Sura 8 · dakika 20 za kusoma
Kulindwa kwa Nguvu za Mungu
Maneno ninayoyazungumzia utayapata katika 1 Petro 1:5. Mistari ya tatu, ya nne na ya tano ni: “Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye . . . alituzaa mara ya pili kwa tumaini lililo hai kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu, tupate urithi usioharibika . . . uliohifadhiwa mbinguni kwa ajili yenu ninyi mnaolindwa kwa nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu.” Maneno ya andiko langu ni: “Mnaolindwa kwa nguvu za Mungu kwa njia ya imani.”
Hapo tunapata kweli mbili za ajabu na zilizobarikiwa kuhusu ulinzi ambao kwao mwaminifu analindwa hata apate wokovu. Kweli moja ni, Kulindwa kwa nguvu za Mungu; na kweli nyingine ni, Kulindwa kwa njia ya imani. Imetupasa kuziangalia pande mbili—upande wa Mungu na nguvu zake za uweza wote, zinazotolewa kwetu ili awe Mlinzi wetu kila dakika ya siku; na upande wa mwanadamu, ambapo hatuna la kufanya isipokuwa kwa imani kumwacha Mungu aifanye kazi yake ya kulinda. Tumezaliwa mara ya pili tupate urithi uliohifadhiwa Mbinguni kwa ajili yetu; nasi tunalindwa hapa duniani kwa nguvu za Mungu. Twaona kuna ulinzi maradufu—urithi uliohifadhiwa kwa ajili yangu Mbinguni, na mimi hapa duniani nikilindwa kwa ajili ya urithi ulioko huko.
Basi, kwa habari ya sehemu ya kwanza ya ulinzi huu, hakuna shaka wala swali. Mungu anaulinda urithi Mbinguni kwa namna ya ajabu na kamili, nao unangoja huko salama. Na Mungu yuleyule ananilinda mimi kwa ajili ya urithi. Hilo ndilo nitakalo kulielewa.
Wajua ni upumbavu mkubwa kwa baba kujitaabisha sana kuwa na urithi kwa ajili ya watoto wake, na kuuhifadhi kwa ajili yao, ikiwa hawahifadhi wao kwa ajili yake. Ungemwaza nini mtu anayetumia wakati wake wote na kujitolea kila dhabihu kukusanya fedha, na apatapo makumi yake ya maelfu, ukamwuliza kwa nini anajitolea hivyo, naye ajibu: “Nataka kuwaachia watoto wangu urithi mkubwa, nami ninauhifadhi kwa ajili yao”—kisha kama ungesikia kwamba mtu huyo hajitaabishi hata kidogo kuwaelimisha watoto wake, kwamba anawaacha wakimbie mitaani ovyo, na kuendelea katika njia za dhambi na ujinga na upumbavu, ungemwaza nini? Je, hungesema: “Maskini mtu huyu! anahifadhi urithi kwa ajili ya watoto wake, lakini hawahifadhi wala hawaandai watoto wake kwa ajili ya urithi”! Nao Wakristo wapo wengi mno wanaofikiri: “Mungu wangu ananihifadhia urithi”; lakini hawawezi kuamini: “Mungu wangu ananilinda mimi kwa ajili ya urithi ule.” Nguvu ileile, upendo uleule, Mungu yuleyule akifanya kazi maradufu.
Sasa, nataka kunena juu ya kazi ambayo Mungu anaifanya ndani yetu—kutulinda kwa ajili ya urithi. Nimekwisha sema kwamba tunazo kweli mbili rahisi sana: moja upande wa Mungu—tunalindwa kwa nguvu za Mungu; na nyingine, upande wa mwanadamu—tunalindwa kwa njia ya imani.
Kulindwa kwa Nguvu za Mungu
Uangalie upande wa Mungu: Wakristo wanalindwa kwa nguvu za Mungu.
Ulinzi Wahusisha Vyote
Fikiri, kwanza kabisa, kwamba ulinzi huu wahusisha vyote.
Ni nini kinacholindwa? Wewe unalindwa. Kiasi gani chako? Nafsi nzima. Je, Mungu hulinda sehemu moja yako na wala si nyingine? La. Watu wengine wana wazo kwamba huu ni ulinzi wa jumla usio dhahiri, na kwamba Mungu atawalinda kwa namna ambayo watakapokufa watafika Mbinguni. Lakini hawalitumii neno hilo la kulindwa kwa kila kitu kilichomo katika nafsi na asili yao. Na hata hivyo ndivyo Mungu atakavyo.
