Sura 5 · dakika 12 za kusoma · dakika 16 za kusikiliza
Jinsi ya Kuwashughulikia Wale Wanaotaka Sana Kuokolewa na Wanajua Jinsi, Lakini Wana Magumu
Idadi kubwa sana ya watu tunaojaribu kuwaongoza kwa Kristo, tutakuta kwamba kwa kweli wanataka sana kuokolewa na wanajua jinsi ya kuokolewa, lakini wanakabiliwa na magumu wanayoyaona kuwa hayawezi kushindika.
1. Mojawapo ya magumu hayo ni, “Mimi ni mwenye dhambi mkubwa mno.” 1 Timotheo 1:15 linalijibu hili kikamilifu. Jumapili moja asubuhi mtu mmoja aliyekuwa ameishi maisha ya ufisadi na ya kutangatanga, na ambaye hivi karibuni alikuwa amepoteza dola 35,000 na kutengana na mkewe, aliniambia, nilipomwuliza kwa nini hakuwa Mkristo, “Mimi ni mwenye dhambi mkubwa mno kuweza kuokolewa.” Mara moja niligeukia 1 Timotheo 1:15. “Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi, ambao wa kwanza wao ni mimi.” Upesi akajibu, “basi, mimi ndiye wa kwanza wa wenye dhambi.” “Vema,” nikasema, “basi mstari huo unakuhusu wewe.” Akajibu, “Ni ahadi ya thamani.” Nikasema, “Je, utaipokea sasa?” naye akasema, “Nitaipokea.” Kisha nikasema, “Na tupige magoti tumwambie Mungu hivyo,” nasi tukapiga magoti, naye akamwungamia Mungu dhambi zake, akamwomba Mungu amsamehe dhambi zake kwa ajili ya Kristo. Nilimwuliza kama kweli amempokea Kristo, naye akasema amempokea. Nilimwuliza kama kweli anaamini kwamba ameokolewa, naye akasema anaamini. Alitumia nafasi ya mapema kumkiri Kristo. Baada ya muda mfupi aliondoka mjini, lakini niliweza kuendelea kumfuatilia. Akawa Mkristo mwenye bidii kubwa mno, akifanya kazi ya biashara yake mchana, lakini akijishughulisha na kazi fulani ya Kikristo kila usiku wa juma. Aliunganishwa tena na mkewe, wakamchukua mtoto mdogo kutoka kituo cha yatima kumlea kama wao, wakawa na nyumba ya Kikristo yenye furaha. Luka 19:10 pia ni fungu lenye kufaa sana kutumia unaposhughulika na watu wa aina hii; hasa linafaa mtu asemapo, “Nimepotea.” Waweza kusema, “Nina fungu lililokusudiwa hasa kwa ajili yako. Ikiwa kweli unamaanisha usemalo, wewe ndiye hasa mtu ambaye Yesu anamtafuta. ‘Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.’” Warumi 5:6‒8 ni fungu lenye nguvu sana. Usiku mmoja nilimsimamisha mtu mmoja alipokuwa akitoka kwa haraka katika mkutano. Nikiweka mkono wangu begani mwake nilisema “Je, hukuinua mkono wako usiku huu uombewe?” Akasema “ndiyo.” Nikasema, “Basi mbona unaondoka kwa haraka? Je, unajua kwamba Mungu anakupenda?” Akajibu, “Hujui unazungumza na nani.” “Sijali ninazungumza na nani, lakini najua kwamba Mungu anakupenda.” Akasema: “Mimi ndiye mwizi mwovu kuliko wote katika Minneapolis.” Nikasema “Ikiwa wewe ndiye mwizi mwovu kuliko wote katika Minneapolis, basi najua kwamba Mungu anakupenda,” nami nikafungua Biblia yangu kwenye Warumi 5:8. “Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.” “Sasa,” nikasema, “Ikiwa