Ulazima wa Maombi
Maombi na Neno la Mungu (Inaendelea)

Sura 14 · dakika 8 za kusoma · dakika 10 za kusikiliza

Maombi na Neno la Mungu (Inaendelea)

“Miaka kadhaa iliyopita mtu mmoja alikuwa akisafiri katika nyika za Kentucky. Alikuwa amebeba kiasi kikubwa cha fedha, naye alikuwa amejihami vema kwa silaha. Usiku mmoja alifikia katika nyumba ya magogo, lakini alihangaika sana kwa kuwaona watu wenye sura ya ukorofi waliokuwa wakiingia na kutoka katika makao hayo. Alikwenda kulala mapema, lakini si kwa kupata usingizi. Usiku wa manane alisikia mbwa wakibweka kwa ukali, na sauti ya mtu akiingia kibandani. Akichungulia katika ufa wa mbao za chumba chake, alimwona mgeni mwenye bunduki mkononi. Mtu mwingine alikuwa ameketi mbele ya moto. Msafiri yule akadhani kwamba walikuwa wakipanga kumnyang’anya, akajiandaa kujitetea na kuzilinda mali zake. Punde si punde yule aliyewasili akaitwaa Biblia, akasoma sura moja kwa sauti, kisha akapiga magoti akaomba. Msafiri akaziacha hofu zake, akaiweka bastola yake kando, akajilaza, akalala kwa amani mpaka nuru ya asubuhi. Na hayo yote ni kwa sababu Biblia ilikuwamo kibandani, na mwenyewe alikuwa mtu wa maombi.” — MCHUNGAJI F. F. SHOUP.

MAOMBI yana uhusiano kamili na kufanikiwa kwa kuhubiriwa kwa Neno. Jambo hili Paulo analifundisha waziwazi katika ombi lile linalojulikana na lenye msisitizo alilowapa Wathesalonike:

“Hatimaye, ndugu, tuombeeni, ili neno la Bwana lipate kuenea na kutukuzwa.”

Maombi hufungua njia ili Neno la Mungu liende bila kizuizi wala pingamizi, na huumba mazingira yanayofaa ili neno litimize kusudi lake. Maombi huliwekea Neno la Mungu magurudumu, na humpa mabawa malaika wa Bwana “mwenye Injili ya milele, awahubirie wakaao juu ya nchi, kila taifa na kabila na lugha na jamaa.” Maombi hulisaidia sana Neno la Bwana.

Mfano wa Mpanzi ni somo mashuhuri juu ya kuhubiri, ukionyesha matokeo yake yanayotofautiana na kueleza aina mbalimbali za wasikilizaji. Wasikilizaji wa kando ya njia ni wengi mno. Udongo umelala bila kutayarishwa kwa kutafakari au kwa maombi yaliyotangulia; kwa sababu hiyo, Ibilisi huichukua mbegu kwa urahisi (ambayo ndiyo Neno la Mungu), na kwa kuzitawanya mvuto wote mwema, huifanya kazi ya mpanzi kuwa bure. Hakuna hata mmoja anayeamini kwa kitambo kwamba upanzi mwingi hivi wa siku hizi ungekosa kuzaa matunda, kama wasikilizaji wangeitayarisha tu ardhi ya mioyo yao mapema kwa maombi na kutafakari.

Vivyo hivyo na wasikilizaji wa penye miamba, na wasikilizaji wa penye miiba. Ingawa neno hukaa mioyoni mwao na kuanza kuchipuka, lakini yote hupotea, hasa kwa sababu hakuna maombi wala kukesha wala kupalilia kunakofuata. Wasikilizaji wa udongo mzuri hufaidika na upanzi kwa sababu tu akili zao zimetayarishwa kuipokea mbegu, na kwamba, baada ya kusikia, wameipalilia mbegu iliyopandwa mioyoni mwao kwa kudumu katika maombi. Hayo yote yanaupa mkazo wa pekee mwisho wa mfano huu wa kushangaza: “Jiangalieni basi jinsi msikiavyo.” Na ili sisi tujiangalie jinsi tunavyosikia, ni lazima tujitoe daima kwa maombi.

Hatuna budi kuamini kwamba chini ya Neno la Mungu kuna maombi, na kwamba kufanikiwa kwake hatimaye kutategemea maombi. Katika Kitabu cha Isaya twasoma:

“Ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.”

