Sura 7 · dakika 12 za kusoma · dakika 16 za kusikiliza
Imewapasa Watu Kuomba Sikuzote
Nashuku kwamba kwa desturi nimekuwa nikitenga wakati mchache mno kwa mazoezi ya kidini kama ibada ya faragha, kutafakari mambo ya Mungu, kusoma Maandiko, na kadhalika. Ndiyo sababu nimekonda, nimepoa, na nimekuwa mgumu. Huenda Mungu angenifanikisha zaidi katika mambo ya kiroho kama ningekuwa na bidii zaidi katika kuzitumia njia za neema. Ni afadhali nitenge wakati zaidi, tuseme saa mbili au saa moja na nusu, kwa mazoezi ya kidini kila siku, na nijaribu kama kwa kufanya hivyo siwezi kudumisha hali ya roho iliyo ya ibada zaidi kwa desturi, hisia iliyo hai zaidi ya mambo yasiyoonekana, upendo wa moto zaidi kwa Mungu, kiasi kikubwa zaidi cha njaa na kiu ya haki, moyo usioelekea sana kuchafuliwa na masumbufu ya dunia, mipango yake, tamaa zake na hofu zake, na shauku ya kweli isiyo na unafiki ya kuitamani mbingu, furaha zake na usafi wake.—William Wilberforce
“Imewapasa kuomba sikuzote, wala wasikate tamaa.” Maneno haya ni maneno ya Bwana wetu, ambaye si tu kwamba daima alijitahidi kuwafundisha wafuasi wake uharaka na umuhimu wa maombi, bali pia aliwawekea kielelezo ambacho wao, ole wetu, wamekuwa wazito mno kukiiga.
Neno sikuzote lajieleza lenyewe. Maombi si kazi isiyo na maana wala wajibu wa kusukumizwa katika pembe za siku zilizojaa shughuli au uchovu; wala hatulitii agizo la Bwana wetu tunaporidhika na dakika chache magotini katika pilikapilika za asubuhi, au usiku sana wakati akili, zikiwa zimechoshwa na kazi za mchana, zinalilia pumziko. Ni kweli kwamba Mungu yuko karibu sikuzote tumwitapo; sikio lake ni sikivu daima kwa kilio cha mtoto wake. Lakini hatuwezi kamwe kumjua ikiwa tunatumia chombo cha maombi kama tutumiavyo simu—kwa maneno machache ya mazungumzo ya haraka. Urafiki wa ndani huhitaji kukuzwa. Hatuwezi kamwe kumjua Mungu kama tulivyopewa fursa ya kumjua, kwa kurudiarudia kwa ufupi, kwa vipande vipande na bila kufikiri, maombi ambayo ni maombi ya fadhili za kibinafsi na zaidi ya hayo si kitu. Hiyo si njia ambayo kwayo twaweza kuingia katika mawasiliano na Mfalme wa mbinguni. “Lengo la maombi ni sikio la Mungu,” nalo ni lengo linaloweza kufikiwa tu kwa kumngoja kwa saburi, kwa kudumu na bila kukoma, tukimmiminia mioyo yetu na kumruhusu atuzungumzie. Kwa kufanya hivyo tu ndipo twaweza kutazamia kumjua; na kadiri tunavyozidi kumjua, ndivyo tutakavyokaa muda mrefu zaidi mbele zake, na kuona kwamba kuwako kwake ni furaha ya daima inayozidi kuongezeka.
Sikuzote haimaanishi kwamba tuyapuuze majukumu ya kawaida ya maisha. Maana yake ni kwamba nafsi iliyoingia katika ushirika wa ndani na Mungu katika ukimya wa chumba cha maombi haiachi kamwe kufahamu kwamba iko karibu na Baba; kwamba moyo daima unamwelekea kwa ushirika wa upendo; na kwamba mara akili inapoachiliwa kutoka katika kazi inayoishughulisha, hurudi kwa Mungu kwa kawaida kama ndege arudivyo kiotani mwake. Tazama jinsi wazo la maombi linavyokuwa zuri tukiyaangalia katika nuru hii, tukiyaona kuwa ushirika wa daima, mazungumzo yasiyokatika mbele ya Mfalme. Hapo maombi hupoteza kila chembe ya hofu yaliyokuwa nayo huenda zamani; hatuyaoni tena kuwa wajibu unaopaswa kutimizwa, bali fursa ya kufurahiwa, furaha adimu inayofunua daima uzuri fulani mpya.
