Maombi na Watu Walioomba
Hezekia, Mfalme Aliyeomba

Sura 7 · dakika 12 za kusoma · dakika 15 za kusikiliza

Hezekia, Mfalme Aliyeomba

Mtu anaweza kujijengea mazoea ya kujifunza hata nia ikaonekana kuwa imepumzika na akili peke yake ndiyo inayofanya kazi, nia ikiwa imejitoa kabisa katika juhudi. Hivyo sivyo yalivyo maombi ya kweli. Ikiwa hisia za moyo ni goigoi, baridi na zisizojali, ikiwa akili haitoi chochote cha kulivika ombi picha na bidii, basi ombi hilo ni mvuke tu wa zoezi la akili, wala hakuna jambo lolote la maana linalotimizwa.—Mchungaji Homer W. Hodge

Matengenezo makuu ya kidini chini ya Mfalme Hezekia na nabii Isaya yalijaa maombi kabisa katika hatua zake zote. Mfalme Hezekia wa Yuda atatufaa kama kielelezo cha mzee wa Kanisa la Mungu aliyeomba, aliyevikwa mavazi meupe na taji ya dhahabu. Alikuwa na kipaji na nguvu, hekima na utauwa. Alikuwa mwanasiasa, jemadari, mshairi na mtengenezaji wa dini. Yeye ni jambo la kutushangaza kweli, si sana kwa sababu ya nguvu zake na kipaji chake—hivyo vilitarajiwa—bali kwa utauwa wake, tukizingatia hali zote zilizomhusu. Maneno yale adimu, “Akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana,” ni mshangao wenye furaha na wa kusisimua tunapofikiri juu ya asili yake yote na mazingira yake. Alitoka wapi? Utoto wake aliupitisha katika hali gani? Wazazi wake walikuwa nani, na tabia yao ya kidini ilikuwa ya namna gani? Kupenda dunia, moyo wa nusu nusu na uasi kamili viliutia alama utawala wa baba yake, wa babu yake na wa babu wa babu yake. Mazingira ya nyumbani mwake alipokuwa akikua yalikuwa mbali sana na kuufaa utauwa na imani katika Mungu. Hata hivyo, jambo moja lilimfaa. Alibahatika kuwa na Isaya kama rafiki na mshauri wake alipotwaa taji ya Yuda. Ni faida iliyoje kwa mtawala kuwa na mtu amchaye Mungu kama mshauri na mwenzi wake!

Jinsi alivyomwombea Mungu kwa maombi ya kawaida kwake na yenye kufanikiwa kunaonekana katika sikukuu ya Pasaka, ambayo idadi fulani ya watu hawakustahili kushiriki. Walikuwa hawajajiandaa kwa utakaso wa kiibada uliotakiwa, na ilikuwa muhimu waruhusiwe kula sikukuu ya Pasaka pamoja na wengine wote.

Hii hapa habari fupi, hasa kuhusu maombi ya Hezekia na matokeo yake:

“Kwa maana walikuwako wengi katika kusanyiko ambao hawakuwa wamejitakasa; kwa hiyo Walawi walikuwa na kazi ya kuchinja pasaka kwa ajili ya kila mtu asiyekuwa safi, ili kuwatakasa kwa BWANA.

“Kwa maana wengi wa watu walikuwa hawajajisafisha, lakini wakala pasaka vinginevyo kuliko ilivyoandikwa. Lakini Hezekia akawaombea, akisema, Bwana mwema amsamehe kila mtu

“aelekezaye moyo wake kumtafuta Mungu, Bwana, Mungu wa baba zake, ingawa hakutakaswa kwa kadiri ya utakaso wa patakatifu.

“BWANA akamsikia Hezekia, akawaponya watu.”

Basi Bwana alimsikia alipoomba, na hata kuvunjwa kwa sheria takatifu kuliko zote ya Pasaka kulisamehewa kwa kujibu maombi ya mfalme huyu aliyeomba na kumcha Mungu. Sheria lazima iisalimishe fimbo yake ya enzi kwa maombi.

