Jinsi ya Kuwaleta Watu kwa Kristo
Ubatizo wa Roho Mtakatifu

Sura 13 · dakika 16 za kusoma · dakika 21 za kusikiliza

Ubatizo wa Roho Mtakatifu

Kuna sharti moja la kufanikiwa katika kuwaleta watu kwa Kristo lililo la umuhimu mkuu sana, tena lisiloeleweka kwa kiasi kikubwa, hata linastahili sura yake peke yake. Nakusudia Ubatizo wa Roho Mtakatifu. Katika Matendo 1:5; Luka 24:49 (linganisha Matendo 1:8), na Matendo 2:4, tuna maneno matatu; “kubatizwa katika Roho Mtakatifu,” “kuvikwa uwezo utokao juu” na “kujazwa Roho Mtakatifu.” Kwa kulinganisha kwa makini mafungu haya na mengine yanayohusiana nayo tutaona kwamba maneno haya mbalimbali yanarejea uzoefu mmoja ule ule. Uzoefu huu, kama tutakavyoona tunapoendelea kujifunza somo hili, ni sharti la lazima kabisa la utumishi ukubalikao na wenye matokeo kwa ajili ya Kristo.

1. Ubatizo wa Roho Mtakatifu ni nini?

1. Ni kazi dhahiri na ya pekee ya Roho Mtakatifu ambayo mtu aweza kujua kama imetendeka ndani yake au la. Jambo hili ni wazi kutokana na ukweli kwamba Yesu aliwaagiza wanafunzi wake wakae Yerusalemu mpaka wawe wamepokea kuvikwa huku uwezo, (Luka 24:49, linganisha Matendo 1:8), na kama isingekuwa kazi dhahiri na ya pekee ambayo wangeweza kujua kama wameipokea au la, bila shaka wasingejua ni lini amri hii ya Kristo imetimizwa na ni lini walikuwa tayari kuanza kushuhudia kwao.

2. Ni kazi ya Roho Mtakatifu iliyo tofauti na kazi yake ya kuzaa upya. Jambo hili laonekana katika Matendo 1:5, ambapo wanafunzi wanaambiwa “ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache.” Lakini kutoka Yohana 15:3; 13:10 twajifunza kwamba wanafunzi walikuwa tayari wamezaliwa upya. Laonekana pia katika Matendo 8:15, 16 ambapo twaambiwa habari za watu fulani waliokuwa wamekwisha kuamini na kubatizwa kwa maji, lakini ambao Roho Mtakatifu alikuwa bado hajawashukia. Jambo lilo hilo laonyeshwa na Matendo 19:1‒6, ambapo twaambiwa habari za watu fulani waliokuwa wanafunzi, lakini ambao hawakuwa wamempokea Roho Mtakatifu tangu walipoamini. Basi mtu aweza kuzaliwa upya na Roho Mtakatifu bila kubatizwa kwa Roho Mtakatifu. Mtu wa namna hiyo ameokoka lakini bado hajastahilishwa kwa utumishi. Kila mwamini anaye Roho Mtakatifu, Warumi 8:9, lakini si kila mwamini aliye na Ubatizo wa Roho Mtakatifu, (Matendo 8:12‒16; 19:1‒2). Tutaona hivi karibuni kwamba kila mwamini aweza kuwa na ubatizo wa Roho Mtakatifu.