Hapa nina saa. Tuseme saa hii ningeazima kwa rafiki, naye akaniambia:
“Utakapokwenda Ulaya, nitakuruhusu uichukue pamoja nawe, lakini uwe mwangalifu uihifadhi salama na uirudishe.”
Na tuseme ningeiharibu saa, nikavunja mishale yake, nikaharibu uso wake, na baadhi ya magurudumu na kamani zake zikaharibika, kisha nikairudisha katika hali hiyo, nikampa rafiki yangu; angesema:
“Aha, lakini nilikupa saa ile kwa sharti kwamba ungeihifadhi.”
“Je, sikuihifadhi? Saa ndiyo hiyo.”
“Lakini sikutaka uihifadhi kwa namna ile ya jumla, hata unirudishie ganda tu la saa, au mabaki yake. Nilitazamia uihifadhi kila sehemu yake.”
Na hivyo Mungu hataki kutulinda kwa namna hii ya jumla, hata mwishoni, kwa jinsi fulani, tuokolewe kama kwa moto, na kuingia tu Mbinguni. Bali nguvu za ulinzi na upendo wa Mungu vyahusika kwa kila sehemu ndogo ya nafsi yetu.
Wapo watu wengine wanaofikiri Mungu atawalinda katika mambo ya kiroho, lakini si katika mambo ya kidunia. Haya ya mwisho, wanasema, yako nje ya mstari wake. Basi, Mungu anakutuma ufanye kazi ulimwenguni, lakini hakusema: “Ni lazima sasa nikuache uende ukajipatie fedha zako mwenyewe, na kujitafutia riziki yako mwenyewe.” Yeye anajua wewe huwezi kujilinda mwenyewe. Bali Mungu asema: “Mwanangu, hakuna kazi utakayoifanya, wala biashara yoyote unayoishughulikia, wala senti moja utakayoitumia, ila mimi, Baba yako, nitaichukua katika ulinzi wangu.” Mungu hajali mambo ya kiroho tu, bali na ya kidunia pia. Sehemu kubwa ya maisha ya watu wengi lazima itumike, mara nyingine saa nane au tisa au kumi kwa siku, katikati ya majaribu na visumbufu vya biashara; lakini Mungu atakutunza huko. Ulinzi wa Mungu wahusisha vyote.
Wapo watu wengine wanaofikiri: “Aha! wakati wa jaribu Mungu hunilinda, lakini wakati wa kufanikiwa sihitaji ulinzi wake; ndipo nasahau naye namwacha aende.” Wengine, tena, wanafikiri kinyume kabisa. Wanafikiri: “Wakati wa kufanikiwa, mambo yanapokuwa laini na tulivu, naweza kuambatana na Mungu, lakini majaribu mazito yanapokuja, kwa jinsi fulani nia yangu inaasi, na Mungu hanilindi wakati huo.”
Basi, nawaletea ujumbe kwamba katika kufanikiwa kama katika mateso, katika mwanga wa jua kama katika giza, Mungu wako yu tayari kukulinda wakati wote.
Tena, wapo wengine wanaoufikiria ulinzi huu hivi: “Mungu atanilinda nisitende uovu mkubwa sana, lakini kuna dhambi ndogo ndogo nisizoweza kutazamia Mungu anilinde nazo. Kuna dhambi ya hasira. Siwezi kutazamia Mungu aishinde hiyo.”
Usikiapo habari za mtu fulani aliyejaribiwa akapotoka au akaanguka katika ulevi au uuaji, wamshukuru Mungu kwa nguvu zake za kulinda.
“Nami ningeweza kutenda kama mtu yule,” wasema, “kama Mungu asingenilinda.” Nawe waamini kwamba alikulinda usianguke katika ulevi na uuaji.
Na kwa nini hukuamini kwamba Mungu aweza kukulinda usilipuke kwa hasira? Uliona kwamba jambo hili lina umuhimu mdogo; hukukumbuka kwamba amri kuu ya Agano Jipya ni—“Mpendane kama vile nilivyowapenda ninyi” (Yohana 13:34). Na hasira yako na hukumu ya haraka na maneno makali yalipotoka, ulikosa juu ya sheria iliyo juu zaidi—sheria ya upendo wa Mungu. Na hata hivyo wasema: “Mungu hatataka, Mungu hawezi”—la, hutasema, Mungu hawezi; bali wasema, “Mungu hanilindi na jambo hilo.” Labda wasema: “Aweza; lakini kuna kitu ndani yangu kisichoweza kulifikia, ambacho Mungu hakiondoi.”
