Ulazima wa Maombi
Maombi na Kusihi kwa Bidii

Sura 7 · dakika 9 za kusoma · dakika 12 za kusikiliza

Maombi na Kusihi kwa Bidii

“Tunazungumza kwa wepesi kiasi gani juu ya kuomba bila kukoma! Hata hivyo tuko tayari kabisa kuacha, kama maombi yetu yangekaa bila kujibiwa juma moja tu au mwezi mmoja! Tunadhani kwamba kwa pigo moja la mkono wake au kwa tendo moja la mapenzi yake, Mungu atatupa tunachoomba. Haitujii kamwe akilini kwamba yeye ndiye Bwana wa maumbile, kama alivyo wa neema, na kwamba wakati mwingine huchagua njia moja, na wakati mwingine nyingine, ya kufanya kazi yake. Wakati mwingine huchukua miaka kujibu ombi; na likiisha kujibiwa, tukitazama nyuma, twaweza kuona kwamba ndivyo ilivyokuwa. Lakini Mungu anajua wakati wote, na ni mapenzi yake kwamba tuombe, na tuombe, na bado tuombe, na hivyo tufike kujua, kwa hakika na kwa kweli, maana ya kuomba bila kukoma.” — ASIYEJULIKANA.

BWANA wetu Yesu alitangaza kwamba “imewapasa kuomba sikuzote, wala wasikate tamaa,” na mfano ambamo maneno yake yamo ulifundishwa kwa kusudi la kuwaokoa watu na kuzimia moyo na udhaifu katika maombi. Bwana wetu alikuwa akitaka kufundisha kwamba ulegevu sharti ujihadhariwe, na kudumu kukuzwe na kutiwa moyo. Hapawezi kuwa na maoni mawili juu ya umuhimu wa kuitumia sifa hii, isiyoweza kukosekana, katika kuomba kwetu.

Maombi ya kusihi ni mwendo mkuu wa nafsi kumwelekea Mungu. Ni kuchochewa kwa nguvu zilizo ndani kabisa ya nafsi, kuelekea kiti cha neema cha mbinguni. Ni uwezo wa kushikilia, kusonga mbele, na kungoja. Shauku isiyotulia, saburi yenye utulivu, na nguvu ya kushika, vyote vimo ndani yake. Si tukio la kupita, wala onyesho, bali ni moto wa nafsi. Si hitaji la nusu nusu, bali ni lazima kabisa.

Sifa ya kushindana iliyo katika maombi ya kusihi haitokani na ukali wa kimwili wala nguvu za mwili. Si msukumo wa nguvu tu, wala si bidii tu ya nafsi; ni nguvu iliyofanyizwa ndani, uwezo uliopandwa na kuamshwa na Roho Mtakatifu. Kwa kweli, ni maombezi ya Roho wa Mungu ndani yetu; tena ni “kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, kukiwa kwa bidii.” Roho wa Mungu, akijaza kila sehemu iliyo ndani yetu nguvu ya kujitahidi kwake mwenyewe, ndiye kiini cha kusihi kunakotusukuma kuomba mbele ya kiti cha rehema, tuendelee mpaka moto ushuke na baraka iteremke. Kushindana huku katika maombi huenda kusiwe kwa makelele wala kwa ukali, bali kwa utulivu, kwa ushupavu na kwa haraka ya moyo. Huenda kukawa kimya, wakati nguvu zake kuu hazina njia za kuonekana.

Hakuna kitu kinachowatofautisha watoto wa Mungu waziwazi na kwa nguvu kama maombi. Ndiyo alama moja isiyokosea, na kipimo, cha kuwa Mkristo. Wakristo ni watu wa maombi; watu wa dunia hawaombi. Wakristo humwita Mungu; watu wa dunia humpuuza Mungu, wala hawaliitii Jina lake. Lakini hata Mkristo alihitaji kukuza maombi ya daima. Maombi sharti yawe desturi, lakini zaidi sana ya desturi. Ni wajibu, lakini wajibu unaopanda juu sana, na kupita maana ya kawaida ya neno hilo. Ni kielelezo cha uhusiano na Mungu, shauku ya ushirika na Mungu. Ni mtiririko wa uzima wa ndani kwenda nje na juu, kuelekea chemchemi yake ya asili. Ni tamko la nafsi juu ya Baba yake, kuudai ule uana unaomuunganisha mwanadamu na Yeye wa Milele.

