Sura 5 · dakika 21 za kusoma · dakika 26 za kusikiliza
Kwa nini mambo yote hufanya kazi kwa mema
1. Sababu kuu inayofanya mambo yote yafanye kazi kwa mema, ni uhusiano wa karibu na wa thamani alio nao Mungu na watu wake. Bwana amefanya agano nao. “Nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao” (Yeremia 32:38). Kwa nguvu ya agano hilo, mambo yote hufanya kazi, tena hayana budi kufanya kazi, kwa mema yao. “Mimi ndimi Mungu, Mungu wako” (Zaburi 50:7). Neno hili, ‘Mungu wako,’ ndilo neno tamu kuliko yote katika Biblia; linaonyesha mahusiano yaliyo bora kuliko yote; na haiwezekani kuwe na mahusiano haya kati ya Mungu na watu wake, kisha kila jambo lisifanye kazi kwa mema yao. Usemi huu, ‘Mimi ni Mungu wako,’ unaonyesha,
(1). Uhusiano wa tabibu: ‘Mimi ni Tabibu wako.’ Mungu ni Tabibu stadi. Yeye anajua lililo bora. Mungu huzitazama tabia mbalimbali za wanadamu, naye anajua ni nini kitakachofanya kazi kwa nguvu zaidi. Wengine wana tabia ya upole zaidi, nao huvutwa kwa rehema. Wengine ni kama vipande vya mti vigumu vyenye mafundo; hao Mungu huwashughulikia kwa njia ya nguvu zaidi. Vitu vingine huhifadhiwa katika sukari, vingine katika maji ya chumvi. Mungu hawatendei wote sawasawa; ana majaribu kwa wenye nguvu na dawa za kutia moyo kwa walio dhaifu. Mungu ni Tabibu mwaminifu, kwa hiyo atageuza yote kuwa kwa mema. Kama Mungu hakupi kile unachokipenda, atakupa kile unachokihitaji. Tabibu hajishughulishi sana kuifurahisha ladha ya mgonjwa, bali kuuponya ugonjwa wake. Tunalalamika kwamba majaribu makali sana yametulemea; na tukumbuke kwamba Mungu ni Tabibu wetu, kwa hiyo anajitahidi zaidi kutuponya kuliko kutubembeleza. Mungu anavyowatendea watoto wake, ingawa ni kwa ukali, ni salama, tena ni kwa ajili ya kuwaponya; “ili akufanyie mema mwisho wako” (Kumbukumbu la Torati 8:16).
(2). Neno hili, ‘Mungu wako’, linaonyesha uhusiano wa Baba. Baba humpenda mtoto wake; kwa hiyo likiwa ni tabasamu au ni pigo, ni kwa mema ya mtoto. Mimi ni Mungu wako, Baba yako, kwa hiyo yote ninayoyafanya ni kwa mema yako. “Kama vile mtu amrudivyo mwanawe, ndivyo Bwana Mungu wako akurudivyo wewe” (Kumbukumbu la Torati 8:5). Kurudi kwa Mungu si kwa kuangamiza bali kwa kurekebisha. Mungu hawezi kuwadhuru watoto wake, kwa maana yeye ni Baba mwenye moyo wa huruma, “Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao” (Zaburi 103:13). Je! baba atatafuta maangamizi ya mtoto wake, mtoto aliyetoka kwake mwenyewe, aichukuaye sura yake? Uangalifu wake wote na mipango yake yote ni kwa ajili ya mtoto wake: je! humwachia nani urithi, ila mtoto wake? Mungu ndiye “Baba wa rehema” mwenye moyo wa huruma (2 Wakorintho 1:3). Yeye ndiye azaaye rehema zote na wema wote ulio katika viumbe.
Mungu ni Baba wa milele (Isaya 9:6). Alikuwa Baba yetu tangu milele; kabla hatujawa watoto, Mungu alikuwa Baba yetu, naye atakuwa Baba yetu hata milele. Baba humtunza mtoto wake maadamu yu hai; lakini baba hufa, na hapo mtoto aweza kuachwa wazi kwa madhara. Lakini Mungu hakomi kamwe kuwa Baba. Wewe uliye mwamini, una Baba asiyekufa kamwe; na ikiwa Mungu ni baba yako, huwezi kamwe kuangamia. Mambo yote hayana budi kufanya kazi kwa mema yako.