Nataka kuwauliza, Je, waaminio waweza kuishi maisha matakatifu zaidi kuliko yanavyoishiwa kwa kawaida? Je, waaminio waweza kuionja nguvu ya Mungu ya kulinda mchana kutwa, iwalinde na dhambi? Je, waaminio waweza kulindwa katika ushirika na Mungu? Nami nawaletea ujumbe kutoka katika Neno la Mungu, kwa maneno haya: Kulindwa kwa nguvu za Mungu. Hakuna kifungu cha masharti kwao. Maana yake ni kwamba, ukijikabidhi mwenyewe kwa ukamilifu na moja kwa moja kwa uweza wote wa Mungu, atafurahi kukulinda.
Watu wengine wanafikiri kwamba kamwe hawawezi kufikia kiasi hicho kwamba kila neno la kinywa chao liwe kwa utukufu wa Mungu. Lakini ndivyo Mungu atakavyo kwao, ndivyo Mungu anavyowatazamia. Mungu yu radhi kuweka ulinzi mlangoni pa kinywa chao, na kama Mungu atafanya hivyo, je, hawezi kuulinda ulimi wao na midomo yao? Aweza; na ndivyo Mungu atakavyowafanyia wanaomtumaini. Ulinzi wa Mungu wahusisha vyote, na kila mtu anayetamani kuishi maisha matakatifu na afikiri mahitaji yake yote, na udhaifu wake wote, na mapungufu yake yote, na dhambi zake zote, na aseme kwa makusudi: “Je, iko dhambi yoyote ambayo Mungu wangu hawezi kunilinda nayo?” Na moyo utalazimika kujibu: “La; Mungu aweza kunilinda na kila dhambi.”
Ulinzi Wahitaji Nguvu
Pili, kama unataka kuuelewa ulinzi huu, kumbuka kwamba si ulinzi unaohusisha vyote tu, bali ni ulinzi wa uweza wote.
Nataka kweli hiyo ichomeke ndani ya nafsi yangu; nataka kumwabudu Mungu hata moyo wangu wote ujae wazo la uweza wake wote. Mungu ni mwenye uweza wote, naye Mungu Mwenyezi anajitoa mwenyewe afanye kazi ndani ya moyo wangu, aifanye kazi ya kunilinda; nami nataka kuunganishwa na Uweza Wote, au afadhali, kuunganishwa na Yule Mwenye Uweza Wote, na Mungu aliye hai, na kupata mahali pangu katika kiganja cha mkono wake. Wewe wasoma Zaburi, nawe wafikiri mawazo ya ajabu katika maneno mengi anayoyatumia Daudi; kwa mfano, aneneapo juu ya Mungu kuwa Mungu wetu, Ngome yetu, Kimbilio letu, Mnara wetu imara, Nguvu zetu na Wokovu wetu. Daudi alikuwa na maono ya ajabu sana ya jinsi Mungu wa milele mwenyewe alivyo mahali pa kujificha pa nafsi iaminiyo, na jinsi anavyomchukua yeye aaminiye na kumlinda ndani ya kiganja cha mkono wake, katika siri ya hema yake, chini ya uvuli wa mbawa zake, chini ya manyoya yake hasa. Na hapo ndipo Daudi aliishi. Na oh, sisi tulio watoto wa Pentekoste, sisi tuliomjua Kristo na damu yake na Roho Mtakatifu aliyeshushwa toka Mbinguni, kwa nini tunajua kidogo hivyo juu ya kutembea kwa kutetemeka hatua kwa hatua pamoja na Mungu Mwenyezi kama Mlinzi wetu?
Je, umepata kufikiri kwamba katika kila tendo la neema ndani ya moyo wako unao uweza wote wa Mungu ukishughulika kukubariki? Nimwendeapo mtu naye akanipa zawadi ya fedha, naipokea na kuondoka nayo. Amenipa kitu chake; kilichobaki hujiwekea mwenyewe. Lakini si hivyo kwa nguvu za Mungu. Mungu hawezi kuachana na chochote cha nguvu zake mwenyewe, na kwa hiyo naweza kuionja nguvu na wema wa Mungu kadiri tu ninavyokuwa katika kugusana na ushirika naye mwenyewe; na ninapoingia katika kugusana na ushirika naye mwenyewe, naingia katika kugusana na ushirika na uweza wote wa Mungu, nami ninao uweza wote wa Mungu wa kunisaidia kila siku.