Katika Zaburi 19, Daudi analitukuza Neno la Mungu kwa kauli sita juu yake. Huiponya nafsi, huwatia hekima wanyofu, huufurahisha moyo, huyatia macho nuru, hudumu milele, nalo ni kweli na la haki kabisa. Neno la Mungu ni kamilifu, ni amini, ni la adili, ni safi. Huuchunguza moyo, na wakati uo huo hutakasa katika matokeo yake. Kwa hiyo si ajabu kwamba, baada ya kuutafakari utu wa kiroho wa ndani wa Neno la Mungu, uweza wake wa kuuchunguza utu wa ndani wa mwanadamu, na usafi wake mkuu, Mtunga Zaburi aimalize hoja yake kwa fungu hili:

“Ni nani awezaye kuyatambua makosa yake?” Kisha akiomba hivi: “Unitakase na mambo ya siri. Umzuie mtumishi wako, asije akatenda dhambi za kiburi; nazo zisinitawale. Maneno ya kinywa changu, na mawazo ya moyo wangu, yapate kibali mbele zako, Ee Bwana, mwamba wangu, na mkombozi wangu.”

Yakobo anatambua utu wa kiroho wa ndani wa Neno, na uweza wake wa asili wa kuokoa, katika mawaidha yafuatayo:

“Kwa hiyo wekeni mbali uchafu wote na wingi wa uovu, mkipokee kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu.”

Naye Petro anazungumza kwa namna hiyo hiyo, anapoeleza uweza wa Neno la Mungu wa kuokoa:

“Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika, kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele.”

Si tu kwamba Petro anazungumza juu ya kuzaliwa mara ya pili kwa Neno la Mungu lisiloharibika, bali anatujulisha kwamba ili kukua katika neema hatuna budi kuwa kama watoto wachanga waliozaliwa sasa, tukiyatamani, au kujilisha kwa, “maziwa yasiyoghoshiwa ya Neno.”

Hata hivyo, hii haimaanishi kwamba umbo tupu la maneno kama yalivyo katika Biblia lina ndani yake nguvu yo yote ya kuokoa. Lakini Neno la Mungu, na ikumbukwe, limejazwa Roho Mtakatifu. Na kama vile kulivyo na sehemu ya Kimungu katika maneno ya Maandiko, ndivyo sehemu hiyo hiyo ya Kimungu inavyopatikana katika kila mahubiri ya kweli ya Neno, yawezayo kuokoa na kuiongoa nafsi.

Maombi daima huzaa upendo kwa Neno la Mungu, na huwafanya watu walisome. Maombi huwaongoza watu kulitii Neno la Mungu, na hutia ndani ya moyo utiio furaha isiyoneneka. Watu waombao na watu wasomao Biblia ni watu wa aina moja. Mungu wa Biblia na Mungu wa maombi ni mmoja. Mungu husema na mwanadamu katika Biblia; mwanadamu husema na Mungu katika maombi. Mtu husoma Biblia ili ayajue mapenzi ya Mungu; huomba ili apokee nguvu ya kuyatenda mapenzi hayo. Kusoma Biblia na kuomba ndizo alama bainifu za wale wanaojitahidi kumjua Mungu na kumpendeza. Na kama vile maombi yanavyozaa upendo kwa Maandiko, na kuwafanya watu waisome Biblia, ndivyo pia maombi yanavyowafanya wanaume na wanawake waende nyumbani mwa Mungu, kuyasikia Maandiko yakifafanuliwa. Kwenda kanisani kunahusiana kwa karibu na Biblia, si sana kwa sababu Biblia inatuonya tusiache “kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine,” bali kwa sababu katika nyumba ya Mungu, mhudumu wa Mungu aliyechaguliwa hulitangaza Neno lake kwa watu wanaokufa, huyafafanua Maandiko, na kuyatilia nguvu mafundisho yake kwa wasikilizaji wake. Na maombi huotesha azimio, ndani ya wale wanaoyazoea, la kutoiacha nyumba ya Mungu.

Maombi huzaa dhamiri ya kwenda kanisani, moyo upendao kanisa, roho ya kulitegemeza kanisa. Ni watu waombao wanaoufanya kuwa jambo la dhamiri kuhudhuria kuhubiriwa kwa Neno; wanaofurahia kusomwa kwake na kufafanuliwa kwake; wanaolitegemeza kwa mvuto wao na kwa mali zao. Maombi hulitukuza Neno la Mungu na kulipa nafasi ya kwanza katika makadirio ya wale wanaoliitia Jina la Bwana kwa uaminifu na kwa moyo wote.

