Sura 12 · dakika 2 za kusoma
Maombi ya Wokovu
Ukristo si dini; ni kuishi maisha ya aina ya Mungu.
Mungu aliupenda ulimwengu kiasi kwamba akamtoa Mwanawe, Yesu Kristo, afe kwa ajili ya kila mtu. Kwa nini? Ili wewe na mimi tusipotee bali tuwe na uzima wa milele! Lo, ni jambo la ajabu! Mimi nina uzima wa milele, na wewe pia unao ikiwa umezaliwa mara ya pili. Kama bado hujazaliwa mara ya pili, wakati huu ndio nafasi yako. Utakuwa na uzima wa milele ikiwa utamwamini Yesu Kristo kwa moyo wako na kumtangaza kuwa Bwana juu ya maisha yako!
“Lakini ulisema Yesu Kristo alikufa kwa ajili ya kila mtu, kwa nini basi kusema ni wale tu waliozaliwa mara ya pili ndio wenye uzima wa milele?” Waweza kuuliza. Nitaanza kwa kutoa mfano wa rafiki anayesema amekuandikia hundi. Kama ijulikanavyo, fedha hiyo ni yako. Hata hivyo, kama hutakwenda benki kuchukua fedha yako na badala yake ukaitupa hundi yako, hutakuwa na fedha hiyo, hata kama walikuandikia. Ndivyo ilivyo kuhusu uzima wa milele. Bwana wetu, Yesu Kristo, alikufa kwa ajili ya ulimwengu wote. Hata hivyo, uzima wa milele hutolewa kwa wale wanaomwamini Bwana wetu Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai, wakiamini kwamba alikuja, akafa, akafufuliwa na yu hai leo. Unapojua, unapokubali, na unapokiri kwamba Yesu Kristo ni Bwana wa maisha yako, uzima wa milele hutiwa mara moja katika roho yako. Ndivyo uzima wa milele upokewavyo. Bwana asifiwe!
Je, sasa ungependa kupokea uzima huu wa milele, maisha ya aina ya Mungu? Nakualika hapa umfanye Yesu Kristo kuwa Bwana wa maisha yako, kama bado hujafanya hivyo. Tafadhali amini na uombe hivi: “Ee Bwana Mungu, naamini kwa moyo wangu wote katika Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Naamini kwamba alikufa kwa ajili yangu, na Mungu akamfufua kutoka kwa wafu. Naamini kwamba yu hai leo. Nakiri kwa kinywa changu kwamba Yesu Kristo ni Bwana wa maisha yangu tangu leo. Kupitia kwake na kwa Jina lake, nina uzima wa milele; nimezaliwa mara ya pili. Ahsante, Bwana, kwa kuiokoa nafsi yangu! Sasa mimi ni mtoto wa Mungu. Haleluya!”
Hongera! Sasa wewe ni mtoto wa Mungu, uliyezaliwa kwa Neno la Mungu. Wewe ni kiumbe kipya kilicho kamili na chenye haki kwa sababu Kristo Bwana sasa anaishi ndani yako, na amekufanya kuwa haki yake. Huhitaji kuhisi jambo hili bali amini kwamba sasa wewe ni mtu tofauti, mshindi kabisa na sasa unaweza kufanya maamuzi ya busara kuliko wakati wowote. Hakuna lisilowezekana kwako sasa! Anza kusoma Biblia na umruhusu Mungu aseme nawe na kukuongoza katika mapenzi yake makamilifu.
Mungu akubariki!
MWISHO