(3). Neno hili, ‘Mungu wako,’ linaonyesha uhusiano wa Mume. Huu ni uhusiano wa karibu na mtamu. Mume hutafuta mema ya mkewe; angekuwa mtu asiye na utu yule ambaye angejaribu kumwangamiza mke wake. “Maana hakuna mtu aliyeuchukia mwili wake wakati wowote,” (Waefeso 5:29). Kuna uhusiano wa ndoa kati ya Mungu na watu wake. “Muumba wako ndiye mume wako” (Isaya 54:5). Mungu huwapenda watu wake kwa moyo wote. Huwachora katika vitanga vya mikono yake (Isaya 49:16). Huwaweka kama muhuri juu ya kifua chake (Wimbo Ulio Bora 8:6). Atatoa falme kuwa fidia yao (Isaya 43:3). Hilo laonyesha jinsi walivyo karibu na moyo wake. Ikiwa yeye ni Mume ambaye moyo wake umejaa upendo, basi atatafuta mema ya mkewe. Ama atalizuia dhara, ama ataligeuza kuwa kwa mema.
(4). Neno hili, ‘Mungu wako,’ linaonyesha uhusiano wa Rafiki. “Huyu ndiye rafiki yangu” (Wimbo Ulio Bora 5:16). Rafiki, kama asemavyo Augustino, ni nusu ya nafsi ya mtu. Hujitahidi na kutamani jinsi atakavyomtendea rafiki yake mema; huistawisha hali yake kama yake mwenyewe. Yonathani alihatarisha kukasirikiwa na mfalme kwa ajili ya rafiki yake Daudi (1 Samweli 19:4). Mungu ni Rafiki yetu, kwa hiyo atageuza mambo yote kuwa kwa mema yetu. Kuna marafiki wa uongo; Kristo alisalitiwa na rafiki: lakini Mungu ndiye Rafiki aliye bora kuliko wote.
Yeye ni Rafiki mwaminifu. “Basi jua ya kuwa Bwana, Mungu wako, ndiye Mungu; Mungu mwaminifu” (Kumbukumbu la Torati 7:9). Yeye ni mwaminifu katika upendo wake. Alitupa moyo wake hasa, alipotupa Mwana kutoka kifuani mwake. Hapo palikuwa na kielelezo cha upendo kisicho na mfano. Yeye ni mwaminifu katika ahadi zake. “Mungu, asiyeweza kusema uongo, aliahidi” (Tito 1:2). Aweza kuibadili ahadi yake, lakini hawezi kuivunja. Yeye ni mwaminifu katika matendo yake; hata anapotutesa yeye ni mwaminifu. “Kwa uaminifu umenitesa” (Zaburi 119:75). Anatupepeta na kutusafisha kama fedha (Zaburi 66:10).
Mungu ni Rafiki asiyebadilika. “Sitakuachilia kamwe hata kidogo, na kamwe, kamwe sitakutelekeza” (Waebrania 13:5). Marafiki mara nyingi huangusha wakati wa shida. Wengi huwatendea rafiki zao kama wanawake wanavyoyatendea maua; maadamu ni mabichi huyaweka vifuani mwao, lakini yanapoanza kunyauka huyatupa. Au kama msafiri anavyoitendea saa ya jua; jua likiiangazia saa hiyo, msafiri ataiacha njia, na kuitazama saa: lakini jua lisipoiangazia, atapita tu, wala hataiangalia kabisa. Vivyo hivyo, ufanisi ukiwaangazia watu, rafiki watawatazama; lakini wingu la taabu likiwa juu yao, hawatawakaribia. Lakini Mungu ni Rafiki milele; amesema, “Sitakuachilia kamwe hata kidogo.” Ingawa Daudi alipita katika uvuli wa mauti, alijua kwamba alikuwa na Rafiki karibu naye. “Sitaogopa mabaya, kwa maana Wewe upo pamoja nami” (Zaburi 23:4). Mungu hauondoi kamwe upendo wake wote kwa watu wake. “Aliwapenda hata mwisho” (Yohana 13:1). Kwa kuwa Mungu ni Rafiki wa namna hiyo, atafanya mambo yote yafanye kazi kwa mema yetu. Hakuna rafiki asiyetafuta mema ya rafiki yake.
