolinena kwa kutupa yo yote tuombayo, na kusimama juu ya ahadi kama ilivyoletwa moyoni na Roho, yaweza kujua kwa hakika kabisa kwamba yapokea sawasawa kile iombacho. Tazama tu jinsi Bwana anavyotuwekea hili wazi katika mstari wa 23: “Kila mtu asiyeona shaka moyoni mwake, bali akaamini kwamba hayo asemayo yatatukia, atayapata.” Hii ndiyo baraka ya maombi ya imani ambayo Yesu anena juu yake.
“Aminini ya kwamba mmekwisha kupokea.” Hili ni neno la maana kuu kabisa, ambalo maana yake mara nyingi hueleweka vibaya. Amini kwamba umepokea! sasa, ukiwa unaomba, kile ukiombacho. Yaweza kuwa ni baadaye tu ndipo utakapokipata katika uzoefu wa binafsi, ndipo utakapoona kile uaminicho; lakini sasa, bila kuona, wapaswa kuamini kwamba umekwisha kupewa na Baba aliye mbinguni. Kupokea au kukubali jibu la maombi ni kama vile kumpokea au kumkubali Yesu au msamaha, ni jambo la kiroho, ni tendo la imani lililo mbali na hisia zote. Nijapo kama mwombaji wa msamaha, naamini kwamba Yesu aliye mbinguni yu kwa ajili yangu, na hivyo napokea au namchukua. Nijapo kama mwombaji wa zawadi yo yote maalum, iliyo kulingana na neno la Mungu, naamini kwamba kile niombacho napewa: naamini kwamba ninacho, nakishika kwa imani; namshukuru Mungu kwamba ni changu. “Kama tukijua kwamba atusikia, kwa lo lote tuombalo, twajua kwamba tunayo yale maombi tuliyomwomba.”
“Nanyi mtayapata.” Yaani, zawadi ile ambayo kwanza twaishika kwa imani kama iliyotunukiwa kwetu mbinguni itakuwa pia yetu katika uzoefu wa binafsi. Lakini je, itakuwa lazima kuendelea kuomba mara tukiisha kujua kwamba tumesikiwa na tumepokea kile tulichoomba? Kuna hali ambazo maombi kama hayo hayatakuwa ya lazima, ambazo baraka iko tayari kupenya mara moja, kama tukishikilia tu uhakika wetu, na kuthibitisha imani yetu kwa kusifu kwa ajili ya kile tulichopokea, ijapokuwa bado hatujakipata katika uzoefu. Kuna hali nyingine ambazo imani iliyokwisha pokea inahitaji kujaribiwa zaidi na kuimarishwa katika maombi ya kudumu. Mungu peke yake ndiye ajuaye ni lini kila kitu kilichomo ndani yetu na kinachotuzunguka kimekomaa kabisa kwa ajili ya kudhihirishwa kwa baraka iliyokwisha tolewa kwa imani. Eliya alijua kwa hakika kwamba mvua itakuja; Mungu alikuwa ameiahidi; na bado ilimbidi aombe mara saba. Nayo maombi hayo hayakuwa maonyesho wala mchezo; yalikuwa uhalisi wa kiroho ulio mkali moyoni mwa yeye aliyelala pale akisihi, na mbinguni juu ambapo yalikuwa na kazi yake yenye matokeo ya kutenda. Ni “kwa imani na uvumilivu twarithi zile ahadi.” Imani yasema kwa uhakika mkubwa kabisa, Nimekwisha kupokea tayari. Uvumilivu hudumu katika maombi hata zawadi iliyotunukiwa mbinguni ionekane duniani. “Aminini ya kwamba mmekwisha kupokea, nanyi mtapata.” Kati ya kupokea kule mbinguni, na kupata kule duniani, amini: sifa na maombi ya kuamini ndiyo kiunganishi.
