Sura 6 · dakika 10 za kusoma · dakika 13 za kusikiliza
Omba Wala Usikate Tamaa
“Hakuna lisilowezekana kwa bidii ya kazi, “alisema mmoja wa wale wenye hekima saba wa Ugiriki. Na tubadilishe neno bidii ya kazi kuwa maombi ya kudumu, nao msemo huo utakuwa wa Kikristo zaidi na unaostahili zaidi kukubaliwa na wote. Nimesadiki kwamba sote tumepungukiwa na roho ya maombi kuliko neema nyingine yo yote. Mungu hupenda maombi ya kusihi bila kuchoka kiasi kwamba hatatupa baraka nyingi bila hayo. Na sababu ya kuyapenda maombi hayo ni kwamba anatupenda na anajua kwamba ni maandalizi ya lazima ili tupokee baraka tele kuliko zote ambazo anangoja na kutamani kutupa.
Sijawahi kuomba kwa unyofu na kwa bidii kwa ajili ya jambo lo lote bila kulipata wakati fulani—haidhuru ni siku ya mbali kiasi gani, kwa njia fulani, kwa sura fulani, pengine ile ambayo ningeibuni mwisho kabisa, lilikuja.—Adoniram Judson
Naona ni vema kudumu katika juhudi za kuomba. Hata kama siwezi kuomba kwa kudumu au kuendelea muda mrefu katika kumwomba Mungu, nimeona kwamba kadiri ninavyofanya mengi katika maombi ya siri ndivyo ninavyozidi kufurahia kuyafanya, na nimefurahia zaidi roho ya maombi; na mara nyingi nimeona kinyume chake, nilipokosa faragha kwa sababu ya safari au vinginevyo.—David Brainerd
Kristo anaweka kusihi kwa kudumu kuwa alama ya kutambulisha ya kuomba kwa kweli. Hatupaswi tu kuomba, bali hatuna budi kuomba kwa haraka kubwa, kwa nia moja na kwa kurudia-rudia. Hatupaswi tu kuomba, bali hatuna budi kuomba tena na tena. Hatupaswi kuchoka kuomba. Hatuna budi kuwa na bidii kabisa, tukijali sana mambo tunayoyaomba, kwa maana Yesu Kristo alionyesha wazi kabisa kwamba siri ya maombi na ya kufanikiwa kwake imo katika bidii yake ya kusisitiza. Hatuna budi kumsisitizia Mungu maombi yetu.
Katika mfano wenye huruma na urahisi wa ajabu, Bwana wetu alifundisha si tu kwamba imewapasa watu kuomba, bali kwamba imewapasa kuomba kwa moyo wote, na kulisisitiza jambo kwa nguvu tele na mioyo shujaa.
“Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kuomba sikuzote, wala wasikate tamaa; akisema, Palikuwa na kadhi katika mji mmoja, asiyemcha Mungu wala hajali watu: na katika mji ule palikuwa na mjane mmoja; akamwendea mara kwa mara, akisema, Nipatie haki na adui wangu. Naye kwa muda alikataa: lakini baadaye alisema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu, wala sijali watu; lakini kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. Na Mungu, je! hatawapatia haki wateule wake, wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi. Walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! ataiona imani duniani?”
Hali ya mwanamke huyu maskini ilikuwa ya kukatisha tamaa kabisa, lakini kusihi kwa kudumu huleta tumaini kutoka katika ulimwengu wa kukata tamaa na huzaa mafanikio pale ambapo hapakuwa na mafanikio wala mazingira yake. Hakungeweza kuwa na kisa chenye nguvu zaidi cha kuonyesha jinsi kusihi kusikochoka wala kuogopa kunavyofikia lengo lake pale ambapo kila kitu kingine hushindwa. Utangulizi wa mfano huu wasema: “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kuomba sikuzote, wala wasikate tamaa.” Alijua kwamba watu wangekata tamaa upesi katika kuomba, kwa hiyo ili kututia moyo anatupa picha hii ya uwezo wa ajabu wa kusihi kwa kudumu.
Mjane, dhaifu na asiye na msaada, ndiye kutokuwa na msaada kwenyewe katika umbo la mtu; akiwa amenyang’anywa kila tumaini na kila mvuto uwezao kumsukuma kadhi dhalimu, hata hivyo ashinda shauri lake kwa kusihi kwake kusikochoka na kwa kuudhi peke yake. Je, ulazima wa kusihi kwa kudumu, uwezo wake na umuhimu wake mkubwa katika maombi, ungeweza kuchorwa kwa rangi nzito zaidi au za kugusa zaidi? Huvuka au huondoa vizuizi vyote, hushinda kila nguvu ipingayo na hufikia lengo lake mbele ya vizuizi visivyoshindika. Hatuwezi kufanya kitu bila maombi. Mambo yote yaweza kufanywa kwa maombi ya kusihi bila kuchoka.