Nguvu, unyoofu na msingi wa imani yake na maombi yake vinaonekana katika maneno yake kwa jeshi lake. Ni maneno ya kukumbukwa, yenye nguvu na uweza kuliko majeshi yote ya Senakeribu:

“Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msifadhaike kwa sababu ya mfalme wa Ashuru, wala kwa sababu ya jeshi lote lililo pamoja naye; kwa maana yu mkuu zaidi aliye pamoja nasi kuliko aliye pamoja naye.

“Pamoja naye u mkono wa mwili; bali pamoja nasi yu Bwana, Mungu wetu, atusaidie, na kupigana vita vyetu. Watu wakajituliza juu ya maneno ya Hezekia, mfalme wa Yuda.”

Ngome yake dhidi ya adui wakuu wa Mungu ilikuwa maombi. Adui zake walitetemeka na kuangamizwa kwa maombi yake wakati majeshi yake mwenyewe yalipokuwa hayana nguvu. Watu wa Mungu walikuwa salama daima wakuu wao walipokuwa wakuu katika maombi.

Wakati wa utawala wake, jambo zito liliwapata watu wa Mungu, ambalo lingeijaribu imani yake katika Mungu na kumpa nafasi ya kutumia chombo cha maombi ili kupata wokovu. Yuda ilibanwa sana na Waashuru, na, kwa jinsi ya kibinadamu, kushindwa na kuchukuliwa mateka kulionekana kumekaribia. Mfalme wa Ashuru alituma ujumbe kulitukana na kulikufuru jina la Mungu na kumtukana Mfalme Hezekia, nao wakatamka matukano yao na kufuru zao hadharani. Angalia kile ambacho Hezekia alifanya mara moja bila kusita:

“Ikawa, mfalme Hezekia aliposikia, akararua nguo zake, akajivika gunia, akaingia nyumbani mwa BWANA.”

Wazo lake la kwanza kabisa lilikuwa kumgeukia Mungu kwa kwenda kwenye “nyumba ya sala.” Mungu alikuwa katika mawazo yake, na maombi yalikuwa jambo la kwanza kufanywa. Kwa hiyo akatuma wajumbe kwa Isaya ili aungane naye katika maombi. Katika dharura kama hiyo Mungu hapaswi kuachwa nje ya hesabu. Mungu lazima aombwe kuwaokoa na adui hawa wa Mungu na wa watu wake wanaomkufuru.

Wakati huo huo hasa, majeshi ya mfalme wa Ashuru yaliyokuwa yakimzingira Hezekia yaligeuzwa yasiushambulie Yerusalemu mara moja. Hata hivyo, mfalme wa Ashuru alimtumia Hezekia barua ya kashfa na kufuru.

Kwa mara ya pili, akiwa ametukanwa na kuzingirwa na majeshi ya mfalme huyu wa kipagani, anaingia nyumbani mwa Bwana, “nyumba ya sala.” Angeenda wapi pengine? Na amwombe nani isipokuwa Mungu wa Israeli?

“Hezekia akaipokea barua mkononi mwa wajumbe, akaisoma; Hezekia akapanda nyumbani mwa BWANA, akaikunjua mbele za BWANA.

“Hezekia akaomba mbele za BWANA, akasema, Ee BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, uketiye juu ya makerubi, wewe ndiwe Mungu, wewe peke yako, wa falme zote za dunia. Wewe ndiwe uliyezifanya mbingu na nchi.

“Basi sasa, Ee BWANA, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, ili falme zote za dunia zijue ya kuwa wewe ndiwe BWANA, wewe peke yako.”

Na angalia jibu la upesi na matokeo ya ajabu ya maombi kama hayo ya mfalme huyu amchaye Mungu. Kwanza, Isaya alimpa mfalme uhakika kamili kwamba hakuhitaji kuogopa chochote. Mungu alikuwa amesikia maombi, naye angeleta wokovu mkuu.

Kisha, pili, malaika wa Bwana alikuja kwa mabawa mepesi akawapiga Waashuru 185,000. Mfalme alithibitishwa kuwa na haki, Mungu aliheshimiwa, na watu wa Mungu waliokolewa.

