Karibu na Lango Jembamba ·Kuamshwa.

Sura 1 · dakika 5 za kusoma

Kuamshwa.

Watu wengi mno hawana hangaiko lolote juu ya mambo ya milele. Wanajali zaidi paka na mbwa wao kuliko roho zao. Ni rehema kuu kufanywa tuwaze juu yetu wenyewe, na jinsi tulivyosimama mbele za Mungu na ulimwengu wa milele. Mara nyingi hii ni ishara kwamba wokovu unatujia. Kwa asili hatupendi ile wasiwasi ambayo hangaiko la kiroho hutuletea, nasi hujaribu, kama walegevu, kusinzia tena. Huu ni upumbavu mkuu; kwa maana ni hatari yetu kuzembea wakati kifo kiko karibu hivyo, na hukumu ni ya hakika hivyo. Ikiwa Bwana ametuchagua kwa uzima wa milele, hatatuacha turudi usingizini mwetu. Tukiwa na busara, tutaomba kwamba wasiwasi wetu juu ya roho zetu usikome kamwe hata tuwe tumeokoka kweli kweli. Na tuseme kutoka mioyoni mwetu:—

"Yeye aliyeteseka badala yangu, Ndiye atakayekuwa Tabibu wangu; Sitafarijika, Hata Yesu anifariji."

Ingekuwa jambo la kutisha kuteremka kuzimu kama katika ndoto, na huko kuinua macho yetu hali kuna shimo kubwa lililowekwa kati yetu na mbinguni. Ni jambo la kutisha vilevile kuamshwa ili kuikimbia ghadhabu itakayokuja, kisha kuutupilia mbali ule mwelekeo wa onyo, na kurudi katika ubutu wetu. Naona kwamba wale washindao maonyo ya dhamiri zao na kuendelea katika dhambi zao hawaguswi kwa urahisi mara ya pili: kila kuamshwa kunakotupwa huiacha roho ikiwa na usingizi zaidi kuliko mbeleni, na isiyowezekana tena kuchochewa kwa hisia takatifu. Kwa hiyo moyo wetu unapaswa kufadhaishwa sana na wazo la kuondoa taabu yake kwa njia yoyote isiyo ile njia iliyo sawa. Mtu mmoja aliyekuwa na gauti aliponywa kwa dawa ya waganga wa uongo, iliyoisukuma maradhi ndani, naye mgonjwa akafa. Kuponywa taabu ya akili kwa tumaini la uongo, kungekuwa jambo la kutisha: dawa ingekuwa mbaya kuliko ugonjwa wenyewe. Ni afadhali sana kwamba wororo wa dhamiri zetu utuletee miaka mingi ya uchungu, kuliko tuupoteze, na kuangamia katika ugumu wa mioyo yetu.

Walakini kuamshwa si jambo la kupumzikia ndani yake, wala la kutamani kurefushwa mwezi baada ya mwezi. Nikiamka kwa hofu, na kuiona nyumba yangu inateketea, siketi ukingoni mwa kitanda, na kujiambia, "Natumaini nimeamshwa kweli! Naam, nashukuru sana kwamba sikuachwa niendelee kulala!" La, nataka kuikimbia mauti inayonitisha, kwa hiyo naharakisha kwenda mlangoni au dirishani, ili nipate kutoka, nisiangamie pale nilipo. Ingekuwa neema ya kutiliwa shaka kuamshwa, na hata hivyo kutoikimbia hatari. Kumbuka, kuamshwa si wokovu. Mtu aweza kujua kwamba amepotea, na hata hivyo asiokoke kamwe. Aweza kufanywa mwenye mawazo, na hata hivyo akafa katika dhambi zake. Ukijua kwamba umefilisika, kuzitafakari deni zako hakutazilipa. Mtu aweza kuzichunguza jeraha zake mwaka mzima, wala hazitakaribia kupona kwa sababu anahisi maumivu yake, na kuzihesabu idadi yake. Ni hila mojawapo ya shetani kumshawishi mtu atosheke na hisia ya dhambi; na hila nyingine ya mdanganyifu yuleyule kudokeza kwamba mwenye dhambi asiridhike kumtumaini Kristo, isipokuwa aweze kuleta kiasi fulani cha kukata tamaa ili kukiongeza kwenye kazi ya Mwokozi iliyokamilika. Kuamshwa kwetu si kwa kumsaidia Mwokozi, bali kutusaidia sisi kumwendea Mwokozi. Kudhani kwamba hisia yangu ya dhambi itasaidia katika kuiondoa dhambi ni upuuzi. Ni kana kwamba nilisema maji hayawezi kuutakasa uso wangu isipokuwa nimejitazama muda mrefu zaidi kiooni, na kuzihesabu doa juu ya paji la uso wangu. Hisia ya kuhitaji wokovu kwa neema ni ishara nzuri sana ya afya; lakini mtu ahitaji hekima kuitumia vizuri, wala si kuifanya sanamu.