Basi, tufumbuapo macho asubuhi, mawazo yetu hupanda mbinguni mara moja. Kwa Wakristo wengi saa za asubuhi ndizo sehemu ya thamani kuliko zote ya siku, kwa sababu zinatoa nafasi ya ule ushirika mtakatifu unaoweka msingi wa mpango mzima wa siku. Na ni utangulizi gani ulio bora zaidi kwa utukufu na ajabu isiyokoma ya siku mpya kuliko kuianza peke yako pamoja na Mungu? Yasemekana kwamba Bwana Moody, wakati ambapo hapakuwa na mahali pengine, alikuwa akiifanya ibada yake ya asubuhi ndani ya kibanda cha makaa ya mawe, akimmiminia Mungu moyo wake, na kuona katika Biblia yake ya thamani “karamu ya vinono” kweli kweli.
George Müller naye aliunganisha kujifunza Biblia na maombi katika saa tulivu za asubuhi. Wakati mmoja desturi yake ilikuwa kujitoa kwa maombi asubuhi, baada ya kuvaa. Kisha mpango wake ukabadilika. Kama alivyoeleza mwenyewe: “Niliona kwamba jambo la muhimu kuliko yote nililopaswa kufanya ni kujitoa kwa kusoma Neno la Mungu, na kulitafakari, ili hivyo moyo wangu ufarijiwe, utiwe moyo, uonywe, ukemewe, ufundishwe; na ili hivyo, kwa njia ya Neno la Mungu, nikilitafakari, moyo wangu uletwe katika ushirika halisi na Bwana. Kwa hiyo nilianza kutafakari Agano Jipya asubuhi na mapema. Jambo la kwanza nililofanya, baada ya kuomba kwa maneno machache baraka ya Bwana juu ya Neno lake la thamani, lilikuwa kuanza kulitafakari Neno la Mungu, nikichunguza, kwa kusema hivyo, kila mstari ili kupata baraka ndani yake; si kwa ajili ya huduma ya hadhara ya Neno, si kwa ajili ya kuhubiri yale niliyoyatafakari, bali kwa ajili ya kupata chakula kwa nafsi yangu mwenyewe. Matokeo niliyoyaona karibu sikuzote ni haya: kwamba baada ya dakika chache tu nafsi yangu imeongozwa kwenye kuungama, au kushukuru, au kuomba kwa ajili ya wengine, au kusihi; hata ingawa, kwa kusema hivyo, sikujitoa kwa maombi bali kwa kutafakari, hata hivyo kutafakari huko kuligeuka karibu mara moja, kwa kiasi fulani, kuwa maombi.”
Kujifunza Neno na maombi huenda pamoja; na pale tuonapo kimoja kikifanywa kwa kweli, kingine hakika kitaonekana kando yake katika muungano wa karibu.
Lakini hatuombi sikuzote. Hiyo ndiyo shida ya wengi wetu. Twahitaji kuomba zaidi sana kuliko tunavyoomba, na kwa muda mrefu zaidi sana kuliko tunavyoomba.
Robert Murray McCheyne, mwenye vipawa na mtakatifu, ambaye ilisemwa juu yake kwamba “Akitazamwa kama mwana, kama ndugu, kama rafiki, au kama mchungaji, alikuwa kielelezo kisicho na kasoro kabisa na cha kuvutia kabisa cha Mkristo wa kweli waliyewahi kumwona akiwa katika umbo la mtu aliye hai,” alijua maana ya kukaa muda mrefu magotini, wala hakuchoka kamwe kuwasihi wengine waione furaha na thamani ya maombezi matakatifu. “Watoto wa Mungu hawana budi kuomba,” alisema. “Hawana budi kumlilia mchana na usiku. Mungu husikia kila kilio chenu katika saa yenye shughuli za mchana na katika makesha ya upweke ya usiku.” Kwa kila njia, kwa kuhubiri, kwa kuonya alipokuwapo na kwa barua alipokuwa mbali, McCheyne alisisitiza wajibu ulio wa uhai wa maombi, maombi ya kusihi bila kuchoka na yasiyokoma.