Maombi ya pamoja ya mfalme aliyeomba na nabii aliyeomba yalikuwa nguvu zenye uweza wote katika kuleta wokovu na kuwaangamiza adui za Mungu. Majeshi yalikuwa mikononi mwao, bila ulinzi; na malaika, wenye mabawa mepesi na waliojihami kwa uweza na kisasi cha Mwenyezi, walikuwa washirika wao.

Hezekia alikuwa amehudumu kwa maombi katika kuiangamiza ibada ya sanamu na kuutengeneza ufalme wake. Katika kukabiliana na adui zake, maombi yalikuwa silaha yake kuu. Sasa anakuja kujaribu nguvu yake dhidi ya makusudi ya Mungu Mwenyezi yaliyokwisha kukusudiwa na kutangazwa. Je, yatafaa katika uwanja huu mpya wa kazi? Hebu tuone. Hezekia alikuwa mgonjwa sana, na Mungu anamtuma rafiki yake wa karibu, mshauri wake mwenye hekima na nabii, Isaya, kumwonya juu ya mwisho wake unaokaribia, na kumwambia ayatengeneze mambo yake yote kwa ajili ya kuondoka kwake kwa mwisho. Hii ndiyo habari ya Maandiko:

“Siku zile Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa. Nabii Isaya, mwana wa Amozi, akamwendea, akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; kwa maana utakufa, wala hutapona.”

Amri ilikuja moja kwa moja kutoka kwa Mungu kwamba atakufa. Ni nini kinachoweza kuiweka kando au kuigeuza amri hiyo ya kimungu ya mbinguni? Hezekia hakuwahi kuwa katika hali isiyoshindika namna hii, akiwa na amri iliyo wazi na dhahiri hivyo kutoka kwa Mungu. Je, maombi yanaweza kubadili makusudi ya Mungu? Je, maombi yanaweza kumnyakua kutoka katika taya za mauti mtu aliyekwisha kuamriwa kufa? Je, maombi yanaweza kumwokoa mtu na ugonjwa usiotibika? Haya ndiyo maswali ambayo imani yake sasa ilipaswa kushughulika nayo. Lakini imani yake haionekani kusita hata kwa kitambo kimoja. Imani yake haitikisiki hata dakika moja kwa habari ya ghafla na ya wazi aliyoletewa na nabii wa Bwana. Maswali kama yale ambayo kutoamini au kukataa kuamini kwa nyakati hizi kungeyainua hayaanzi akilini mwake. Mara moja anajitoa kwa maombi. Papo hapo bila kukawia anamwendea Mungu aliyetoa amri ile. Angeenda kwa nani mwingine? Je, Mungu hawezi kubadili makusudi yake mwenyewe akipenda?

Angalia kile alichofanya Hezekia katika dharura hii, akiwa amebanwa sana, na uone matokeo ya neema:

“Ndipo Hezekia akageuza uso wake kuelekea ukuta, akamwomba BWANA, akasema,

“Ee Bwana, nakusihi, kumbuka sasa jinsi nilivyokwenda mbele zako kwa kweli, na kwa moyo mkamilifu, nami nimefanya yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana.”

Halikuwa ombi la kujiona mwenye haki ambalo alimtolea Mungu ili apone. Alikuwa akiutaja tu uaminifu wake, kama vile Kristo alivyofanya miaka mingi baadaye:

“Mimi nimekutukuza duniani.”

Yeye ni mkumbushaji wa Bwana, naye anamkumbusha juu ya unyofu wake, uaminifu wake na utumishi wake, jambo lililokuwa halali kwa kila namna. Ombi hili lilikwenda sambamba kabisa na lile la Daudi katika Zaburi 26:1, “Ee BWANA, unihukumu, kwa maana nimekwenda katika ukamilifu wangu.” Hili si jaribio la maombi kwa upande wa Hezekia, wala si uponyaji wa imani, bali ni kumjaribu Mungu. Lazima uwe uponyaji wa Mungu, ikiwa uponyaji utakuja hata kidogo.

