Sura 2 · dakika 10 za kusoma · dakika 14 za kusikiliza
Maombi na Imani
“Rafiki yangu mpendwa, aliyekuwa mpenzi mkubwa wa uwindaji, alinisimulia habari hii: ‘Nilipoamka asubuhi na mapema siku moja,’ alisema, ‘nilisikia mbweko wa mbwa wa kuwinda paa wapatao ishirini wakimfukuza windo lao. Nilipotazama mbali kwenye shamba pana, wazi, lililokuwa mbele yangu, nilimwona mwana-paa mchanga akilivuka, tena akionyesha dalili kwamba mbio zake zilikuwa karibu kwisha. Alipofika kwenye ua wa boma, aliruka juu yake, akajikunyata hatua kumi hivi kutoka mahali niliposimama. Muda mfupi baadaye mbwa wawili waliruka ua, naye mwana-paa akakimbia upande wangu, akaupenyeza kichwa chake katikati ya miguu yangu. Nikamwinua kiumbe yule mdogo kifuani pangu, nikizunguka-zunguka, nikawafukuza mbwa. Wakati ule ule nilihisi kwamba mbwa wote wa Magharibi wasingeweza, tena wasingeruhusiwa, kumkamata mwana-paa yule, kwa kuwa udhaifu wake ulikuwa umeikimbilia nguvu yangu.’ Ndivyo ilivyo, unyonge wa mwanadamu unapomkimbilia Mungu Mwenyezi. Nakumbuka vema wakati mbwa wa dhambi walipokuwa wakiifuatia nafsi yangu, hata mwishowe nikakimbilia mikononi mwa Mungu Mwenyezi.” — A. C. DIXON.
KATIKA kujifunza kokote juu ya kanuni na taratibu za maombi, juu ya shughuli na juhudi zake, nafasi ya kwanza, kwa lazima, sharti ipewe imani. Imani ndiyo sifa ya kwanza katika moyo wa mtu ye yote anayethubutu kuzungumza na Yeye Asiyeonekana. Kwa sababu ya unyonge mtupu, hana budi kunyosha mikono ya imani. Ni lazima aamini, pale asipoweza kuthibitisha. Mwishowe kabisa, maombi ni imani tu, ikidai haki zake za asili na za ajabu — imani ikiumiliki urithi wake usio na mipaka. Utauwa wa kweli ni wa kweli, thabiti, na wa kudumu katika ulimwengu wa imani sawasawa na ulivyo katika eneo la maombi. Tena: imani inapoacha kuomba, inaacha kuishi.
Imani hufanya yasiyowezekana kwa sababu humleta Mungu ashughulike kwa ajili yetu, na hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Jinsi ilivyo kuu — bila sharti wala kikomo — nguvu ya imani! Ikiwa shaka imefukuzwa moyoni, na kutokuamini kukafanywa mgeni humo, tumwombacho Mungu kitatukia hakika, na mwamini hujaliwa kupata “lo lote alisemalo.”
Maombi huielekeza imani kwa Mungu, na Mungu kwa ulimwengu. Ni Mungu peke yake awezaye kuhamisha milima, lakini imani na maombi humhamisha Mungu. Alipolilaani mtini, Bwana wetu alionyesha uweza wake. Baada ya hapo aliendelea kutangaza kwamba nguvu kubwa zimekabidhiwa imani na maombi, si kwa kuua bali kwa kuhuisha, si kwa kuharibu bali kwa kubariki.
Mahali hapa katika kujifunza kwetu, twaligeukia neno moja la Bwana wetu, ambalo yafaa kulikazia, kwa kuwa ndilo jiwe la katikati la tao la imani na maombi.
“Kwa sababu hiyo nawaambia, yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.”
Yatupasa kulitafakari vema neno hilo — “aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.” Hapa imeelezwa imani itambuayo, imani ijitwaliayo, ipokeayo. Imani ya namna hiyo ni kuutambua uwepo wa Mungu, ni ushirika unaoonjwa, ni uhakika uliothibitika.
Je, imani inakua au inapungua kadiri miaka inavyopita? Je, imani inasimama imara na thabiti siku hizi, maovu yanapozidi na upendo wa wengi unapopoa? Je, imani inashikilia msimamo wake, dini inapoelekea kuwa desturi tupu na mambo ya dunia yanapozidi kutawala? Swali la Bwana wetu laweza, kwa kufaa kabisa, kuwa swali letu. “Atakapokuja Mwana wa Adamu,” auliza, “je! ataiona imani duniani?” Twaamini kwamba ataiona, na ni wajibu wetu, katika siku zetu hizi, kuhakikisha kwamba taa ya imani imetengenezwa na inawaka, kwa maana yeye ajaye atakuja bila shaka, tena upesi sana.