wewe ndiye mwizi mwovu kuliko wote katika Minneapolis, wewe ni mwenye dhambi, na mstari huu unasema kwamba Mungu anawapenda wenye dhambi.” Mtu yule akavunjika moyo, akaingia nami katika chumba kingine akanisimulia habari zake. Alikuwa ametoka kifungoni punde kwa sababu ya uhalifu; alikuwa ametoka usiku ule ule kwenda kufanya kile alichosema kingekuwa mojawapo ya wizi wa kuvunja nyumba wa kuthubutu zaidi kuwahi kufanyika katika mji wa Minneapolis; pamoja na wenzake wawili wa uhalifu alikuwa akipita kwenye kona moja ambapo kwa bahati alisikia mkutano wa hadhara ukiendelea nje, akasimama dakika chache kusikiliza, na licha ya malalamiko na viapo vya wenzake alikaa mpaka mwisho wa mkutano, akaenda pamoja nasi hadi Misheni. Baada ya kunisimulia habari zake tulipiga magoti kuomba. Kwa machozi alimlilia Mungu amrehemu, akiwa ameongozwa na ahadi ya thamani ya Mungu kuamini kwamba Mungu alimpenda mwenye dhambi hata aliye mchafu kama yeye. Mathayo 9:12, 13; Warumi 10:13 (Sisitiza “kila mtu”); Yohana 3:16 (Sisitiza ule “kila mtu”); Isaya 1:18; 1 Yohana 4:14; 1 Yohana 2:1‒2; Isaya 44:22; Isaya 43:25 pia ni mafungu yenye kufaa katika kushughulika na watu wa aina hii. Isaya 1:18 na Zaburi 51:14 yanafaa hasa katika kushughulika na watu waliofanya uuaji. Kamwe usimwambie mtu yeyote kwamba dhambi zake si kubwa. Wakati mwingine ni vema kuwaambia watu hawa, “Ndiyo, dhambi zako ni kubwa, kubwa kuliko unavyodhani, lakini zote zimeshughulikiwa” na kuwaonyesha Isaya 53:6; 1 Petro 2:24. Mwanamke mmoja aliwahi kunijia akiwa amefadhaika sana. Baada ya majaribio mengi yasiyofaulu hatimaye aliweza kuufungua moyo wake. Miaka kumi na minne iliyopita alikuwa ameua mtu, naye alikuwa amebeba kumbukumbu ya tendo hilo dhamirini mwake mpaka karibu limtie wazimu. Alipotusimulia habari hiyo mimi na Mkristo mwingine, tuligeukia Isaya 53:6. Baada ya kumsomea mstari huo kwa uangalifu sana, nilimwuliza Bwana ameifanya nini dhambi yake. Baada ya kufikiri kwa kina na kwa wasiwasi kwa muda mfupi alisema, “Ameiweka juu ya Kristo,” Nikashika kitabu mkononi. “Sasa,” nikasema “mkono wangu wa kulia na uwakilishe wewe, na mkono wangu wa kushoto Kristo, na kitabu hiki dhambi yako.” Niliweka kitabu juu ya mkono wangu wa kulia nikasema: “Dhambi yako iko wapi sasa?” Akasema “Juu yangu.” “Sasa,” nikasema, “Mungu ameifanya nini?” Akasema “Ameiweka juu ya Kristo,” nami nikakihamishia kitabu kwenye mkono ule mwingine. “Dhambi yako iko wapi sasa?” nikauliza. Ilichukua muda mrefu kabla hajapata ujasiri wa kujibu, kisha kwa juhudi ya mwisho kabisa akasema, “Juu ya Kristo.” Nikasema, “basi je, bado iko juu yako?” Polepole nuru ikaingia usoni mwake, naye akapaza sauti kwa kilio, “Hapana, iko juu yake, iko juu ya Kristo.” Yohana 1:29; Matendo 10:43; Waebrania 7:25, pia ni mafungu yenye kusaidia katika kushughulika na watu wa aina hii.
