Sura 2 · dakika 9 za kusoma · dakika 11 za kusikiliza
Maombi Hubadilisha Kusudi la Mungu
Kwamba yatupasa kujitoa kwa Mungu katika mambo ya muda na ya kiroho pia, na kutafuta kuridhika kwetu katika kuyatimiza mapenzi yake tu, kwamba atuongoze kwa mateso au kwa faraja, kwa maana yote yangekuwa sawa kwa Nafsi iliyojisalimisha kweli. Maombi si kitu kingine ila kuhisi kuwapo kwa Mungu.—Ndugu Lawrence
Hakikisha unaitunza ibada yako ya siri; idumishe hiyo lo lote ufanyalo. Nafsi haiwezi kufanikiwa ikiipuuza. Kuasi imani kwa kawaida huanzia mlangoni pa chumba cha siri. Kaa sana katika ushirika wa siri na Mungu. Ni biashara ya siri inayomtajirisha Mkristo.
Omba peke yako. Maombi na yawe ufunguo wa asubuhi na komeo la usiku. Njia bora ya kupigana na dhambi ni kupigana nayo tukiwa magotini.—Philip Henry
Maombi ya imani ndiyo nguvu pekee ulimwenguni ambayo Yehova Mkuu huikubali. Maombi ndiyo dawa kuu.—Robert Hall
Saa moja ya upweke iliyotumiwa katika maombi ya dhati na ya bidii, au kupambana na kushinda tamaa moja tu au dhambi moja ya siri iliyojificha moyoni, itatufundisha zaidi juu ya kufikiri, itaamsha kwa ufanisi zaidi uwezo wa kutafakari na kujenga zoea lake, kuliko mwaka mzima wa kusoma vyuoni bila hayo.—Coleridge
Mtu aweza kuomba usiku na mchana na kujidanganya mwenyewe, lakini hakuna mtu asiyeomba awezaye kuwa na hakika ya unyofu wake. Maombi ni imani ikigeuka kuwa tendo. Ni muungano wa nia na akili ukitimizwa katika tendo la akili. Ni mtu mzima wote anayeomba. Kilicho pungufu ya hapo ni kutamani tu au kazi ya midomo, ni udanganyifu au mchezo wa kuigiza.
Mungu akinirudishia afya tena nimeazimia kutojifunza kitu kingine ila Biblia. Elimu ya vitabu ni adui wa hali ya kiroho isipotiishwa kwa mkono imara.—Richard Cecil
Utakaso wetu hautegemei kubadilisha kazi zetu, bali kufanya kwa ajili ya Mungu yale tuyafanyayo kwa kawaida kwa ajili yetu wenyewe. Kwangu wakati wa shughuli hautofautiani na wakati wa maombi. Maombi si kitu kingine ila kuhisi kuwapo kwa Mungu.—Ndugu Lawrence
Na niteketee kwa ajili ya Mungu. Hata hivyo, lo lote Mungu atakaloamuru, maombi ndilo jambo kuu. Laiti ningekuwa mtu wa maombi.—Henry Martyn
Uwezekano na ulazima wa maombi, nguvu zake na matokeo yake, hudhihirishwa katika kuyazuia na kuyabadilisha makusudi ya Mungu na katika kuliondoa pigo la uweza wake. Abimeleki alipigwa na Mungu:
Basi Ibrahimu akamwomba Mungu; naye Mungu akamponya Abimeleki, na mkewe, na wajakazi wake; nao wakazaa watoto.
Kwa kuwa Bwana alikuwa ameyafunga kabisa matumbo yote ya nyumba ya Abimeleki, kwa ajili ya Sara, mkewe Ibrahimu.
Wafariji wa Ayubu, wanyonge na waliokosea, walikuwa wamejiendesha hivyo katika mabishano yao na Ayubu hata hasira ya Mungu ikawaka juu yao. “Mtumishi wangu Ayubu atawaombeeni,” Mungu alisema, “kwa maana yeye nitamkubali.”
“Bwana akaugeuza uteka wa Ayubu, alipowaombea rafiki zake.”
Yona alikuwa katika hali mbaya kabisa “Bwana alipovumisha upepo mkuu baharini, kukawa na tufani kuu.” Kura zilipopigwa, “kura ikamwangukia Yona.” Alitupwa baharini, lakini “Bwana alikuwa ameweka tayari samaki mkubwa ammeze Yona ... Ndipo Yona akamwomba Bwana, Mungu wake, akiwa ndani ya tumbo la samaki ... na Bwana akasema na yule samaki, naye akamtapika Yona pwani.”
Nabii yule asiyetii alipopaza sauti yake katika maombi, Mungu alisikia na kumletea wokovu.