Maombi yanahusika kabisa na kuifinyanga nafsi katika sura ya Mungu, na kuongeza na kupanua kipimo cha neema ya Mungu. Yanahusika kabisa na kuileta nafsi katika ushirika kamili na Mungu. Yanahusika kabisa na kuutajirisha, kuupanua na kuukomaza ujuzi wa nafsi juu ya Mungu. Mtu yule asiyeomba hawezi kamwe kuitwa Mkristo. Kwa kisingizio cho chote hawezi kudai haki ya jina hilo, wala ya maana yake. Asipoomba, yeye ni mwenye dhambi, si zaidi wala pungufu, kwa maana maombi ndiyo njia pekee ambayo kwayo nafsi ya mwanadamu yaweza kuingia katika ushirika na umoja na Chanzo cha roho na nguvu zote zilizo kama za Kristo. Kwa hiyo, asipoomba, yeye si wa familia ya imani.

Lakini katika funzo hili tunaelekeza fikira zetu kwenye upande mmoja wa maombi — ule wa kusihi kwa bidii; yaani kumsihi Mungu kwa haja zetu kwa haraka na kwa kudumu; kuomba kwa ushupavu na kwa nguvu ile isiyolegea wala kukoma mpaka ombi lake limesikiwa, na shauri lake limeshinda.

Yeye aliye na maono wazi juu ya Mungu, na mawazo ya Kimaandiko juu ya tabia ya Mungu; anayethamini pendeleo lake la kumkaribia Mungu; anayefahamu hitaji lake la ndani la yote ambayo Mungu anayo kwa ajili yake — mtu huyo atakuwa na hamu kuu, atasema wazi, na atasihi kwa bidii. Katika Maandiko Matakatifu, wajibu wa kuomba wenyewe unahimizwa kwa maneno yaliyo makali kidogo tu kuliko yale yanayoeleza ulazima wa kusihi kwa bidii. Maombi yanayomgusa Mungu yametangazwa kuwa yale ya mtu mwenye haki, yakimiminwa kwa bidii na kwa kufaa. Maana yake ni kwamba, ni maombi yanayowaka moto, yasiyo na mwali dhaifu unaopepesuka, wala mmweko wa kitambo, bali yanayong’aa kwa mwanga wenye nguvu na thabiti.

Maombezi ya Ibrahimu yaliyorudiwa kwa ajili ya wokovu wa Sodoma na Gomora ni mfano wa mapema wa ulazima wa maombi ya kusihi, na wa faida itokanayo nayo. Yakobo, akishindana usiku kucha na malaika, anatia mkazo wenye maana juu ya nguvu ya kudumu kwa ukaidi katika kuomba, na anaonyesha jinsi, katika mambo ya kiroho, kusihi kunavyofaulu sawasawa na kunavyofaulu katika mambo ya wakati huu na ya hisia.

Kama tulivyokwisha kuona mahali pengine, Musa aliomba siku arobaini mchana na usiku, akitafuta kuizuia ghadhabu ya Mungu dhidi ya Israeli, na mfano wake na kufanikiwa kwake ni kichocheo kwa imani ya leo katika saa yake ya giza kuu. Eliya alirudia na kusisitiza ombi lake mara saba kabla wingu la mvua halijatokea juu ya upeo wa macho, likitangaza kufanikiwa kwa ombi lake na ushindi wa imani yake. Wakati mmoja Danieli, ingawa alikuwa amezimia na dhaifu, alisisitiza shauri lake majuma matatu, kabla jibu na baraka havijaja.

