Sura 2 · dakika 7 za kusoma
Yesu Peke Yake.
Hatuwezi, kwa mara nyingi au kwa uwazi wa kutosha, kumwambia nafsi itafutayo kwamba tumaini lake pekee la wokovu liko katika Bwana Yesu Kristo. Liko ndani yake kikamilifu, peke yake, na yeye tu. Ili kuokoa kutokana na hatia na nguvu ya dhambi pia, Yesu anatosha kabisa. Jina lake anaitwa Yesu, kwa sababu "yeye atawaokoa watu wake na dhambi zao." "Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani ya kusamehe dhambi." Ametukuzwa juu "ili awape toba na msamaha wa dhambi." Ilimpendeza Mungu tangu zamani kubuni njia ya wokovu ambayo yote ingekuwemo ndani ya Mwanawe pekee. Bwana Yesu, kwa ajili ya kutimiza wokovu huu, alifanyika mwanadamu, na alipoonekana ana umbo la mwanadamu, alijitiisha hata kufa, naam, kifo cha msalaba. Kama njia nyingine ya ukombozi ingewezekana, kikombe cha uchungu kingempita. Ni jambo la akili kwamba mpendwa wa mbingu asingekufa ili kutuokoa kama tungeweza kuokolewa kwa gharama ndogo zaidi. Neema isiyo na mwisho iliandaa dhabihu kuu; upendo usio na mwisho ulijitiisha hata kufa kwa ajili yetu. Tuwezaje kuota kwamba yaweza kuwapo njia nyingine zaidi ya njia ile ambayo Mungu ameiandaa kwa gharama kubwa namna hiyo, na kuiweka wazi katika Maandiko Matakatifu kwa urahisi na kwa msisitizo namna hiyo? Hakika ni kweli kwamba "Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote; kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo."
Kudhani kwamba Bwana Yesu amewaokoa wanadamu nusu tu, na kwamba yahitajika kazi au hisia fulani yao wenyewe ili kuikamilisha kazi yake, ni uovu. Kuna nini chetu ambacho kingeweza kuongezwa kwenye damu yake na haki yake? "Matendo yetu yote ya haki ni kama nguo iliyotiwa unajisi." Je, haya yaweza kubandikwa kwenye kitambaa cha thamani cha haki yake ya kimungu? Matambara na kitani safi nyeupe! Takataka zetu na dhahabu yake safi! Ni tusi kwa Mwokozi kuota jambo kama hilo. Tumetenda dhambi za kutosha, bila kuongeza hili kwenye makosa yetu mengine yote.
Hata kama tungekuwa na haki yoyote ambayo tungeweza kujivunia; kama majani yetu ya mtini yangekuwa mapana kuliko kawaida, na yasiyonyauka kabisa, ingekuwa hekima kuyaweka mbali, na kuipokea haki ile ambayo lazima impendeze Mungu zaidi sana kuliko chochote chetu wenyewe. Lazima Bwana aone kilicho cha kukubalika zaidi katika Mwanawe kuliko katika aliye bora kati yetu. Aliye bora kati yetu! Maneno haya yaonekana kama ni ya kejeli, ingawa hayakukusudiwa hivyo. Kuna ubora gani juu ya yeyote kati yetu? "Hakuna atendaye mema; la, hata mmoja." Mimi niandikaye maneno haya, ningekiri kwa uhuru kabisa kwamba sina hata uzi mmoja wa wema wangu mwenyewe. Nisingeweza kutengeneza hata tambara, wala kipande cha tambara. Mimi ni maskini kabisa. Lakini kama ningekuwa na vazi zuri kabisa la matendo mema ambalo hata kiburi kingeweza kuwazia, ningelirarua ili nisivae kitu kingine ila mavazi ya wokovu, ambayo hutolewa bure na Bwana Yesu, kutoka katika ghala la mbinguni la sifa zake mwenyewe.