Mwana, labda, anaye baba tajiri sana, na huyo mwana anapokaribia kuanza biashara baba asema: “Waweza kupata fedha kadiri utakavyo kwa shughuli yako.” Vyote alivyo navyo baba viko tayari kwa matumizi ya mwana. Na ndivyo ilivyo kwa Mungu, Mungu wako Mwenyezi. Hukupata kulipokea vyema; wajiona kama funza mdogo hivi. Uweza wake wote wahitajika kumlinda funza mdogo! Naam, uweza wake wote wahitajika kumlinda kila funza mdogo aishiye mavumbini, na pia kuulinda ulimwengu wote, na kwa hiyo uweza wake wote wahitajika zaidi sana katika kuilinda nafsi yako na yangu na nguvu ya dhambi.
Oh, kama unataka kukua katika neema, jifunze kuanzia hapa. Katika hukumu zako zote na tafakari na mawazo na matendo na maulizo na masomo na maombi, jifunze kulindwa na Mungu wako Mwenyezi. Ni nini ambacho Mungu Mwenyezi hatakifanya kwa mtoto anayemtumaini? Biblia yasema: “mwenye kuweza kufanya nyingi mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo” (Waefeso 3:20). Ni Uweza Wote ambao ni lazima ujifunze kuujua na kuutumaini, ndipo utakapoishi kama impasavyo Mkristo kuishi. Tumejifunza kidogo mno kumtafiti Mungu, na kuelewa kwamba maisha ya utauwa ni maisha yaliyojaa Mungu, maisha yampendayo Mungu na kumngoja, na kumtumaini, na kumruhusu ayabariki! Hatuwezi kuyafanya mapenzi ya Mungu ila kwa nguvu za Mungu. Mungu hutupa uzoefu wa kwanza wa nguvu zake ili kutuandaa tutamani zaidi, na kuja kudai yote awezayo kufanya. Mungu na atusaidie kumtumaini kila siku.
Ulinzi Ni Wa Kudumu
Wazo lingine. Ulinzi huu si wa kuhusisha vyote na wa uweza wote tu, bali pia ni wa kudumu na usiokatika.
Watu mara nyingine husema: “Kwa juma au mwezi Mungu amenilinda kwa namna ya ajabu sana: nimeishi katika nuru ya uso wake, nami siwezi kusema furaha nisiyokuwa nayo katika ushirika naye. Amenibariki katika kazi yangu kwa ajili ya wengine. Amenipa roho za watu, na nyakati fulani nilihisi kana kwamba nachukuliwa kuelekea mbinguni juu ya mbawa za tai. Lakini haikudumu. Ilikuwa njema mno; haikuweza kudumu.” Na wengine husema: “Ilikuwa lazima nianguke ili kunifanya mnyenyekevu.” Na wengine husema: “Najua ilikuwa kosa langu mwenyewe; lakini kwa jinsi fulani huwezi kuishi juu kileleni sikuzote.”
Oh, wapendwa, kwa nini iwe hivyo? Je, kwaweza kuwa na sababu yoyote ya ulinzi wa Mungu usiwe wa kudumu na usiokatika? Fikiri tu. Uhai wote uko katika mfululizo usiokatika. Kama uhai wangu ungesimamishwa kwa nusu saa ningekuwa nimekufa, na uhai wangu ungekuwa umepotea. Uhai ni kitu cha kuendelea, na uhai wa Mungu ndio uhai wa Kanisa lake, na uhai wa Mungu ni nguvu zake za uweza wote zikifanya kazi ndani yetu. Na Mungu anatujia kama Yule Mwenye Uweza Wote, na bila sharti lolote anajitolea kuwa Mlinzi wangu, na ulinzi wake wamaanisha kwamba siku kwa siku, dakika kwa dakika, Mungu atatulinda.
Kama ningewauliza swali: “Je, wafikiri Mungu aweza kukulinda siku moja usifanye kosa halisi?” ungejibu: “Sijui tu kwamba aweza kulifanya, bali nafikiri amekwisha kulifanya. Zimekuwapo siku ambazo ameulinda moyo wangu katika uwepo wake mtakatifu, ambapo, ingawa sikuzote nimekuwa na asili ya dhambi ndani yangu, amenilinda nisifanye kosa halisi kwa kujua.”