Hezekia alikuwa hajamaliza maombi yake vizuri, na Isaya alikuwa karibu kwenda nyumbani, Mungu alipompa ujumbe mwingine kwa ajili ya Hezekia, safari hii wenye kupendeza zaidi na wa kutia moyo. Nguvu kuu ya maombi ilikuwa imemgusa Mungu, ikabadili amri yake na kumgeuza katika kusudi lake kuhusu Hezekia. Ni nini kile ambacho maombi hayawezi kufanya? Ni nini kile ambacho mtu wa maombi hawezi kukitimiza kwa njia ya maombi?

“Ikawa, kabla Isaya hajatoka katika ua wa kati, neno la BWANA likamjia, kusema,

“Rudi, umwambie Hezekia, mkuu wa watu wangu, BWANA, Mungu wa Daudi baba yako, asema hivi, Nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitakuponya; siku ya tatu utapanda nyumbani mwa BWANA.

“Nami nitaziongeza siku zako miaka kumi na mitano; nami nitakuokoa wewe na mji huu na mkono wa mfalme wa Ashuru; nami nitaulinda mji huu kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu.”

Ombi lilielekezwa kwa Mungu. Lilikuwa kwamba Mungu afikiri tena na kubadili nia yake. Bila shaka Isaya alirudi nyumbani kwake na moyo mwepesi kuliko alipoutoa ujumbe wake wa kwanza. Mungu alikuwa ameombwa na mfalme huyu mgonjwa, na alikuwa ameombwa aitangue amri yake, na Mungu alijishusha kulikubali ombi hilo. Mungu wakati mwingine hubadili nia yake. Ana haki ya kufanya hivyo. Sababu za yeye kubadili nia yake ni sababu zenye nguvu. Mtumishi wake Hezekia anataka ifanyike. Hezekia alikuwa mtumishi mwaminifu na alikuwa amemfanyia Mungu mengi. Kweli, ukamilifu na wema vimekuwa ndivyo viini vya utumishi wa Hezekia na kanuni ya maisha yake. Machozi ya Hezekia na maombi yake yamesimama njiani mwa Mungu kutekeleza amri yake ya kuyaondoa maisha ya mtumishi wake. Maombi na machozi ni mambo yenye nguvu mbele za Mungu. Kwake yana uzito mkubwa kuliko kushikamana na msimamo, na mkubwa zaidi kuliko amri. “Nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitakuponya.”

Ugonjwa hufa mbele ya maombi. Afya huja kwa kujibu maombi. Mungu alijibu zaidi ya kile Hezekia alichoomba. Hezekia aliomba uhai wake tu, na Mungu akampa uhai na zaidi ya hayo akamwahidi ulinzi na usalama kutoka kwa adui zake.

Lakini Isaya alihusika na kupona kwa mfalme huyu aliyeomba. Palikuwa na kitu zaidi ya maombi ndani yake. Maombi ya Isaya yaligeuzwa kuwa ustadi wa tabibu. “Isaya akasema, Twaeni mkate wa tini. Wakautwaa, wakauweka juu ya jipu, naye akapona.”

Mara nyingi Mungu hutumia dawa katika kujibu maombi. Mara kwa mara inahitaji imani yenye nguvu zaidi kuinuka juu ya njia hizo na kutozitegemea, kuliko kukataa kabisa njia zote. Hapa palikuwa na dawa sahili, ili wote wajue kwamba si hiyo iliyoponya ugonjwa ule wa kufisha, lakini ilikuwa njia ya kusaidia au kujaribu imani. Lakini maombi zaidi yalikuwa bado yafanyike. Isaya na Hezekia hawakuweza kufanya mambo bila kuomba sana:

“Hezekia akamwambia Isaya, Ni nini dalili ya kuwa BWANA ataniponya, nami nitapanda nyumbani mwa BWANA siku ya tatu?

“Isaya akasema, Dalili utakayopewa na BWANA, ya kuwa BWANA atalitenda jambo hilo alilolinena, ni hii: Je, kivuli kiende mbele madaraja kumi, au kirudi nyuma madaraja kumi?

“Hezekia akajibu, Ni jambo jepesi kivuli kushuka madaraja kumi; sivyo, bali kivuli na kirudi nyuma madaraja kumi.

“Isaya nabii akamlilia BWANA; naye akakirudisha kivuli nyuma madaraja kumi, kwa madaraja yale kilichokuwa kimeshuka katika saa ya jua ya Ahazi.”