Farao aliamini kabisa uwezekano wa maombi, na uwezo wake wa kuleta nafuu. Alipokuwa akiyumbayumba chini ya laana za kutisha za Mungu, alimsihi Musa amwombee. “Niombeeni kwa Bwana,” ndiyo iliyokuwa dua yake ya kusikitisha, iliyorudiwa mara nne mapigo yalipokuwa yakiipiga Misri. Mara nne Musa aliombwa hivyo kwa haraka, na mara nne maombi yaliiondoa laana ile ya kutisha juu ya mfalme yule mgumu na nchi yake iliyohukumiwa.
Kufuru na ibada ya sanamu ya Israeli, walipomfanya ndama wa dhahabu na kutangaza ibada yao kwake, lilikuwa kosa la kutisha. Hasira ya Mungu iliwaka, naye akatangaza kwamba angewaangamiza watu wale waliokosa. Bwana alimkasirikia Haruni pia sana, naye akamwambia Musa, “Niache, ili nipate kuwaangamiza—Lakini Musa aliomba, akaendelea kuomba; mchana na usiku aliomba siku arobaini. Yeye mwenyewe anaandika habari ya mapambano yake ya maombi. “Nikaanguka,” asema, “mbele za Bwana siku arobaini za kwanza mchana na usiku; sikula mkate wala sikunywa maji, kwa sababu ya dhambi zenu mlizozifanya, kwa kufanya yaliyo maovu mbele za Bwana, kwa kumkasirisha. Kwa kuwa naliogopa hasira na ukali wa ghadhabu ambayo Bwana aliwakasirikia, hata kutaka kuwaangamiza. Lakini Bwana akanisikiza wakati huo nao. Bwana akamkasirikia Haruni sana hata kutaka kumwangamiza. Nikamwombea Haruni naye wakati ule ule.”
“Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. Lilikuwa kusudi la Mungu kuuangamiza mji ule mkubwa na mwovu. Lakini Ninawi uliomba, ukiwa umevikwa magunia; ukiketi katika majivu ulimlilia “Mungu kwa nguvu,” na “Mungu akaghairi ule ubaya aliosema ya kwamba atawatenda; wala hakuutenda.”
Ujumbe wa Mungu kwa Hezekia ulikuwa huu: “Tengeneza mambo ya nyumba yako; kwa maana utakufa, wala hutapona.” Hezekia akageuza uso wake kuelekea ukuta, akamwomba Bwana, akasema: “Ee Bwana, nakusihi, kumbuka sasa jinsi nilivyokwenda mbele zako kwa kweli, na kwa moyo mkamilifu, nami nimefanya yaliyo mema machoni pako.” Hezekia akalia sana. Mungu akamwambia Isaya, “Enenda ukamwambie Hezekia, Nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaongeza siku zako miaka kumi na mitano.”
Watu hawa walijua jinsi ya kuomba na jinsi ya kushinda katika maombi. Imani yao katika maombi haikuwa mwelekeo wa kupita tu, uliobadilika pamoja na upepo au pamoja na hisia na hali zao wenyewe; ilikuwa kweli kwamba Mungu alisikia na kujibu, kwamba sikio lake lilikuwa wazi daima kwa kilio cha watoto wake, na kwamba uwezo wake wa kufanya aliloombwa ulilingana na nia yake ya kulifanya. Na hivyo watu hawa, hodari katika imani na katika maombi, “walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga, walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni.”
Basi kila kitu, zamani kama sasa, kiliwezekana kwa wanaume na wanawake waliojua jinsi ya kuomba. Kwa kweli maombi yalifungua ghala lisilo na mpaka, na mkono wa Mungu haukuzuia kitu. Maombi yaliwaingiza wale walioyazoea katika ulimwengu wa fursa, na kuzileta nguvu na utajiri wa mbinguni chini kumsaidia mwanadamu mwenye mipaka. Ilikuwa nguvu tajiri na ya ajabu kama nini kwa wale waliojifunza siri ya kumkaribia Mungu kwa ushindi! Kwa Musa maombi yaliliokoa taifa; kwa Ezra yaliliokoa kanisa.
Na bado, ingawa ni ajabu tunapoyatafakari maajabu ambayo watu wa Mungu walikuwa wameyashuhudia, ulegevu katika maombi ulikuja. Ushiko ule wenye nguvu juu ya Mungu, ambao mara nyingi ulikuwa umetia hofu na kitisho mioyoni mwa adui zao, ulilegea. Watu, wakiwa wamerudi nyuma na kuasi, walikuwa wameacha kuomba—ikiwa wengi wao waliwahi kuomba kweli kweli. Maombi baridi na yasiyo na uhai ya Mfarisayo yalichukua mahali pa kila namna ya kumkaribia Mungu kwa kweli, na kwa sababu ya njia ile ya maombi ya desturi tu ibada yote ikawa kichekesho cha kusudi lake halisi. Ulikuwa mpango mtukufu, ulioendeshwa kwa utukufu na Musa, na Ezra, na Danieli na Eliya, na Hana na Samweli; lakini duara hilo laonekana kuwa dogo na la muda mfupi; waombaji walikuwa wachache, tena nadra. Hawakuwa na waliowafuata, hakuna wa kuiga ujitoaji wao kwa Mungu, hakuna wa kuihifadhi orodha ya wateule.