Hilo ndilo fundisho la Yesu Kristo.
Mfano mwingine aliotoa Yesu wasisitiza kweli ile ile kuu. Mtu mmoja usiku wa manane amwendea rafiki yake ili amkopeshe mikate. Hoja zake zina nguvu, zikiwa zimejengwa juu ya urafiki na juu ya madai ya kuaibisha na ya kubana ya uhitaji, lakini hizi zote zashindwa. Hapati mikate, lakini anakaa na kusisitiza, na kungoja na kupata. Kusihi kwa kudumu peke yake kunafanikiwa pale ambapo hoja na mivuto mingine yote ilikuwa imeshindwa.
Kisa cha mwanamke Msirofoinike ni mfano ulio katika matendo. Azuiliwa anapomkaribia Kristo kwa habari kwamba hataki kumwona mtu ye yote. Anyimwa kuingia mbele zake, kisha mbele zake anatendewa kwa kutojali kunakoonekana, kwa baridi ya ukimya na ya kutoshughulika: anasisitiza na kukaribia, nako kusisitiza na kukaribia kwake kwarudishwa nyuma kwa tamko kali na la kuponda kwamba hakutumwa kwa jamaa yake wala kabila lake, kwamba yeye ametengwa na kazi yake na uweza wake. Anadhalilishwa kwa kuitwa mbwa. Hata hivyo anakubali yote, anashinda yote, anapata yote kwa kusihi kwake kwa unyenyekevu, bila hofu, kusikoshindika. Mwana wa Mungu, akiwa amependezwa, ameshangaa, ameshindwa na kusihi kwake kusikoshindika, amwambia: “Mama, imani yako ni kubwa; na ufanyiwe kama utakavyo.” Yesu Kristo anajitoa mwenyewe kwa kusihi kwa kudumu kwa imani kubwa. “Na Mungu, je! hatawapatia haki wateule wake, wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?”
Yesu Kristo anaweka uwezo wa kusihi kwa kudumu kuwa mojawapo ya viungo vya maombi, mojawapo ya masharti makuu ya maombi. Maombi ya mwanamke Msirofoinike ni udhihirisho wa uwezo usio na kifani wa kusihi kwa kudumu, wa mapambano yaliyo halisi zaidi na yanayohusisha nguvu za uhai zaidi, ustahimilivu, na sifa zote za juu, kuliko yalivyowahi kuonyeshwa katika mashindano ya Isthmia au Olimpia.
Mafundisho ya kwanza ya kusihi kwa kudumu yanafundishwa katika Mahubiri ya Mlimani—“Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa.” Hizi ni hatua za kusonga mbele—“Kwa maana kila aombaye hupokea, naye atafutaye huona, naye abishaye atafunguliwa.”
Bila kudumu maombi yaweza kukosa jibu. Kusihi kwa kudumu kunajengwa na uwezo wa kushikilia, kusonga mbele, kungoja kwa mshiko usiolegea na usioweza kulegea, kwa shauku isiyotulia na saburi yenye utulivu. Maombi ya kusihi kwa kudumu si tukio la nasibu, bali ni jambo kuu; si onyesho bali ni shauku inayowaka; si hitaji tu bali ni lazima.
Maombi katika hali yake ya juu kabisa na mafanikio yake makuu huchukua mkao wa mtu ashindanaye mweleka na Mungu. Ni mashindano, jaribu na ushindi wa imani; ushindi usiopatikana kutoka kwa adui, bali kutoka kwake yeye aijaribuye imani yetu ili aiongeze: aipimaye nguvu yetu ili atufanye wenye nguvu zaidi. Ni mambo machache yanayoipa nafsi nguvu ya kuhuishwa na ya kudumu kama kipindi kirefu cha kuchosha cha maombi ya kusihi. Hufanya uzoefu, enzi, kalenda mpya kwa roho, uzima mpya kwa dini, mafunzo ya kiaskari. Biblia haichoki kamwe kusisitiza na kuonyesha kwa mifano ukweli kwamba mema ya juu kabisa ya kiroho hupatikana kama malipo ya kumiminwa kwa juhudi ya kiroho iliyo ya juu kabisa. Hakuna kitia moyo wala nafasi katika dini ya Biblia kwa shauku dhaifu, juhudi zisizo na moyo, mikao ya uvivu; yote hayana budi kuwa ya nguvu, ya haraka, ya bidii. Shauku zinazowaka, kusisitiza kwa moto bila kuchoka, huifurahisha mbingu. Mungu angetaka watoto wake wawe na bidii isiyorekebishika na ujasiri wa kudumu katika juhudi zao. Mbingu ina shughuli nyingi mno kuweza kusikiliza maombi ya nusu moyo au kuitikia ziara za kupita tu.
