Majibu ya Maombi ·Nyongeza B

Sura 4 · dakika 6 za kusoma

Nyongeza B

KUSOMA MAANDIKO MATAKATIFU KWA MAKINI NA KWA MFULULIZO

"Nilianguka katika mtego ambao waamini wengi wachanga huanguka ndani yake, yaani kusoma vitabu vya kidini badala ya Maandiko. Sikuweza tena kusoma riwaya za Kifaransa na Kijerumani, kama nilivyokuwa nikifanya zamani, ili kulisha nia yangu ya mwilini; lakini hata hivyo sikuweka mahali pa vitabu hivyo kitabu bora kuliko vyote. Nilisoma vijitabu, magazeti ya kimisionari, mahubiri, na wasifu wa watu watauwa. Aina ya mwisho ya vitabu niliiona kuwa yenye faida zaidi kuliko nyingine, na kama vingekuwa vimechaguliwa vizuri, au kama nisingesoma sana maandishi ya namna hiyo, au kama kimojawapo kingeelekea hasa kunipendezesha Maandiko, vingeweza kunifanyia mema mengi.—Sikuwahi wakati wowote maishani mwangu kuwa na desturi ya kusoma Maandiko Matakatifu. Nilipokuwa chini ya umri wa miaka kumi na mitano, mara kwa mara nilisoma kidogo cha hayo shuleni; baadaye kitabu cha thamani cha Mungu kiliwekwa kando kabisa, hata kwamba sikusoma hata sura moja yake, kadiri ninavyokumbuka, mpaka ilipompendeza Mungu kuanza kazi ya neema moyoni mwangu. Basi njia ya kufikiri kwa mujibu wa Maandiko ingekuwa hii: Mungu mwenyewe amejinyenyekeza kuwa mwandishi, nami sijui kitu kuhusu kitabu hicho cha thamani, ambacho Roho wake Mtakatifu amekifanya kiandikwe kwa kutumia watumishi wake, nacho kina yale ambayo yanipasa kuyajua, na ujuzi wake utaniongoza kwenye furaha ya kweli; kwa hiyo yanipasa kukisoma tena na tena kitabu hiki chenye thamani kuliko vyote, kitabu hiki cha vitabu, kwa bidii kubwa, kwa maombi mengi, na kwa kutafakari sana; na katika desturi hii yanipasa kudumu siku zote za maisha yangu. Kwa maana nilifahamu, ijapokuwa nilikisoma kidogo tu, kwamba sikujua karibu chochote juu yake. Lakini badala ya kutenda hivyo, na kuongozwa na kutokujua kwangu neno la Mungu ili nilisome zaidi, ugumu wangu wa kulielewa, na furaha ndogo niliyokuwa nayo ndani yake, vilinifanya nizembee kulisoma (kwa maana kusoma Neno kwa wingi na kwa maombi, hakutoi ujuzi zaidi tu, bali huongeza pia furaha tuliyo nayo katika kulisoma); na hivyo, kama waamini wengi, kwa vitendo nilipendelea, kwa miaka minne ya kwanza ya maisha yangu ya kimungu, kazi za watu wasiopuliziwa kuliko maneno ya Mungu aliye hai. Matokeo yake yalikuwa kwamba nilibaki mtoto mchanga, katika ujuzi na katika neema. Katika ujuzi nasema; kwa maana ujuzi wote wa kweli lazima upatikane, kwa Roho, kutoka katika Neno. Na kwa kuwa nililipuuza Neno, kwa muda wa karibu miaka minne nilikuwa sijui kiasi kwamba sikujua waziwazi hata mambo ya msingi ya imani yetu takatifu. Na upungufu huu wa ujuzi kwa masikitiko makubwa ulinizuia nisitembee kwa uthabiti katika njia za Mungu. Kwa maana ni kweli ndiyo itufanyayo huru, (Yohana 8:31, 32) kwa kutuokoa kutoka utumwa wa tamaa za mwili, tamaa za macho, na kiburi cha uzima. Neno linalithibitisha. Uzoefu wa watakatifu unalithibitisha; na pia uzoefu wangu mwenyewe unalithibitisha bila shaka kabisa. Kwa maana ilipompendeza Bwana mwezi Agosti 1829, kunileta kwelikweli kwenye Maandiko, maisha yangu na mwenendo wangu vilibadilika sana. Na ingawa hata tangu wakati huo nimepungukiwa sana na yale ningeweza na yanipasayo kuwa, lakini, kwa neema ya Mungu, nimewezeshwa kuishi karibu zaidi naye kuliko hapo awali.