Maombi huupata uhai wake wenyewe kutoka katika Biblia, wala hayana mahali pa kusimama nje ya kibali cha Maandiko. Kuwapo kwake na tabia yake vinategemea ufunuo uliotolewa na Mungu kwa mwanadamu katika Neno lake takatifu. Maombi nayo, kwa upande wake, huutukuza ufunuo huo huo, na kuwageuza watu walielekee Neno hilo. Asili, ulazima na tabia ya maombi inayokumbatia yote, vimejengwa juu ya Neno la Mungu.

Zaburi 119 ni mwongozo wa Neno la Mungu. Isipokuwa mistari mitatu au minne, kila mstari una neno linalolitaja, au kulionyesha, Neno la Mungu. Mara nyingi mwandishi hububujika katika dua, akiomba mara kadhaa, “Unifundishe amri zako.” Ameguswa sana na maajabu ya Neno la Mungu, na hitaji la nuru ya Kimungu ya kuyaona na kuyaelewa mambo ya ajabu yaliyoandikwa humo, hata anaomba kwa bidii:

“Unifumbue macho yangu nipate kuyaona maajabu yatokayo katika sheria yako.”

Tangu mwanzo wa Zaburi hii ya ajabu hadi mwisho wake, maombi na Neno la Mungu vimesokotwa pamoja. Karibu kila upande wa Neno la Mungu unaguswa na mwandishi huyu aliyevuviwa. Mtunga Zaburi alikuwa amesadiki kabisa uweza wa kiroho wa ndani wa Neno la Mungu, hata akatoa tamko hili:

“Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, nisije nikakutenda dhambi.”

Hapa Mtunga Zaburi aliipata kinga yake dhidi ya kutenda dhambi. Kwa kuwa na Neno la Mungu limefichwa moyoni mwake; kwa kuwa na utu wake wote umejaa kabisa Neno hilo; kwa kuletwa kikamilifu chini ya mvuto wake mwema na wa neema, aliwezeshwa kwenda huko na huko duniani, salama kutokana na mashambulizi ya yule Mwovu, na akiwa amelindwa dhidi ya mwelekeo wa kutangatanga nje ya njia.

Tena twaona uweza wa maombi wa kuumba upendo halisi kwa Maandiko, na kutia ndani ya watu tabia itakayolifurahia Neno. Katika furaha takatifu anapiga kelele, “Sheria yako naipenda mno ajabu! Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa.” Na tena: “Jinsi maneno yako yalivyo matamu kwangu! Naam, matamu kupita asali kinywani mwangu.”

Je, tungependa kulionea ladha Neno la Mungu? Basi na tujitoe daima kwa maombi. Yeye atakaye kuwa na moyo wa kusoma Biblia hana budi — hathubutu — kusahau kuomba. Mtu ambaye yaweza kusemwa juu yake, “Sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,” ndiye mtu awezaye kusema kwa kweli, “Napenda kwenda mahali pa maombi.” Hakuna mtu aipendaye Biblia asiyependa kuomba. Hakuna mtu apendaye kuomba asiyefurahia sheria ya Bwana.

Bwana wetu alikuwa mtu wa maombi, naye alilitukuza Neno la Mungu, akinukuu Maandiko mara nyingi. Katika maisha yake yote ya duniani Yesu aliishika Sabato, alikwenda katika nyumba ya ibada, na kulisoma Neno la Mungu, na maombi yalichanganyika na hayo yote:

“Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome.”

Hapa na isemwe kwamba hakuna mambo mawili yaliyo ya lazima zaidi kwa maisha yaliyojazwa Roho kuliko kusoma Biblia na maombi ya siri; hakuna mambo mawili yasaidiayo zaidi kwa kukua katika neema; kwa kupata furaha iliyo kuu kabisa katika maisha ya Kikristo; kwa kumthibitisha mtu katika njia za amani ya milele. Kupuuzwa kwa wajibu huu muhimu kabisa hutabiri kukonda kwa nafsi, kupotea kwa furaha, kukosekana kwa amani, ukavu wa roho, kuoza katika yote yahusuyo maisha ya kiroho. Kuyapuuza mambo haya hutayarisha njia ya ukengeufu, na humpa yule Mwovu nafasi ambayo hana uwezekano wa kuiacha. Kulisoma Neno la Mungu kwa utaratibu, na kuomba kwa mazoea mahali pa siri pake Aliye juu, humweka mtu mahali ambapo yu salama kabisa kutokana na mashambulizi ya adui wa roho za watu, na humhakikishia wokovu na ushindi wa mwisho, kwa uweza ushindao wa Mwanakondoo.

Umemaliza Maombi na Neno la Mungu (Inaendelea)