Imani ndiyo msingi wa tabia ya Kikristo na usalama wa nafsi. Yesu alipokuwa akiliona mbele kukana kwa Petro, na kumwonya juu yake, alimwambia mwanafunzi wake:
“Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike.”
Bwana wetu alikuwa akitangaza kweli ya msingi; ilikuwa imani ya Petro aliyokuwa akitaka kuilinda; kwa maana alijua vema kwamba imani ikivunjika, misingi ya maisha ya kiroho huanguka, na jengo zima la uzoefu wa dini huporomoka. Ilikuwa imani ya Petro iliyohitaji kulindwa. Ndiyo sababu ya kujali kwa Kristo hali ya roho ya mwanafunzi wake, na nia yake ya kuiimarisha imani ya Petro kwa maombi yake mwenyewe yashindayo yote.
Katika Waraka wake wa Pili, Petro ana wazo hili moyoni anaposema juu ya kukua katika neema kama kinga ya usalama katika maisha ya Kikristo, na kama jambo linaloleta kuzaa matunda.
“Na zaidi ya hayo,” atangaza, “mkijitahidi sana, katika imani yenu ongezeni wema; na katika wema maarifa; na katika maarifa kiasi; na katika kiasi saburi; na katika saburi utauwa.”
Katika kazi hii ya kuongeza, imani ndiyo iliyokuwa mahali pa kuanzia — msingi wa neema nyingine za Roho. Imani ndiyo msingi ambao juu yake mambo mengine yalipaswa kujengwa. Petro hawaagizi wasomaji wake waongeze katika matendo, au vipawa, au fadhila, bali katika imani. Mengi hutegemea kuanza vizuri katika shughuli hii ya kukua katika neema. Kuna mpango wa Mungu, ambao Petro aliujua; kwa hiyo anaendelea kutangaza kwamba imetupasa kujitahidi kufanya imara wito wetu na uteule wetu, na uteule huo hufanywa hakika kwa kuongeza katika imani, nako, kwa upande wake, hufanyika kwa kuomba daima kwa bidii. Hivyo imani hudumishwa hai kwa maombi, na kila hatua inayochukuliwa, katika kuongeza neema juu ya neema, huambatana na maombi.
Imani ileteayo maombi yenye nguvu ni imani ijikitayo katika Mtu mwenye nguvu. Imani katika uwezo wa Kristo wa kutenda na wa kutenda makuu, ndiyo imani iombayo makuu. Hivyo ndivyo yule mwenye ukoma alivyoushika uweza wa Kristo. “Bwana, ukitaka,” alilia, “waweza kunitakasa.” Katika tukio hili twaonyeshwa jinsi imani ilivyojikita katika uwezo wa Kristo wa kutenda, na jinsi ilivyoipata nguvu ya kuponya.
Ilikuwa ni kwa ajili ya jambo hili hasa ndipo Yesu alipowauliza wale vipofu waliomjia ili wapate kuponywa:
“Mnaamini kwamba naweza kufanya hivi?” auliza. “Wakamwambia, Ndiyo, Bwana. Ndipo akayagusa macho yao, akisema, Iwe kwenu kama imani yenu ilivyo.”
Ilikuwa ni kwa kuchochea imani katika uwezo wake wa kutenda ndipo Yesu akaacha nyuma yake lile neno kuu la mwisho, ambalo, kwa kweli kabisa, ni mwito mkuu kwa imani. “Nimepewa mamlaka yote,” alitangaza, “mbinguni na duniani.”
Tena: imani hutii; huenda inapoamriwa, kama alivyofanya yule diwani aliyemjia Yesu, siku za mwili wake, ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa sana.
Zaidi ya hayo: imani ya namna hiyo hutenda. Kama yule mtu aliyezaliwa kipofu, huenda kunawa katika birika la Siloamu kwa sababu imeambiwa inawe. Kama Petro katika Gennesareti, hushusha nyavu pale Yesu anapoamuru, mara moja, bila swali wala shaka. Imani ya namna hiyo hukiondoa jiwe kaburini mwa Lazaro bila kukawia. Imani iombayo huzishika amri za Mungu, na kuyatenda yapendezayo machoni pake. Huuliza, “Bwana, wataka nifanye nini?” na hujibu upesi, “Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia.” Utii huisaidia imani, nayo imani, kwa upande wake, huusaidia utii. Kuyafanya mapenzi ya Mungu ni lazima kwa imani ya kweli, na imani ni lazima kwa utii kamili.