3. Ubatizo wa Roho Mtakatifu sikuzote huhusiana na ushuhuda au utumishi, (tazama 1 Wakorintho 12:4‒13; Matendo 1:5‒8; Luka 24:49; Matendo 2:4; 4:8, 31; 7:55; 9:17, 20; 10:45‒46; 19:6.) Ubatizo wa Roho Mtakatifu hauna uhusiano wa moja kwa moja na kusafishwa dhambi. Hili ni jambo muhimu la kukumbuka kwa sababu nyingi. Kuna mkondo wa mafundisho juu ya somo hili unaowafanya watu watazamie kwamba wakipokea Ubatizo wa Roho Mtakatifu, asili ya kale ya kimwili itang’olewa kabisa. Hakuna hata mstari mmoja wa Maandiko unaounga mkono msimamo huu. Kama ilivyosemwa hapo juu, na kama mtu yeyote aweza kujifunza mwenyewe akichunguza mafungu yote ambamo ubatizo wa Roho Mtakatifu umetajwa, sikuzote huhusiana na ushuhuda na utumishi. Kwa hakika huandamana na kuinuliwa kukubwa kimaadili na kiroho, tena hutanguliwa, kama tutakavyoona, na kujisalimisha kabisa kwa nia kwa Kristo, lakini kusudi lake la kwanza na la moja kwa moja ni kumwezesha mtu kwa ajili ya utumishi. Tutapata wazo lililo dhahiri zaidi la Ubatizo wa Roho Mtakatifu ni nini, tukiangalia udhihirisho wake na matokeo yake kama yalivyoelezwa katika Biblia. (a.) Tuangalie kwanza fungu linaloingia kwa undani zaidi katika somo hili, 1 Wakorintho 12:4‒13. Twaona mara moja kwamba udhihirisho au matokeo ya Ubatizo wa Roho Mtakatifu si sawa kabisa katika watu wote. Kwa mfano, Ubatizo wa Roho Mtakatifu hautamfanya kila mmoja anayeupokea kuwa mhubiri wa injili au mwalimu aliyefanikiwa. Huenda akapewa karama tofauti kabisa. Ukweli huu mara nyingi husahaulika, na matokeo yake ni kukata tamaa sana na shaka. Udhihirisho au matokeo hutofautiana kulingana na nyanja za utumishi ambazo Mungu amewaitia watu mbalimbali. Mmoja hupokea karama ya mhubiri wa injili, mwingine ya mwalimu, mwingine ya uongozi, mwingine ya msaidizi, mwingine ya mama, (1 Wakorintho 12:28‒31; Waefeso 4:8, 11.) (b.) 1 Wakorintho 12:7, 11. Kutakuwa na karama fulani katika kila kisa. Si karama ile ile bali karama fulani, ya mhubiri wa injili, au ya mchungaji, au ya mwalimu au nyingine. (c.) 1 Wakorintho 12:11. Roho Mtakatifu Mwenyewe ndiye aamuaye karama au karama zipi atakazompa kila mtu. Si juu yetu kujichagulia mahali fulani pa utumishi kisha kumwomba Roho Mtakatifu atustahilishe kwa utumishi huo, wala si juu yetu kujichagulia karama fulani, kisha kumwomba Roho atupe karama hiyo. Ni juu yetu kujiweka kabisa mikononi mwa Roho Mtakatifu ili atutume po pote “apendapo,” katika nyanja yoyote ya utumishi “apendayo” (Matendo 13:2,) na kutupa karama yoyote “apendayo.” Yeye ndiye mtawala kabisa, na mahali petu panapotupasa ni kujisalimisha kwake kabisa bila masharti. Hapa ndipo wengi hukosa baraka na kukutana na kukata tamaa. Namjua mtu mmoja mnyofu sana na mwenye kujitoa sana aliyeacha biashara yenye faida kubwa akaingia katika kazi ya mhubiri wa injili. Alikuwa amesikia habari za Ubatizo wa Roho Mtakatifu; na alikuwa ameongozwa kudhani kwamba, akiupokea, ungemstahilisha kwa kazi ya