Katika shajara yake twaona haya: “Asubuhi nilijishughulisha na kuandaa kichwa, kisha moyo. Hili limekuwa kosa langu mara kwa mara, nami sikuzote nimehisi uovu wake, hasa katika maombi. Basi lirekebishe, Ee Bwana.” Alipokuwa katika safari yake ya Nchi Takatifu aliandika: “Kwa sehemu kubwa ya usalama wetu najiona kuwa mdeni wa maombi ya watu wangu. Kama pazia la mitambo ya ulimwengu lingeondolewa, tungeona ni mangapi yatendekayo kwa kujibu maombi ya watoto wa Mungu.” Katika hubiri alilolihubiri mhubiri mmoja alipowekwa wakfu, alimwambia mhubiri huyo: “Jitoe kwa maombi na kwa huduma ya Neno. Usipoomba, huenda Mungu atakuweka kando ya huduma yako, kama alivyonifanyia mimi, ili akufundishe kuomba. Kumbuka msemo wa Luther, “Kuomba vema ni kujifunza vema.” Pata maandiko yako kutoka kwa Mungu, na mawazo yako, na maneno yako. Wachukue majina ya kundi lako dogo kifuani mwako kama Kuhani Mkuu. Shindana kwa ajili ya wasioongoka. Luther alitumia saa zake bora tatu katika maombi; John Welch aliomba saa saba au nane kwa siku. Alikuwa akiweka shuka kitandani mwake ili ajifunike nayo alipoinuka usiku. Wakati mwingine mkewe alimkuta chini amelala akilia. Alipolalamika, angejibu, “Aa, mwanamke, ninazo nafsi za watu elfu tatu za kutoa hesabu yao, wala sijui hali ya wengi wao ilivyo.” Watu wake aliwaonya na kuwaagiza: “Mwombeeni mchungaji wenu. Ombeeni mwili wake, ili alindwe akiwa na nguvu na kuachwa hai miaka mingi. Ombeeni nafsi yake, ili alindwe akiwa mnyenyekevu na mtakatifu, taa iwakayo na kung’aa. Ombeeni huduma yake, ili ibarikiwe kwa wingi, ili apakwe mafuta kuhubiri habari njema. Pasiwe na maombi ya siri yasiyomtaja jina mbele za Mungu wenu, wala maombi ya jamaa yasiyomchukua mchungaji wenu mioyoni mwenu mpaka kwa Mungu.”
“Mambo mawili,” asema mwandishi wa historia yake, “yaonekana hakuacha kamwe kuyafanya—kukuza utakatifu wa nafsi yake mwenyewe, na juhudi za bidii kuu za kuwavuta watu kwa Kristo.” Mambo haya mawili ndiyo wenzi wasioweza kutenganishwa na huduma ya maombi. Maombi hushindwa pale shauku na juhudi ya utakatifu wa nafsi inaposhindwa. Hakuna mtu awezaye kuwavuta watu kwa Kristo asiye stadi katika huduma ya maombi. “Ni wajibu wa wahudumu,” asema mtu huyu mtakatifu, “kuanza matengenezo ya dini na mwenendo kwao wenyewe, kwa jamaa zao, na kadhalika, kwa kuungama dhambi za zamani, kwa maombi ya bidii ya kuongozwa, kwa neema, na kwa kusudi kamili la moyo.” Anaanza na nafsi yake mwenyewe chini ya kichwa “Matengenezo katika Maombi ya Siri,” naye aazimia hivi:
“Sipaswi kuacha sehemu yo yote ya maombi—kuungama, kuabudu, kushukuru, kuomba na kuombea wengine. Kuna mwelekeo wa kutisha wa kuacha kuungama, unaotokana na mawazo duni juu ya Mungu na sheria yake, mawazo mepesi juu ya moyo wangu, na juu ya dhambi ya maisha yangu ya zamani. Mwelekeo huu hauna budi kupingwa. Kuna mwelekeo wa daima wa kuacha kuabudu ninaposahau ni Nani ninayezungumza naye, ninapokimbilia bila kujali mbele za Yehova bila kufikiri juu ya jina lake la kutisha na tabia yake. Ninapokuwa na macho haba ya kuuona utukufu wake, na kustaajabia kidogo maajabu yake, ninao mwelekeo wa asili wa moyo wa kuacha kutoa shukrani, nayo imeamriwa hasa. Mara nyingi moyo unapokuwa umekufa kwa habari