2. Gumu lingine tunalokutana nalo mara kwa mara, ni “Siwezi kudumu,” au “Naogopa kushindwa.” 1 Petro 1:5 linafaa katika kuonyesha kwamba hatupaswi kujilinda wenyewe, bali sisi ni wale “tunaolindwa kwa nguvu za Mungu.” Yohana 10:28, 29 linaonyesha kwamba usalama wa yule ampokeaye Kristo hautegemei “kudumu” kwake, bali uweza wa Baba na wa Mwana wa kulinda. 2 Timotheo 1:12 linaonyesha kwamba ni kazi ya Kristo, wala si yetu, kukilinda kile kilichowekwa amana kwake, na kwamba yeye anaweza kufanya hivyo. Isaya 41:10, 13 pia yanasaidia. Yuda 24 linaonyesha kwamba, tuweze kujizuia tusianguke au tusiweze, Kristo aweza kutulinda tusianguke. 2 Nyakati 32:7, 8; Warumi 14:4; 2 Wathesalonike 3:3, pia ni mafungu mazuri ya kutumia. 1 Wakorintho 10:13 linafaa hasa mtu anapoogopa kwamba jaribu fulani kubwa litampata naye ataanguka.
3. Gumu lingine linalofanana sana na lile lililotangulia, ni “Mimi ni dhaifu mno.” Kwa mtu wa namna hiyo, tumia 2 Wakorintho 12:9, 10. Mwulize “uweza wa Kristo hukamilika wapi?” Atakapojibu “katika udhaifu,” mwambie “basi kadiri unavyokuwa dhaifu zaidi katika nguvu zako mwenyewe, ndivyo ilivyo bora.” Wafilipi 4:13 linaonyesha kwamba hata tuwe dhaifu namna gani, twayaweza mambo yote katika Kristo atutiaye nguvu. 1 Wakorintho 10:13 litaonyesha kwamba Mungu anajua yote kuhusu udhaifu wetu, wala hatatuacha tujaribiwe kupita nguvu zetu.
4. “Siwezi kuziacha njia zangu mbaya au tabia zangu mbaya.” Wagalatia 6:7, 8, litawaonyesha kwamba sharti waziache, ama sivyo wataangamia. Wafilipi 4:13 litawaonyesha kwamba wanaweza kuziacha kwa nguvu za Kristo. Ni mpango bora kabisa kumwelekeza yule anayeogopa kwamba hawezi kuziacha tabia zake mbaya, kwa Kristo, kama Mwokozi aliyefufuka, 1 Wakorintho 15:3, 4. Mtu mmoja aliwahi kunijia akasema: “Nimekuja kwako ili nijue kama kuna njia yoyote ya kupata nguvu za kushinda tabia zangu mbaya.” Alinisimulia habari zake; alikuwa ameongoka utotoni, lakini alikuwa amekuja Chicago, akajiunga na wenzi waovu, akaanguka, na sasa hakuweza kujinasua kutoka katika dhambi zake. Nilimwambia: “Unaijua nusu tu ya injili, injili ya Mwokozi aliyesulibiwa. Kwa kumtumaini Mwokozi aliyesulibiwa ulipata msamaha. Lakini Yesu Kristo pia ni Mwokozi aliyefufuka, 1 Wakorintho 15:4, ‘Amepewa mamlaka yote,’ Mathayo 28:18. Yeye ana uwezo wa kukupa ushindi juu ya tabia zako mbaya. Je, unaamini hilo?” Akasema, “ndiyo.” “Ulimtumaini,” niliendelea, “Kristo aliyesulibiwa ukapata msamaha, sivyo?” “Ndiyo,” akajibu. “Sasa,” nikasema, “je, utamtumaini Kristo aliyefufuka akuokoe na nguvu za dhambi zako?” “Ndiyo, nitamtumaini.” “Basi na tupige magoti, tumwambie hivyo.” Tulipiga magoti tukazungumza na Mwokozi juu ya jambo hilo lote. Alipoinuka hata uso wake ulikuwa umebadilika. “Nimefurahi sana kwamba nimekuja,” akasema. Muda fulani baadaye nilipokea barua kutoka kwake ikinieleza jinsi alivyopata ushindi wa daima kwa kumtumaini Kristo aliyefufuka.