(5). Neno hili, ‘Mungu wako,’ linaonyesha uhusiano ulio karibu zaidi tena, yaani uhusiano kati ya Kichwa na viungo. Kuna muungano wa siri kati ya Kristo na watakatifu. Yeye anaitwa “kichwa cha kanisa” (Waefeso 5:23). Je! kichwa hakishughuliki na mema ya mwili? Kichwa huuongoza mwili, huona uchungu pamoja nao, ni chemchemi ya nguvu za uhai, hupeleka nguvu na faraja ndani ya mwili. Sehemu zote za kichwa zimewekwa kwa mema ya mwili. Jicho limewekwa kana kwamba katika mnara wa ulinzi; husimama kama mlinzi ili kuona hatari yoyote inayoweza kuujia mwili, na kuizuia. Ulimi ni mwonjaji, tena ni msemaji. Ikiwa mwili ni ulimwengu mdogo, kichwa ndicho jua katika ulimwengu huu, ambamo hutoka nuru ya akili. Kichwa kimewekwa kwa mema ya mwili. Kristo na watakatifu ni mwili mmoja wa kiroho. Kichwa chetu kiko mbinguni, na hakika hataruhusu mwili wake udhuriwe, bali atashughulikia usalama wake, na kufanya mambo yote yafanye kazi kwa mema ya mwili huo wa kiroho.
2. Mafundisho yatokanayo na kweli hii, kwamba mambo yote hufanya kazi kwa mema ya watakatifu.
(1). Ikiwa mambo yote hufanya kazi kwa mema, jifunzeni hapa kwamba kuna maongozi ya Mungu. Mambo hayafanyi kazi yenyewe, bali Mungu huyaweka kufanya kazi kwa mema. Mungu ndiye Mpangaji mkuu wa matukio yote na matokeo yake; yeye huweka kila kitu kufanya kazi. “Na ufalme wake unatawala juu ya vitu vyote” (Zaburi 103:19). Hili linanenwa juu ya ufalme wake wa maongozi. Mambo ya ulimwengu hayatawaliwi na visababishi vya pili, wala na mashauri ya wanadamu, wala na nyota na sayari, bali na maongozi ya Mungu. Maongozi ndiyo malkia na mtawala wa ulimwengu. Kuna mambo matatu katika maongozi: Mungu kujua mapema, Mungu kuamua, na Mungu kuyaelekeza mambo yote kwenye nyakati zake na matokeo yake. Mambo yoyote yafanyayo kazi ulimwenguni, Mungu ndiye anayeyaweka kufanya kazi. Tunasoma katika sura ya kwanza ya Ezekieli habari za magurudumu, na macho ndani ya magurudumu, na mwendo wa magurudumu. Magurudumu ni ulimwengu wote, macho ndani ya magurudumu ni maongozi ya Mungu, mwendo wa magurudumu ni mkono wa Maongozi, unaoyageuza mambo yote ya hapa chini. Kile ambacho wengine hukiita bahati si kitu kingine ila matokeo ya maongozi.
Jifunzeni kuyastahi maongozi ya Mungu kwa kicho. Maongozi yana mvuto juu ya mambo yote ya hapa chini. Ndiyo yanayochanganya viungo, na kuutengeneza mchanganyiko wote.
(2). Angalieni hali ya heri ya kila mtoto wa Mungu. Mambo yote hufanya kazi kwa mema yake, yaliyo bora na yaliyo mabaya kabisa. “Kwa wanyofu huzuka nuru gizani” (Zaburi 112:4). Maongozi ya Mungu yaliyo na giza na mawingu mengi kuliko yote yana mwanga wa jua ndani yake. Mwamini wa kweli yuko katika hali ya heri jinsi gani! Afapo, huenda kwa Mungu: na maadamu yu hai, kila kitu kitamfanyia mema. Dhiki ni kwa mema yake. Moto unaidhuru dhahabu kwa nini? Unaisafisha tu. Pepeto linaidhuru nafaka kwa nini? Linatenganisha tu makapi nayo. Ruba wanaudhuru mwili kwa nini? Wanafyonza tu damu mbaya. Mungu hatumii kamwe fimbo yake ila kwa kupiga vumbi litoke. Dhiki hufanya kile ambacho mara nyingi Neno halitafanya; “huyafunua masikio yao wapate maonyo” (Ayubu 36:10). Mungu anapowalaza watu chali, hapo ndipo wanapotazama juu mbinguni. Mungu kuwapiga watu wake ni kama mwanamuziki anavyoipiga fidla, nayo hutoa sauti tamu ya kupendeza. Ni mema mengi jinsi gani yanayowajia watakatifu kwa njia ya dhiki! Wanapotwangwa na kuvunjwa, ndipo hutoa harufu yao nzuri kuliko zote. Dhiki ni shina chungu, lakini huzaa tunda tamu. “Huzaa matunda ya haki yenye amani” (Waebrania 12:11). Dhiki ndiyo njia kuu ya kwenda mbinguni; ingawa ina mawe magumu na miiba, bado ndiyo njia iliyo bora. Umaskini utazifisha njaa dhambi zetu; ugonjwa utaifanya neema iwe ya msaada zaidi (2 Wakorintho 4:16). Lawama zitamfanya “Roho wa Mungu na wa utukufu” atukalie (1 Petro 4:14). Mauti itaifunga chupa ya machozi, na kulifungua lango la Paradiso. Siku ya kufa kwake mwamini ndiyo siku yake ya kupaa kwenda utukufuni. Ndiyo sababu watakatifu wameziweka dhiki zao katika orodha ya mali zao (Waebrania 11:26). Themistokles, alipofukuzwa kutoka nchi yake mwenyewe, baadaye alipata kibali kwa mfalme wa Misri, ndipo akasema, “Ningalipotea, kama nisingalipotea.” Vivyo hivyo mtoto wa Mungu aweza kusema, “ Kama nisingalitaabishwa, ningaliangamizwa; kama afya yangu na mali yangu visingalipotea, roho yangu ingalipotea.”