mhubiri wa injili. Mtu huyo alisafiri zaidi ya maili elfu nne kuja nchi hii, lakini kazi haikumfungukia. Alikuwa katika fadhaa kubwa na shaka mpaka alipoongozwa kuona kwamba haikuwa juu yake kujichagulia kazi ya mhubiri wa injili, ingawa kazi hiyo ni njema, kisha kumtazamia Roho Mtakatifu amstahilishe kwa kazi hii aliyojichagulia. Akajitoa ili atumwe katika kazi yoyote ambayo Roho angependa. Katika kazi ile aliyotumwa uwezo wa Roho ukamjia juu yake, naye akapokea karama hii hii ya mhubiri wa injili aliyokuwa ameitamani. (d.) Matendo 1:5, 8. Ubatizo wa Roho Mtakatifu sikuzote hutoa nguvu kwa ajili ya utumishi, ule utumishi ambao Mungu atuitia. Katika mji mmoja palikuwa na kijana asiye na elimu aliyeongozwa kwa Kristo. Katika kazi yake duni sana alianza kumshuhudia Yesu. Akaendelea hatua kwa hatua katika kazi ya Kristo. Nilielekezwa kwake na bwana mmoja aliyejali habari zake, aliyesema kwamba angependa nikutane naye. Bwana huyo akamleta Chicago, nami nikamkaribisha usiku mmoja aseme katika mojawapo ya mahema yetu. Hema hilo lilikuwa katika mtaa mgumu mno. Katika hema hilo hilo kundi la wafanya fujo lililojipanga liliwahi kuja kuuvuruga mkutano. Ulikuwa umati mgumu kuushika. Kijana yule alianza kwa namna iliyonionekea kuwa ya kawaida sana, nami nikaogopa kwamba nimekosea kumwalika aseme, lakini niliomba na kuutazama umati. Hapakuwa na kitu cha ajabu katika hotuba yake alipokuwa akiendelea—isipokuwa sarufi mbovu. Lakini niliona kwamba watu wote walikuwa wakisikiliza. Wakaendelea kusikiliza mpaka mwisho. Nilipouliza kama yuko mtu yeyote aliyetaka kumpokea Kristo, watu walisimama katika sehemu mbalimbali za hema kuonyesha kwamba walitaka. Nikiyatafakari yote, nilimweleza habari hizo mtu mmoja aliyekuwa amemjua msemaji yule hapo awali. “Ndivyo ilivyo kila aendako” lilikuwa jibu. Maelezo yake yalikuwa nini? Kijana huyu asiye na elimu alikuwa amepokea Ubatizo wa Roho Mtakatifu na alikuwa amepokea nguvu. Usiku mmoja mwishoni mwa hotuba juu ya Ubatizo wa Roho Mtakatifu, mchungaji mmoja alinijia jukwaani akasema: “Nahitaji nguvu hizi, je! hutaniombea?” “Tupige magoti hapa hapa sasa hivi,” nilijibu, nasi tukafanya hivyo. Majuma machache baadaye nilikutana na bwana mmoja aliyekuwa amesimama karibu. “Je! wakumbuka,” alisema “yule mchungaji uliyeomba pamoja naye huko New Britain. Alirudi kanisani kwake; kanisa lake hujaa tele jioni za Jumapili, sehemu kubwa ya wasikilizaji ni vijana wa kiume na watu wanaongoka kwake mfululizo.” Alikuwa amepokea Ubatizo wa Roho Mtakatifu na “nguvu.” (e.) Matendo 4:29‒31. Ubatizo wa Roho Mtakatifu sikuzote hutoa ujasiri katika ushuhuda na utumishi. Petro ni mfano mashuhuri wa jambo hili. Linganisha Petro katika Matendo 4:8‒12 na Petro katika Marko 14:66‒72. Huenda mtu fulani asomaye kitabu hiki ana tamaa kubwa ya kusema na wengine na kuwavuta kwa Kristo, lakini woga usioshindika unasimama njiani. Ukipata tu Ubatizo wa Roho Mtakatifu, hayo yote yatashindwa.