5. “Nitaudhiwa nikiwa Mkristo.” Kamwe usimwambie mtu yeyote kwamba hataudhiwa, bali mwonyeshe kutoka katika mafungu kama 2 Timotheo 2:12; 2 Timotheo 3:12; Mathayo 5:10, 11, 12; Marko 8:35; Matendo 14:22, kwamba mateso ndiyo njia pekee ya kuufikia Utukufu. Waonyeshe kutoka Warumi 8:18 kwamba mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kama Utukufu ule utakaofunuliwa kwetu. Waonyeshe kutoka Matendo 5:41; 1 Petro 2:20, 21, kwamba ni fursa kuudhiwa kwa ajili ya Kristo. Waebrania 12:2, 3 linafaa katika kuwaonyesha mahali pa kutazama ili wapate ushindi katika mateso.
6. “Itaharibu biashara yangu,” au “Siwezi kuwa Mkristo katika biashara yangu ya sasa.” Mwelekeze mtu wa namna hiyo kwa Marko 8:36. Hili litamwonyesha kwamba ni afadhali kupoteza biashara yake kuliko kupoteza roho yake. Wazo hili likishakazwa moyoni mwake vya kutosha, mwonyeshe Mathayo 6:32, 33, lenye ahadi ya Mungu kwamba tukimweka Mungu na ufalme wake kwanza, yeye atatupatia mahitaji yetu yote ya kweli ya maisha haya. Mathayo 16:24‒27; Luka 12:16‒21; 16:24‒26 pia ni mafungu yenye nguvu sana ya kutumia kwa watu wa aina hii.
7. “Ni vitu vingi mno vya kuacha.” Marko 8:36 litawaonyesha kwamba ni afadhali waache kila kitu kuliko kupoteza roho zao. Wafilipi 3:7, 8; Zaburi 16:11 yatawaonyesha kwamba kile wanachokiacha si kitu ukilinganisha na kile wanachokipata. Zaburi 84:11; Warumi 8:32 yatawaonyesha kwamba Mungu hatawaomba waache kitu chochote kilicho chema; kwa maneno mengine, kwamba vitu pekee ambavyo Mungu anawaomba waviache ni vile vinavyowadhuru. Mwanamke mmoja kijana aliwahi kukataa kuja kwa Mwokozi akisema, “Kuna vitu vingi mno vya kuacha.” “Je, unadhani Mungu anakupenda?” nilijibu. “Bila shaka.” “Unadhani anakupenda kiasi gani?” Alifikiri kidogo akajibu, “Kiasi cha kumtoa mwanawe afe kwa ajili yangu.” “Je, unadhani, ikiwa Mungu alikupenda kiasi cha kumtoa mwanawe afe kwa ajili yako, atakuomba uache kitu chochote ambacho ni kwa faida yako kukishika?” “Hapana.” “Je, unataka kushika kitu chochote ambacho si kwa faida yako kukishika?” “Hapana.” “Basi ni afadhali uje kwa Kristo mara moja.” Naye akaja. 1 Yohana 2:17; Luka 12:16‒21 yatawaonyesha jinsi vitu wanavyojaribu kuvishika visivyo na thamani.
8. “Maisha ya Kikristo ni magumu mno.” Mwambie mtafutaji, “Niruhusu nikuonyeshe kutoka katika neno la Mungu kwamba umekosea kudhani kwamba maisha ya Kikristo ni magumu.” Kisha mgeuzie Mathayo 11:30; Mithali 3:17; Zaburi 16:11; 1 Yohana 5:3, umwonyeshe kwamba maisha ya Kikristo si magumu bali yanapendeza mno. Kisha mgeuzie Mithali 13:15, umwonyeshe kwamba ni maisha ya mwenye dhambi ndiyo yaliyo magumu.