(3). Basi angalieni hapa kuna kitia-moyo kilichoje cha kuwa wacha Mungu. Mambo yote yatafanya kazi kwa mema. Laiti jambo hili lingeuvuta ulimwengu kuipenda dini! Je! kunaweza kuwa na sumaku kubwa zaidi ya kuvutia utauwa? Je! kuna kitu kinachoweza kutushawishi zaidi kuwa wema kuliko hiki: kwamba mambo yote yatafanya kazi kwa mema yetu? Dini ndiyo jiwe la kweli la wanafalsafa ligeuzalo kila kitu kuwa dhahabu. Chukua sehemu ya dini iliyo chungu kuliko zote, yaani sehemu ya mateso, nayo ina faraja ndani yake. Mungu huyatia mateso utamu kwa furaha; huipaka pakanga yetu sukari. Lo, jinsi jambo hili linavyoweza kutuvuta kwa utauwa! “Basi patana naye Mungu, upate amani; kwa njia hiyo mema yatakujilia” (Ayubu 22:21). Hakuna mtu aliyewahi kupata hasara kwa kujuana na Mungu. Kwa njia hiyo mema yatakujilia, mema tele, matone matamu ya neema, mana iliyofichwa, naam, kila kitu kitafanya kazi kwa mema. Basi, jitahidini kujuana na Mungu, mshike upande wake.
(4). Angalieni hali ya taabu ya watu waovu. Kwa walio wacha Mungu, mambo mabaya hufanya kazi kwa mema; kwa walio waovu, mambo mema hufanya kazi kwa madhara.
(i.) Mambo mema ya kidunia hufanya kazi kwa madhara ya waovu. Mali na ufanisi si faida bali ni mitego, kama asemavyo Seneka. Mambo ya dunia hupewa waovu, kama Mikali alivyopewa Daudi, ili awe mtego (1 Samweli 18:21). Inasemekana kwamba tai mla mizoga hupata ugonjwa kutokana na manukato: ndivyo waovu wanavyopata ugonjwa kutokana na manukato matamu ya ufanisi. Rehema zao ni kama mkate wenye sumu wanaopewa mbwa; meza zao zimeandaliwa kwa fahari, lakini kuna ndoano chini ya chambo: “Meza yao mbele yao na iwe tanzi” (Zaburi 69:22). Starehe zao zote ni kama kware wa Israeli, waliokolezwa ghadhabu ya Mungu (Hesabu 11:33). Kiburi na anasa ni mapacha wa ufanisi. “Umenenepa” (Kumbukumbu la Torati 32:15). Hapo akamwacha Mungu. Mali si kama utando wa buibui tu, usio na faida, bali kama yai la fira, lenye kuangamiza. “Mali iliyowekwa akiba na mwenyewe kwa hasara yake” (Mhubiri 5:13). Rehema za kawaida walizo nazo watu waovu si sumaku za kuwavuta karibu zaidi na Mungu, bali ni mawe ya kusagia ya kuwazamisha chini zaidi jehanamu (1 Timotheo 6:9). Vyakula vyao vitamu ni kama karamu ya Hamani; baada ya karamu zao zote za kifalme, mauti italeta hesabu, nao hawana budi kuilipa jehanamu.
(ii.) Mambo mema ya kiroho hufanya kazi kwa madhara ya waovu. Kutoka katika ua la baraka za mbinguni wao hufyonza sumu.