Lakini imani huitwa, tena mara nyingi sana, kungoja kwa saburi mbele za Mungu, nayo imejiandaa kwa yale yaonekanayo kuwa ni kuchelewa kwa Mungu katika kujibu maombi. Imani haikati tamaa kwa sababu maombi hayajibiwi mara moja; humshika Mungu kwa Neno lake, na kumwacha atumie muda wowote apendao katika kutimiza makusudi yake, na katika kuiendeleza kazi yake. Imani ya kweli haina budi kukutana na kuchelewa kwingi na siku ndefu za kungoja, lakini imani hukubali masharti hayo — hujua kwamba kutakuwa na kuchelewa katika kujibiwa kwa maombi, na huhesabu kuchelewa huko kuwa nyakati za kujaribiwa, ambazo ndani yake hupewa fursa ya kuonyesha ushujaa wake, na ugumu wa kitu ambacho kwacho imeumbwa.
Habari ya Lazaro ilikuwa mfano wa mahali palipokuwa na kuchelewa, ambapo imani ya wanawake wawili wema ilijaribiwa vikali: Lazaro alikuwa mgonjwa mahututi, na dada zake wakatuma kumwita Yesu. Lakini, bila sababu yo yote ijulikanayo, Bwana wetu alikawia kwenda kumsaidia rafiki yake mgonjwa. Ombi lilikuwa la haraka na lenye kugusa moyo — “Bwana, tazama, yeye umpendaye hawezi,” — lakini Bwana haguswi nalo, na ombi la dhati la wale wanawake likaonekana kuangukia masikio yasiyosikia. Ni jaribu lililoje kwa imani! Tena: kukawia kwa Bwana wetu kulionekana kuleta msiba usio na tumaini. Yesu alipokuwa akikawia, Lazaro alikufa.
Lakini kukawia kwa Yesu kulifanyika kwa ajili ya faida iliyo kubwa zaidi. Mwishowe anaelekea nyumbani kule Bethania.
“Basi ndipo Yesu alipowaambia waziwazi, Lazaro amekufa. Nami nafurahi kwa ajili yenu kwa kuwa sikuwako huko, ili mpate kuamini; lakini na twende kwake.”
Usiogope, Ee mwamini uliyejaribiwa na kupimwa, Yesu atakuja hakika, ikiwa saburi itadumishwa, na imani ikashikilia kwa nguvu. Kukawia kwake kutaufanya kuja kwake kuwe kwenye baraka tele zaidi. Endelea kuomba. Endelea kungoja. Huwezi kushindwa. Kristo akikawia, mngojee. Kwa wakati wake mwema, yeye atakuja , wala hatakawia.
Mara nyingi kuchelewa ndiko kipimo na nguvu ya imani. Ni saburi kiasi gani inayohitajika nyakati hizi za kujaribiwa zinapokuja! Lakini imani hupata nguvu kwa kungoja na kuomba. Saburi ina kazi yake kamilifu katika shule ya kuchelewa. Katika mambo mengine, kuchelewa ndiko kiini hasa cha maombi. Mungu hana budi kufanya mambo mengi kabla ya kutoa jibu la mwisho — mambo yaliyo ya lazima kwa ajili ya faida ya kudumu ya yeye anayeomba fadhili mikononi mwake.
Yakobo aliomba, kwa makusudi na kwa bidii, apate kuokolewa na Esau. Lakini kabla ombi hilo halijajibiwa, palikuwa na mengi ya kufanywa pamoja na Yakobo, na kwa ajili yake. Ilimpasa abadilishwe, kama vile Esau. Ilimpasa Yakobo afanywe mtu mpya kabla Esau hajafanywa. Ilimpasa Yakobo aongolewe kwa Mungu kabla Esau hajaongolewa kwa Yakobo.
Kati ya matamko makuu na yenye nuru ya Yesu kuhusu maombi, hakuna linalovuta usikivu kuliko hili:
“Amin, amin, nawaambia, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa sababu mimi naenda kwa Baba. Na lo lote mtakaloliomba kwa jina langu, nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lolote kwa jina langu, nitalifanya.”