Ni jambo la kumtukuza sana Bwana wetu Yesu Kristo kwamba tutumaini kila kitu chema kutoka kwake yeye peke yake. Hii ndiyo kumtendea kama anavyostahili kutendewa; kwa maana kwa kuwa yeye ni Mungu, na zaidi yake hakuna mwingine, twapaswa kumtazama yeye na kuokoka.
Hii ndiyo kumtendea kama apendavyo kutendewa, kwa maana huwaita wote wanaotaabika na wenye kulemewa na mizigo waje kwake, naye atawapumzisha. Kudhani kwamba hawezi kuokoa kabisa kabisa ni kumwekea mipaka yeye Mtakatifu wa Israeli, na kuidharau nguvu zake; au sivyo ni kuukashifu moyo wa upendo wa Rafiki wa wenye dhambi, na kutia shaka juu ya upendo wake. Katika hali yoyote ile; tungetenda dhambi ya kikatili na ya kupita kiasi dhidi ya sehemu nyororo kabisa za heshima yake, ambazo ni uwezo wake na utayari wake wa kuokoa wote wanaomjia Mungu kwa njia yake.
Mtoto, aliye hatarini ya moto, humshikilia tu mzima-moto, na kumtumaini yeye peke yake. Hauliza swali lolote juu ya nguvu za viungo vyake vya kumbeba, wala juu ya bidii ya moyo wake ya kumwokoa; bali hushikilia tu. Joto ni la kutisha, moshi wapofusha macho, lakini yeye hushikilia; na mwokozi wake humpeleka salama kwa haraka. Kwa uthabiti kama huo wa kitoto mshikilie Yesu, awezaye na atakayekubeba na kukutoa katika hatari ya miali ya dhambi.
Asili ya Bwana Yesu yapaswa kutuvuvia uthabiti kamili kabisa. Kwa kuwa yeye ni Mungu, ni mwenye uwezo wote wa kuokoa; kwa kuwa yeye ni mwanadamu, amejaa utimilifu wote wa kubariki; kwa kuwa yeye ni Mungu na mwanadamu katika Nafsi moja Tukufu, humkuta mwanadamu katika hali yake ya kiumbe na Mungu katika utakatifu wake. Ngazi ni ndefu ya kutosha kufika kutoka kwa Yakobo aliyelala kifudifudi juu ya nchi, hadi kwa Yehova atawalaye mbinguni. Kuleta ngazi nyingine kungekuwa ni kudhani kwamba alishindwa kuunganisha umbali huo; na hili lingekuwa ni kumvunjia heshima vibaya sana. Ikiwa hata kuyaongezea maneno yake ni kujiletea laana juu yetu wenyewe, itakuwaje kujifanya kumwongezea yeye mwenyewe? Kumbuka kwamba yeye, mwenyewe, ndiye Njia; na kudhani kwamba lazima, kwa namna fulani, tuiongezee ile barabara ya kimungu, ni kuwa na kiburi cha kutosha hata kuwaza kumwongezea yeye. Iondoke fikira kama hiyo! Ichukie kama vile ungechukia kufuru; kwa maana kwa asili yake ni kufuru mbaya kabisa dhidi ya Bwana wa upendo.
Kumjia Yesu na bei mkononi mwetu, kungekuwa ni kiburi kisichovumilika, hata kama tungekuwa na bei yoyote ambayo tungeweza kuileta. Ana haja gani nasi? Tungeweza kuleta nini kama angekuwa na haja nayo? Je, angeziuza baraka zisizo na thamani za ukombozi wake? Kile alichokitimiza kwa damu ya moyo wake, je, angekibadilishana nasi kwa machozi yetu, na nadhiri, au kwa taratibu za kimila, na hisia, na matendo? Yeye hajashushwa hata kujifanya bidhaa ya kuuzwa: atatoa bure, kama ipasavyo upendo wake wa kifalme; lakini yeye amletaye bei hajui anashughulika na nani, wala jinsi anavyoihuzunisha vibaya Roho yake iliyo huru. Wenye dhambi wenye mikono mitupu waweza kupata watakalo. Yote wawezayo kuhitaji yamo ndani ya Yesu, naye huyatoa kwa kuyaomba tu; lakini lazima tuamini kwamba yeye ni yote katika yote, wala hatupaswi kuthubutu kutamka neno lolote juu ya kukamilisha kile alichokimaliza, au kujiandaa wenyewe kwa kile atupacho sisi tulio wenye dhambi tusiostahili.