9. “Ninawaogopa wenzangu wasiomcha Mungu;” au “Nitapoteza marafiki zangu nikimpokea Kristo.” Mithali 29:25 litawaonyesha matokeo ya kuikubali hofu ya mwanadamu, na usalama wa yule anayemtumaini Bwana. Mithali 13:20 litawaonyesha matokeo ya kuendelea kushikamana na wenzao, na Zaburi 1:1 litaonyesha heri ya kuwaacha wenzi waovu. 1 Yohana 1:3 linaonyesha jinsi ushirika anaoupata mtu kwa kuja kwa Kristo ulivyo bora sana kuliko ule anaoupoteza.
10. “Moyo wangu ni mgumu mno.” Ezekieli 36:26, 27, litawaonyesha kwamba ijapokuwa mioyo yao ni migumu kama jiwe, hilo halitaleta tofauti yoyote, kwa sababu Mungu atawapa moyo mpya.
11. “Sina hisia yoyote.” Mwulize mtafutaji anadhani ni hisia ya aina gani lazima awe nayo kabla ya kuja kwa Kristo. Ikiwa ni ile amani ambayo Wakristo huizungumzia, mwonyeshe kutoka Wagalatia 5:22; Waefeso 1:13; Matendo 5:32; 1 Petro 1:8; Mathayo 10:32, kwamba hisia hii ni matokeo ya kumpokea Kristo na kumkiri, na kwamba hawezi kuitarajia mpaka ampokee Kristo na kumkiri. Ikiwa hisia anayodhani lazima awe nayo ni hisia ya kwamba yeye ni mwenye dhambi, basi mwonyeshe kwa Isaya 55:7 kwamba kile Mungu anachokidai si hisia ya kwamba sisi ni wenye dhambi, bali ni kugeuka na kuiacha dhambi. Au, kutoka Matendo 16:31; Yohana 1:12; kwamba Mungu hatuombi tujisikie kuwa wenye dhambi, bali tukiri kwamba sisi ni wenye dhambi na tumtumaini Kristo kama Mwokozi. Isaya 55:1; Ufunuo 22:17, yatamwonyesha mtafutaji kwamba hisia pekee anayoihitaji ni kuutamani wokovu.
Hata hivyo, mara nyingi ni vema, kwa watafutaji wa aina hii, kuwaonyesha mafungu ya “Wasiojali” mpaka watakapojisikia kweli kwamba wao ni wenye dhambi.
12. “Ninamtafuta Kristo, lakini siwezi kumwona.”
Yeremia 29:13, linaonyesha kwamba tukimtafuta kwa moyo wote tutamwona. Nilipokuwa nikizungumza na mwanamke mmoja jioni moja katika mkutano wa baadaye, aliniambia, “Nimekuwa nikimtafuta Kristo kwa miaka miwili, wala siwezi kumwona.” Nikajibu, “Naweza kukwambia ni lini utamwona.” Aliniangalia kwa mshangao, nami nikageukia Yeremia 29:13, nikasoma “Nanyi mtanitafuta, na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.” “Haya,” nikasema, “hilo linakuonyesha ni lini utamwona Kristo. Utamwona utakapomtafuta kwa moyo wako wote. Je, umefanya hivyo?” Baada ya kufikiri kidogo akajibu “Hapana.” “Basi,” nikasema, “na tupige magoti hapa hapa sasa hivi.” Akafanya hivyo, na baada ya dakika chache alikuwa akifurahi katika Kristo. Waweza kumwelekeza mtu mwenye gumu hili kwa Luka 15:1‒10; 19:10. Mafungu haya yanaonyesha kwamba Yesu anamtafuta mwenye dhambi, nawe waweza kusema, “ikiwa kweli unamtafuta Kristo, haitachukua muda mrefu kwa Mwokozi anayetafuta na mwenye dhambi anayetafuta kuonana.”