ya wokovu wa wengine, naacha kuwaombea, nayo ndiyo hasa roho ya yule Mwombezi Mkuu aliye na jina la Israeli moyoni mwake. Imenipasa kuomba kabla ya kuonana na mtu ye yote. Mara nyingi ninapolala muda mrefu, au kukutana na wengine mapema, kisha nikawa na maombi ya jamaa na chamshakinywa na wageni wa asubuhi, huwa ni saa tano au saa sita kabla sijaanza maombi ya siri. Huu ni utaratibu mbovu; haupatani na Maandiko. Kristo aliondoka kabla ya mapambazuko akaenda mahali pasipo na watu. Daudi asema, “Nitakutafuta mapema; asubuhi utaisikia sauti yangu.” Mariamu Magdalene alikuja kaburini kungali giza. Maombi ya jamaa hupoteza sehemu kubwa ya nguvu na utamu wake; wala siwezi kuwafaa lo lote wale wanaokuja kunitafuta. Dhamiri huhisi hatia, nafsi haijalishwa, taa haijatengenezwa. Nahisi ni afadhali sana kuanza na Mungu, kuuona uso wake kwanza, kuileta nafsi yangu karibu naye kabla haijawa karibu na mwingine. “Niamkapo nikali pamoja nawe.” Ikiwa nimelala muda mrefu mno, au ninakwenda safari ya mapema, au wakati wangu umepunguzwa kwa njia yo yote, ni afadhali kuvaa haraka na kupata dakika chache peke yangu pamoja na Mungu kuliko kuacha yote kana kwamba yamepotea. Lakini kwa kawaida ni bora kuwa na angalau saa moja peke yangu pamoja na Mungu kabla ya kujishughulisha na jambo lo lote jingine. Yanipasa kutumia saa zilizo bora kabisa za siku katika ushirika na Mungu. Niamkapo usiku, yanipasa kuinuka na kuomba kama Daudi na John Welch.”
McCheyne aliamini katika kuwa katika maombi sikuzote, na maisha yake yaliyozaa matunda, ingawa yalikuwa mafupi, ni kielelezo cha nguvu itokayo katika kutembelea mara nyingi na kwa muda mrefu mahali pa siri tunapokutana na Bwana wetu kama tulivyoagana.
Watu wa aina ya McCheyne wanahitajika leo—watu wa maombi, wanaojua jinsi ya kujitoa kwa kazi kuu kuliko zote inayodai wakati wao na uangalifu wao; watu wawezao kuutoa moyo wao wote kwa kazi takatifu ya maombezi, watu wawezao kuomba hata wapate jibu. Kazi ya Mungu imekabidhiwa kwa wanadamu; Mungu hujikabidhi kwa wanadamu. Watu wa maombi ndio wawakilishi wa Mungu; hufanya kazi yake na kutekeleza mipango yake.
Tumelazimika kuomba ikiwa sisi ni raia wa Ufalme wa Mungu. Kutokuomba ni kujiondoa uraia, au zaidi ya hayo, katika Ufalme wa Mungu. Ni kujiweka nje ya sheria, ni kosa kubwa, ni kuivunja katiba. Mkristo anayeyaweka maombi mahali pa chini maishani mwake upesi hupoteza bidii yo yote ya kiroho aliyokuwa nayo zamani; na Kanisa linalodharau maombi haliwezi kudumisha utauwa ulio hai, wala halina nguvu ya kuieneza Injili. Injili haiwezi kuishi, kupigana, wala kushinda bila maombi—maombi yasiyokoma, ya kudumu na ya moto.
Maombi haba ndiyo alama ya kizazi kilichorudi nyuma na ya Kanisa lililorudi nyuma. Kila mahali palipo na maombi haba mimbarini au viti vya waabudu, ufilisi wa kiroho uko karibu, wala hauepukiki.
Kazi ya Mungu haina kizazi cha biashara, wala kizazi cha ustaarabu, wala kizazi cha elimu, wala kizazi cha fedha. Lakini inacho kizazi kimoja cha dhahabu, nacho ni kizazi cha maombi. Viongozi wake wanapokuwa watu wa maombi, maombi yanapokuwa ndiyo sehemu itawalayo katika ibada, kama uvumba unaotoa harufu nzuri ya daima katika huduma yake, ndipo kazi ya Mungu itakaposhinda.