Basi, kama aweza kulifanya hilo kwa saa moja au siku moja, kwa nini si kwa siku mbili? Oh! na tuufanye uweza wote wa Mungu kama ulivyofunuliwa katika Neno lake kuwa kipimo cha matarajio yetu. Je, Mungu hakusema katika Neno lake: “Mimi, Bwana, nalilinda, nami nitalinyweshea kila dakika” (Isaya 27:3)? Hilo laweza kumaanisha nini? Je, “kila dakika” maanisha kila dakika? Je, Mungu aliahidi juu ya shamba lile la mizabibu au divai nyekundu kwamba kila dakika angelinyweshea ili joto la jua na upepo unaounguza visilikaushe kamwe? Naam. Katika Afrika ya Kusini mara nyingine hufanya kipandikizi, na juu yake hufunga chupa ya maji, ili mara kwa mara kuwe na tone la kuloweka walichokiweka kandokando yake. Na hivyo unyevunyevu huwekwa hapo bila kukoma hata kipandikizi kipate wakati wa kushika mizizi, na kustahimili joto la jua.
Je, Mungu wetu, katika upendo wake wa huruma kwetu, hatatulinda kila dakika ijapokuwa ameahidi kufanya hivyo? Oh! kama tungelilishika wazo hili mara moja: Maisha yetu yote ya kiroho yapasa yawe kazi ya Mungu—“Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema” (Wafilipi 2:13)—mara tupatapo imani ya kulitazamia hilo kutoka kwa Mungu, Mungu atatufanyia yote.
Ulinzi wapasa uwe wa kudumu. Kila asubuhi Mungu atakukuta uamkapo. Si swali: Kama nikisahau kuamka asubuhi nikiwa na wazo lake, kutatokea nini? Kama ukiukabidhi kuamka kwako kwa Mungu, Mungu atakukuta asubuhi uamkapo kwa mwanga wake wa kiungu na upendo, naye atakupa ufahamu kwamba mchana kutwa unaye Mungu wa kukusimamia daima kwa nguvu zake za uweza wote. Na Mungu atakukuta siku ifuatayo na kila siku; wala usijali kama katika kutenda ushirika kunakuja kushindwa mara nyingine. Ukiishika hali yako na kusema: “Bwana, nitakutazamia ufanye uwezalo lote, nami nitakutumaini siku kwa siku unilinde kabisa,” imani yako itazidi kuwa na nguvu zaidi na zaidi, nawe utaijua nguvu ya Mungu ya kulinda katika kutokatika.
Kulindwa kwa Njia ya Imani
Na sasa upande ule mwingine—Kuamini. “Kulindwa kwa nguvu za Mungu kwa njia ya imani.” Twapasaje kuiangalia imani hii?
Imani Yadokeza Kutoweza
Na niseme, kwanza kabisa, kwamba imani hii yamaanisha kutoweza kabisa na kutokuwa na uwezo mbele za Mungu.
Chini ya imani yote kuna hisia ya kutoweza. Kama nina shughuli kidogo ya kufanya, labda kununua nyumba, ni lazima wakili aifanye kazi ya kuhamisha mali kwa jina langu na kufanya matayarisho yote. Siwezi kuifanya kazi hiyo, na katika kumtumaini wakili yule nakiri kwamba siwezi kuifanya. Na hivyo imani sikuzote yamaanisha kutoweza. Katika hali nyingi yamaanisha: naweza kuifanya kwa taabu nyingi, lakini mwingine aweza kuifanya vizuri zaidi. Lakini katika hali nyingi ni kutoweza kabisa; ni lazima mwingine anifanyie. Na hiyo ndiyo siri ya maisha ya kiroho. Ni lazima mtu ajifunze kusema: “Naacha kila kitu; nimejaribu na kutamani na kufikiri na kuomba, lakini kushindwa kumekuja. Mungu amenibariki na kunisaidia, lakini bado, hatimaye, kumekuwa na dhambi na huzuni nyingi mno.” Ni badiliko kubwa lililoje lijalo mtu anapovunjwavunjwa hivi hata kufikia kutoweza kabisa na kukata tamaa ya nafsi, na kusema: “Siwezi kufanya lolote!”
