Sura 44 · dakika 1 za kusoma · dakika 1 za kusikiliza
Maagizo ya mitume
Mitume wetu nao walijua, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba kungekuwa na ugomvi kwa ajili ya cheo cha uaskofu. Basi kwa sababu hii, kwa kuwa walikuwa wamepata kujua jambo hili mapema kikamilifu, waliwaweka wale [wahudumu] waliokwisha kutajwa, kisha wakatoa maagizo kwamba hao watakapolala usingizi wa mauti, watu wengine waliothibitika wapokee huduma yao. Kwa hiyo tuna maoni kwamba wale waliowekwa nao, au baadaye na watu wengine mashuhuri, kwa ridhaa ya Kanisa zima, na ambao wamelihudumia kundi la Kristo bila lawama, kwa roho ya unyenyekevu, ya amani na isiyo na tamaa ya faida, na ambao kwa muda mrefu wameshuhudiwa vema na wote, hawawezi kwa haki kuondolewa katika huduma. Kwa maana dhambi yetu haitakuwa ndogo, tukiwaondoa katika uaskofu wale ambao wameitimiza kazi yake bila lawama na kwa utakatifu. Heri wale wazee ambao, wakiisha kumaliza mwendo wao kabla ya sasa, wamepata kuondoka [katika ulimwengu huu] kwa kuzaa matunda na kwa ukamilifu; kwa maana hawana hofu kwamba mtu atawaondoa katika mahali walipowekewa sasa. Lakini tunaona kwamba ninyi mmewaondoa katika huduma baadhi ya watu wenye mwenendo bora, huduma waliyoitimiza bila lawama na kwa heshima.