Nafsi yetu yote haina budi kuwa katika kuomba kwetu; kama John Knox, hatuna budi kusema na kuhisi, “Nipe Uskoti, la sivyo nife.” Uzoefu wetu na mafunuo yetu ya Mungu huzaliwa na dhabihu zetu za gharama, mapambano yetu ya gharama, kuomba kwetu kwa gharama. Mweleka, kuomba usiku kucha, kwa Yakobo kulifanya enzi isiyosahaulika kamwe katika maisha ya Yakobo, kulimleta Mungu kumwokoa, kulibadilisha mtazamo na mwenendo wa Esau, kulibadilisha tabia ya Yakobo, kuliokoa na kuyagusa maisha yake na kuingia katika mazoea ya taifa zima.
Vipindi vyetu vya maombi ya kusihi hujichora, kama alama ya almasi, katika sehemu zetu ngumu zaidi, na huziwekea tabia zetu alama zisizofutika. Hivyo ndivyo vipindi vikuu vya maisha yetu! Mawe ya ukumbusho yanayodumu na ambayo tunayarudia.
Kusihi kwa kudumu, na turudie, ni sharti la maombi. Tunapaswa kulisisitiza jambo, si kwa marudio matupu, bali kwa marudio ya bidii. Tunarudia, si ili tuhesabu mara, bali ili tupate ombi. Hatuwezi kuacha kuomba kwa sababu moyo na nafsi vimo ndani yake. Tunaomba “mkikesha kwa jambo hilo na kudumu.” Tunayashikilia maombi yetu kwa sababu kwayo tunaishi. Tunasisitiza hoja zetu kwa sababu ni lazima tupate majibu au tufe. Kristo anatupa mifano miwili yenye maana sana ili kusisitiza ulazima wa kusihi kwa kudumu katika kuomba. Pengine Ibrahimu aliipoteza Sodoma kwa kushindwa kulisisitiza hadi mwisho pendeleo lake la kuomba. Yoashi, twajua, alipoteza kwa sababu aliacha kupiga.
Kudumu kuna uzito mkubwa kwa Mungu kama kwa mwanadamu. Kama Eliya angeacha baada ya ombi lake la kwanza, mbingu zisingalitoa mvua yake kwa maombi yake dhaifu. Kama Yakobo angeacha kuomba saa ya kawaida ya kulala, asingeweza kunusurika katika kukutana na Esau siku iliyofuata. Kama mwanamke Msirofoinike angeiacha imani yake ikate tamaa kwa ukimya, kudhalilishwa, kukataliwa, au angesimamisha katikati mapambano yake, nyumba yake iliyojaa huzuni isingalitiwa nuru kamwe kwa kuponywa kwa binti yake.
Omba wala usikate tamaa, ndio msemo Kristo anaotupa kwa ajili ya kuomba. Ndio kipimo cha imani yetu, na kadiri jaribu lilivyo kali zaidi na kungoja kulivyo kurefu zaidi, ndivyo matokeo yalivyo matukufu zaidi.
Faida na ulazima wa kusihi kwa kudumu vinafundishwa na watakatifu wa Agano la Kale. Watu waombao hawana budi kuwa hodari katika tumaini, na imani, na maombi. Hawana budi kujua jinsi ya kungoja na kusisitiza, kumngoja Mungu na kuwa na bidii katika kumkaribia kwetu.
Ibrahimu ametuachia mfano wa maombezi ya kusihi katika kumsihi Mungu kwake kwa moyo wa moto kwa ajili ya Sodoma na Gomora, na kama, kama ilivyokwisha kudokezwa, asingeacha kuomba, pengine Mungu asingeacha kutoa.
“Ibrahimu aliacha kuomba kabla Mungu hajaacha kutoa.” Musa alifundisha uwezo wa kusihi kwa kudumu alipowaombea Israeli siku arobaini mchana na usiku, kwa kufunga na kuomba. Naye alifaulu katika kusihi kwake.