Mkumbuke Paulo. Alikuwa akiishi maisha yaliyobarikiwa, naye alikuwa amenyakuliwa hata Mbingu ya tatu, kisha mwiba katika mwili ukaja, “mjumbe wa Shetani ili anipige ngumi.” Na kilichotokea ni nini? Paulo hakuweza kukielewa, naye akamwomba Bwana mara tatu akiuondoe; lakini Bwana akasema, kwa maana hii:
“La; yamkini ungeweza kujitukuza mwenyewe, na kwa hiyo nimekuletea jaribu hili ili kukuweka dhaifu na mnyenyekevu.”
Ndipo Paulo akajifunza somo ambalo hakulisahau kamwe, nalo ni—kufurahia udhaifu wake. Alisema kwamba kadiri alivyokuwa dhaifu ndivyo ilivyokuwa afadhali kwake, kwa kuwa alipokuwa dhaifu, alikuwa na nguvu ndani ya Bwana wake Kristo.
Je, wataka kuingia katika kile watu wanachokiita “maisha ya juu zaidi”? Basi shuka hatua moja chini zaidi. Namkumbuka Dkt. Boardman akisimulia jinsi mara moja alivyoalikwa na bwana mmoja kwenda kutazama kiwanda ambapo walitengeneza risasi laini, nami naamini wafanyakazi walifanya hivyo kwa kumwaga risasi iliyoyeyuka toka juu sana. Bwana huyu alitaka kumpandisha Dkt. Boardman hata juu ya mnara ili aone jinsi kazi ilivyofanywa. Daktari alifika mnarani, akaingia kwa mlango, akaanza kupanda ngazi; lakini alipokwisha panda hatua chache bwana yule akapaza sauti:
“Hiyo ndiyo njia isiyo sahihi. Ni lazima ushuke huku; ngazi hiyo imefungwa.”
Bwana yule akamshusha ngazi nyingi tu chini, na hapo lifti ilikuwa tayari kumpandisha juu; naye akasema:
“Nimejifunza somo kwamba kushuka mara nyingi ndiyo njia iliyo bora ya kupanda juu.”
Aha, naam, itamlazimu Mungu kutushusha chini sana; itatupasa kujiliwa na hisia ya utupu na kukata tamaa na ubatili. Ni tunapozama chini katika kutoweza kabisa ndipo Mungu wa milele atakapojidhihirisha mwenyewe katika nguvu zake, na ndipo mioyo yetu itakapojifunza kumtumaini Mungu peke yake.
Ni nini kinachotuzuia kumtumaini kikamilifu?
Wengi husema: “Naamini unayoyasema, lakini kuna ugumu mmoja. Kama tumaini langu lingekuwa kamili na lenye kudumu daima, yote yangekuwa sawa, kwa maana najua Mungu atatuheshimu tumaini. Lakini nitalipataje tumaini hilo?”
Jibu langu ni: “Kwa kufa kwa nafsi. Kizuizi kikubwa cha tumaini ni juhudi za nafsi. Maadamu unayo hekima yako mwenyewe na mawazo na nguvu, huwezi kumtumaini Mungu kikamilifu. Lakini Mungu akikuvunja, kila kitu kianzapo kuwa hafifu mbele ya macho yako, nawe ukiona kwamba huelewi lolote, ndipo Mungu anakaribia, na ukiinama katika ubatili na kumngoja Mungu, atakuwa yote.”
Maadamu sisi ni kitu, Mungu hawezi kuwa yote, na uweza wake wote hauwezi kufanya kazi yake kamili. Huo ndio mwanzo wa imani—kukata tamaa kabisa na nafsi, kuacha mwanadamu na kila kitu kilicho duniani, na kuliona tumaini letu katika Mungu peke yake.
Imani Ni Pumziko
Na tena, baadaye, ni lazima tuelewe kwamba imani ni pumziko.
Mwanzoni mwa maisha ya imani, imani inahangaika; lakini maadamu imani inahangaika, imani haijafikia nguvu yake. Lakini imani, katika kuhangaika kwake, ifikiapo mwisho wake, na kujitupa tu juu ya Mungu na kupumzika juu yake, ndipo hufika furaha na ushindi.