Usiku mwingi wakati wa maisha yake duniani Mwokozi aliyebarikiwa aliukesha katika maombi. Katika Gethsemane aliomba ombi lile lile mara tatu, kwa kusihi kusikopungua, kwa haraka, lakini kwa kujisalimisha, kulikohusisha kila sehemu ya nafsi yake, na kukaishia katika machozi na jasho la damu. Nyakati kuu za maisha yake zilitambulika wazi, na ushindi wote wa maisha yake ulipatikana, katika saa za maombi ya kusihi. Naye mtumwa si mkuu kuliko bwana wake.

Mfano wa Mjane Aliyesihi ni kielelezo kikuu cha maombi yasiyokoma. Itatufaa kujikumbusha upya mfano huo, mahali hapa katika funzo letu:

“Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kuomba sikuzote, wala wasikate tamaa; akisema, Palikuwa na kadhi katika mji mmoja, asiyemcha Mungu wala kujali watu; na katika mji ule palikuwa na mwanamke mjane; akamwendea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. Naye kwa muda alikataa; lakini baadaye akasema moyoni mwake, Ingawa simchi Mungu wala sijali watu, lakini kwa kuwa mjane huyu ananisumbua, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. Naye Mungu, je! hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi.”

Mfano huu unasisitiza kweli kuu ya maombi ya kusihi. Mjane anasisitiza shauri lake mpaka kadhi dhalimu anakubali. Ikiwa mfano huu haufundishi ulazima wa kusihi kwa bidii, basi hauna maana wala mafundisho ndani yake. Liondoe wazo hili moja, nawe hutabaki na kitu cho chote kinachostahili kuandikwa. Bila ubishi wo wote, Kristo alikusudia usimame kama ushahidi wa hitaji lililopo la maombi yasiyokoma.

Tunalo fundisho lilo hilo likisisitizwa katika habari ya mwanamke Msirofoinike, aliyemjia Yesu kwa ajili ya binti yake. Hapa, kusihi kunaonyeshwa, si kama ufidhuli mtupu, bali kama kumevikwa mavazi ya kushawishi ya unyenyekevu, unyofu, na bidii. Tunaonyeshwa kwa kitambo imani ya mwanamke inayoshikilia, huzuni chungu ya mwanamke, na ufahamu wa kiroho wa mwanamke. Bwana alikwenda katika nchi ile ya Sidoni ili kweli hii ionekane kama katika kioo kwa nyakati zote — hakuna ombi linalofaa sana kama maombi ya kusihi, wala hakuna ambalo Mungu hujitoa kwalo kwa ukamilifu na kwa hiari namna hiyo.

Kusihi kwa mama huyu aliyefadhaika kulimpatia ushindi, na kulilifanya ombi lake litimie. Lakini badala ya kumchukiza Mwokozi, kulimtoa maneno ya mshangao, na ya furaha ya kustaajabu. “Mama, imani yako ni kubwa; na ufanyiwe kama utakavyo.”

Haombi kabisa, yeye asiyesisitiza ombi lake. Maombi baridi hayana haki mbinguni, wala hayasikiwi katika nyua za juu. Moto ndio uzima wa maombi, na mbingu hufikiwa kwa kusihi kunakowaka moto, kukipanda juu daraja kwa daraja.

Tukirudi kwenye habari ya mjane aliyesihi, tunaona kwamba ujane wake, kukosa kwake rafiki, na udhaifu wake havikuwa kitu kwa yule kadhi dhalimu. Kusihi ndiko kulikokuwa kila kitu. “Kwa kuwa mjane huyu ananisumbua,” alisema, “nitampatia haki yake upesi, asije akanichosha.” Kwa sababu tu mjane aliusumbua wakati na uangalifu wa kadhi dhalimu, shauri lake lilishinda.