Yesu, katika mafundisho yake na mfano wake, aliionyesha na kuikamilisha kanuni hii ya Agano la Kale ya kusihi na kungoja. Ni ajabu kama nini kwamba Mwana pekee wa Mungu, aliyekuja kwa kazi aliyotumwa moja kwa moja na Baba yake, ambaye mbingu yake pekee duniani, ambaye uzima wake pekee na sheria yake pekee vilikuwa kufanya mapenzi ya Baba yake katika kazi hiyo—ni siri iliyoje kwamba yeye awe chini ya sheria ya maombi, kwamba baraka zilizomjia zilizaliwa na kununuliwa kwa maombi; na la ajabu zaidi kwamba kusihi kwa kudumu katika maombi ndiyo njia ambayo kwayo alipata kwa Mungu mahitaji yake tele kuliko yote. Kama asingeomba kwa kusihi, kugeuka sura kusingalikuwamo katika historia yake, wala matendo makuu yasingaliifanya huduma yake kuwa ya Kimungu. Kuomba kwake usiku kucha ndiko kulikoijaza kazi yake ya mchana kutwa huruma na nguvu. Kuomba kwa kusihi katika maisha yake kuliivika kifo chake taji la ushindi wake. Alijifunza somo kuu la kujisalimisha kwa mapenzi ya Mungu katika mapambano ya maombi ya kusihi kabla hajaonyesha kujisalimisha huko kwa utukufu mkuu hivyo msalabani.
“Tupende tusipende,” alisema Bw. Spurgeon, “kuomba ndiyo kanuni ya Ufalme.” “Ombeni, nanyi mtapata.” Ni kanuni ambayo haitabadilishwa kamwe kwa mtu ye yote. Bwana wetu Yesu Kristo ndiye Ndugu mkubwa wa jamaa, lakini Mungu hakumlegezea kanuni hiyo. Kumbukeni andiko hili: Yehova amwambia Mwanawe mwenyewe, “Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako, na miisho ya dunia kuwa milki yako.” Ikiwa Mwana wa Mungu aliye wa kifalme na wa Kimungu hawezi kusamehewa kanuni ya kuomba ili apate, mimi na wewe hatuwezi kutazamia kanuni hiyo ilegezwe kwa faida yetu. Kwa nini iwe hivyo? Ni sababu gani iwezayo kutolewa ya kwamba tusamehewe maombi? Ni hoja gani iwezayo kuwapo ya kwamba tunyimwe pendeleo hili na kuokolewa na ulazima wa kusihi? Mimi sioni hata moja: je, wewe waona? Mungu atambariki Eliya na kunyesha mvua juu ya Israeli, lakini Eliya sharti aiombee. Kama taifa lililochaguliwa litafanikiwa, Samweli sharti aliombee. Kama Wayahudi watakombolewa, Danieli sharti aombe maombezi. Mungu atambariki Paulo, na mataifa yataongolewa kwa kupitia yeye, lakini Paulo sharti aombe. Naye aliomba bila kukoma; nyaraka zake huonyesha ya kwamba hakutazamia kitu cho chote ila kwa kukiomba. Kama mwaweza kuwa na kila kitu kwa kuomba na hakuna kitu pasipo kuomba, nawasihi mwone jinsi maombi yalivyo ya lazima kabisa, nami nawasihi mzidi ndani yake.”
Hakuna shaka hata kidogo kwamba maombi yetu mengi hushindwa kwa kukosa ushikilivu. Hayana moto na nguvu ya kudumu. Ushikilivu ni kiini cha kuomba kwa kweli. Huenda usihitajike kutumika sikuzote, lakini hauna budi kuwapo kama nguvu ya akiba. Yesu alifundisha kwamba kudumu ndicho kiungo cha lazima cha maombi. Watu hawana budi kuwa na bidii wapigapo magoti mbele ya kiti cha miguu cha Mungu.
Mara nyingi mno tunakata tamaa na kuacha kuomba mahali ambapo tulipaswa kuanza. Tunaachilia mahali pale pale ambapo tulipaswa kushikilia kwa nguvu kuliko pote. Maombi yetu ni dhaifu kwa sababu hayajatiwa moto na nia isiyolegea na isiyozuilika.
Mungu humpenda yule asihiye bila kuchoka, na humtumia majibu ambayo yasingetolewa kamwe kama si kwa ule ushikilivu unaokataa kuachilia hata ombi lililotamaniwa litolewe.