Labda naweza kulifanya liwe wazi zaidi nikisimulia hadithi ya jinsi Kongamano la Keswick lilivyoanza. Canon Battersby alikuwa mchungaji wa kiinjili wa Kanisa la Uingereza kwa zaidi ya miaka ishirini, mtu wa utauwa wa kina na wa upole, lakini hakuwa na ufahamu wa pumziko na ushindi juu ya dhambi, na mara nyingi alikuwa na huzuni kubwa kwa kufikiri kujikwaa na kushindwa na dhambi. Aliposikia juu ya uwezekano wa ushindi, aliona ni jambo la kutamanika, lakini ilikuwa kana kwamba hakuweza kuufikia. Wakati mmoja, alisikia hotuba juu ya “Pumziko na Imani” kutoka hadithi ya yule diwani aliyekuja toka Kapernaumu hata Kana kumwomba Kristo amponye mtoto wake. Katika hotuba ilionyeshwa kwamba diwani yule aliamini kwamba Kristo aweza kumsaidia kwa namna ya jumla, lakini alimjia Yesu kwa kiasi kikubwa kwa njia ya kujaribu. Alitumaini Kristo angemsaidia, lakini hakuwa na uhakika wowote wa msaada huo. Lakini kilichotokea ni nini? Kristo alipomwambia: “Enenda zako, mwanao yu hai,” mtu yule aliamini neno lile Yesu alilolinena; alipumzika katika neno lile. Hakuwa na uthibitisho kwamba mtoto wake amepona tena, na ilimpasa kutembea safari ya saa saba kurudi Kapernaumu. Alitembea kurudi, na njiani akakutana na mtumishi wake, akapata habari za kwanza kwamba mtoto amepona, kwamba saa saba mchana wa siku iliyotangulia, wakati ule ule Yesu aliponena naye, homa ilimwacha mtoto. Baba yule alipumzika juu ya neno la Yesu na kazi yake, akashuka hata Kapernaumu akamkuta mtoto wake amepona; naye akamsifu Mungu, akawa pamoja na nyumba yake yote mwaminifu na mwanafunzi wa Yesu.
Oh, rafiki, hiyo ndiyo imani! Mungu anijiapo na ahadi ya ulinzi wake, nami sina kitu duniani cha kutumaini, namwambia Mungu: “Neno lako latosha; kulindwa kwa nguvu za Mungu.” Hiyo ndiyo imani, hilo ndilo pumziko.
Canon Battersby aliposikia hotuba ile, alikwenda nyumbani usiku ule, na katika giza la usiku akapata pumziko. Alipumzika juu ya neno la Yesu. Na asubuhi iliyofuata, katika njia za Oxford, alimwambia rafiki: “Nimeipata!” Kisha akaenda akawaambia wengine, na akaomba Kongamano la Keswick lianzishwe, na wale watakaokuwapo katika kongamano pamoja naye washuhudie kwa unyofu yale Mungu aliyoyafanya.
Ni jambo kubwa mtu afikapo kupumzika juu ya nguvu za Mungu za uweza wote kwa kila dakika ya maisha yake, akitazamia majaribu ya hasira na haraka na ghadhabu na kutokupenda na kiburi na dhambi. Ni jambo kubwa, katika kuyatazamia haya, kuingia agano na Yehova mwenye uweza wote, si kwa sababu ya lolote asemalo mtu yeyote, wala kwa sababu ya lolote uhisilo moyo wangu, bali kwa nguvu ya Neno la Mungu: “Kulindwa kwa nguvu za Mungu kwa njia ya imani.”
Oh, na tumwambie Mungu kwamba tutamjaribu hata kikomo cha mwisho kabisa. Na tuseme: Hatukuombi zaidi ya uwezavyo kutupa, lakini hatutaki pungufu. Na tuseme: Mungu wangu, maisha yangu na yawe uthibitisho wa yale Mungu mwenye uweza wote awezayo kuyafanya. Haya na yawe mielekeo miwili ya nafsi zetu kila siku—kutoweza kwa kina, na pumziko rahisi, la kitoto.
Imani Yahitaji Ushirika
Hilo lanileta kwa wazo moja tu zaidi kuhusu imani—imani yadokeza ushirika na Mungu.
Watu wengi wanataka kulichukua Neno na kuliamini, nao wanaona hawawezi kuliamini. Aha, la! huwezi kumtenga Mungu na Neno lake. Hakuna wema wala nguvu iwezayo kupokelewa tofauti na Mungu, na kama unataka kuingia katika maisha haya ya utauwa, ni lazima uchukue muda kwa ushirika na Mungu.
Watu mara nyingine huniambia: “Maisha yangu yamejaa mbio na pilikapilika hata sina muda wa ushirika na Mungu.” Mmisionari mmoja mpendwa aliniambia: “Watu hawajui sisi wamisionari tunavyojaribiwa. Naamka saa kumi na moja alfajiri, na wazawa wako wakingoja maagizo yao ya kazi. Kisha ni lazima niende shuleni na kutumia masaa mengi huko; kisha kuna kazi nyingine, na masaa kumi na sita yanapita mbio, nami sipati muda wa kuwa peke yangu na Mungu.”
