Pamoja na Kristo katika Shule ya Maombi
Maombi Yaliyopatana na Kusudi la Mwanadamu

Sura 19 · dakika 7 za kusoma

Maombi Yaliyopatana na Kusudi la Mwanadamu

‘Akawaambia, Ni ya nani sura hii na anwani hii?—Mathayo 21:20.

‘Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu.’—Mwanzo 1:26.

‘SURA HII NI YA NANI?’ Ni kwa swali hili ndipo Yesu alipowashinda adui zake, walipotaka kumkamata, akakata shauri la wajibu kuhusu kodi. Swali hili na kanuni linalobeba yana matumizi ya ulimwengu mzima. Wala si mahali pengine kwa ukweli zaidi kuliko ndani ya mwanadamu mwenyewe. Sura anayoibeba ndiyo huamua kusudi lake. Kwa kuwa anaibeba sura ya Mungu, yeye ni wa Mungu: maombi kwa Mungu ndilo alilokusudiwa kuumbwa. Maombi ni sehemu ya ufanano wa ajabu alio nao mtu na Asili yake ya Kimungu; ile siri ya ndani ya ushirika wa upendo ambamo yule Utatu-Mmoja ana heri yake, maombi ndiyo mfano na sura yake ya kidunia.

Kadiri tunavyotafakari zaidi juu ya maombi ni nini, na nguvu ya ajabu iliyo nayo mbele za Mungu, ndivyo tunavyozidi kulazimika kuuliza mtu ni nani na ni kitu gani, hata apewe nafasi kama hiyo katika mashauri ya Mungu. Dhambi imemshusha kiasi hata, kutokana na alivyo sasa, hatuwezi kupata wazo lo lote la vile alivyokusudiwa kuwa. Ni lazima turudi kwenye kumbukumbu ya Mungu mwenyewe juu ya kuumbwa kwa mwanadamu ili tuone humo kusudi la Mungu lilikuwa nini, na uwezo gani mwanadamu alipewa kwa ajili ya kutimiza kusudi hilo.

Kusudi la mwanadamu laonekana wazi kutokana na maneno ya Mungu wakati wa uumbaji. Lilikuwa ni kuijaza, kuitiisha, kuwa na mamlaka juu ya nchi na vyote vilivyomo. Maneno hayo matatu yote yatuonyesha kwamba mwanadamu alikusudiwa, akiwa mwakilishi wa Mungu, kushika utawala hapa duniani. Akiwa naibu wa Mungu alipaswa kushika nafasi ya Mungu: yeye mwenyewe akiwa chini ya Mungu, alipaswa kuvitunza vyote vingine chini yake. Ilikuwa mapenzi ya Mungu kwamba yote yaliyopaswa kutendeka duniani yatendeke kupitia kwake: historia ya dunia ilipaswa kuwa mikononi mwake kabisa.

Kulingana na kusudi kama hilo ndiyo ilivyokuwa nafasi aliyopaswa kuwa nayo, na nguvu iliyokuwa mkononi mwake. Mfalme wa dunia atumapo naibu kwenda jimbo la mbali, hueleweka kwamba naibu huyo hushauri juu ya sera itakayofuatwa, na kwamba shauri lake hutekelezwa: kwamba yuko huru kuomba askari na njia nyingine zinazohitajika ili kutekeleza sera au kudumisha heshima ya ufalme. Sera yake isipokubaliwa, huitwa arudi ili kumpisha mtu aelewaye vema zaidi matakwa ya mfalme wake; maadamu anaaminiwa, shauri lake hutekelezwa. Akiwa mwakilishi wa Mungu, mwanadamu angetawala; yote yangetendeka chini ya mapenzi na utawala wake; kwa shauri lake na kwa ombi lake mbingu zingeimimina baraka yake duniani. Maombi yake yangekuwa ndio njia ya ajabu, ijapokuwa rahisi na ya asili kabisa, ambamo ushirika kati ya Mfalme aliye mbinguni na mtumishi wake mwaminifu mwanadamu, akiwa bwana wa ulimwengu huu, ungedumishwa. Hatima za ulimwengu zilitiwa katika nguvu ya matakwa, mapenzi, na maombi ya mwanadamu.