Watumishi wa Mungu hufanya kazi kwa madhara yao. Upepo uleule unaoipeleka meli moja bandarini, huipeleka meli nyingine juu ya mwamba. Pumzi ileile ya huduma inayompeleka mcha Mungu mbinguni, humpeleka mwenye dhambi asiyemcha Mungu jehanamu. Wale wanaokuja na neno la uzima vinywani mwao, hata hivyo kwa wengi ni harufu ya mauti. “Uunenepeshe moyo wa watu hawa, ukayafanye mazito masikio yao” (Isaya 6:10). Nabii alitumwa kwa ujumbe wa huzuni, kuhubiri mahubiri ya mazishi yao. Watu waovu huwa wabaya zaidi kwa kuhubiriwa. “Wanamchukia yeye akemeaye langoni” (Amosi 5:10). Wenye dhambi huzidi kukaza nia katika dhambi; Mungu na aseme apendavyo, wao watafanya wapendavyo. “Katika habari ya neno lile ulilotuambia kwa jina la Bwana, hatutakusikiliza wewe” (Yeremia 44:16). Neno linalohubiriwa haliwaponyi, bali linawafanya kuwa wagumu. Na ni jambo la kutisha jinsi gani watu kuzamishwa jehanamu wakiwa wamesheheni mahubiri!
Maombi hufanya kazi kwa madhara yao. “Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana” (Mithali 15:8). Mtu mwovu yuko katika mbano mkubwa: asipoomba, anatenda dhambi; akiomba, anatenda dhambi, “Na sala yake iwe dhambi” (Zaburi 109:7). Ingekuwa hukumu ya huzuni kama chakula chote anachokula mtu kingegeuka kuwa majimaji mabaya, na kuzaa magonjwa mwilini: ndivyo ilivyo kwa mtu mwovu. Ombi lile ambalo lingemfanyia mema, hufanya kazi kwa madhara yake; anaomba dhidi ya dhambi, kisha anatenda dhambi dhidi ya ombi lake; ibada zake zimetiwa doa la ukafiri, zimeoza kwa unafiki kama nyama iliyotagiwa na nzi. Mungu huzichukia.
Meza ya Bwana hufanya kazi kwa madhara yao. “Hamwezi kushiriki meza ya Bwana na meza ya mashetani. Au twamtia Bwana wivu?” (1 Wakorintho 10:21, 22). Baadhi ya waliokiri imani walishika karamu zao za sanamu, hata hivyo walitaka kuja kwenye meza ya Bwana. Mtume asema, “Je! mnamtia Bwana ghadhabu?” Watu wasiomcha Mungu hufanya karamu pamoja na dhambi zao; hata hivyo watakuja kufanya karamu kwenye meza ya Bwana. Huku ni kumchokoza Mungu. Kwa mwenye dhambi kuna mauti katika kikombe, yeye “hula na kunywa hukumu ya nafsi yake” (1 Wakorintho 11:29). Hivyo Meza ya Bwana hufanya kazi kwa madhara ya wenye dhambi wasiotubu. Baada ya tonge, Ibilisi huingia.
Kristo mwenyewe hufanya kazi kwa madhara ya wenye dhambi wakaidi kabisa. Yeye ni “jiwe la kujikwaza mguu, na mwamba wa kuangusha” (1 Petro 2:8). Yuko hivyo kwa sababu ya upotovu wa mioyo ya watu; kwa maana badala ya kumwamini, wanachukizwa naye. Jua, ingawa kwa asili yake ni safi na la kupendeza, hata hivyo linadhuru macho yenye vidonda. Yesu Kristo amewekwa kwa kuanguka, na kwa kuinuka, kwa wengi (Luka 2:34). Wenye dhambi hujikwaa kwa Mwokozi, na kuchuma mauti kutoka katika mti wa uzima. Kama vile mafuta ya dawa yanavyowaponya wagonjwa wengine, lakini kuwaua wengine, ndivyo damu ya Kristo, ingawa kwa wengine ni dawa, kwa wengine ni hukumu. Hapa ndipo ilipo taabu isiyo na mfano ya wale wanaoishi na kufa katika dhambi. Mambo yaliyo bora kuliko yote hufanya kazi kwa madhara yao; hata dawa za kutia nguvu zenyewe huua.