Sababu ya sisi kuweza kutumaini msamaha wa dhambi, na uzima wa milele, kwa imani katika Bwana Yesu, ni kwamba Mungu ameamuru hivyo. Amejifunga mwenyewe katika injili kuwaokoa wote wanaomtumaini kweli Bwana Yesu, wala hatarudi nyuma kamwe kutoka katika ahadi yake. Amependezwa sana na Mwanawe pekee, hata hufurahia wote wanaomshika yeye kama tumaini lao la pekee na la kwanza. Mungu mkuu mwenyewe amemshika yeye aliyemshika Mwanawe. Hufanya wokovu kwa ajili ya wote wanaoutazamia wokovu huo kwa yule Mkombozi aliyekwisha kuchinjwa. Kwa ajili ya heshima ya Mwanawe, hatamwacha mtu anayemtumaini apate aibu. "Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele;" kwa maana Mungu aishiye milele amemtwaa kwake mwenyewe, na amempa kuwa mshiriki wa uzima wake. Ikiwa Yesu peke yake ndiye tumaini lako, huna haja ya kuogopa ila kwamba utaokolewa kwa hakika, sasa na katika siku ya kufunuliwa kwake.
Mtu anapotumaini, kunakuwa na kitovu cha muungano kati yake na Mungu, na muungano huo huhakikisha baraka. Imani hutuokoa kwa sababu hutufanya kumshikilia Kristo Yesu, naye ni mmoja na Mungu, na hivyo hutuleta katika uhusiano na Mungu. Nimeambiwa kwamba, miaka mingi iliyopita, juu ya Maporomoko ya Niagara, mashua ilipinduka, na watu wawili walikuwa wakichukuliwa chini na mkondo, wakati watu waliokuwa ufuoni walipofanikiwa kuwaelekezea kamba juu ya maji, ambayo kamba ilishikwa na wote wawili. Mmoja wao aliishika kwa nguvu, akavutwa salama hadi ukingoni; lakini yule mwingine, alipoona gogo kubwa likielea likija, kwa upumbavu aliiachia kamba, akalishikilia lile gogo kubwa la mti, kwa maana lilikuwa ni kitu kikubwa zaidi kati ya vile viwili, na kwa kuonekana lilikuwa bora zaidi kushikilia. Ole! lile gogo, pamoja na mtu aliyekuwa juu yake, likaenda moja kwa moja juu ya lile shimo kuu, kwa sababu hapakuwa na muungano kati ya mti na ufuo. Ukubwa wa gogo haukuwa na faida kwake yeye aliyelishika; ilihitajika uhusiano na ufuo ili kuleta usalama. Vivyo hivyo, mtu anapotumaini matendo yake, au maombi yake, au sadaka zake, au sakramenti, au kitu chochote cha aina hiyo, hataokoka, kwa sababu hakuna kiungo kati yake na Mungu kupitia Kristo Yesu; bali imani, ijapoonekana kama kamba nyembamba, imo mkononi mwa Mungu mkuu upande wa ufuoni; nguvu isiyo na mwisho huivuta ile kamba iunganishayo, na hivyo humvuta mtu kutoka katika uharibifu. Ee, heri ya imani, kwa sababu hutuunganisha na Mungu kwa njia ya Mwokozi, ambaye amemchagua, naam, Yesu Kristo! Ee msomaji, je, hakuna busara katika jambo hili? Lifikirie, na naam upesi uwepo mfungamano wa muungano kati yako na Mungu, kwa njia ya imani yako katika Kristo Yesu!