13. “Siwezi kuamini.”
Katika visa vingi mtu asemapo hivi, gumu halisi lililo nyuma ya kushindwa kwake kuamini ni kutotaka kuiacha dhambi. Yohana 5:44, ni fungu zuri la kutumia kwa mtu wa namna hiyo, au Isaya 55:7. Unapotumia fungu hili la pili, mfanye mtu yule aendelee kuzingatia ukweli kwamba kitu pekee Mungu anachomwomba ni kwamba aiache dhambi na kumgeukia yeye.
14. “Mungu hatanipokea,” au “Nimeipoteza siku ya neema kwa dhambi zangu,” au “Naogopa kwamba nimetenda dhambi isiyosameheka.”
Watu wanaosema hivi kwa unyofu, kwa kawaida ndio wagumu zaidi kushughulika nao kuliko watu wa aina yoyote utakaokutana nao. Yohana 6:37, ndilo andiko kuu la kutumia kwao, kwa maana linaonyesha kwamba Yesu atampokea mtu yeyote atakayekuja kwake. Mshikilie daima katika jambo hilo, “yeye ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe” na ikiwa wanaendelea kusema “Hatanipokea” rudia andiko hilo, ukimtazamia Roho wa Mungu kuifikisha kweli moyoni. Roho nyingi zilizokata tamaa kabisa zimepata nuru na amani kupitia mstari huu katika neno la Mungu. Ufunuo 22:17, pia linafaa kwa kuwa linaonyesha kwamba mtu yeyote atakaye aweza kuyapata maji ya uzima bure. Isaya 55:1, linaonyesha kwamba mtu yeyote anayeutamani wokovu aweza kuupata. Isaya 1:18, linaonyesha kwamba hata dhambi za mtu ziwe kubwa namna gani, bado msamaha upo hapa. Matendo 10:43, na Yohana 3:16, kwamba “kila mtu” atakayemwamini Kristo atapata msamaha na uzima wa milele. Warumi 10:13, linaonyesha kwamba mtu yeyote, hata awe nani au awe wa namna gani, “atakayeliitia jina la Bwana ataokoka.” Wakati mwingine ni vema kugeukia Waebrania 6:4‒6, na Mathayo 12:31‒32, na kumwonyesha mtafutaji hasa dhambi isiyosameheka ni nini na matokeo yake ni nini. Mathayo 12:31, 32, linaonyesha kwamba ni kumkufuru Roho Mtakatifu, nawe umwulize waziwazi, “je, umewahi kumkufuru Roho Mtakatifu?” Waebrania 6:4‒6, linaonyesha kwamba tatizo haliko katika kutotaka kwa Mungu kusamehe, bali katika kutotaka kwa mtu kutubu, na kwamba mtu yeyote anayejali wokovu wake ni dhahiri hajatenda dhambi isiyosameheka wala hajaipoteza siku yake ya neema kwa dhambi. Mafundisho kidogo katika mwelekeo huu mara nyingi ndiyo yote yanayohitajika.
15. “Imechelewa mno.”
Mtafutaji asemapo hivi, mara nyingi ni vema kutumia 2 Wakorintho 6:2, na kumwambia kwamba Mungu asema, huu ndio wakati hasa. Luka 23:39‒43, linafaa kwa kuonyesha kwamba hata saa ya mwisho Yesu atakisikiliza kilio cha mwenye dhambi. 2 Petro 3:9, litaonyesha kwamba mapenzi yake ni kwamba mtu yeyote asipotee, bali kwamba anaikawisha hukumu ili apate kuwaokoa wengi kadiri watakavyokuja. Kumbukumbu la Torati 4:30, 31, ni fungu linalosaidia hasa kwa kuwa linasema “Hata katika siku za mwisho” ukimrudia Bwana atakurehemu. Isaya 1:18, na Ufunuo 22:17, yanaweza kutumika hapa peke yake.