Sura 1 · dakika 4 za kusoma · dakika 5 za kusikiliza
Utangulizi
Mchungaji Edward McKendrie Bounds alijitoa kwa moyo wake wote kwa Bwana na Mwokozi wake mpendwa Yesu Kristo. Ibada yake ilikuwa ya ajabu kwa kuwa alikuwa akiomba na kuandika juu yake wakati wote, isipokuwa saa za usingizi tu.
Mungu alimpa Bounds moyo mpana na tamaa isiyotosheka ya kumtumikia. Kwa ajili hiyo alifurahia kile ninachopenda kukiita uvuvio uliopita kawaida; la sivyo kamwe asingeweza kutoa katika hazina yake vitu vipya na vya zamani vinavyopita kwa mbali chochote tulichokijua au kukisoma katika nusu karne iliyopita.
Bila shaka Bounds ndiye nyota Betelgeuse ya anga la ibada. Hakuna mtu aliyeishi tangu siku za mitume aliyemzidi katika kina cha utafiti wake wa ajabu kuhusu Maisha ya Maombi.
Alikuwa akishughulika kuandika miswada yake wakati Bwana alipomwambia, “Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ingia katika furaha ya bwana wako.” Barua zake zilikuwa zikinifikia mara kwa mara huko Brooklyn, N.Y., mwaka 1911, 1912 na 1913, zikisema, “Niombee ili Mungu anipe mishipa mipya na maono mapya ya kumaliza miswada hii.”
Wesley alikuwa mtu mpole sana na mwepesi wa kusamehe, lakini alipochochewa alikuwa mtu “mwenye utambuzi mkali kupita wote, na kipawa cha usemi kilichouma kama pigo la mjeledi.” Bounds alikuwa mpole na mnyenyekevu, wala hatukuwahi kumwona akilipiza kisasi juu ya adui zake wowote. Aliwalilia na kutokwa machozi akiwaombea alfajiri na usiku.
Wesley alidanganyika kwa urahisi. “Ndugu yangu,” Charles alisema wakati mmoja kwa sauti ya kuchukizwa, “nadhani alizaliwa kwa faida ya wadanganyifu.” Hakuna mtu aliyeweza kumdanganya Bounds. Alikuwa mpambanuzi mwenye uwezo adimu. Bounds aliwaepuka wote waliojifanya kuwa wacha Mungu kwa udanganyifu, wala hakupoteza muda wowote kwao.
Wesley alikuwa akihubiri na kusafiri juu ya farasi mchana kutwa. Bounds alikuwa akiomba na kuandika mchana na usiku.
Katika miaka yake ya uzeeni Wesley hakukubali mafundisho yake yapotoshwe hata kidogo. Bounds alifanana naye sana katika jambo hili.
Wesley alipata umaarufu wake angali hai. Daima alikuwa mbele ya macho ya watu. Bounds, ingawa alihariri gazeti la Christian Advocate kwa miaka kumi na miwili, hakujulikana sana nje ya kanisa lake.
Wesley akiwa na umri wa miaka themanini na sita bado aliweza kuhubiri barabarani kwa dakika thelathini. Bounds akiwa na miaka sabini na mitano aliweza, katika saa ya kwanza ya zamu ya nne ya usiku, kuomba kwa saa tatu akiwa amepiga magoti.
Wesley, wakati wa kifo chake, alikuwa amefurahia heshima kwa miaka hamsini na sita. Jina lake lilikuwa kinywani mwa kila mtu. Ukristo ulizaliwa upya nchini Uingereza kupitia mahubiri na uongozi wake mkuu. Bounds hakujulikana kwa kiasi kikubwa kwa miaka hamsini, lakini katika miaka hamsini ijayo atarudisha “siri ya kanisa iliyopotea na kusahaulika.”
Utauwa, kipaji na umaarufu wa Wesley vilitiririka tangu ujana wake kama mto mkubwa wenye fahari. Vya Bounds vimezuiliwa kama kwa bwawa, lakini sasa vinaanza kufurika kwa nguvu isiyozuilika, na kabla ya muda mrefu atakuwa ndiye mto Amazon mkuu wa ulimwengu wa ibada.
Henry Crabbe Robinson aliandika katika shajara yake alipomsikia Wesley akihubiri huko Colchester, “Alisimama katika mimbari pana, na kila upande wake alisimama mhudumu, nao wawili walimshikilia. Sauti yake ilikuwa dhaifu na alisikika kwa shida, lakini uso wake wa heshima, hasa nywele zake ndefu nyeupe, vilifanya picha isiyoweza kusahaulika kamwe.” Mwandishi wa mistari hii alimpisha Mchungaji E. M. Bounds mimbari yake huko Brooklyn mwaka 1912, miezi kumi tu kabla ya kifo chake. Sauti yake ilikuwa dhaifu na sentensi zake hazikukamilika vizuri. Mahubiri yake yalichukua dakika ishirini tu, kisha akafika mwisho kwa utulivu na alionekana amechoka kabisa.
Wesley alikuwa na fedha za kutosha, na za ziada, katika maisha yake yote ya huduma. Bounds hakujali fedha. Hakuzidharau; alizihesabu kuwa daraja la chini kabisa la nguvu.
Wesley alikufa “jicho lake likiangaza na midomo yake ikibubujika sifa.” “Lililo bora kuliko yote ni kwamba Mungu yu pamoja nasi,” Bounds alimwandikia mwandishi wa mistari hii. “Atakapokuwa tayari, mimi niko tayari; ninatamani kuonja furaha za ulimwengu wa mbinguni.”
Wesley alisema, “Ulimwengu ndio parokia yangu.” Bounds aliomba kana kwamba ulimwengu wote wa viumbe ndio eneo lake.
Wesley alikuwa kielelezo hai cha kutokuwa na moyo wa kidunia, na mfano kamili wa ukarimu wa moyo. Bounds alikuwa kielelezo hai cha kutokuwa wa dunia hii, cha unyenyekevu na cha kujikana nafsi. Wesley ataishi mioyoni mwa watakatifu kwa nyakati za milele. Bounds ataishi milele.
Wesley amelala katika uwanja wa kanisa la City Road Chapel, kati ya “wafu wake wapendwa,” chini ya marumaru, pamoja na heshima inayostahili iliyochongwa kwa maneno, akingojea Ufufuo. Bounds amelala katika makaburi ya Washington, Georgia, bila marumaru juu yake, akingojea kuja kwake Bwana Arusi.
Watu hawa wawili walishikilia maono ya juu na ya thamani, yasiyofikiwa na watu wengine. Je, jamii hii ya watu imetoweka kabisa duniani sasa kwa kuwa wamekufa? Na tuombe.
Homer W. Hodge
Brooklyn N.Y.