Hezekia anakabili tukio hilo na kulifunika jibu la maombi yake kwa shukrani. Harufu nzuri ya manukato iko pale, na wimbo mtamu wa kinubi pia.

Mambo manne na tuyakumbuke daima: Mungu husikia maombi, Mungu huyajali maombi, Mungu hujibu maombi, na Mungu huokoa kwa njia ya maombi. Mambo haya hayawezi kurudiwa mara nyingi mno. Maombi huvunja makomeo yote, huyeyusha minyororo yote, hufungua magereza yote na hupanua dhiki zote ambazo kwazo watakatifu wa Mungu wamebanwa.

Maisha yalikuwa matamu kwa Hezekia naye alitamani kuishi, lakini ni nini kiwezacho kuistahimili amri ya Mungu? Hakuna kitu ila nguvu ya imani. Moyo wa Hezekia ulivunjika chini ya mzigo huo, na maji yake yakatiririka na kuongeza nguvu na wingi katika maombi yake. Alisihi kwa kujitahidi sana na kwa hoja zenye nguvu; na Mungu akamsikia Hezekia akiomba, akayaona machozi yake, akabadili nia yake, na Hezekia akaishi ili amsifu Mungu na kuwa kielelezo cha nguvu ya maombi yenye uweza.

Kama ilivyokuwa kwa Hezekia, namna ya kuomba iliyo ya heshima tu lakini isiyo na roho haikumfaa Paulo. Anajiweka katika hali ya mshindani mweleka, na kuwaagiza ndugu zake waungane naye katika uchungu wa pambano kuu. “Ndugu zangu, nawasihi,” asema, “kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu.” Alikuwa na bidii mno kiasi cha kutoweza kuigusa kazi ya maombi kwa adabu tu au kwa mikono iliyovaa glavu. Aliiingia kama uchungu mkali, naye alitamani ndugu zake wawe washirika wake katika pambano hili na mweleka huu wa nafsi yake. Epafra alikuwa akifanya maombi ya namna hiyo hiyo kwa ajili ya Wakolosai: “akijitahidi sikuzote kwa ajili yenu katika maombi yake, ili msimame wakamilifu na kuthibitika katika mapenzi yote ya Mungu.” Ni lengo linalostahili kuhangaikiwa kwa uchungu daima. Maombi ya namna hii ya wachungaji hawa wa kwanza wa Kanisa la Mitume yalikuwa siri moja ya usafi wake, chemchemi moja ya nguvu ya Kanisa. Na haya ndiyo maombi ya namna iliyofanywa na Hezekia.

Hapa palikuwa na maombi yaliyozaliwa katika moto wa tamaa kuu, na kufuatiliwa kupitia uchungu mzito kabisa wa pambano na upinzani hadi kufanikiwa. Je, shauku zetu za kiroho hazina nguvu ya kutosha kuyapa uhai mapambano makuu ya maombi? Hazitumii nafsi kiasi cha kutosha kusimamisha biashara, kuzuia shughuli za kidunia, kutuamsha kabla ya mapambazuko, na kutupeleka chumbani, kwenye upweke, na kwa Mungu; kushinda kila nguvu ipingayo na kujipatia ushindi wetu kutoka katika taya zenyewe za jehanamu. Twahitaji wahubiri na wanaume na wanawake wanaoweza kuonyesha kwa mfano matumizi, nguvu, baraka, na mipaka ya mwisho kabisa ya maombi.

Isaya anaomboleza kwamba hapakuwa na mtu aliyejiamsha ili amshike Mungu. Maombi mengi yalifanywa, lakini yalikuwa mepesi mno, yasiyojali, ya kuridhika. Hapakuwa na misukumo mikuu ya nafsi kumwelekea Mungu, wala mpangilio wa nguvu zote zilizotakaswa kunyoosha mkono na kumshika Mungu kwa nguvu na kuzitoa hazina zake kwa matumizi ya kiroho. Maombi yasiyo na nguvu hayana uwezo wa kushinda magumu, hayana uwezo wa kuleta matokeo dhahiri, wala kupata ushindi kamili na wa ajabu.