Bure amri ilikuwa imeuweka utaratibu wa Kimungu, wito wa Kimungu. Uniombe. Kutoka katika kumlilia Mungu kwa bidii na kwa matunda waligeuza nyuso zao kwa miungu ya kipagani, wakalia bure wakingoja majibu yasiyoweza kuja kamwe. Na hivyo walizama katika hali ile ya kukosa uchaji na ya kusikitisha ambayo imepoteza lengo la maisha kiungo na Yeye wa Milele kinapokatika. Mpango wao wa maombi uliobarikiwa ulisahauliwa; hawakujua jinsi ya kuomba.
Ni tofauti kubwa kama nini na mafanikio yanayozing’arisha kurasa nyingine za Maandiko matakatifu. Nguvu iliyotenda kazi kupitia Eliya na Elisha kwa kujibu maombi ilifika hata kaburini. Katika kila kisa mtoto alifufuliwa kutoka kwa wafu, na nguvu za njaa zilivunjwa. “Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana.” Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi. Aliomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake. Yona aliomba akiwa amefungwa ndani ya yule samaki mkubwa, naye akafika nchi kavu, akiwa ameokolewa na dhoruba na bahari na wanyama wa vilindini kwa nguvu kuu ya maombi yake.
Ni pana kama nini riziki ya neema ya kuomba kama ilivyotolewa katika mpango ule wa ajabu. Waliomba kwa namna ya ajabu. Kwa nini maombi yao hayakuweza kuuokoa mpango ule na kuoza na kufa? Je! haikuwa kwa sababu waliupoteza moto ambao bila huo maombi yote huharibika na kuwa desturi isiyo na uhai? Huhitaji juhudi na taabu na uangalifu kuutayarisha uvumba. Maombi si kazi ya mvivu. Neema zote tajiri zenye manukato za mwili wa maombi zikiisha kuchanganywa, kusafishwa na kuunganishwa kwa kazi na kwa kutwangwa, moto huhitajika ili kuufungua uvumba na kuifanya harufu yake nzuri ipande hadi kiti cha enzi cha Mungu. Moto ule uteketezao ndio huumba roho na uhai wa uvumba. Bila moto maombi hayana roho; ni kama manukato yaliyokufa, ya kuoza na ya funza.
Maombi ya hapa na pale, ya kukatika-katika, kamwe hayaogeshwi katika moto huu wa Kimungu. Kwa maana mtu aombaye hivyo amepungukiwa na ile bidii inayomshika Mungu, ikiazimia kutomwachilia mpaka baraka ije. “Ombeni bila kukoma,” alishauri Mtume mkuu. Hilo ndilo zoea linalosukuma maombi hadi ndani ya chokaa inayoshikanisha mawe ya jengo. “Waweza kufanya zaidi ya kuomba baada ya kuomba,” alisema Dk. A. J. Gordon, mtu wa Mungu, “lakini huwezi kufanya zaidi ya kuomba mpaka umeomba.” Habari ya kila tendo kuu la Kikristo ni historia ya maombi yaliyojibiwa.
“Kipawa kikuu na bora kuliko vyote ambacho Mungu humpa mwanamume ye yote au mwanamke ulimwenguni humu ni kipawa cha maombi,” aandika Mkuu wa Chuo Alexander Whyte. “Na riba bora kuliko zote ambayo mwanamume au mwanamke ye yote humrudishia Mungu ajapo kufanya hesabu nao mwisho wa ulimwengu huu ni maisha ya maombi. Na watumishi wale huiweka fedha ya Bwana wao “kwa watoaji” kwa njia bora kuliko wote, ambao huamka mapema na kukaa hadi usiku, muda wote walipo katika ulimwengu huu, wakizitafuta daima na kuzifuata daima njia bora na bora zaidi za maombi, na wakijenga daima mazoea ya maombi yaliyo ya siri zaidi, imara zaidi, na yenye matunda zaidi ya kiroho, mpaka kwa kweli “wanaomba bila kukoma,” na mpaka wanaanzisha daima shughuli mpya katika maombi, na mafanikio mapya, na utajiri mpya.”
Martin Luther, alipoulizwa mara moja mipango yake ya siku iliyofuata ilikuwa nini, alijibu: “Kazi, kazi, tangu asubuhi na mapema mpaka usiku. Kwa kweli nina mengi mno ya kufanya hata nitatumia saa tatu za kwanza katika maombi.” Cromwell pia aliamini katika kukaa sana magotini. Siku moja alipokuwa akitazama sanamu za watu mashuhuri, alimgeukia rafiki yake akasema: “Yangu iwe ya kupiga magoti, kwa maana hivyo ndivyo nilivyoufikia utukufu.”
Ni pale tu moyo wote unaposhikwa na shauku ya maombi ndipo moto utoao uzima hushuka, kwa maana hakuna ila mtu mwenye bidii apataye kulifikia sikio la Mungu.