Sasa tuko katika nafasi ya kuufafanua ubatizo wa Roho Mtakatifu. Ubatizo wa Roho Mtakatifu, ni Roho wa Mungu kumshukia mwamini, kuzimiliki nguvu zake za utu, kumpa karama zisizo zake kwa asili, bali zimstahilishazo kwa ajili ya utumishi ambao Mungu amemwitia.

2. Ulazima wa ubatizo wa Roho Mtakatifu kama maandalizi kwa kazi ya Kikristo.

(1.) Katika Luka 24:49. Yesu aliwaagiza mitume wakae Yerusalemu mpaka “wavikwe uwezo utokao juu.” Watu hawa walikuwa wameteuliwa kuwa mashahidi wa maisha, mauti na ufufuo wa Kristo. (Luka 24:45‒48. Matendo 1:22; 10:39‒41.) Walikuwa wamepokea kile ambacho kingeonekana kuwa mafunzo bora kabisa na ya kutosha kwa kazi hii. Kwa zaidi ya miaka mitatu walikuwa wamesoma chini ya mwalimu aliye bora kuliko wote, Yesu Mwenyewe. Walikuwa mashahidi wa macho wa miujiza yake, mauti yake, kuzikwa kwake, ufufuo wake na kupaa kwake. Lakini bado kitu kimoja kilihitajika. Na hitaji hili lilikuwa la umuhimu mkuu kiasi kwamba Yesu hangewaruhusu kuiingia kazi waliyoteuliwa mpaka hitaji hilo litimizwe. Hitaji hilo lilikuwa Ubatizo wa Roho Mtakatifu. Ikiwa mitume, pamoja na maandalizi yao yasiyo na kifani kwa ajili ya utumishi, hawakuruhusiwa kuuingia utumishi huo mpaka mafunzo yao mengine yote yaongezewe Ubatizo wa Roho Mtakatifu, ni kujidai kwa ujasiri kulioje kwa yeyote kati yetu, wenye mafunzo duni kuliko yao, kuthubutu kufanya hivyo. Lakini haya sio yote, hata Yesu Mwenyewe hakuiingia huduma yake mpaka alipotiwa mafuta kwa namna ya pekee kwa Roho Mtakatifu na nguvu. (Matendo 10:38, linganisha Luka 3:22 na 4:1, 14). Ubatizo huu ni maandalizi ya lazima kabisa kwa kazi ya Kikristo. Ni ama kutojua matakwa yaliyo wazi ya neno la Mungu au kujidai kwa ujasiri mkubwa kabisa kwa upande wetu tunapojaribu kufanya kazi kwa ajili ya Kristo kabla hatujajua kwamba tumebatizwa kwa Roho Mtakatifu.

(2.) Ni pendeleo la kila mwamini kubatizwa kwa Roho Mtakatifu. Jambo hili laonekana katika Matendo 2:39, “Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjilie.” Mazingira ya maneno, matumizi ya neno “ahadi” katika sura hii na ile itanguliayo (sura 1:4; 2:16, 33.) na matumizi ya maneno “kipawa cha Roho Mtakatifu” katika kitabu chote, yote yathibitisha bila shaka yoyote kwamba “ile ahadi” ya mstari huu ni ahadi ya Ubatizo wa Roho Mtakatifu; na mstari huu watuambia kwamba ahadi hii ni kwa ajili ya wote katika zama zote za historia ya kanisa ambao Mungu atawaita wamjilie, yaani kwa ajili ya kila mwamini. Kama hatuna ubatizo huu ni kosa letu wenyewe. Ni kwa ajili yetu, nasi tunawajibika mbele za Mungu kwa kazi yote ambayo tungeweza kuifanya, na roho zote ambazo tungeweza kuzivuta kama tungebatizwa hivyo, nasi tuna hatia kwa kadiri ambayo kazi haikufanyika na roho hazikuvutwa.

3. Twawezaje kuupata Ubatizo wa Roho Mtakatifu?

Sasa twafikia swali la vitendo: twawezaje kuupata Ubatizo huu wa Roho Mtakatifu ambao ni wa lazima kabisa katika kazi yetu kwa ajili ya Kristo? Kwa furaha jibu la swali hili limeelezwa wazi kabisa katika Biblia.

(1) “Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu” (Matendo 2:38) Hatua ya kwanza kuelekea kuupata Ubatizo huu ni toba. Toba maana yake ni “badiliko la nia,” badiliko la nia kuhusu dhambi, kuhusu Mungu, na katika kisa hiki hasa (kama mazingira ya maneno yanavyoonyesha) badiliko la nia kuhusu Kristo. Badiliko halisi la nia la namna inayoongoza kwenye tendo—kugeuka kwetu kuacha dhambi yote, kugeuka kwetu kumwelekea Mungu, kugeuka kwetu kutoka kumkataa Yesu Kristo hadi kumpokea. Hatua ya pili ni kuungama kwamba tumeikataa dhambi na kumpokea Yesu Kristo, kwa njia aliyoiamuru Mungu, yaani kwa ubatizo kwa jina la Yesu Kristo. Ubatizo wa Roho Mtakatifu katika kisa kimoja angalau (Matendo 10:44‒48) ulitangulia ubatizo wa maji, lakini hiki kilikuwa dhahiri kisa cha pekee, na Mungu asema “Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu,” (Matendo 2:38.)