(5). Oneni hapa hekima ya Mungu, awezaye kuyafanya mambo mabaya kabisa yanayowazika yageuke kuwa kwa mema ya watakatifu. Kwa kemia ya kimungu anaweza kutoa dhahabu kutoka katika takataka za madini. “Ee kina cha hekima ya Mungu!” (Warumi 11:33). Ni kusudi kuu la Mungu kuonyesha ajabu ya hekima yake. Bwana alilifanya gereza la Yusufu kuwa ngazi ya kupandishwa cheo. Hapakuwa na njia ya Yona kuokolewa, ila kwa kumezwa. Mungu aliwaacha Wamisri wawachukie Israeli (Zaburi 106:41), na hilo likawa njia ya kuokolewa kwao. Mtakatifu Paulo alifungwa kwa mnyororo, na mnyororo ule uliomfunga ukawa njia ya kuieneza Injili (Wafilipi 1:12). Mungu hutajirisha kwa kufukarisha; huiongeza neema kwa kupunguza mali. Kiumbe kinapokwenda mbali nasi, ni ili Kristo apate kuja karibu nasi. Mungu hufanya kazi kwa njia za ajabu. Huleta utaratibu kutoka katika machafuko, upatano kutoka katika mafarakano. Mara nyingi huwatumia watu wasio haki kufanya lililo haki. “Yeye ni mwenye moyo wa hekima” (Ayubu 9:4). Anaweza kuvuna utukufu wake kutoka katika ghadhabu ya wanadamu (Zaburi 76:10). Ama waovu hawatafanya madhara wanayoyakusudia, ama watafanya mema wasiyoyakusudia. Mara nyingi Mungu husaidia wakati ambapo tumaini ni dogo kabisa, na huwaokoa watu wake kwa njia ile wanayodhani itawaangamiza. Aliutumia uovu wa kuhani mkuu na usaliti wa Yuda kuukomboa ulimwengu. Kwa hasira isiyo na busara, tuko tayari kuyalaumu mambo yanayotokea: hiyo ni kana kwamba mtu asiyesoma angeihukumu falsafa, au kipofu angeilaumu kazi ya mchoraji katika picha ya mandhari. “Mtu mtupu angetaka kuwa na hekima” (Ayubu 11:12). Viumbe wapumbavu hutaka kuyalaumu Maongozi, na kuiita hekima ya Mungu mbele ya kizimba cha akili. Njia za Mungu “hazitafutikani” (Warumi 11:33). Zinastahili kustaajabiwa kuliko kupimwa kina chake. Hakuna hata maongozi moja ya Mungu, ila yana rehema au ajabu ndani yake. Ni ya kushangaza na isiyo na mipaka jinsi gani hekima ile, inayoyafanya maongozi yaliyo kinyume kabisa yafanye kazi kwa mema ya watoto wake!
(6). Jifunzeni basi jinsi tulivyo na sababu ndogo ya kunung’unika juu ya majaribu ya nje na dharura! Nini! Kunung’unika juu ya kile kitakachotufanyia mema! Mambo yote yatafanya kazi kwa mema. Hakuna dhambi ambazo watu wa Mungu huelekea kuziangukia zaidi kuliko kutoamini na kukosa subira. Wako tayari ama kuzimia kwa kutoamini, ama kukasirika kwa kukosa subira. Watu wanapomwasi Mungu kwa manung’uniko na kukosa subira ni dalili kwamba hawaliamini neno hili. Manung’uniko ni dhambi ya kukosa shukrani, kwa sababu tuna rehema nyingi kuliko dhiki; tena ni dhambi isiyo na akili, kwa sababu dhiki hufanya kazi kwa mema. Manung’uniko ni dhambi inayotusukuma kwenye dhambi. “Usikasirike kwa vyo vyote” (Zaburi 37:8), kwa maana mwisho wa kukasirika ni kutenda mabaya. Anayekasirika atakuwa tayari kutenda mabaya: Yona aliyekasirika alikuwa Yona aliyetenda dhambi (Yona 4:9). Ibilisi hupuliza makaa ya hasira na manung’uniko, kisha huota moto huo. Lo, tusimlee nyoka huyu mwenye hasira kifuani mwetu. Neno hili na lizae subira, “katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema” (Warumi 8:28). Je! tutanung’unika juu ya kile kinachofanya kazi kwa mema yetu? Kama rafiki mmoja angemtupia mwenzake mfuko wa fedha, na katika kuutupa, ukamchubua kichwa, hangesumbuka sana, akiona kwamba kwa njia hiyo amepata mfuko wa fedha. Vivyo hivyo Bwana aweza kutuchubua kwa dhiki, lakini ni ili atutajirishe. Dhiki hizi zinatufanyia uzito wa utukufu, nasi je! tutanung’unika?