Baadhi huonekana kana kwamba wamependana na mashaka yao, na hofu zao, na taabu zao. Huwezi kuwaondoa katika vitisho vyao—huonekana wameolewa navyo. Yasemekana kwamba tatizo baya kuliko yote kwa farasi wakati mabanda yao yanaungua, ni kwamba huwezi kuwatoa katika vibanda vyao. Kama wangefuata tu uongozi wako, wangeweza kuziponyoka ndimi za moto; lakini huonekana wamepooza kwa hofu. Hivyo hofu ya moto huwazuia kuukimbia moto. Wewe usomaye, je, hofu yako ya ghadhabu itakayokuja itakuzuia kuikimbia? Twatumaini sivyo.

Mtu mmoja aliyekuwa gerezani muda mrefu hakuwa radhi kutoka. Mlango ulikuwa wazi; lakini aliomba hata kwa machozi aruhusiwe kukaa pale alipokuwa muda mrefu hivyo. Kupenda gereza! Kuolewa na makomeo ya chuma na chakula cha gereza! Bila shaka mfungwa yule alikuwa amegusika kidogo kichwani! Je, wewe u radhi kubaki uliyeamshwa tu, wala si zaidi? Je, huna shauku ya kusamehewa mara moja? Ukikawia katika uchungu na hofu, bila shaka wewe pia u kichaa kidogo! Ikiwa amani yaweza kupatikana, ipate mara moja! Mbona ukawie katika giza la shimo, ambamo miguu yako inazama katika matope ya utelezi? Kuna nuru iwezayo kupatikana; nuru ya ajabu na ya kimbinguni; mbona ukae gizani na kufa katika uchungu? Hujui jinsi wokovu ulivyo karibu nawe. Kama ungejua, bila shaka ungenyosha mkono wako na kuutwaa, kwa maana upo hapo; na waweza kupatikana kwa kuutwaa tu.

Usidhani kwamba hisia za kukata tamaa zingekufaa upate rehema. Yule msafiri, alipokuwa njiani kuelekea Lango Jembamba, alipoanguka katika Bwawa la Kukata Tamaa, je, wadhani kwamba, matope machafu ya bwawa lile yalipogandamana na mavazi yake, yalikuwa sifa kwake, ili kumwezesha kuingia kwa urahisi zaidi mwanzoni mwa njia? Sivyo. Yule msafiri hakudhani hivyo hata kidogo; wala usidhani wewe. Si kile wewe unachohisi kitakachokuokoa, bali kile Yesu alichohisi. Hata kama kungekuwa na thamani fulani ya uponyaji katika hisia, zingelazimika kuwa hisia njema; na ile hisia inayotufanya tuutilie shaka uweza wa Kristo kuokoa, na kutuzuia kupata wokovu ndani yake, si njema hata kidogo, bali ni ukatili wa kuudhi upendo wa Yesu.

Rafiki yetu amekuja kutuona, naye amesafiri kupitia London yetu yenye msongamano kwa reli, au tramu, au basi. Ghafla anabadilika rangi. Twamwuliza kuna nini, naye anajibu, "Nimepoteza pochi yangu, nayo ilikuwa na fedha zangu zote nilizonazo duniani." Anahesabu kiasi hata senti moja, na kueleza hundi, bili, noti, na sarafu. Twamwambia ni lazima iwe faraja kubwa kwake kuufahamu kwa usahihi hivyo ukubwa wa hasara yake. Haonekani kuiona thamani ya faraja yetu. Twamhakikishia kwamba imempasa kushukuru kwa kuwa ana ufahamu ulio wazi hivyo wa hasara yake; kwa maana watu wengi wangaliweza kupoteza pochi zao na kuwa hawawezi kabisa kukokotoa hasara zao. Walakini rafiki yetu hafarijiki hata kidogo. "La," asema, "kujua hasara yangu hakunisaidii kuipata tena. Niambie ni wapi naweza kupata mali yangu, nawe umenitendea huduma ya kweli; lakini kujua hasara yangu tu si faraja hata kidogo." Vivyo hivyo, kuamini kwamba umetenda dhambi, na kwamba roho yako imetwaliwa na haki ya Mungu, ni jambo linalofaa sana; lakini halitaokoa. Wokovu haupatikani kwa kujua uangamivu wetu wenyewe, bali kwa kuushika kikamilifu ule ukombozi uliotolewa katika Kristo Yesu. Mtu akataaye kumtazama Bwana Yesu, bali akaendelea kukazia fikira dhambi yake na uangamivu wake, hutukumbusha mvulana aliyeangusha shilingi katika wavu wazi wa mfereji wa maji taka wa London, na kukawia pale kwa masaa mengi, akipata faraja kwa kusema, "Ilizungukia humo humo! Katikati ya vile viboriti viwili vya chuma nilipoiona ikishuka moja kwa moja." Roho maskini! Angeweza kuzikumbuka habari za hasara yake kwa muda mrefu kabla ya kuweza kwa njia hii kurudisha hata senti moja mfukoni mwake, ili ajinunulie kipande cha mkate. Waona maana ya mfano huu; ufaidike nao.


Yaliyomo

Karibu na Lango Jembamba Charles H. Spurgeon

Ukurasa 1 / 1 · 5 dakika zimebaki katika sura