(2) “Roho Mtakatifu, ambaye Mungu amewapa wale wamtiio.” (Matendo 5:32). Sharti la kupewa Roho Mtakatifu lililotajwa hapa ni kwamba “tumtii.” Utii maana yake ni zaidi ya kufanya tu baadhi ya mambo ambayo Mungu atuamuru kufanya. Maana yake ni kujisalimisha kabisa kwake kwa nia zetu, nafsi zetu na vyote tulivyo navyo. Maana yake ni kwamba twaja kwake na kusema kutoka moyoni, “mimi hapa, mimi ni wako, ulininunua kwa thamani, nakiri umiliki wako. Unitwae, unitendee upendavyo, unipeleke po pote upendapo, unitumie kama upendavyo.” Kujitoa huku kabisa kwa Mungu ndilo sharti la kupokea kwetu Ubatizo wa Roho Mtakatifu, na ni mahali hapa ndipo wengi hukosa baraka hii. Mwishoni mwa kongamano moja bwana mmoja aliharakisha kuja jukwaani akasema kwamba palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa katika dhiki kubwa aliyetaka kusema nami. Ilipita saa moja kabla sijaweza kumfikia, lakini nilimkuta bado katika mateso makuu ya moyo kwa sababu ya ukali wa tamaa yake ya Ubatizo wa Roho Mtakatifu. Wengine walikuwa wamesema naye lakini ilionekana haikumsaidia kitu. Niliketi nyuma yake nikasema, “Je! nia yako imesalimishwa kabisa?” Hakujua. “Wataka kuwa mtendakazi wa Kikristo, sivyo?” “Naam.” “Je! u tayari kurudi Baltimore na kuwa msichana wa kutumikia kama ni mapenzi ya Mungu?” “Hapana!” “Hutaipokea kamwe baraka hii mpaka nia yako mwenyewe iwekwe chini kabisa.” “Siwezi kuiweka chini.” “Je! ungependa Mungu akuwekee chini?” “Naam.” “Basi, tumwombe afanye hivyo.” Tukaomba, akaisikia sala, nia ikawekwa chini, Ubatizo wa Roho Mtakatifu ukapokelewa, naye akatoka kanisani akifurahi.

Utii maana yake pia ni kufanya katika mambo yote, makubwa na madogo, mapenzi ya Mungu kama yalivyofunuliwa katika Neno lake au kwa Roho wake. Kukataa kokote kufanya lile ambalo Mungu atuamuru kufanya, kufanya kokote kwa kujua lile ambalo atukataza kufanya, hata katika mambo madogo sana, kwatosha kutufungia nje ya baraka hii. Ikiwa kuna jambo lolote, hata liwe dogo kiasi gani, linalotujia mbele yetu kutusumbua tunapoomba juu ya jambo hili, twapaswa kulitengeneza na Mungu mara moja. Bwana Finney anasimulia habari za mwanamke mmoja ambaye, katika dhiki kubwa, aliomba kwa siku nyingi apate Ubatizo wa Roho Mtakatifu lakini hakupata jibu. Mwishowe, alipokuwa akiomba usiku mmoja, aliweka mkono wake kichwani akaondoa pambo fulani dogo lililokuwa likimjia mbele yake sikuzote alipoomba, akalitupa mbali. Mara moja akaipokea baraka aliyokuwa ameitamani kwa muda mrefu. Lilionekana jambo dogo sana, lakini lilikuwa jambo la mabishano kati yake na Mungu, nalo liliizuia baraka.

(3.) “Je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?” (Luka 11:13.)