Maombi bora zaidi, na mengi zaidi—hilo ndilo tunalohitaji. Twahitaji wanaume watakatifu zaidi, na wengi zaidi; wanawake watakatifu zaidi, na wengi zaidi, wa kuomba—wanawake kama Hana, ambao kutokana na huzuni zao kubwa kuliko zote na majaribu yao walitengeneza maombi yao makuu kuliko yote. Kwa njia ya maombi Hana alipata faraja. Kila mahali Kanisa lilikuwa limerudi nyuma na kuasi, na adui zake walikuwa wakishinda. Hana alijitoa kwa maombi, na katika huzuni yake akaongeza kuomba kwake. Aliona uamsho mkuu ukizaliwa kutokana na kuomba kwake. Wakati taifa zima lilipokuwa limeonewa, nabii na kuhani pia, Samweli alizaliwa ili kuanzisha ukoo mpya wa ukuhani, na kuomba kwake Hana kukaamsha uzima mpya kwa ajili ya Mungu. Kila mahali dini ilifufuka na kustawi. Mungu, akiwa mwaminifu kwa ahadi yake, “Uniombe,” ingawa kuomba huko kulitoka katika moyo uliovunjika wa mwanamke, alisikia na kujibu, akipeleka siku mpya ya furaha takatifu ili kuwahuisha watu wake.
Basi, kwa mara nyingine tena, na tuweke mkazo na kurudia kwamba hitaji kuu la Kanisa katika kizazi hiki na katika vizazi vyote ni watu wenye imani yenye amri kuu namna hiyo, wenye utakatifu usio na doa namna hiyo, wenye nguvu za kiroho zilizo dhahiri namna hiyo na bidii iteketezayo, kwamba watafanya mapinduzi ya kiroho kwa maombi yao makuu. “Uwezo wa asili na faida za elimu si vipimo katika jambo hili; bali uwezo wa kuamini, uwezo wa kuomba, nguvu ya kujitoa wakfu kikamilifu, uwezo wa kujiona mdogo, kujipoteza kabisa katika utukufu wa Mungu, na shauku iliyopo daima na isiyoshibishwa ya kuutamani na kuutafuta utimilifu wote wa Mungu. Watu wawezao kuliwasha Kanisa moto kwa ajili ya Mungu, si kwa makelele wala kwa kujionyesha, bali kwa joto kali na tulivu liyeyushalo na kusogeza kila kitu kwa ajili ya Mungu.”
Na, kurudi kwenye jambo la msingi, kuomba kwa siri ndicho kipimo, ndicho kigezo, ndicho kinachohifadhi uhusiano wa mtu na Mungu. Chumba cha maombi, kikiwa ndicho kipimo cha unyofu wa kujitoa kwetu kwa Mungu, huwa pia ndicho kipimo cha kiasi cha kujitoa huko. Kujinyima, dhabihu tunazotoa kwa ajili ya vyumba vyetu vya maombi, jinsi tunavyopatembelea mara kwa mara mahali hapo patakatifu pa kukutana na Bwana, kukawia kukaa, kusita kuondoka—hizo ndizo thamani tunazoweka juu ya ushirika peke yetu pamoja na Mungu, gharama tunayolipa kwa ajili ya saa za miadi ya upendo wa mbinguni ambazo Roho ameziweka.
Chumba cha maombi huhifadhi uhusiano wetu na Mungu. Hushona kila pindo lililo wazi; hukunja juu kila vazi linalopepea na kunasa; hukifunga kila kiuno kilichozimia. Nanga kuu haishiki merikebu kwa uhakika na usalama zaidi kuliko chumba cha maombi kinavyotushikamanisha na Mungu. Shetani hana budi kwanza kuuvunja ushikaji wetu wa vyumba vya maombi na kuifunga njia yetu ya kuviendea, kabla hajaweza kuuvunja ushikaji wetu wa Mungu au kuifunga njia yetu ya kwenda mbinguni.
“Usiogope kuomba; kuomba ni haki;
Omba kwa tumaini ukiweza, lakini omba daima,
Ingawa tumaini ni dhaifu au limeugua kwa kukawia sana;
Omba gizani kama hakuna nuru;
Na ikiwa kuna tamaa yo yote usiyothubutu kuiombea,
Basi mwombe Mungu aitupilie mbali tamaa hiyo.”