Kwa kuingia dhambi, haya yote yalipata badiliko la kutisha—kuanguka kwa mwanadamu kuliuleta uumbaji wote chini ya laana. Kwa ukombozi ndipo mwanzo wa marejesho matukufu ulipoonekana. Mara tu Mungu alipoanza kwa Ibrahimu kujifanyizia taifa ambalo kutoka kwao wangetokea wafalme, naam, yule Mfalme Mkuu, ndipo tunapoona nguvu iliyo nayo maombi ya mtumishi mwaminifu wa Mungu kuamua hatima za wale wanaokutana naye. Katika Ibrahimu twaona jinsi maombi yasivyo tu, wala hasa, njia ya kupata baraka kwa ajili yetu wenyewe, bali ni utumizi wa haki yake ya kifalme wa kuathiri hatima za watu, na mapenzi ya Mungu yanayowatawala. Hatumwoni Ibrahimu hata mara moja akijiombea mwenyewe. Ombi lake kwa ajili ya Sodoma na Lutu, kwa ajili ya Abimeleki, kwa ajili ya Ishmaeli, lathibitisha nguvu aliyo nayo mtu aliye rafiki wa Mungu, ya kuitengeneza historia ya wale walio karibu naye.

Hili lilikuwa kusudi la mwanadamu tangu mwanzo. Maandiko hayatuambii tu haya, bali pia yatufundisha jinsi ilivyowezekana Mungu kumkabidhi mwanadamu wito wa juu namna hiyo. Ilikuwa ni kwa sababu alikuwa amemwumba kwa mfano na sura yake mwenyewe. Utawala wa nje haukukabidhiwa kwake bila ufaafu wa ndani: kuibeba sura ya Mungu katika kuwa na mamlaka, katika kuwa bwana wa vyote, kulikuwa na mzizi wake katika ufanano wa ndani, katika asili yake. Kulikuwa na upatano na maelewano ya ndani kati ya Mungu na mwanadamu, na mwanzo wa kufanana na Mungu, kuliyompa mwanadamu ufaafu wa kweli wa kuwa mpatanishi kati ya Mungu na ulimwengu wake, kwa maana alipaswa kuwa nabii, kuhani, na mfalme, kutafsiri mapenzi ya Mungu, kuwakilisha mahitaji ya viumbe, kupokea na kugawa ukarimu wa Mungu. Ni kwa kuibeba sura ya Mungu ndipo angeweza kubeba utawala wa Mungu; kwa kweli alifanana na Mungu kwa kiasi hicho, aliweza kwa kiasi hicho kuingia katika makusudi ya Mungu, na kutekeleza mipango yake, hata Mungu angeweza kumwamini kwa pendeleo la ajabu la kuomba na kupata kile ambacho ulimwengu ungehitaji. Na ijapokuwa dhambi imezuia mipango ya Mungu kwa kitambo, maombi yangali kama yangalivyokuwa kama mwanadamu asingaliyeanguka kamwe: ushahidi wa kufanana kwa mwanadamu na Mungu, chombo cha ushirika wake na Yule Asiyeonekana Asiye na Mwisho, nguvu inayoruhusiwa kuushika mkono unaozishika hatima za ulimwengu wote. Maombi si kilio cha mwenye kuomba rehema tu; ni kutokezwa kwa juu kabisa kwa mapenzi ya mwanadamu, akijijua mwenyewe kuwa wa asili ya Kimungu, aliyeumbwa kwa ajili ya na awezaye kuwa, katika uhuru kama wa kifalme, mtekelezaji wa mashauri ya Aliye wa Milele.