(a.) Ni lazima pawe na sala dhahiri kwa ajili ya Ubatizo huu. Mara nyingi husemwa kwamba Roho Mtakatifu yuko hapa tayari na kwamba kila mwamini anaye Roho, kwa hiyo hatupaswi kumwombea Roho Mtakatifu. Hoja hii haizingatii tofauti iliyopo kati ya kuwa na Roho Mtakatifu na kuwa na kazi hii mahususi ya Roho Mtakatifu. (tazama 1. 2.) Tena inapingana na fundisho lililo wazi la neno la Mungu kwamba yeye huwapa “Roho Mtakatifu hao wamwombao.” Zaidi ya hayo, udanganyifu wake unaonyeshwa na ukweli kwamba Ubatizo wa Roho Mtakatifu katika kitabu cha Matendo ulitolewa daima pamoja na sala na kwa kuitikia sala. (Matendo 1:14; 2:1‒4; 4:31; 8:15,17.)

(b.) Sala hudokeza tamaa. Hakuna sala ya kweli kwa ajili ya Ubatizo wa Roho isipokuwa pana tamaa ya ndani kwa ajili yake. Maadamu mtu adhani kwamba aweza kuendelea kwa namna fulani bila baraka hii, hana uwezekano wa kuipata; lakini mtu afikapo mahali ambapo anahisi kwamba ni lazima awe nayo hata igharimu nini, yuko mbali katika njia ya kuipokea. Wachungaji wengi wa injili na watendakazi wengine wamefikishwa mahali ambapo wamehisi kwamba hawawezi kuendelea na huduma yao bila kipawa hiki, na ndipo kipawa kimefuata upesi na tabia ya kazi yao imebadilishwa kabisa.