Na sasa, tena, kumbuka jambo moja zaidi: Ni Yesu aliyesema hili. Tunapoona mbingu ikifunguliwa hivi kwetu, na Baba juu ya Kiti cha Enzi akijitolea kutupa yo yote tuombayo kwa imani, mioyo yetu hujaa aibu kwamba tumejinufaisha kidogo hivyo na pendeleo letu, na kujaa hofu kwamba imani yetu dhaifu bado itashindwa kushika kile kilichowekwa waziwazi hivyo ndani ya uwezo wetu wa kufikia. Kuna jambo moja lipasalo kutufanya wenye nguvu na wenye tumaini tele: ni Yesu mwenyewe aliyetuletea ujumbe huu kutoka kwa Baba. Yeye mwenyewe, alipokuwa duniani, aliishi maisha ya imani na maombi. Ni wakati wanafunzi walipoonyesha mshangao wao juu ya kile alichokitenda kwa mtini, ndipo alipowaambia kwamba maisha yale yale aliyoyaishi yangeweza kuwa yao; kwamba wangeweza si kuuamuru mtini tu, bali hata mlima wenyewe, nao ni lazima uutii. Naye ndiye uzima wetu: yote aliyokuwa duniani ndivyo alivyo ndani yetu sasa; yote afundishayo hutupa kweli. Yeye mwenyewe ndiye Mwanzilishi na Mkamilishaji wa imani yetu: yeye hutoa roho ya imani; tusiogope kwamba imani kama hiyo haikukusudiwa kwa ajili yetu. Imekusudiwa kwa kila mtoto wa Baba; iko ndani ya uwezo wa kufikia wa kila mmoja wetu atakayekuwa kama mtoto, akijitoa kwa Mapenzi na Upendo wa Baba, akiliamini Neno na Uweza wa Baba. Ndugu Mkristo mpendwa! wazo la kwamba neno hili huja kupitia Yesu, Mwana, Ndugu yetu, na litupe ujasiri, na jibu letu na liwe: Naam, Bwana mbarikiwa, twaliamini Neno lako, twaamini kwamba twapokea.
“BWANA, UTUFUNDISHE KUOMBA.”
Bwana mbarikiwa! Wewe ulikuja kutoka kwa Baba ili kutuonyesha upendo wake wote, na hazina zote za baraka ambazo upendo huo unangoja kuzitoa. Bwana! leo tena umezifungua wazi hivyo lango, na kutupa ahadi kama hizi juu ya uhuru wetu katika maombi, hata ni lazima tuone haya kwamba mioyo yetu maskini imezipokea kidogo hivyo. Kwa kweli zimekuwa kubwa mno kwetu hata kuziamini.
Bwana! sasa twakutazama wewe utufundishe kulichukua na kulitunza na kulitumia neno lako hili la thamani: “Yo yote mtakayo, aminini ya kwamba mmekwisha kupokea.” Yesu mbarikiwa! ni wewe mwenyewe ambaye ndani yako ni lazima imani yetu iote mizizi ikiwa itakuwa na nguvu. Kazi yako imetuweka huru kabisa na nguvu ya dhambi, na kuifungua njia kwa Baba; Upendo wako sikuzote unatamani kutuleta katika ushirika kamili wa utukufu na uweza wako; Roho wako sikuzote hutuvuta juu katika maisha ya imani kamili na uhakika; twahakikishiwa kwamba katika mafundisho yako tutajifunza kuomba maombi ya imani. Wewe utatuzoeza kuomba hata tuamini kwamba twapokea, kuamini kwamba kweli tunacho kile tuombacho. Bwana! nifundishe hivyo kukujua na kukutumaini na kukupenda, hivyo kuishi na kukaa ndani yako, hata maombi yangu yote yapande na kuja mbele za Mungu ndani yako, na nafsi yangu iwe na uhakika ndani yako kwamba nasikiwa. Amina.
Sura ya 12 imekamilika
Imani Ipokeayo