"Ikiwa waamini wowote watasoma haya, ambao kwa vitendo wanapendelea vitabu vingine kuliko Maandiko Matakatifu, na ambao wanafurahia maandishi ya wanadamu zaidi sana kuliko neno la Mungu, na waonywe kwa hasara yangu. Nitakiona kitabu hiki kuwa kimekuwa njia ya kufanya mema mengi, ikiwa itampendeza Bwana, kupitia kwacho, kuwaongoza baadhi ya watu wake wasiyapuuze tena Maandiko Matakatifu, bali kuyapa upendeleo ule, ambao hadi sasa wameutoa kwa maandishi ya wanadamu. Kutopenda kwangu kuongeza idadi ya vitabu kungetosha kunizuia nisiandike kurasa hizi, kama nisingelisadikishwa, kwamba hii ndiyo njia pekee ambayo ndugu kwa jumla wanaweza kunufaika kupitia makosa na hitilafu zangu, na kuvutwa na tumaini, kwamba kwa kujibiwa maombi yangu, kusoma uzoefu wangu kunaweza kuwa njia ya kuwaongoza kuyathamini Maandiko zaidi, na kuyafanya kuwa kanuni ya matendo yao yote. * * *

"Kama mtu yeyote angeniuliza, jinsi anavyoweza kusoma Maandiko kwa faida zaidi, ningemshauri, kwamba:

"I.—Zaidi ya yote anapaswa kutafuta kuwa na uhakika akilini mwake, kwamba Mungu peke yake, kwa Roho wake, ndiye awezaye kumfundisha, na kwa hiyo, kwa kuwa Mungu ataombwa kwa ajili ya baraka, yampasa kutafuta baraka ya Mungu kabla ya kusoma, na pia wakati wa kusoma.

"II.—Anapaswa, tena, kuwa na uhakika akilini mwake, kwamba, ingawa Roho Mtakatifu ndiye mwalimu aliye bora na atoshaye, lakini mwalimu huyu hafundishi sikuzote papo hapo tunapotamani, na kwamba, kwa hiyo, huenda tukalazimika kumsihi tena na tena kwa ajili ya ufafanuzi wa mafungu fulani; lakini kwamba hakika atatufundisha mwishoni, ikiwa kweli tunatafuta nuru kwa maombi, kwa saburi, na kwa nia ya utukufu wa Mungu.

"III.—Ni jambo la umuhimu mkubwa kwa kulielewa neno la Mungu, kulisoma kwa mpangilio, ili kwamba tusome kila siku sehemu ya Agano la Kale na sehemu ya Agano Jipya, tukiendelea pale tulipoishia awali. Hili ni la maana—1, Kwa sababu linaangaza mwanga juu ya uhusiano; na mpango tofauti, ambao kwao mtu kwa mazoea huchagua sura fulani, utafanya isiwezekane kabisa kuelewa sehemu kubwa ya Maandiko. 2, Tukiwa katika mwili, tunahitaji mabadiliko hata katika mambo ya kiroho; na mabadiliko haya Bwana ameyaandaa kwa neema katika utofauti mkubwa unaopatikana katika neno lake. 3, Huelekea kwenye utukufu wa Mungu; kwa maana kuacha sura fulani hapa na pale, kwa vitendo ni kusema, kwamba sehemu fulani ni bora kuliko nyingine: au, kwamba kuna sehemu fulani za kweli iliyofunuliwa zisizo na faida au zisizohitajika. 4, Yaweza kutuhifadhi, kwa baraka ya Mungu, kutokana na maoni yenye makosa, kwani kwa kusoma hivyo kwa ukawaida katika Maandiko yote tunaongozwa kuona maana ya jumla, na pia tunahifadhiwa tusikaze mno maoni fulani tunayoyapenda. 5, Maandiko yana mapenzi yote ya Mungu yaliyofunuliwa, na kwa hiyo yatupasa kutafuta kusoma mara kwa mara katika mapenzi hayo yote yaliyofunuliwa. Kuna waamini wengi, nachelea, katika siku zetu, ambao hawajasoma hata mara moja Maandiko yote; na hata hivyo katika miezi michache, kwa kusoma sura chache tu kila siku wangeweza kuyakamilisha.

"IV.—Pia ni jambo la umuhimu mkubwa kutafakari juu ya yale tusomayo, ili kwamba labda sehemu ndogo ya yale tuliyosoma, au, kama tuna wakati, yote yaweze kutafakariwa katika mwendo wa siku. Au sehemu ndogo ya kitabu, au ya waraka, au ya injili, ambayo tunaipitia kwa ukawaida kwa ajili ya kutafakari, yaweza kutafakariwa kila siku, bila, hata hivyo, kujiacha kuletwa katika utumwa na mpango huu.

"Vitabu vya ufafanuzi vya kitaaluma nimeona kwamba hujaza kichwa, kwa dhana nyingi na mara nyingi pia kwa kweli ya Mungu; lakini Roho afundishapo, kupitia maombi na kutafakari, moyo huguswa. Aina ya kwanza ya ujuzi kwa kawaida hujivuna, na mara nyingi hukanushwa, wakati kitabu kingine cha ufafanuzi kinapotoa maoni tofauti, na mara nyingi pia hukutwa hakifai kitu, wakati kinapopaswa kutekelezwa kwa vitendo. Aina ya pili ya ujuzi kwa kawaida hunyenyekesha, hutoa furaha, hutuongoza karibu zaidi na Mungu, na haitolewi kirahisi kwa hoja; na kwa kuwa umepatikana kutoka kwa Mungu, na hivyo kuingia moyoni, na kuwa mali yetu, kwa kawaida pia hutekelezwa."


Yaliyomo

Majibu ya Maombi George Müller

Ukurasa 1 / 1 · 6 dakika zimebaki katika sura