(c.) Ili sala iwe na matokeo ni lazima iwe katika imani (Marko 11:24). Yakobo asema kuhusu sala ya kuomba hekima, “Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Mtu kama huyo asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.” (Yakobo 1:6, 7.) Kanuni hiyo hiyo, bila shaka, hushika kuhusu sala ya kumwomba Roho Mtakatifu. Ni mahali hapa hapa ndipo wengi hukosa baraka. Jinsi ya kumkaribia Mungu kwa imani kunafundishwa wazi katika 1 Yohana 5:14, 15. “Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho cho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.” Tunapomwomba Ubatizo wa Roho Mtakatifu twajua kwamba tumeomba kitu sawasawa na mapenzi yake, kwa maana kimeahidiwa waziwazi katika neno lake. Kwa hiyo twajua kwamba “atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, twajua kwamba tunazo zile haja” tulizomwomba. Basi mara nijuapo kwa hakika kwamba nimetimiza masharti yaliyotajwa hapo juu ya kupewa Roho Mtakatifu, na kumwomba Mungu kipawa hicho, nina haki ya kuihesabu baraka hii kuwa yangu—sala imesikiwa nami ninayo haja niliyomwomba—na kuinuka na kuingia kazini kwangu nikiwa na uhakika kwamba katika kazi yangu nguvu za Roho zitaonekana. “Lakini,” mtu fulani atasema, “je! tusitazamie udhihirisho wowote?” Naam, lakini wapi? Katika utumishi. Nijuapo kwa mamlaka ya neno la Mungu kwamba sala yangu imesikiwa, nina haki ya kuuingia utumishi wowote anaoniitia na kutazamia kwa uhakika udhihirisho wa nguvu za Roho katika utumishi huo. Ni kosa kungoja au kutafuta, kama wengi wanavyofanya, udhihirisho katika mishtuko kama ya umeme au katika uzoefu wa pekee wa hisia. Huenda vikaandamana, na mara nyingi huandamana, na Ubatizo wa Roho Mtakatifu. Lakini Biblia yatufundisha wazi (1 Wakorintho 12:4‒11) kwamba mahali pa kutafuta udhihirisho, ni katika utumishi, na udhihirisho ulio muhimu zaidi, wa kutegemewa na wa kimaandiko hupatikana katika kazi yetu. “Je! si lazima tungoje,” yaweza kuulizwa, “mpaka tujue kwamba tumepokea ubatizo wa Roho Mtakatifu?” Hakika kabisa, lakini tutajuaje? Kwa njia ile ile tunayojua kwamba tumeokoka, kwa ushuhuda wa neno la Mungu. Nijuapo kwamba nimetimiza masharti na nimeomba kipawa hiki kilicho “sawasawa na mapenzi yake” najua kwa neno la Mungu (1 Yohana 5:14, 15.) kwamba sala yangu imesikiwa, na kwamba ninayo haja niliyomwomba. Nina haki ya kuinuka bila ushahidi mwingine wowote ila ushahidi utoshelezao wote wa neno la Mungu, na kuingia katika utumishi ambao Mungu ananiitia. “Je! wanafunzi wa kwanza hawakungoja siku kumi?” yaweza kuulizwa tena. Naam, na sababu yake imetolewa wazi katika Matendo 2:1.—“Hata ilipowadia siku ya Pentekoste.” Katika mifano ya Agano la Kale siku ya Pentekoste ilikuwa imewekwa, katika mpango wa Mungu, kuwa siku ya kutolewa kwa mara ya kwanza kwa Roho Mtakatifu na ya kutolewa kwa malimbuko (kanisa), na kwa hiyo Roho Mtakatifu hangeweza kutolewa mpaka siku hiyo. (Mambo ya Walawi 23:9‒17.) Lakini Roho alipokwisha kutolewa mara moja hatuoni kipindi kirefu cha kungoja kwa upande wa wale walioitafuta baraka hii. (Matendo 4:31; 8:15, 17; 9:17, 20; 19:6.) Watu hulazimika kungoja leo, lakini ni kwa sababu tu hawajatimiza masharti, au hawaamini na kuidai baraka kwa urahisi juu ya Neno la Mungu. Mara tu tutimizapo masharti na kuidai baraka, ni yetu. (Marko 11:24) Mtoto yeyote wa Mungu aweza kukiweka chini kitabu hiki, kutimiza masharti, kuomba baraka, kuidai na kuwa nayo. Katika Shule ya Kiangazi ya Wanafunzi huko Lake Geneva, baada ya hotuba ya F. B. Meyer juu ya Ubatizo wa Roho Mtakatifu, mwanafunzi mmoja alibaki ili kuzungumza nami. Alisema kwamba alikuwa amesikia habari zake hapo awali na alikuwa akiutafuta kwa miezi lakini hakuweza kuupata. Nikaona kwamba nia yake haikuwa imesalimishwa, lakini jambo hilo lilimalizwa upesi. Ndipo nikasema, “Tupige magoti tumwombe Mungu Ubatizo wa Roho Mtakatifu.” Akafanya hivyo. Je! ombi hilo lilikuwa “sawasawa na mapenzi yake?” niliuliza. “Naam.” “Je! sala ilisikiwa?” Baada ya kusitasita kidogo, “Ni lazima ilisikiwa.” “Je! unacho ulichomwomba?” “Sihisi.” Nilisoma 1 Yohana 5:15 katika Biblia iliyokuwa wazi mbele yetu: “Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho cho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.” “Je! sala ilisikiwa?” “Naam.” “Je! unacho ulichoomba?” “Ni lazima ninacho; kwa maana Mungu asema hivyo.” Tukainuka na muda mfupi tukaachana. Niliporudi shuleni baada ya siku chache nilikutana na kijana yule tena. Uso wake sasa ulikuwa uking’aa, naye alijua kwamba amepokea kile ambacho mwanzoni alikitwaa juu ya neno tupu la Mungu.

4. Kurudiwa kwa Ubatizo wa Roho Mtakatifu.

Jambo moja zaidi lahitaji kusemwa kabla hatujaliacha somo hili. Ubatizo wa Roho Mtakatifu ni uzoefu unaohitaji kurudiwa mara kwa mara. Jambo hili laonekana kwa kulinganisha Matendo 2:4—ambapo Petro pamoja na wengine alijazwa Roho Mtakatifu—na Matendo 4:8.—ambapo Petro alijazwa tena,—na Matendo 4:31 ambapo Petro pamoja na wengine alijazwa tena mara nyingine. Jaza jipya lahitajika, nalo lapaswa kutafutwa, kwa kila dharura mpya ya utumishi wa Kikristo. Wako wengi ambao wakati fulani walijua kwa uzoefu maana ya Ubatizo wa Roho Mtakatifu, ambao leo wanajaribu kufanya kazi katika nguvu za uzoefu ule wa zamani, nao wanafanya kazi bila Mungu. Wanahitaji, tena ni lazima wapate, Ubatizo mpya kabla Mungu hajaweza kuwatumia.

Iliyotangulia