(7). Oneni hapa Andiko lile likitimizwa, “Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli” (Zaburi 73:1). Tunapoyatazama maongozi yaliyo kinyume, na kumwona Bwana akiwafunika watu wake kwa majivu, na “kuwalevya kwa pakanga” (Maombolezo 3:15), tunaweza kuwa tayari kuutilia shaka upendo wa Mungu, na kusema kwamba anawatendea watu wake kwa ukali. Lakini, la hasha, bado Mungu ni mwema kwa Israeli, kwa sababu hufanya mambo yote yafanye kazi kwa mema. Je! yeye si Mungu mwema, ageuzaye yote kuwa mema? Huitoa dhambi, na kuitia neema; je! hili si jema? “Tunarudiwa na Bwana, ili tusihukumiwe pamoja na dunia” (1 Wakorintho 11:32). Kina cha dhiki ni cha kutuokoa na kina cha hukumu ya milele. Na tumhesabie Mungu haki siku zote; hali yetu ya nje iwe mbaya kiasi gani, na tuseme, “Hata hivyo Mungu ni mwema.”
(8). Oneni watakatifu wana sababu gani ya kudumu katika kazi ya kushukuru. Katika jambo hili Wakristo wamepungukiwa; ingawa wamo sana katika kuomba, hata hivyo ni kidogo katika kushukuru. Mtume asema, “Shukuruni kwa kila jambo” (1 Wathesalonike 5:18). Kwa nini hivyo? Kwa sababu Mungu hufanya kila jambo lifanye kazi kwa mema yetu. Tunamshukuru tabibu, ingawa anatupa dawa chungu inayotufanya wagonjwa, kwa sababu ni ya kutufanya wazima; tunamshukuru mtu yeyote anayetutendea wema; je! hatutamshukuru Mungu, afanyaye kila jambo lifanye kazi kwa mema yetu? Mungu humpenda Mkristo mwenye shukrani. Ayubu alimshukuru Mungu alipoondoa vyote: “BWANA ameondoa; jina la BWANA libarikiwe” (Ayubu 1:21). Wengi watamshukuru Mungu anapotoa; Ayubu anamshukuru anapoondoa, kwa sababu alijua kwamba Mungu angeleta mema kutoka humo. Tunasoma habari za watakatifu wenye vinubi mikononi mwao (Ufunuo 14:2), mfano wa sifa. Tunakutana na Wakristo wengi wenye machozi machoni mwao, na malalamiko vinywani mwao: lakini ni wachache wenye vinubi mikononi mwao, wanaomsifu Mungu katika dhiki. Kushukuru katika dhiki ni kazi ya pekee ya mtakatifu. Kila ndege anaweza kuimba wakati wa majira ya kuchipua, lakini ndege wengine wataimba katikati ya majira ya baridi kali. Karibu kila mtu anaweza kushukuru katika ufanisi, lakini mtakatifu wa kweli anaweza kushukuru katika taabu. Mkristo mwema atamhimidi Mungu, si wakati wa jua kuchomoza tu, bali pia wakati wa jua kutua. Inafaa kabisa sisi, hata katika lililo baya kabisa linalotupata, kuwa na zaburi ya shukrani, kwa sababu mambo yote hufanya kazi kwa mema. Lo, dumuni sana katika kumhimidi Mungu: sisi humshukuru yeye anayetufanyia urafiki.
(9). Fikirini, ikiwa mambo mabaya kabisa hufanya kazi kwa mema ya mwamini, mambo yaliyo bora kabisa — Kristo, na mbingu — yatafanya nini! Je! haya hayatafanya kazi kwa mema zaidi sana! Ikiwa msalaba una mema mengi hivyo, taji ina nini? Ikiwa vishada vya thamani hivyo vinamea Golgotha, ni tamu jinsi gani tunda lile linalomea Kanaani? Ikiwa kuna utamu wowote katika maji ya Mara, kuna nini katika divai ya Paradiso? Ikiwa fimbo ya Mungu ina asali mwishoni mwake, fimbo yake ya enzi ya dhahabu ina nini? Ikiwa mkate wa mateso una ladha nzuri hivyo, mana ni nini? Chakula kitamu cha mbinguni ni nini? Ikiwa pigo na dharuba ya Mungu hufanya kazi kwa mema, tabasamu za uso wake zitafanya nini? Ikiwa majaribu na mateso yana sababu ya furaha ndani yake, utukufu utakuwa na nini? Ikiwa kuna mema mengi hivyo yatokayo katika mabaya, basi ni mema ya namna gani yale ambamo hakutakuwa na baya lolote? Ikiwa rehema za Mungu za kuturudi ni kubwa hivyo, rehema zake za kututia taji zitakuwaje? Basi, farijianeni kwa maneno haya.