Mungu hungoja kwa uvumilivu wakati wateule wake wanapomlilia mchana na usiku. Yeye huguswa na maombi yao mara elfu zaidi kuliko alivyoguswa kadhi huyu dhalimu. Kukawia kwake kunawekewa kikomo na maombi ya kusihi ya watu wake, na jibu hutolewa kwa wingi. Mungu huiona imani katika mtoto wake anayeomba — imani ile inayodumu na kulia — naye huiheshimu kwa kuiruhusu iendelee kutumika, ili iimarishwe na kutajirishwa. Kisha huithawabisha kwa kumpa kile alichokuwa akiomba kwa uzito wa moyo, kwa wingi kamili na kwa ukamilifu wa mwisho.

Habari ya mwanamke Msirofoinike tuliyoitaja hapo awali ni mfano mashuhuri wa kusihi kulikofanikiwa, unaowatia moyo sana wote wanaotaka kuomba kwa mafanikio. Ulikuwa mfano wa ajabu wa kusisitiza na kudumu hadi ushindi wa mwisho, mbele ya vizuizi na pingamizi ambavyo karibu haviwezi kushindwa. Lakini mwanamke huyo alivishinda vyote kwa imani ya kishujaa na roho ya kudumu, ambazo zilikuwa za ajabu kama zilivyofanikiwa. Yesu alikuwa amekwenda katika nchi yake, “akataka mtu asijue.” Lakini yeye analipenya kusudi lake, anaivunja faragha yake, anavuta uangalifu wake, na kummiminia ombi lenye kuchoma moyo la uhitaji na imani. Moyo wake ulikuwa ndani ya ombi lake.

Mwanzoni, Yesu anaonekana kutojali uchungu wake, na kupuuza kilio chake cha kuomba msaada. Hampi jicho, wala sikio, wala neno. Kimya, kizito na cha kutia baridi, kinakipokea kilio chake cha shauku. Lakini yeye hageuzwi kando, wala hakati tamaa. Anashikilia. Wanafunzi, wakichukizwa na kelele zake zisizofaa, wanamwombea, lakini wananyamazishwa Bwana anapotangaza kwamba mwanamke huyo yuko nje kabisa ya mipaka ya utume wake na huduma yake.

Lakini wala kushindwa kwa wanafunzi kumpatia nafasi ya kusikilizwa, wala kujua — jambo la kukatisha tamaa kwa asili yake — kwamba amezuiliwa asipate faida za utume wake, havimvunji moyo; bali vinamtia tu nguvu zaidi na ujasiri ulioongezeka katika kumkaribia Kristo. Alisogea karibu zaidi, akilikata ombi lake vipande viwili, akaanguka miguuni pake, akamsujudia, akaifanya shida ya binti yake kuwa kilio chake mwenyewe, kwa ufupi wenye kuchoma — “Bwana, unisaidie!” Kilio hiki cha mwisho kilimpatia ushindi; binti yake aliponywa saa ile ile. Mwenye tumaini, mwenye haraka ya moyo, na asiyechoka, anakaa karibu na Bwana, akisisitiza na kuomba mpaka jibu limetolewa. Ni funzo kubwa kama nini la kusihi, la bidii, la kudumu, vilivyoendelezwa na kusukumwa mbele katika hali ambazo zingemkatisha tamaa mtu ye yote isipokuwa nafsi ya kishujaa na thabiti.

Katika mifano hii ya maombi ya kusihi, Bwana wetu anaeleza, ili tujue na tutiwe moyo, magumu makubwa yanayosimama katika njia ya maombi. Wakati huo huo anafundisha kwamba kusihi hushinda hali zote zisizofaa na kujipatia ushindi juu ya jeshi zima la vizuizi. Tena anafundisha kwamba jibu la maombi hutegemea kiasi cha imani kilichotiwa katika ombi. Ili kulipima jambo hili, huchelewesha jibu. Mwombaji wa juu juu hunyamaza, jibu linapochelewa. Lakini mtu wa maombi hushikilia, na kuendelea kushikilia. Bwana huitambua na kuiheshimu imani yake, na humpa jibu tajiri na tele kwa maombi yake ya kusihi, yanayoshuhudia imani yake.