Aha! hapo ndipo penye upungufu. Nawasihi, kumbukeni mambo mawili. Sikuwaambia mtumaini uweza wote wa Mungu kama kitu, wala sikuwaambia mliamini Neno la Mungu kama kitabu kilichoandikwa, bali nimewaambia mwende kwa Mungu wa uweza wote na Mungu wa Neno. Shughulika na Mungu kama vile diwani yule alivyoshughulika na Kristo aliye hai. Kwa nini aliweza kuliamini neno lile Kristo alilomwambia? Kwa sababu katika macho na sauti na mlio wa Yesu, Mwana wa Mungu, aliona na kusikia kitu kilichomfanya ahisi kwamba angeweza kumtumaini. Na ndilo Kristo awezalo kukufanyia wewe na mimi. Usijaribu kuichochea na kuiamsha imani toka ndani. Mara ngapi nimejaribu kufanya hivyo, nikajifanya mpumbavu! Huwezi kuichochea imani toka vilindi vya moyo wako. Uache moyo wako, na uangalie uso wa Kristo, na usikilize akuambiavyo jinsi atakavyokulinda. Angalia juu uso wa Baba yako mpendevu, na uchukue muda kila siku pamoja naye, na uanze maisha mapya kwa utupu wa kina na umaskini wa mtu asiye na kitu, na anayetaka kupata kila kitu kutoka kwake—kwa pumziko la kina la mtu apumzikaye juu ya Mungu aliye hai, Yehova mwenye uweza wote—na umjaribu Mungu, na umthibitishe kama hatafungua madirisha ya Mbinguni na kumwaga baraka hata pasiwe na nafasi ya kuipokea.
Namaliza kwa kuuliza kama u tayari kuonja kwa ukamilifu kabisa ulinzi wa mbinguni kwa ajili ya urithi wa mbinguni? Robert Murray M’Cheyne asema, mahali fulani: “Oh, Mungu, nifanye mtakatifu kadiri awezavyo kufanywa mtakatifu mwenye dhambi aliyesamehewa.” Na kama sala hiyo imo moyoni mwako, njoo sasa, na tuingie agano na Yehova wa milele na mwenye uweza wote upya, na katika kutoweza kukubwa, lakini katika pumziko kubwa tujiweke mikononi mwake. Na kisha tuingiapo agano letu, na tuwe na sala moja—kwamba tupate kuamini kwa ukamilifu kwamba Mungu wa milele atakuwa Mwenzetu, akishika mkono wetu kila dakika ya siku; Mlinzi wetu, akitutunza pasipo kitambo hata kimoja; Baba yetu, akifurahia kujidhihirisha mwenyewe katika nafsi zetu sikuzote. Anayo nguvu ya kufanya mwanga wa jua wa upendo wake uwe pamoja nasi mchana kutwa. Usiogope kwa sababu unayo biashara yako kwamba huwezi kuwa na Mungu pamoja nawe sikuzote. Jifunze somo kwamba jua la asili lakuangazia mchana kutwa, nawe wafurahia mwanga wake, na popote ulipo unalo jua; Mungu huhakikisha kwamba lakuangazia. Na Mungu atahakikisha kwamba mwanga wake mwenyewe wa kiungu wakuangazia, na kwamba utakaa katika mwanga huo, kama utamtumaini tu kwa ajili yake. Na tumtumaini Mungu afanye hivyo kwa tumaini kuu na kamili.
Huu hapa ni uweza wote wa Mungu, na hii hapa ni imani ikinyoosha mkono kufikia kipimo cha uweza huo. Je, hatutasema: “Yote awezayo uweza huo kuyafanya, nitamtumaini Mungu wangu kwa ajili yake”? Je, pande hizi mbili za maisha haya ya mbinguni si za ajabu? Uweza wote wa Mungu wanifunika, na nia yangu katika udogo wake wapumzika katika uweza huo, na kuufurahia!
Dakika kwa dakika, nalindwa katika upendo wake;
Dakika kwa dakika, ninao uzima toka juu;
Nikimtazama Yesu, utukufu wang’aa;
Dakika kwa dakika, Oh, Bwana, mimi ni wako!