Jinsi yalivyo ya ajabu matamko haya ya yale ambayo Mungu atayatenda kwa kujibu maombi! Jinsi yalivyo na umuhimu mkubwa maneno haya ya kuvuma, yaliyotanguliwa, kama yalivyo, na kweli iliyo nzito kuliko zote! Imani katika Kristo ndiyo msingi wa kazi yote, na wa maombi yote. Kazi zote za ajabu hutegemea maombi ya ajabu, na maombi yote hufanywa katika Jina la Yesu Kristo. Ni somo la kushangaza, la urahisi wa ajabu, hili la kuomba katika jina la Bwana Yesu! Masharti mengine yote yanashushwa thamani, kila kitu kingine kinakataliwa, isipokuwa Yesu peke yake. Jina la Kristo — Nafsi ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo — sharti liwe na mamlaka ya juu kabisa, katika saa na tendo la maombi.
Ikiwa Yesu anakaa kwenye chemchemi ya uhai wangu; ikiwa mikondo ya uhai wake imeiondoa na kuchukua mahali pa mikondo yote ya nafsi; ikiwa utii kamili kwake ndio uvuvio na nguvu ya kila mwendo wa maisha yangu, basi aweza bila hatari kuyakabidhi maombi kwa mapenzi yangu, na kujifunga, kwa wajibu ulio mzito kama asili yake mwenyewe, kwamba lo lote liombwalo litatolewa. Hakuna kitu kiwezacho kuwa wazi zaidi, dhahiri zaidi, kisicho na kikomo zaidi katika matumizi na upana wake, kuliko mausia na msisitizo wa Kristo, “Mwaminini Mungu.”
Imani hufunika mahitaji ya kimwili pamoja na ya kiroho. Imani huondoa wasiwasi wote usiofaa na masumbufu yasiyo na maana juu ya tutakachokula, tutakachokunywa, tutakachovaa. Imani huishi katika wakati uliopo, na huhesabu kwamba yatosha kwa siku maovu yake. Huishi siku kwa siku, na kuondoa hofu zote za kesho. Imani huleta utulivu mkubwa wa akili na amani kamilifu ya moyo.
“Wewe utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini.”
Tunapoomba, “Utupe leo mkate tunaouhitaji,” kwa kiasi fulani tunaifungia kesho nje ya ombi letu. Hatuishi katika kesho bali katika leo. Hatutafuti neema ya kesho wala mkate wa kesho. Wale wanaoishi katika wakati uliopo ulio hai ndio wanaostawi vizuri zaidi, na kupata mengi zaidi maishani. Wanaoomba vizuri zaidi ni wale waombao kwa ajili ya mahitaji ya leo, si ya kesho, ambayo huenda yakayafanya maombi yetu kuwa yasiyo ya lazima na ya ziada kwa kutokuwepo kabisa!
Maombi ya kweli huzaliwa na majaribu ya sasa na mahitaji ya sasa. Mkate wa leo ni mkate wa kutosha. Mkate uliotolewa kwa ajili ya leo ni ahadi iliyo imara kuliko zote kwamba kesho kutakuwa na mkate. Ushindi wa leo ni uhakika wa ushindi wa kesho. Maombi yetu yanahitaji kuelekezwa juu ya wakati uliopo. Imetupasa kumtumaini Mungu leo, na kuiacha kesho mikononi mwake kabisa. Wakati uliopo ni wetu; wakati ujao ni mali ya Mungu. Maombi ni kazi na wajibu wa kila siku inayokuja — maombi ya kila siku kwa ajili ya mahitaji ya kila siku.
Kama vile kila siku inavyodai mkate wake, ndivyo kila siku inavyodai maombi yake. Hakuna kiasi cha maombi yaliyofanywa leo kitakachotosha kwa maombi ya kesho. Kwa upande mwingine, hakuna kuomba kwa ajili ya kesho kulicho na thamani kubwa kwetu leo. Mana ya leo ndiyo tunayoihitaji; kesho Mungu atahakikisha kwamba mahitaji yetu yametimizwa. Hii ndiyo imani ambayo Mungu hutafuta kuivuvia. Basi iache kesho, pamoja na masumbufu yake, mahitaji yake, na taabu zake, mikononi mwa Mungu. Hakuna kuweka akiba ya neema ya kesho wala maombi ya kesho; wala hakuna kuweka akiba ya neema ya leo ili kukidhi mahitaji ya kesho. Hatuwezi kuwa na neema ya kesho, hatuwezi kula mkate wa kesho, hatuwezi kufanya maombi ya kesho. “Yatosha kwa siku maovu yake;” na, kwa hakika kabisa, ikiwa tuna imani, mema nayo yatatosha.