Kile dhambi ilichokiharibu, neema imekirejesha. Kile Adamu wa kwanza alichokipoteza, wa pili amekipata tena. Katika Kristo mwanadamu aipata tena nafasi yake ya asili, na Kanisa, likikaa ndani ya Kristo, larithi ile ahadi: ‘Ombeni mtakalo lote, nanyi mtatendewa.’ Ahadi kama hiyo, kwa vyo vyote, haihusu kwanza neema au baraka tunayoihitaji sisi wenyewe. Yahusu nafasi yetu kama matawi yazaayo matunda ya ule Mzabibu wa Mbinguni, ambao, kama yeye, huishi kwa ajili ya kazi na utukufu wa Baba tu. Ni kwa ajili ya wale wanaokaa ndani yake, walioziacha nafsi zao ili kufanya makao yao ndani yake pamoja na maisha yake ya utii na kujitoa, walioipoteza roho yao na kuiona ndani yake, ambao sasa wamejitoa kabisa kwa masilahi ya Baba na ufalme wake. Hawa ndio wanaoelewa jinsi kuumbwa kwao kwa upya kulivyowarudisha kwenye kusudi lao la asili, kumeirejesha sura na mfano wa Mungu, na pamoja nao nguvu ya kuwa na mamlaka. Hao kwa kweli wana nguvu, kila mmoja katika mzunguko wake, ya kupata na kugawa nguvu za mbinguni hapa duniani. Kwa ujasiri mtakatifu waweza kudhihirisha watakalo: huishi kama makuhani mbele za Mungu; kama wafalme nguvu za ulimwengu ujao huanza kuwa mkononi mwao. Waingia katika utimizo wa ile ahadi: ‘Ombeni lo lote mtakalo, nanyi mtatendewa.’

Ee Kanisa la Mungu aliye hai! wito wako ni wa juu na mtakatifu kuliko ujuavyo. Kupitia viungo vyako, kama wafalme, na makuhani kwa Mungu, Mungu angeutawala ulimwengu; maombi yao huitoa na kuizuia baraka ya mbinguni. Katika wateule wake wasioridhika tu kuokolewa wenyewe, bali hujitoa kabisa, ili kupitia kwao, kama vile kupitia kwa Mwana, Baba atimize shauri lake lote tukufu, katika hao wateule wake, wamliliao mchana na usiku, Mungu angethibitisha jinsi kusudi la asili la mwanadamu lilivyokuwa la ajabu. Akiwa mchukuaji wa sura ya Mungu duniani, kwa kweli dunia ilitiwa mkononi mwake. Alipoanguka, vyote vilianguka pamoja naye: viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja. Lakini sasa amekombolewa; kurejeshwa kwa heshima ya asili kumeanza. Kwa kweli kabisa ni kusudi la Mungu kwamba utimizo wa kusudi lake la milele, na kuja kwa ufalme wake, kutegemee wale wa watu wake ambao, wakikaa ndani ya Kristo, wako tayari kuishika nafasi yao ndani yake Kichwa chao, yule Kuhani-Mfalme mkuu, na katika maombi yao wana ujasiri wa kutosha wa kusema watakalo Mungu wao alitende. Akiwa mchukuaji wa sura na mwakilishi wa Mungu duniani, mwanadamu aliyekombolewa apaswa kwa maombi yake kuamua historia ya dunia hii. Mwanadamu aliumbwa, na sasa amekombolewa tena, apate kuomba, na kwa maombi yake kuwa na mamlaka.

‘BWANA, UTUFUNDISHE KUOMBA.’

Bwana! mwanadamu ni kitu gani hata umkumbuke? na mwana wa Adamu hata umwangalie? kwa maana umemfanya mdogo kidogo kuliko malaika, ukamvika taji ya utukufu na heshima. Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako: umevitia vitu vyote chini ya miguu yake. Ee Bwana, Bwana wetu, jina lako ni tukufu kama nini katika nchi yote!

Bwana Mungu! jinsi dhambi ilivyomtumbukiza mwanadamu chini kabisa. Na jinsi ilivyoutia giza akili yake vibaya, hata haijui kusudi lake la Kimungu, la kuwa mtumishi na mwakilishi wako. Ole! kwamba hata watu wako, macho yao yanapofunguliwa, wako tayari kidogo mno kuukubali wito wao na kutafuta kuwa na nguvu mbele za Mungu, ili wapate kuwa na nguvu na wanadamu pia kwa kuwabariki.

Bwana Yesu! ni ndani yako ambako Baba amemvika tena mwanadamu utukufu na heshima, na ametufungulia njia ili tuwe vile atakavyo tuwe. Ee Bwana, uwahurumie watu wako, na uujilie urithi wako! Tenda kwa nguvu katika Kanisa lako, na uwafundishe wanafunzi wako waaminio watoke katika ukuhani wao wa kifalme, na katika nguvu ya maombi, ambayo umeipa ahadi za ajabu namna hiyo, kulitumikia ufalme wako, kuwatawala mataifa, na kulifanya jina la Mungu kuwa tukufu duniani. Amina.

Ukurasa 1 / 1 · 7 dakika zimebaki katika sura