(10). Fikirini kwamba, ikiwa Mungu hufanya mambo yote yageuke kuwa kwa mema yetu, ni haki jinsi gani sisi kuyafanya mambo yote yaelekee utukufu wake! “Fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu” (1 Wakorintho 10:31). Malaika humtukuza Mungu, huimba nyimbo za kimungu za sifa. Basi imempasa mwanadamu kiasi gani kumtukuza yeye, ambaye Mungu amemfanyia mengi kuliko malaika! Ametuheshimu kupita wao kwa kuiunganisha asili yetu na Uungu. Kristo amekufa kwa ajili yetu, wala si kwa ajili ya malaika. Bwana ametupa, si kutoka katika hazina ya kawaida ya ukarimu wake tu, bali ametutajirisha kwa baraka za agano; ametupa Roho wake. Hushughulikia hali yetu njema, hufanya kila jambo lifanye kazi kwa mema yetu; neema ya bure imeweka mpango wa wokovu wetu. Ikiwa Mungu hutafuta mema yetu, je! sisi hatutautafuta utukufu wake?
Swali. Tunawezaje kusemwa kwa haki kwamba tunamtukuza Mungu. Yeye hana mipaka katika ukamilifu wake, wala hawezi kuongezewa kitu na sisi?
Jibu. Ni kweli kwamba kwa maana halisi kabisa hatuwezi kumletea Mungu utukufu, lakini kwa maana ya Injili twaweza. Tunapofanya yote yaliyo katika uwezo wetu kuliinua jina la Mungu ulimwenguni, na kuwafanya wengine wawe na mawazo ya juu ya kicho juu ya Mungu, hilo Bwana hulihesabu kuwa ni kumtukuza; kama vile mtu anavyosemwa kumvunjia Mungu heshima, anaposababisha jina la Mungu litukanwe.
Tunasemwa kuuendeleza utukufu wa Mungu kwa njia tatu: (i.) Tunapoukusudia utukufu wake; tunapomfanya kuwa wa kwanza katika mawazo yetu, na wa mwisho katika kusudi letu. Kama mito yote inavyotiririka kuingia baharini, na mistari yote inavyokutana katikati, vivyo hivyo matendo yetu yote huishia na kukutana ndani ya Mungu. (ii.) Tunauendeleza utukufu wa Mungu kwa kuzaa matunda katika neema. “Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo matunda mengi” (Yohana 15:8). Utasa humletea Mungu aibu. Tunamtukuza Mungu tunapokua katika uzuri kama yungiyungi, katika urefu kama mwerezi, katika kuzaa matunda kama mzabibu. (iii.) Tunamtukuza Mungu tunapomrudishia Mungu sifa na utukufu wa yote tunayoyafanya. Lilikuwa neno bora na la unyenyekevu la mfalme mmoja wa Uswidi; aliogopa kwamba watu kumpa yeye utukufu uliompasa Mungu kungesababisha aondolewe kabla kazi haijamalizika. Funza wa hariri anaposuka kazi yake ya ustadi, hujificha chini ya hariri, wala haonekani. Tunapokuwa tumefanya kwa kadiri ya uwezo wetu wote, hatuna budi kutoweka katika mawazo yetu wenyewe, na kumhamishia Mungu utukufu wa yote. Mtume Paulo alisema, “nalitaabika zaidi kuliko wote” (1 Wakorintho 15:10). Mtu angedhani kwamba neno hili lilikuwa na harufu ya kiburi; lakini mtume anaivua taji kichwani pake mwenyewe, na kuiweka juu ya kichwa cha neema ya bure, “wala si mimi, bali neema ya Mungu iliyokuwa pamoja nami.” Konstantino alikuwa na desturi ya kuandika jina la Kristo juu ya mlango; vivyo hivyo sisi tuliandike juu ya ibada zetu.
Basi na tujitahidi kulifanya jina la Mungu liwe tukufu na lenye sifa kuu. Ikiwa Mungu hutafuta mema yetu, na sisi tuutafute utukufu wake. Ikiwa yeye hufanya mambo yote yaelekee kujengwa kwetu, na sisi tufanye mambo yote yaelekee kutukuzwa kwake. Hayo yatosha kuhusu baraka hii ya pekee iliyotajwa katika neno hili.